Lem'alar

The Twenty-Sixth Gleam

Source: risaleinur multilingual dataset, risale.site source · Risale-Nur multilingual research corpus
Risale reading plan
§1

(Mng’ao huu ni ibara ya nuru ishirini na sita za matumaini na mwanga wa faraja) Tanbihi Hakika sababu iliyonipelekea kusajili kile kilichokuwa kikinisumbua katika maumivu ya kimaanawi mwanzoni mwa kila tarajio kwa mtindo wenye kuathiri mno kiasi cha kukusababishieni maumivu pia, si vinginevyo ila kwa kubainisha kiasi cha nguvu ya utendaji kazi wa dawa iliyokuja katika Qur’an yenye hekima na kiasi kikubwa cha kuathiri kwake. Ijapokuwa “Mng’ao” huu unaowahusu wazee haukuhifadhi ubainifu mzuri na uzuri wa kuleta manufaa kwa sababu kadhaa: Ya kwanza: Ni kwa sababu unahusu matukio ya maisha yangu binafsi na matukio yake. Hivyo kwenda kimawazo katika zama hizo, na kuishi na matukio yake, na hivyo kuyaandika kwa hali hiyo, kumesababisha kutohifadhi nidhamu, katika ubainifu na maelezo. Ya Pili: Maelezo yameingiwa na mkanganyiko, kwa sababu uandishi ulifanyika baada ya sala ya alfajiri, kwa kuwa katika kipindi hicho nilikuwa nahisi uchovu sana, ukiachilia mbali kulazimika kuandika kwa haraka. Ya Tatu: Hatukuwa na wakati wa kutosha wa kusahihisha kikamilifu; kwa sababu mwandishi aliyekuwa amechoka kutokana na mambo ya Risale-i Nur na mara nyingi alikuwa akitoa udhuru wa kutoweza kuhudhuria jambo lililopelekea kwa madhumuni kupoteza mpangilio uliotakiwa. Ya Nne: Tumetosheka tu na masahihisho pamoja na marekebisho ya juu juu bila ya kuzama katika maana; kwa sababu ya tabu na uchovu tuliokuwa tukihisi mwisho wa uandishi, basi bila ya shaka maudhui iliambatana na upungufu katika kueleza na kufikisha. Hivyo tunawaomba wazee wakarimu waangalie mapungufu yangu ya ufikishaji kwa jicho la msamaha, na wanijumuishe katika dua zao wanapoinua mikono yao wakinyenyekea kwa Allah Mwenye kurehemu ambaye hayarejeshi maombi ya wazee wema... بِسْمِ اللّٰهِ الرَّحْمٰنِ الرَّح۪يمِ كٓهٰيٰعٓصٓ ۝ ذِك۟رُ رَح۟مَتِ رَبِّكَ عَب۟دَهُ زَكَرِيَّا ۝ اِذ۟ نَادٰى رَبَّهُ نِدَٓاءً خَفِيًّا ۝ قَالَ رَبِّ اِنّٖى وَهَنَ ال۟عَظ۟مُ مِنّٖى وَاش۟تَعَلَ الرَّا۟سُ شَي۟بًا وَلَم۟ اَكُن۟ بِدُعَٓائِكَ رَبِّ شَقِيًّا ۝ Şu Lem’a yirmi altı ricadır.

§2

Enyi mliofika umri wa ukamilifu, enyi ndugu zangu wazee watukufu, na enyi ndugu zangu wazee wa kike wenye heshima! Mimi ni kama nyinyi ni mkongwe, nitakuandikieni baadhi ya hali zilizonipitia na niliyoyapata baina ya muda na mwingine miongoni mwa milango na ming’aro ya matumaini katika kipindi cha uzee, huenda mkashirikiana nami katika nuru za faraja zenye kung’aa kutoka katika matumaini hayo. Hakika nilichokiona katika mwanga, na alichonifungulia Allah miongoni mwa milango ya nuru na matumaini, si vingine isipokuwa niliyashuhudia hayo kulingana na uwezo wangu wenye upungufu na maandalizi yangu yenye kutatiza, na maandalizi yenu mema – kwa idhini ya Allah – yataufanya mwanga huo kung’aa zaidi ya nilivyouona, na yatafanya tumaini hilo kuwa lenye nguvu na imara zaidi ya nilivyolikuta. Na hapana shaka kwamba chanzo cha mianga na matumaini tutakayoyataja si kingine ila ni (Imani).

