Lem'alar

The Twenty-Fourth Gleam

Source: risaleinur multilingual dataset, risale.site source · Risale-Nur multilingual research corpus
Risale reading plan
§1

Hili lilikuwa ndio suala la pili na la tatu kutoka katika “Kumbukumbu ya Kumi na Tano” isipokuwa umuhimu wake umelifanya kuwa “Mng’ao wa Ishirini na Nne” يَٓا اَيُّهَا النَّبِىُّ قُل۟ لِاَز۟وَاجِكَ وَبَنَاتِكَ وَنِسَٓاءِ ال۟مُؤ۟مِنٖينَ يُد۟نٖينَ عَلَي۟هِنَّ مِن۟ جَلَابٖيبِهِنَّ … اِلٰى اٰخِرِ Aya hii tukufu inaamuru kujistiri, wakati ambapo ustaarabu wa bandia unakwenda kinyume na hukumu hii ya kiungu, hivyo hauoni kujistiri ni jambo la kimaumbile kwa wanawake, bali unaliona ni utumwa na kifungo kwao. Na tutabainisha katika kujibu hekima nne tu kati ya hekima nyingi zenye kujulisha kwamba hukumu hii ya ki-Qur’an inawajibishwa na maumbile ya wanawake na kinyume chake si maumbile.

§2

Hakika ya kujistiri ni jambo la kimaumbile kwa wanawake linawajibishwa na maumbile yao, kwa sababu wanawake wameumbwa na sifa ya ulaini na udhaifu, hivyo wanajikuta kuwa na haja ya mwanaume atakayewalinda wao na kulinda watoto wao ambao wanawatanguliza kabla ya nafsi zao. Hivyo wao wameelekezwa kimaumbile upande wa kujipendezesha kwa wengine na kutosababisha kukataliwa na kuchukiwa na wengine. Kisha idadi inayokaribia wanawake saba kati ya kumi: Ima ni wazee, au wabaya hawataki kudhihirisha uzee au ubaya wao, au ni wenye kubeba wivu mkubwa kwenye nafsi zao wanahofia wenye uzuri wasiwe bora kuliko wao, au wanachelea kuvunjiwa heshima na kutuhumiwa. Basi wanawake hawa kimaumbile hutaka kujistiri wakichukua tahadhari kuvunjiwa heshima na kuepuka kuwa sehemu ya kutuhumiwa na waume zao, bali tunaona wazee ndio wenye kuzingatia zaidi kujistiri kuliko wengine. Na huenda wasizidi wawili au watatu katika kila wanawake kumi ambao ni: Vijana wari wazuri hawachukizwi na kuonesha mapambo yao! Kwani inajulikana kuwa mwanadamu anachukizwa na kuangaliwa na asiowapenda. Na hata tukijaalia kuwa mwanamke mzuri anataka kuonekana na wawili au watatu kati ya ambao si maharimu zake basi bila ya shaka anachukizwa na kutazamwa na saba au nane kati yao, bali anakataa hilo. Basi mwanamke kwa kuwa kiasili ni laini ni mwenye kuathirika kwa haraka anakataa kabisa – kama tabia zake hazijaharibika na kukosa heshima – kutokana na mitazamo mibaya inayoelekezwa kwake na ambayo ina taathira ya kimaada kama sumu – kama ilivyojaribiwa – hata tunasikia kuwa: Wanawake wengi wa Ulaya ambao ndio wasiojistiri na kutembea nusu uchi, hushtaki kwa askari kutokana na kukodolewa macho wakisema: Hawa washenzi wanatusumbua kwa kutuangalia sana! Muhtasari wa kilichotangulia: Ustaarabu wa sasa kuondoa kujistiri na kuandaa mazingira kwa ajili ya kutojisitiri ni kinyume na maumbile ya mwanadamu. Na kuwa agizo la Qur’an la kujistiri –ukiongezea na kuwa ni jambo la kimaumbile – linawalinda wanawake kutokana na kudhalilika, kudharaulika, machafu na kifungo cha kimaanawi nao ni asili ya upole, huruma na ni marafiki wapendwa wa waume zao. Na wanawake - ukiachilia mbali tuliloeleza –katika maumbile wanawaogopa wanaume wageni, na hofu hii inalazimu kujistiri, ambapo inakatika ladha isiyo halali ya dakika tisa kwa kubeba adha ya kubeba mtoto kwa miezi tisa, na baadaye kulea mtoto asiye na mlezi kwa muda wa miaka tisa! Na kwa kutokea kwa uwezekano kama huu sana, wanawake huwahofia wasiyo maharimu zao hofu ya kweli, na kuwaepuka kimaumbile, hivyo, maumbile yake dhaifu humzindua kweli kweli kujistiri, ili kuzuia kuchochea matamanio ya wasiyo maharimu zake, na kuzuia kuvunjiwa heshima, na maumbile yake humjulisha kuwa mavazi yake ndio ngome madhubuti na handaki lenye amani. Na tumewahi kusikia kuwa: Mng’arisha viatu alimtongoza mke wa mtu mwenye cheo kikubwa cha kidunia, alikuwa mwenye kudhihirisha mapambo yake, na alimtongoza mchana kweupe katika mji mkuu wa Ankara! Je, kitendo hichi kibaya hakiwi pigo kubwa mbele ya nyuso za wale ambao hawatambui maana ya kuona-haya miongoni mwa maadui wa kujihifadhi na kujistiri?