§3

Nilipoukaribia uzee, katika majira ya Vuli, na katika wakati wa alasiri, niliiangalia dunia kutoka kwenye kilele cha mlima, ghafla nikahisi hali ya kuhuzunisha pamoja na giza likiifunika, ikipita katika kina cha nafsi yangu, niliiona nafsi yangu: Kwamba nimefikia umri wa uzee, na mchana umekua mzee, na mwaka umezeeka, na dunia pia imezeeka. Nikatikiswa na uzee huu ambao umefunika kila kitu pembezoni mwangu kwa mtikiso mkubwa. Umekaribia wakati wa kuiacha dunia, na umekaribia wakati wa kuviacha vipenzi, wakati nikigeukageuka hali ya kuwa ni mwenye kukata tamaa na mwenye huzuni tahamaki rehema ya kiungu inadhihiri mbele yangu kwa udhahiri ambao umeigeuza huzuni ile yenye kuumiza kuwa ni furaha yenye kung’aa moyoni, na ukaubadilisha ule utengano wenye kuumiza wa vipenzi kuwa ni faraja yenye kuangaza pembe zote za nafsi. Naam, enyi wazee wenzangu! Hakika ya Allah (s.w) ambaye anaileta dhati yake tukufu kwetu, na kuitambulisha kwetu katika sehemu zaidi ya mia moja ndani ya Qur’an tukufu, kwa sifa ya “Ar-Rahmaan Ar-Rahiim” na ambaye anaipeleka rehema yake kwa kile anachokileta juu ya mgongo wa ardhi katika neema bila ya kukatika, ili uwe ni msaada kwa wahitaji wa rehema hiyo katika viumbe hai, na ambaye anatuma zawadi zake kutoka kwenye ulimwengu wa ghaibu na kujaza majira ya machipuo neema zisizo hesabika kila mwaka, anazituma kwetu sisi wahitaji wa riziki, akidhihirisha kwazo kwa uwazi kabisa madhihirisho ya rehema yake enevu, kwa mujibu wa viwango vya udhaifu na mapungufu yaliyomo ndani yetu. Basi rehema hii ya muumbaji wetu mwenye kurehemu ni tumaini kubwa mno, na tarajio kubwa zaidi katika kipindi hiki cha uzee wetu huu, bali ni nuru yenye kuangaza zaidi kwetu. Hakika kuidiriki na kuipata rehema hiyo, inakuwa kwa kujinasibisha na huyo (Mwingi wa rehema) kwa imani, na kwa kumtii yeye (s.w) kwa kutekeleza faradhi na mambo ya wajibu.