§3

Hakika uhusiano thabiti na upendo wa kina baina ya mwanaume na mwanamke havitokani tu na mahitaji ya maisha ya kidunia, mwanamke si mwenza wa mumewe katika maisha ya kidunia pekee, bali ni mwenza wake pia katika maisha ya kudumu milele. Maadamu ni mwenza wake katika maisha ya kubaki hapaswi kuelekeza macho ya asiyekuwa mwenza wake wa kudumu na rafiki wake wa milele kwenye mapambo yake, wala asimuudhi mumewe na kumfanya awe na hasira na wivu. Na kwa kuwa mumewe muumini kwa hukumu ya Imani yake hafungamanishi upendo wake kwa maisha ya kidunia tu wala hampi upendo wa kinyama unaokuwa wakati wa uzuri wake tu, bali anakuwa na upendo juu yake na heshima ya dhati na ya kudumu, haziwi sifa hizo wakati wa ujana wake na uzuri wake tu bali zinadumu hadi wakati wa uzee na kuondoka kwa uzuri wake, kwa sababu ni mwenza wake katika maisha ya kudumu milele... Kutokana na hili mwanamke hana budi kuufanya uzuri wake na mapambo yake kuwa maalumu kwa mumewe tu na kumpenda yeye tu, kama ulivyo ubinaadamu, kama si hivyo atapoteza vingi na hatapata ila kichache. Kisha kinachohitajika kisheria: Ni mwanaume kulingana na mwanamke, na hii ina maana kila mmoja kuendana na mwenziwe na kufanana naye, na cha muhimu zaidi katika kufanana huku ni kufanana kidini kama inavyojulikana. Basi furaha iliyoje ya mume huyo mwenye kugundua kushikamana na dini kwa mkewe na kumuiga, na kuwa mwenye dini, ili asije kumpoteza mwenza wake mwaminifu katika maisha ya kudumu milele! Na ni kiasi gani cha bahati kwa mwanamke ambaye anagundua kushikamana na dini kwa mumewe na kuhofia kumpoteza mshirika wake mwaminifu wa maisha ya kudumu, hivyo hushikamana na imani na ucha Mungu. Ole wake kisha ole wake mtu anayezama katika maovu yatakayomkosesha mke wake mwema. Na huzuni iliyoje kwa mwanamke ambaye hamuigi mumewe mcha Mungu, na kumpoteza mwenza wake mkarimu wa kudumu mwenye furaha. Na ole wao wanandoa wasiyo na furaha ambao huigana katika ufuska na maovu, na kila mmoja kushindana katika kumsukuma mwenziwe motoni.

§4

Hakika ya furaha ya familia katika maisha na kuendelea kwake ni kwa kubadilishana uaminifu baina ya wanandoa, heshima inayofaa, na upendo wa kweli baina yao, isipokuwa kutojistiri kunaharibu uaminifu huo, heshima na upendo wa kubadilishana. Ampapo wanawake tisa kati ya kumi hukutana na wanaume wenye kuwazidi uzuri wa waume zao, wakati ambapo haoni ila mmoja kati yao ambaye ni mchache wa uzuri kuliko mumewe wala haipendezeshi nafsi yake kwake. Na hali ni hivyo hivyo kwa wanaume haoni ila mmoja kati ya ishirini ambaye ni mchache wa uzuri kuliko mke wake, wakati ambapo waliobaki wanaona mbele yao wanaowazidi wake zao kwa uzuri. Hali hii inaweza kupelekea kupatikana hisia duni na mbaya katika nafsi ukiongezea ya kuwa inasababisha kuondoka kwa upendo wa dhati na kupotea kwa heshima hiyo, na hiyo ni: Kuwa mwanadamu kimaumbile hawezi kubeba hisia duni za kinyama kwa maharimu zake - kama dada – kwa sababu nyuso za maharimu huonesha hisia za upole na upendo wa kisheria unaotokana na undugu. Basi hisia hizi tukufu huzuia misukumo ya kimatamanio ya nafsi, isipokuwa kuonesha kisichofaa kama mguu, kunaweza kuchochea kwa nafsi duni hisia mbaya na chafu kwa sababu ya kuondoka hisia za uharamu, ambapo alama za maharimu hufanya undugu uhisiwe, na kwa kuwa kwake ni haramu na kutofautiana na wengine. Hivyo kuonesha sehemu kama hizo za mwili huwa sawa maharimu na wasiokuwa maharimu, kwa sababu ya kukosekana alama za kutofautisha zenye kuwajibisha kujizuia kutazama kulikoharamishwa, na huenda kukachochea kwa baadhi ya maharimu wasiyo na heshima matamanio ya mtazamo wa kishetani! Mfano wa mtazamo kama huu ni kuporomoka kubaya kwa uanadamu, ubaya wake husababisha ngozi kusisimka.

§5

Inafahamika kwamba wingi wa kizazi ni jambo linalotakiwa na watu wote, hakuna umma wala Dola isiyohimiza wingi wa kizazi, na Mtume Mkarimu (s.a.w) amesema: (Oaneni mpate kukithiri, kwani mimi nitajivunia kwa umma zingine siku ya kiama). Japo kutojistiri na kuruhusu kuonesha mapambo kunazuia ndoa, bali kunapunguza sana kukithiri kwa watu, kwa sababu kijana hata awe mwenye ufuska kiasi gani, hutaka mwenza wake katika maisha kuwa mwenye kujihifadhi, wala hataki awe aliyekosa heshima asiyejihifadhi kama yeye. Hivyo utamuona anapendelea kuwa kapera kuliko kuoa. Na huenda akaelekea katika uharibifu. Ama mwanamke yeye si kama mwanaume ambapo hawezi kuchagua wa kumuoa. Na mwanamke kwa kuwa ni mwangalizi wa mambo ya ndani ya nyumba, na ndiye aliyeamrishwa kuwatunza watoto wa mumewe, mali yake, na kila kinachomuhusu, basi tabia zake kuu kabisa ni: Utiifu na uaminifu. Isipokuwa kutojistiri kwake kunaharibu utiifu huo na huteteresha imani ya mume juu yake, na kumpa mume maumivu ya kimaanawi na adhabu ya moyo. Hata ushujaa na ukarimu ambazo ni sifa mbili njema kwa wanaume zinapokuwa kwa wanawake huzingatiwa ni katika tabia mbaya kwa kukosekana ndani yake utiifu na uaminifu, kwani hupelekea katika ubaya na israfu. Na kwa vile wadhifa wa mume hauishii tu katika uaminifu wa mali yake, na kufungamana naye bali unakusanya kumlinda, kumhurumia na kumuheshimu, hivyo hayamlazimu yale yanayomlazimu mke, yaani haufungwi uchaguzi wake kwa mke mmoja, na anaweza kuoa wanawake wengine. Hakika nchi zetu haziwezi kulinganishwa na nchi za Ulaya, kwa kuwa kuna njia kali za kuhifadhi – kwa kiasi fulani – heshima na wema katikati ya kutojistiri, ikiwemo mapambano na mfano wa hivyo. Basi yeyote anayemtazama kwa ubaya mke wa mmoja kati ya wenye heshima anapaswa kutundika sanda katika shingo yake kwanza. Na hii ukiongezea kuwa tabia za wakazi wa Ulaya ni zimepooza ngumu kama hali yao ya hewa. Ama hapa hasa katika nchi za ulimwengu wa Kiislamu ni katika nchi za joto zikilinganishwa na za Ulaya, na inafahamika kiasi cha taathira ya mazingira kwa tabia za mwanadamu. Katika sehemu hizo za baridi, na kwa watu waliopooza huenda kutojistiri ambako kunachochea matamanio ya kinyama na ya nafsi kuvuka mipaka, kama kunavyopelekea kuvuka mipaka na israfu kwa watu wenye hisia ambao huchochewa kwa haraka katika sehemu zenye joto. Kutojistiri ambako kunachochea matamanio ya nafsi, bila ya shaka kunapelekea kuvuka mipaka na kudhoofika kwa kizazi na kupotea nguvu. Ambapo mtu ambaye anaweza kukidhi haja yake ya kimaumbile mara moja kwa mwezi au siku ishirini anadhani kuwa analazimika kukidhi kila baada ya siku chache. Na kwa vile kuna vizuizi vya kimaumbile – kama hedhi – vinavyomtenga na mke wake na huenda vikadumu kwa siku kumi na tano, utamuona anaelekea katika uchafu anaposhindwa kujizuia. Kisha watu wa mijini hawapaswi kuwaiga watu wa vijijini katika maisha yao ya kijamii na kuondoa kujistiri baina yao, kwa sababu watu wa vijijini hushughulishwa na kutafuta riziki nao wanawajibika kufanya juhudi kubwa za kimwili ili kupata riziki zao, na mara nyingi wanawake hushirikiana katika kazi zenye kuchosha, hivyo vile vinavyoweza kuonekana miongoni mwa sehemu za miili yao migumu havichochei matamanio kwa wengine, ukiachilia mbali kuwa vijijini hakuna wajinga waliokosa kazi kama ilivyo mijini. Basi uharibifu wake haufikii moja ya kumi ya ule wa mijini, na kwa hiyo miji hailingani na vijiji. بِاس۟مِهٖ سُب۟حَانَهُ