§4

Nilipozinduka kwenye asubuhi ya uzee, kutoka katika usingizi wa usiku wa ujana, niliiangalia nafsi yangu kwa mazingatio, nikaikuta kana kwamba inaporomoka kuelekea chini kwenda katika usawa wa kaburi, kama alivyoelezea NiyazAl-Misriy: Jengo la umri linadhoofika kwa kuanguka jiwe baada ya jingine, Roho imeghafilika hali ya kuwa jengo lake limeshabomoka. Mwili wangu ambao ndio makaazi ya roho yangu, umeanza kuporomoka jiwe moja baada ya jingine kila siku zinavyosogea, na matarajio yangu ambayo yalikua yakinivuta kwa nguvu kwenye dunia, kamba zake zimeanza kunyambuka na kukatika. Hisia za kukaribia wakati wa kutengana na idadi isiyodhibitika ya vipenzi na marafiki zikanipitikia nafsini mwangu, basi nikaanza kutafuta tiba ya dondandugu la kimaanawi ambalo inavyoonekana halitarajiwi kuwa na dawa yenye kuponya! Sikuweza kulipatia dawa, pia nikasema kama alivyosema Niyaz Al-Misriy: Hekima ya Allah inataka kutoweka kwa mwili, Na moyo ni wenye kupenda umilele Nafsi yangu inahuzunika kutokana na balaa na dhiki Hata Luqman ameshindwa kuipatia maponyo Na wakati nikiwa katika hali hii tahamaki nuru ya Mtume Mkarimu (s.a.w) ambaye ni rehema ya Allah kwa walimwengu, na mfano wake ambao unaielezea, mlinganiaji wake, na mwenye kuitamka. Na tahamaki uombezi wake, na kile alichompa katika zawadi ya uongofu kwa wanaadamu anakuwa ni dawa yenye kuponya ya maradhi hayo mabaya niliyoyadhania hayana dawa, na anabadilisha ukataji tamaa huo mbaya ulionizunguka kuwa ni nuru yenye kung’aa ya tumaini. Naam, enyi wazee waheshimiwa wa kiume na wa kike na enyi wenye kuhisi uzee kama mimi! Sisi ni wenye kuondoka na hilo haliepukiki, na hatutaruhusiwa kukaa hapa kuihadaa nafsi na kufumba jicho, sisi ni wenye kupelekwa kwenye mafikio yasiyo na shaka. Lakini ulimwengu wa Barzakh, sio kama unavyoonekana kwetu kutokana na viza vya dhana zinazotokana na mghafala, wala si kwa namna watu wa upotevu wanavyoujengea taswira. Huo si ulimwengu wa utengano, wala si ulimwengu wenye giza bali ni pahala pa mkusanyiko wa vipenzi, na ulimwengu wa kukutana na vipenzi na marafiki, na mwanzoni mwa hao ni kipenzi cha Mola wa walimwengu na mwombezi wetu kwake siku ya kiama - rehema na amani ziwe juu yake. Naam, hakika yule ambaye ni mfalme wa watu milioni mia tatu na hamsini katika kila zama, kwa kipindi cha miaka elfu moja mia tatu na hamsini na ambaye ni mlezi wa roho zao, na mwongozaji wa akili zao, na kipenzi cha nyoyo zao, na ambaye hunyanyuliwa katika ukurasa wa mema yake kila siku mfano wa kile walichokitanguliza umma wake katika mema, kwa kuwa “Sababu ni kama mtendaji” na ambaye ni kiini cha makusudio ya kiungu Mola Mlezi, na mhimili wa malengo matukufu ya kiungu ulimwenguni, na ambaye ni sababu ya kuongezeka kwa thamani ya vilivyomo, huyo ni Mtume Mkarimu (s.a.w), kama alivyosema katika dakika za mwanzo ambapo ulimwengu ulipata hadhi kwa sababu yake (Umma wangu.. umma wangu..) kama ilivyokuja katika mapokezi sahihi na maono ya kweli, kwani hakika yeye pia atasema katika ufufuo: “Umma wangu.. umma wangu..” na atafanya juhudi kwa uombezi wake kuwasaidia umma wake na kuuokoa kwa rehema kuu iliyotukuka, katika wakati ambao kila mmoja katika mikusanyiko mikubwa atasema: “Nafsi yangu.. nafsi yangu..”. Kwa hivyo basi, sisi ni wenye kuelekea katika ulimwengu ambao ameelekea Nabii huyu Mkarimu, ni wenye kusafiri kwenda katika ulimwengu ambao umepata nuru kwa nuru ya taa hiyo yenye kung’aa na kwa wale waliokuwa pembezoni mwake miongoni mwa nyota za wateule na mawalii ambao idadi haiwezi kuwadhibiti. Naam, hakika kufuata sunna tukufu za Nabii huyu Mkarimu (s.a.w) ndiko kunakoongoza katika kuungana chini ya bendera ya uombezi wake na kuchota katika nuru zake, na kuokoka kutokana na viza vya Barzakh.

§5

Miguu yangu ilipokanyaga kizingiti cha uzee, afya yangu ya kimwili ambayo inaachia na kukunjua hatamu za kughafilika, yenyewe imepatwa na maradhi pia, uzee na maradhi kwa pamoja vikaafikiana kunihujumu, na vikaendelea kuvurumisha kichwani mwangu mapigo baada ya mapigo mpaka vikaniondolea usingizi wa mghafala. Na hakukuwa na chochote chenye kunifungamanisha na dunia miongoni mwa mali, watoto, au chenye kufana na hivyo, nikakuta kwamba kiini cha umri wangu ambao nimeupoteza kwa mghafala wa ujana ni makosa na madhambi tu, nikaomba msaada nikipiga kelele kama alivyopiga kelele Niyaz Al-Misriy: Umri umeenda bure, na sikupata kitu ndani yake, Nimekuja njiani na kukuta msafara umeshaondoka, nikabakia, Nimeendelea kufuata njia mpweke, mgeni niliyepotea na machoni mwangu kuna chemchem ya machozi, Na kifuani kwangu kukiwa na moto wa shauku, ukiifanya akili yangu itahayari! Wakati huo nikawa katika ugeni wa hakika, nikahisi huzuni ya mkata tamaa, na masikitiko ya mwenye kujuta yenye kuunguza kwa kile kilichopita katika umri. Nikapiga ukelele kutoka ndani ya nafsi yangu nikiomba msaada na mwanga wa matumaini, na tahamaki Qur’an yenye hekima na muujiza wa ubainifu inanisaidia na kunifariji na kufungua mbele yangu mlango wa tumaini kubwa na kunitunuku nuru yenye kuangaza ya tarajio na tumaini yenye uwezo wa kuondosha ukataji tamaa wangu mara dufu ya mara, na inaweza kuteketeza viza hivyo vya kutisha pembezoni mwangu. Naam, enyi wazee waheshimiwa wa kiume na wa kike, enyi ambao mafungamano ya uhusiano wao na dunia yameanza kuachana kama mimi! Hakika Muumba (s.w) aliyeumba dunia hii kuwa ni mji ulio kamilika na kunadhimika, kana kwamba ni kasri refu, je inawezekanaje kwa Muumba huyu mkarimu asizungumze na vipenzi vyake na wageni wakarimu katika mji huu au kasri hili? Na je inawezekana asikutane nao?!! Maadam ameumba kasri hili refu kwa ujuzi na kulinadhimu kwa utashi, na akalipamba kwa hiari, basi hapana budi kwamba anazungumza; kama ilivyo kwamba mjenzi anajua, basi mjuzi anaongea. Na maadam amejaalia kasri hili kuwa ni nyumba nzuri ya ugeni na yenye kufurahisha, na mji huu ni sehemu ya bishara nzuri, basi ni lazima awe na vitabu na nyaraka ambapo anabainisha ndani yake anachokitaka kwetu, na kuweka wazi mahusiano yake pamoja nasi. Na hapana shaka kwamba kitabu kamilifu zaidi katika vitabu hivyo vitukufu alivyoviteremsha, si kingine ila ni Qur’an ya Hekima ya muujiza, ambapo muujiza wake umethibiti kwa namna arobaini miongoni mwa namna za miujiza, na ambayo kwa uchache husomwa katika kila dakika na ndimi milioni mia moja za watu, na ambayo inaeneza nuru na kuongoza katika njia, na ambayo kila herufi miongoni mwa herufi zake ina thawabu kumi, na malipo kumi kwa uchache, na baadhi ya wakati mema elfu kumi, bali thawabu elfu thelathini, kama ilivyo kwenye usiku wenye cheo. Na kama hivi inatunuku katika matunda ya peponi na nuru ya Barzakh kile alichotaka Allah kukitunuku. Je katika ulimwengu wote kuna kitabu kinashindana nacho katika daraja hii, na je kuna yeyote anayeweza kudai hilo katu? Kwa kuwa Qur’an hii Tukufu ambayo iko mbele yetu ni maneno ya Mola Mlezi wa walimwengu, nayo ni Amri yake iliyofikishwa kwetu, nayo ni chanzo cha rehema yake ambayo imeenea kwenye kila kitu, nayo inatoka kwa muumba wa mbingu na ardhi (s.w), kutoka katika upande wa uungu wake Mola Mlezi usiyo na mipaka, na kutoka katika upande wa utukufu wa uungu wake mkusudiwa wa ibada, na kutoka katika upande wa rehema yake pana na iliyoenea, basi shikamana nayo, kwani ndani yake kuna dawa ya kila maradhi, na nuru kwa kila giza, na tumaini kwa kila ukataji tamaa, na ufunguo wa hazina ya milele ni imani, kujisalimisha, kuisikiliza, kuifuata, na kuburudika kwa kuisoma.