§6

Nilipokuwa nikitazama katika idadi kadhaa za wilaya wanawake kuitilia umuhimu sana Risale-i Nur, na nilipotambua kutegemea kwao masomo yangu yanayohusu Nuru kwa namna ambayo ni zaidi ya ninavyostahiki, nimekuja kwa mara ya tatu katika madrasa ya Az-Zahra ya kimaanawi, mji huu uliobarikiwa wa (Isparta), basi nikasikia kuwa wanawake hao wema waliyobarikiwa, ndugu zangu wa akhera, wananisubiri niwape somo, kwa mtindo wa masomo ya mawaidha na mwongozo yanayotolewa misikitini. Isipokuwa nasumbuliwa na maradhi kadhaa, pamoja na udhaifu na uchovu mkubwa kiasi kwamba siwezi kuongea wala kutafakari, lakini pamoja na hayo imepita fikra nzito moyoni mwangu usiku huu, nayo ni: Kwamba uliandika kabla ya miaka kumi na tano risala ya (Mwongozo kwa vijana) kwa maombi kutoka kwa vijana wenyewe, na wengi wamefaidika nayo, wakati ambapo wanawake ni wenye kuhitajia zaidi mwongozo kama huu katika zama hizi. Katikati ya fikra hii na japo nasumbuliwa na kukanganyikiwa, udhaifu na kutojiweza nimeandika kwa kufupisha mno kwa ajili ya dada zangu waliyobarikiwa na mabinti zangu vijana wa kimaanawi baadhi ya mambo yanayowalazimu, ndani ya nukta tatu.