§6

Mwanzoni mwa uzee wangu, na shauku yangu ya kujitenga na watu, roho yangu ilitafuta raha katika upweke na kujitenga katika bonde la (Yushaa) lililopo (Al-Busfur). Siku moja, nilipokuwa nikifikiri kwa uoni wangu kuelekea juu kutoka katika bonde lile refu, nimeona kwa nadhiri ya uzee bango miongoni mwa mabango ya utengano likichuruzika huzuni, ambapo nilitembea kwa uoni wangu kutoka katika kilele cha mti wa umri wangu, kutoka katika tawi la arobaini na tano la mti huo hadi nikaishia kwenye kina cha matabaka ya chini ya uhai wangu, nikaona kwamba katika kila tawi miongoni mwa matawi hayo yaliyokuwepo huko ndani ya kila mwaka, majeneza yasiyohesabika katika majeneza ya vipenzi na marafiki zangu na kila mwenye uhusiano na mimi. Nikaathirika kwa taathira ya hali ya juu kutokana na kutengana na vipenzi na kufarikiana nao, na nikalia kilio cha (Fudhuli Al-Baghdadiy) pale alipofarikiana na vipenzi kwa kusema: Kila ninapokumbuka usuhuba wao nalia, Hivyo, maadam nina pumzi sitaacha kulia. Kwa hakika nimetafuta kupitia majuto hayo yenye kuumiza mlango wa tumaini, na dirisha la nuru ili kuifariji nafsi yangu. Tahamaki nuru ya kuamini akhera inaniokoa na kunisaidia kwa nuru yenye kuangaza. Hakika imenipa nuru isiyozimika milele, na tumaini lisilovunja moyo kabisa. Naam, enyi ndugu zangu wazee wa kiume na wa kike! Maadam akhera ipo, na maadam ni yenye kubakia milele, na maadam ni nzuri zaidi kuliko dunia, na maadam aliyetuumba ni mwenye hekima na mwenye kurehemu; kwa hiyo hatupaswi kulalamika kutokana na uzee au kuchoshwa nao, hiyo ni kwa sababu uzee uliofungamana na imani na ibada, wenye kufikisha katika umri wa ukamilifu, si chengine ila ni alama ya kumaliza wajibu na majukumu ya maisha, na ni ishara ya kuhama kwenda katika ulimwengu wa rehema ili kudumu katika raha ya milele. Hivyo, hakuna budi kuuridhia ridhaa ya hali ya juu. Naam, hakika kueleza kwa wateule mia moja na ishirini na nne elfu ambao ni Manabii na Mursalina rehema na amani ziwe juu yao - kama hadithi ilivyoeleza kwa ijmai na tawatur baadhi yao wakiegemea katika shuhuda na wengine wakiegemea katika haki ya yakini, kuhusu uwepo wa makaazi ya akhera, na kutangaza kwao kwa ijmai kwamba watu watapelekwa huko, na kwamba Muumba (s.w) bila ya shaka ataleta makaazi ya akhera, kama alivyoahidi kwa ahadi ya uhakika kabisa. Na hakika kusadikisha kwa mawalii milioni mia moja na ishirini na nne kwa ufunuo na kwa shuhuda yaliyo elezwa na manabii hawa (a.s) na kushuhudia kwao juu ya uwepo wa akhera kwa elimu ya yakini ni dalili yenye nguvu kabisa na dalili iliyoje juu ya uwepo wa akhera.. Na vile vile hakika madhihirisho ya majina yote mazuri ya muumba wa ulimwengu yenye kudhihiri katika pande za ulimwengu wote, yanalazimu kwa uwazi uwepo wa ulimwengu mwingine wa kudumu, na yanajulisha kwa dalili ya wazi juu ya uwepo wa akhera. Na vile vile uweza wa kiungu na hekima yake isiyo kuwa na mpaka ambao hauna israfu wala upuuzi, na ambao unahuisha majeneza ya miti iliyokufa, na matawi yake yaliyo wima, unaihuisha nayo haidhibitiki kwa idadi juu ya mgongo wa ardhi katika kila majira ya michipuo, na katika kila mwaka kwa amri ya (كن فيكون) na kuifanya kuwa ni alama ya (Ufufuo baada ya mauti) basi hufufua aina mia tatu elfu za makundi ya mimea na wanyama na kuyasambaza, ukidhihirisha kwa hilo mamia ya maelfu ya vielelezo vya ufufuo na dalili za uwepo wa akhera. Na vile vile rehema pana ambayo inadumisha uhai wa viumbe hai vyote vyenye kuhitajia riziki, na kuvipa maisha ya aina yake kwa ukamilifu wa huruma, na matunzo ya kudumu ambayo yanadhihirisha aina za mapambo na uzuri kwa namna isiyohesabika wala kudhibitika, katika kipindi kifupi sana katika kila majira ya machipuo. Hapana shaka kwamba viwili hivyo vinasisitiza uwepo wa akhera kwa uwazi kabisa. Na vile vile hamu ya kubakia, na shauku ya kuishi milele na matarajio ya milele yaliyopandikizwa kwa mpandikizo usiyoachana katika maumbile ya mwanadamu huyu ambaye ndio tunda kamilifu zaidi la ulimwengu huu, na kiumbe mpendwa zaidi kwa muumba wa ulimwengu, naye ndio mwenye uhusiano madhubuti zaidi na vilivyomo ulimwenguni kote, hapana shaka kwamba anaashiria kwa uwazi kabisa uwepo wa ulimwengu wa kudumu baada ya ulimwengu huu wenye kutoweka, na pia uwepo wa ulimwengu wa akhera na nyumba ya furaha ya milele. Basi dalili zote hizi zinathibitisha kwa uhakika kamili – kiasi cha kusisitiza kukubali – uwepo wa akhera kwa mfano wa uwazi wa uwepo wa dunia. Basi maadam somo muhimu zaidi ambalo Qur’an inatusomesha ni (Kuamini akhera) na somo hili ni madhubuti kwa kiasi hiki, na katika imani hiyo kuna nuru inayoangaza, tumaini lenye nguvu na faraja kubwa ambapo lau uzee mia moja elfu ungekusanyika kwa mtu mmoja basi kwa hakika nuru hiyo, tumaini hilo na faraja hiyo inayotokana na imani hii vingemtosha. Hivyo ni wajibu wetu sisi wazee kufurahia uzee wetu tukisema: “Alhamdulillahi kwa ukamilifu wa imani”.