§7

Na ilivyokuwa moja ya misingi muhimu zaidi ya Risale-i Nur ni (Huruma) na kwamba wanawake ni viongozi wa huruma na mabingwa wa upendo, wamekuwa ndio wenye mafungamano zaidi na Risale-i Nur kimaumbile. Uhusiano huu wa kimaumbile umekuwa ukihisiwa katika maeneo mengi, sifa zote njema na shukrani ni kwa Allah (s.w). Na kujitolea kulikokusanya huruma na upendo kumekuwa ni kwenye umuhimu mkubwa katika zama zetu hizi, kwa kuwa kunaonesha ikhlasi ya kweli na kujitolea bila ya mbadala. Naam, hakika kujitolea kwa mama roho yake kwa ajili ya kumuokoa mwanawe kutokana na kuangamia bila ya kusubiri ujira, na kujitolea kwake kwa ikhlasi ya kweli kwa watoto wake kwa kuzingatia wadhifa wake kimaumbile, kunajulisha kuwepo ushujaa wa hadhi ya juu kwa wanawake, ambapo wanaweza kuyaokoa maisha yao ya kidunia na akhera kwa kudhihiri kwa ushujaa huu ndani ya nafsi zao, isipokuwa makundi ya ufisadi yanazuia kudhihiri kwa sifa hiyo yenye thamani iliyonyooka, au kuielekeza sifa hiyo nzuri sehemu isiyo yake na kuharibu matumizi yake. Tunaleta hapa mfano mmoja katika mifano yake mingi: Hakika mama mwenye upendo huweka mbele ya macho yake kila namna ya kujitolea ili kumkinga mwanawe kutokana na mabalaa na kuangamia, ili awe salama mwenye uzima hapa duniani. Basi anamlea mwanawe kwa msingi huu, anatoa mali yake yote ili mwanawe awe bwana mkubwa mwenye kuamrisha. Utamwona anamchukua mwanawe kutoka katika madrasa za elimu ya dini na kumpeleka Ulaya, bila ya kufikiria kuhusu maisha ya milele ya mwanawe ambayo yanakuwa katika hatari. Basi wakati ambapo anafanya juhudi kumuokoa na jela la kidunia, hajali kuhusu kutumbukia kwake katika jela la Jahanamu la milele, na kutenda tofauti kabisa na maumbile yake, ambapo badala ya kumfanya mwanawe asiye na hatia kuwa mwombezi wake siku ya kiama anamfanya mwenye madai dhidi yake, kwa kuwa atalalamika mtoto huyo huko kwa kusema: “Kwanini hukuimarisha Imani yangu hadi umesababisha kuangamia kwangu huku?!”. Na kwa vile hakuchukua malezi ya kutosha ya Kiislamu, hivyo hajali huruma ya ajabu ya mzazi wake, bali anaweza asimtimizie haki zake. Lakini kama mzazi huyo atafanya juhudi katika kumuokoa mwanawe dhaifu kutokana na jela la milele ambayo ni Jahanamu, na kutokana na kutoweka kwa milele ambako ni kufa katika upotevu, kwa huruma yake ya kweli aliyopewa bila ya kuitumia vibaya, basi hakika ya mtoto wake atafikisha Nuru daima kwa roho yake baada ya kufa kwake, kwa kuwa atasajili katika ukurasa wa amali zake mfano wa mema yote anayoyafanya mtoto. Kama vilevile atakavyokuwa na mtoto mwema aliyebarikiwa wakineemeka kwa pamoja katika maisha ya milele, akiwa ni mwombezi wake kwa Allah kwa kadri atakavyoweza kumuombea, si mwenye kumlalamikia wala mwenye madai dhidi yake. Naam, hakika Ustadhi wa kwanza wa mwanadamu na ambaye ana taathira kubwa katika elimu ni mama yake. Kwa mnasaba huu nitabainisha maana hii ambayo ninaihisi daima kwenye haiba yangu, nayo ni: Naapa kwa Allah kwamba somo lililothibiti zaidi nililolichukua, nalo ni kama linakuwa jipya kwangu, ni maelekezo ya mama yangu Allah amrehemu na masomo yake ya kimaanawi, hadi yamethibiti katika kina cha maumbile yangu yakawa kama mbegu mwilini mwangu, kwenye umri wangu ambao unakaribia miaka themanini japokuwa nimechukua masomo kutoka kwa watu elfu themanini bali naona kwa yakini kwamba masomo mengine yote hujengwa juu ya mbegu hizo. Kwa maana kwamba somo la mama yangu – Allah amrehemu – na maelekezo yake kwa maumbile na roho yangu nikiwa nina umri wa mwaka mmoja, nashuhudia kuwa ni mbegu za msingi ndani ya hakika kubwa ambazo naziona sasa hivi nikiwa na umri wa miaka themanini. Mfano wa hilo: Kwamba “huruma” ambayo ni msingi muhimu zaidi kati ya misingi minne katika mwenendo wangu wa maisha. Na upole na rehema ambavyo ni hakika kuu pia miongoni mwa hakika za Risale-i Nur, ninavishuhudia kwa yakini kwamba vinatokana na matendo ya mama huyo mpole, hali zake za huruma na masomo yake ya kimaanawi. Naam, hakika huruma na upendo uliyo katika umama na ambao anaubeba kwa ikhlasi ya kweli na kujitolea kumetumiwa vibaya katika wakati huu, ambapo mama hafikirii atakachokipata mwanawe huko Akhera miongoni mwa hazina zenye thamani zaidi ya almasi, bali anaelekeza uso wake katika dunia hii ambayo hailingani na kipande cha kioo chenye kutoweka, kisha anamuonea huruma mwanawe katika upande huu wa maisha. Na hii si vinginevyo ila ni kuitumia vibaya huruma hiyo. Hakika kinachothibitisha ushujaa wa wanawake katika kujitolea kwao bila ya kusubiri ujira wala mbadala, bila ya faida wanayoipata kwa ajili ya nafsi zao na bila ya ria na kujionesha, ni kule kuwa tayari kujitolea kwa roho zao kwa ajili ya mtoto, nasema hakika ya kinachothibitisha hilo ni kile tukionacho kwa kuku ambaye anabeba mfano mdogo wa huruma hiyo, huruma ya mama na upendo wake, kwani anamshambulia simba, na kujitolea muhanga, roho yake, kwa ajili ya kuvilinda vifaranga vyake vidogo. Na katika wakati wa sasa, hakika kitu cha lazima zaidi na msingi muhimu zaidi katika malezi ya Kiislamu na amali za akhera ni ikhlasi. Basi ubingwa huu wa hali ya juu katika huruma ndani yake kuna ikhlasi ya kweli. Basi nukta hizi mbili zinapodhihiri katika kundi hilo lililobarikiwa, kundi la wanawake, basi zitakuwa ni njia ya furaha kubwa katika ukanda wa Kiislamu. Ama kujitolea kwa kina baba hakui bila ya mbadala kabisa, bali kunahitaji ujira kwa pande nyingi zinazofika mia moja. Na kwa uchache kunahitaji fahari na sifa. Lakini kwa masikitiko makubwa hakika wanawake wanaingiza ria kwa namna nyingine kutokana na udhaifu na kushindwa kwao, na hiyo ni kwa ajili ya kuepukana na shari za waume zao wenye kudhulumu na kuwatawala kimabavu.