§7

Nilipokuwa uhamishoni kile kifungo chenye kuumiza nilibaki peke yangu hali ya kujitenga na watu katika kilele cha mlima wa (Çam) uliyopo katika milima ya (Barla) nilikuwa nikitafuta nuru katika upweke huo. Usiku mmoja katika chumba hicho kidogo kisichokuwa na dari, kilichoinuliwa kwa mti wa msonobari juu ya kilele cha mlima huo, tahamaki uzee wangu unanifanya nihisi aina za ugeni ndani ya ugeni – kama ilivyokuja katika (Andiko la sita) kwa uwazi -. Katika kutulia kwa usiku huo ambapo hakuna athari wala sauti yoyote isipokuwa mivumo ya huzuni ya miti na parakacha zake, nilihisi kwamba mivumo hiyo yenye kuumiza imejeruhi hisia zangu, uzee na ugeni wangu, uzee ukanong’ona katika sikio langu ukinionya kwa kusema: (Hakika mchana umebadilika na kuwa ni kaburi hili la giza, na dunia imevaa sanda yake nyeusi, basi mchana wa umri wako utabadilika na kuwa usiku, na mchana wa dunia utabadilika na kuwa usiku wa Barzakh, na mchana wa kiangazi cha uhai utabadilika na kuwa usiku wa majira ya baridi ya mauti). Nafsi yangu itajibu kwa uchungu: Naam, kama ambavyo ni mgeni hapa na kuwa mbali na mji wangu, basi hakika utengano wangu wa vipenzi vyangu walio wengi katika kipindi cha umri wangu ambao umekaribia miaka hamsini na similiki chochote isipokuwa michirizi ya machozi nyuma yao ni ugeni unaozidi ugeni wangu kwa nchi yangu, na mimi katika usiku huu ninahisi ugeni wenye huzuni na maumivu makali kutokana na ugeni wangu juu ya mlima huu ambao umegubika ugeni na huzuni, basi uzee wangu unanionya kukaribia wakati wa kutengana moja kwa moja na dunia na vilivyomo ndani yake. Basi katika ugeni huu uliojawa na huzuni na kupitia huzuni hii ambayo nayo inagubikwa na huzuni, nikaanza kutafuta nuru, tarajio na mlango wa tumaini, na haraka ilikuja “kumwamini Allah” kwa ajili ya kuniokoa, na ikanipa tulizo kubwa kiasi kwamba lau kama maumivu na ukiwa wangu ungeongezeka mara dufu basi tulizo hilo lingetosha kuiondosha huzuni ile. Naam, enyi wazee wa kiume na wa kike! Maadam tuna muumba mwenye kurehemu, basi hatuna ukiwa abadani, na maadam (s.w) yupo basi kila kitu chetu kipo pia, na maadam yeye yupo na malaika wapo, basi hii dunia siyo tupu bila ya rafiki wala chochote, na milima hii mitupu na majangwa yale matupu yote ni yenye kukaliwa na waja wa Allah waliokirimiwa, na kwa malaika wakarimu. Naam, hakika nuru ya imani ya Allah (s.w), na kuuangalia ulimwengu kwa ajili yake inafanya miti bali hata mawe kana kwamba ni marafiki wema ukiachilia mbali wenye hisia katika waja wake, ambapo vilivyomo hivyo vinaweza kuzungumza nasi – kwa ulimi wa hali – kwa yale yenye kutufariji. Naam, hakika dalili ya uwepo wake (s.w) ni kwa idadi ya vilivyomo katika ulimwengu huu, na kwa idadi ya herufi za kitabu hiki kikubwa cha ulimwengu, na pia zipo dalili na shuhuda juu ya rehema yake kwa idadi ya viungo vya wenye roho na neema maalumu alizowapa na vyakula ambavyo ndio kiini cha huruma, rehema na matunzo, vyote hivyo vinajulisha mlango wa muumba wetu mwenye kurehemu na mkarimu, na mtengenezaji wetu mwema, na mlinzi wetu mpendwa, na hapana shaka kwamba kushindwa na udhaifu ni waombezi wawili wenye kutarajiwa katika mlango huo mtukufu. Na kwamba kipindi cha uzee ni wakati wa viwili hivyo, na ni wakati wa kudhihiri kwake, hivyo ni juu yetu kuupenda uzee, na siyo kuupuuza; kwani ndio mwombezi mtarajiwa mbele ya mlango huo wa hadhi ya juu.