§8

Nilipokuwa nimejitenga na watu na maisha ya kijamii katika mwaka huu, niliiangalia dunia kwa kushuka katika mahitaji ya ndugu wa Nuru; kike kwa kiume, nikasikia kwa marafiki wengi niliokutana nao malalamiko kuhusu maisha yao ya kifamilia. Nikasikitika sana nikasema: “Je ufisadi umeingia katika maisha haya pia?” Hakika maisha ya kifamilia ni ngome madhubuti ya mwanadamu, na hasa Mwislamu kwani ni kama pepo yake ndogo na dunia yake ndogo”. Nikatafuta sababu iliyopelekea katika ufisadi wake. Nikafahamu kwamba kuna mashirika ya siri yanafanya juhudi ili kuwapotosha vijana na kuwaharibu kwa kuwawepesishia njia za matamanio na kuwapeleka katika uovu ili kuiharibu jamii ya Kiislamu na kuidhuru dini ya Uislamu, kama nilivyohisi pia kwamba mashirika yanafanya kazi kwa kujificha na kufanya juhudi kubwa yenye kuathiri ili kuwashawishi walioghafilika miongoni mwa wanawake wema kwenye njia zisizo sahihi za dhambi. Na nikatambua kwamba pigo kubwa kwa umma huu wa Kiislamu linakuja kutoka upande huo. Basi mimi ninabainisha kinagaubaga, enyi ndugu zangu, mabinti zangu vijana wa kimaanawi! Hakika tiba mujarabu ni kuokoa furaha ya wanawake kutokana na ufisadi duniani na akhera kwa pamoja, na kwamba njia pekee ya kuhifadhi sifa zao laini zilizo katika maumbile yao kutokana na ufisadi, si vinginevyo ila ni kuwalea malezi ya kidini ndani ya mipaka ya Uislamu uliyokusanya kila kitu. Mnasikia kilichotokea kwa kundi lile lililobarikiwa Urusi! Na katika sehemu ya Risale-i Nur pamesemwa: Hakika mume mwema hajengi mapenzi yake kwa mkewe kwa uzuri wa nje wenye kutoweka usiodumu miaka kumi, bali anatakiwa kujenga mapenzi yake kwake kwa huruma yake ambayo ni mapambo mazuri zaidi na ya kudumu kwa wanawake na ayathibitishe kwa uanauke wake kwa uzuri wa mwenendo wake, ili mapenzi yake yadumu kila atakapokuwa anazeeka mke huyo dhaifu, kwani sio mwenza wake katika maisha ya kidunia ya muda, bali ni mwenza wake kipenzi katika maisha ya milele ya kudumu. Basi wanalazimika kupendana kwa heshima ya ziada na rehema pana, kila wanavyokua. Ama maisha ya kifamilia yanayokulia katika ustaarabu wa kisasa yapo katika hatari ya kuporomoka na kuharibika, ambapo uhusiano huo unajengwa juu ya urafiki wa muda unaofuatiwa na utengano wa milele. Na vilevile pamesemwa katika sehemu ya Risale-i Nur: Hakika mwenye furaha ni yule mume anayemuiga mkewe mwema, hivyo anakuwa mwema kama yeye, ili asimpoteze mwenza wake katika maisha ya kudumu ya milele. Na ni mke mwenye furaha kiasi gani anayemuona mumewe kashikamana na dini naye anashikamana na dini ili asimpoteze mwenza wake wa kudumu, na kufuzu furaha ya akhera yake pamoja na ya dunia yake. Na mume huyo ni mwenye huzuni kiasi gani anayemfuata mkewe ambaye amejitupa katika uovu na akashirikiana naye bila ya kufanya juhudi kumuokoa! Na ni kiasi gani cha huzuni kwa mke ambaye anaangalia uovu wa mumewe na ufasiki wake na kumuiga kwa namna nyingine. Ole wao wanandoa hao ambao kila mmoja anamsaidia mwingine katika kumsukuma motoni, yaani kila mmoja anampotosha mwenziwe kuzama katika mapambo ya kiustaarabu. Na maana ya sentensi zilizokuja kwa maana hii ndani ya “Risale-i Nur” ni kuwa haiwezekani - katika zama hizi – kuneemeka kwa maisha ya kifamilia na kufikia furaha ya dunia na akhera na kudhihiri kwa sifa za hadhi ya juu kwa wanawake isipokuwa kwa kujipamba na tabia za Uislamu ambazo sharia imeziweka. Hakika nukta muhimu na upande wa maisha ya kifamilia katika wakati huu ni kuwa mke anaposhuhudia uharibifu kwa mumewe na khiyana na kutokuwepo uaminifu, naye kwa upande wake - kwa ajili ya kumkomoa – akaacha wadhifa wake wa kifamilia nao ni uaminifu, hapo nidhamu ya familia hiyo inaharibika kikamilifu na kupotea bure, kama kuharibu nidhamu jeshini. Hivyo hapana budi kwa mke kufanya bidii kukamilisha upungufu wa mumewe na kurekebisha upungufu wake ili amwokoe mwenza wake wa milele, kinyume na hivyo atapata hasara na madhara kila upande akijaribu kuidhihirisha nafsi yake na kuipendezesha kwa wengine kwa kujionesha na kujipamba, kwa sababu anayeacha uaminifu atapata malipo yake hapa duniani pia. Kwa kuwa maumbile yake yanaepuka wasiokuwa maharimu zake na kupata karaha kwao. Anawaepuka watu kumi na nane kati ya ajinabi ishirini, wakati ambapo mwanamme haoni karaha kumwangalia mwanamke mmoja kati ya kila mia ajinabi kwake. Kama ilivyo mke anateseka na adhabu kwa upande huu, basi anaiweka nafsi yake sehemu ya kutuhumiwa pia kwa kutokuwa na uaminifu, basi hawezi kuhifadhi haki zake ukiachilia mbali udhaifu wake. Ufupisho: Kama ilivyo wanawake hawafanani na wanaume - kwa upande wa huruma na upendo - katika kujitolea muhanga wala katika ikhlasi, na kwamba wanaume hawafikii kiwango chao katika kujitolea muhanga. Vilevile mwanamke hamfikii mwanaume katika uovu na upotevu kwa sura yoyote ile, hivyo anaogopa sana kwa maumbile yake dhaifu wasiokuwa maharimu zake na anajikuta akilazimika kujihifadhi kwa hijabu. Hiyo ni kwa kuwa mwanaume atakapotongoza kwa ajili ya kupata utamu wa dakika nane hapati madhara isipokuwa kupoteza lira kadhaa, wakati ambapo mwanamke atalipa kwa ladha ya dakika nane kwa uzito wa miezi minane na atabeba majukumu ya ulezi wa mtoto bila ya kuwa na mlinzi kipindi chote cha miaka minane. Kwa maana mwanamke hamfikii mwanamme katika uovu na anapata adhabu juu ya hilo maradufu kwa maradufu ya adhabu ya mwanamme. Hakika matukio haya si nadra kutokea kwake, na yanajulisha kuwa wanawake ni viumbe waliyobarikiwa wameumbwa ili wawe chanzo cha tabia nzuri, kwani inakaribia kukosekana kwao maandalizi ya ufuska na uovu ili kustarehe na vionjo vya kidunia. Kwa maana wanawake ni aina ya viumbe wema waliyobarikiwa, wameumbwa ili kuendesha maisha ya furaha ya kifamilia ndani ya mipaka ya malezi ya Kiislamu. Basi laana iwe kwa mashirika hayo ambayo yanafanya juhudi katika kuwaharibu wanawake hawa wema. Na ninamwomba (s.w) kuwahifadhi dada zangu kutokana na shari za hawa wajinga waharibifu.. Amin. Enyi dada zangu! Nakuambieni maneno haya kwa namna ya kipekee: Fanyeni kazi ya kupata riziki zenu kwa mikono yenu kama wanavyofanya wanawake wema wa vijijini na toshekeni na uchumi na ukinaifu vilivyomo katika maumbile yenu. Na hii ni bora kuliko kujidhalilisha kwa sababu ya dhiki ya maisha kwa kujiweka katika umiliki wa mume mwovu, mwenye tabia mbaya, mwenye kujifanya mzungu. Na kama ikiwa bahati ya mmoja wenu na riziki yake ni mume asiyeendana naye, basi na aridhie riziki yake na akinai, huenda Allah akamfanya mumewe kuwa mwema kwa kule kuridhia na kukinai kwake. Na kama si hivyo atakuwa ni mwenye kukimbilia mahakamani kwa ajili ya talaka - kama nisikiavyo katika wakati huu – na hii ni kinyume na utukufu wa Kiislamu na heshima ya umma.

§9

Dada zangu vipenzi! Tumbueni kwa hakika! Kwamba vionjo na starehe zilizo nje ya mipaka ya sharia, ndani yake kuna maumivu na tabu maradufu ya maradufu ya ladha zake. Na (Risale-i Nur) imethibitisha ukweli huu kwa mamia ya hoja zenye nguvu na matukio ya uhakika. Na mnaweza kupata ufafanuzi wake ndani ya (Risale-i Nur). Kwa mfano: Neno la sita, saba, na la nane kutoka katika kitabu “Maneno Mafupi” na “Mwongozo kwa Vijana” yanakubainishieni ukweli huu kwa uwazi uliotimia kwa niaba yangu. Hivyo ni juu yenu kukinai na kuwa na utulivu na kutosheka na kile kilicho ndani ya mipaka ya sharia miongoni mwa vionjo na ladha. Hivyo kucheza na watoto wenu wasio na hatia na kukaa nao katika nyumba zenu ni starehe safi na bora kwa mara mia kuliko starehe ya sinema. Na tambueni kwa yakini! Kwamba ladha ya hakika hapa duniani ipo katika Imani na katika mipaka ya Imani tu. Na kwamba katika kila amali njema kuna ladha ya kimaanawi, wakati ambapo katika upotevu kuna maumivu yenye kukupa dhiki katika dunia hii pia. Ukweli huu umethibitishwa na (Risale-i Nur) kwa mamia ya hoja madhubuti. Mimi mwenyewe nimeshuhudia kwa jicho la yakini kupitia uzoefu mwingi na matukio mengi: Kwamba katika Imani kuna mbegu ya pepo, na katika upotevu kuna mbegu ya Jahanamu. Na nimeandika ukweli huu mara kwa mara katika (Risale-i Nur) kiasi kwamba mkaidi zaidi kati ya Wataalamu maafisa na mahakama wameshindwa kuutengua ukweli huu. Basi wacha (Risala ya Hijabu) mwanzoni na “Mwongozo kwa Vijana” na “Maneno Mafupi” viwe naibu wangu katika kutoa darasa kwenu enyi ndugu zangu wanawake wema mliobarikiwa na enyi ambao ni kama mabinti zangu wadogo. Nimesikia kwamba mnataka niwafundishe darsa msikitini, lakini maradhi yangu ni makali, ukiachilia mbali udhaifu wangu, na sababu nyingine, vinanizuia kufanya hivyo. Hivyo, enyi dada zangu mnaosoma somo hili ambalo nimeliandika kwa ajili yenu, nimeamua kukufanyeni washirika wangu katika mapato yangu yote ya kimaanawi na katika dua zangu, kama wanafunzi wa Nuru. Na mkiweza kupata (Risale-i Nur) na kuisoma au kuisikia, kwa niaba yangu, basi mnakuwa washirika wa ndugu zenu wanafunzi wa Nuru katika mapato yao yote ya kimaanawi na dua zao kwa mujibu wa kanuni yetu iliyothibiti. Nilitaka kukuandikieni zaidi ya hiki lakini nimetosheka na kiasi hiki kutokana na maradhi yangu makali, kudhoofika kwangu na uzee wangu, na majukumu mengi yananisubiri kama kuhariri risala. Mwenye kubaki, yeye ni mwenye kubaki Ndugu yenu muhitaji wa dua zenu Said Nursî

Private reading note

This note stays on this device and is never uploaded to a server.

Up to 1,200 characters