§8

Wakati mmoja, mwanzoni mwa uzee, pindi kicheko cha “Said wa zamani” kilipobadilika na kuwa kilio cha “Said mpya”, watu wa dunia jijini “Ankara” waliniita pale wakidhani kuwa mimi ni “Said wa zamani”, nami nikaenda. Siku moja mwishoni mwa majira ya Kupukutika, nilipanda mpaka juu ya “ngome ya Ankara”, ambayo ilikuwa chakavu na kongwe mno kuliko mimi. Ilionekana kwangu kana kwamba ni matukio ya kutisha ya kihistoria. Nikapatwa na huzuni na majonzi makubwa kutokana na uzee wa mwaka katika msimu wa mapukutiko, uzee wangu, ukongwe wa ngome, ukongwe wa watu, na ukongwe wa Dola tukufu la Uthman, na kuanguka kwa utawala wa Kikhalifa, na ukongwe wa dunia. Hali hiyo ikanilazimu kuangalia kutoka kileleni mwa ngome hiyo ya juu hadi mabonde ya muda uliyopita na miinuko ya mustakabali huku nikiitafuta nuru, tumaini na faraja ili inimulikie yale niliyokuwa nikiyahisi katika giza totoro lililoigubika roho yangu huko ikiwa imezama katika usiku wa ukongwe huu uliotanda . Nilipoitazama kuliani ambako ndio wakati uliopita nikitafuta nuru na tumaini, upande huo ukanidhihirikia kwa mbali kwa namna ya kaburi kubwa la baba yangu na babu zangu na binadamu wengine, basi likanizidishia upweke badala ya kunifariji. Kisha nikaangalia kushoto ambako ndio mustakabali nikitafuta tiba, ukanidhihirikia kwa namna ya kaburi kubwa linalonitia giza mimi na wenzangu kama mimi na kizazi kijacho, likanitisha badala ya kunituliza. Kisha nikaangalia wakati uliopo baada ya moyo wangu kujawa na ukiwa kutoka kulia na kushoto, siku hiyo ikanidhihirikia kwenye mazingatio yangu yenye simanzi na mtazamo wangu wa kihistoria katika namna ya jeneza la kiwiliwili changu kinachotweta kama kichinjwa kikiwa kati ya uhai na mauti. Kisha, nilipokata tamaa kwenye upande huo pia, nilikiinua kichwa changu na kuangalia kileleni mwa mti wa uhai wangu, nikaona juu ya mti huo tunda moja tu, likiniangalia. Tunda hilo ni jeneza langu. Basi, nikainamisha kichwa changu huku nikiangalia kwenye mizizi ya mti wa umri wangu, nikaona kwamba mchanga uliokuwepo hapo si kitu kingine isipokuwa ni mabaki ya mifupa yangu na mchanga ambao ni chanzo cha kuumbwa kwangu vikiwa vimechanganyika pamoja, huku vikikanyagwa kwa miguu. Basi gonjwa langu likazidi maradhi bila ya kunitunukia dawa. Halafu nikageuzwa kwa uchungu niangalie nyuma yangu, nikaona kuwa dunia hii ya mpito na yenye kutoweka ikiviringika mabondeni msimo na maana na kuporomokea katika giza la kutoweka. Basi mtazamo huu ukamwaga sumu vidondani mwangu badala ya kuvipoza kwa malhamu na matibabu. Kwa kuwa sikuona jema wala tumaini lolote katika upande huo, nikageuza uso wangu kuangalia mbele na kutupa jicho mbali, nikaona kuwa kaburi linanivizia katikati ya njia yangu, likiwa limefungua kinywa chake likinikodolea mimi, na nyuma yake ipo njia iliyorefuka kuelekea kwenye umilele, huku misafara ya wapita njia hiyo ikionekanwa kwa mbali. Wala sina pa kuegemea dhidi ya majanga haya ya kutisha yanayonijia kutoka pande sita, wala similiki silaha nitakayojilinda kwayo isipokuwa ni sehemu finyu ya hiari. Basi, mbele ya maadui wote hao na vitu vyenye kudhuru visivyohisabika, sina kingine chochote mbele ya maadui hao wasio na idadi na vitu vyenye madhara visivyohesabika isipokuwa silaha ya kiutu pekee ambayo ni sehemu ya hiari. Lakini kwa vile silaha hii ni pungufu na haina nguvu ya kupatisha chochote, na uwezo wake ni kuchuma tu, ambapo haiwezi kurudi wakati wa uliyopita na kuniondoshea majonzi na kuyatuliza, wala haiwezi kuelekea kwenye mustakabali ili inikinge na fazaa na vitisho vyake, nikaamini kwamba hakuna manufaa yoyote kwa yale yanayonikumba katika maumivu yaliyopita na yajayo. Nikiwa nimechanganyikiwa katikati ya pande sita, na kila aina ya upweke, mshituko, kukata tamaa na giza kunijia kwa kufuatana. Tahamaki kukawa na nuru za imani zinazong’aa katika Qur’an yenye miujiza wa ubainifu, zinanisaidia na kumulika pande hizo sita na kuzing’arisha kwa nuru ya ajabu ambayo lau kama zilizonisumbua katika aina mbali mbali za upweke na giza zingeliongezeka mara mia, nuru hiyo ingetosha kuziangaza. Nuru hizo zikabadilisha mlolongo mrefu wa upweke kuwa ni liwazo na tumaini, na zikageuza vitisho vyote kuwa ni tulizo la moyo na tumaini la roho moja baada ya nyengine. Ndio, kwa hakika imani imerarua sura hiyo ya kutisha ya muda uliyopita ambayo ni kama kaburi kubwa, na kuibadilisha kuwa baraza yenye mwanga na tulizo na pahala pa kukutana na wapenzi. Na yamedhihiri hayo kwa jicho na haki ya yakini... Kisha imani imedhihirisha kwa elimu ya yakini kwamba mustakabali unaotutokea kwa mtazamo wa kughafilika, kama vile ni kaburi pana na kubwa si kingine isipokuwa ni baraza la mapokezi na huruma lililoandaliwa katika kasri za furaha ya milele. Kisha ni kuwa imani imeivunja sura ya jeneza la wakati wa sasa inaoonekana hivyo kwa mtazamo wa kughafilika. Na kunipa ushahidi kwamba leo ya sasa ni duka la kufanyia biashara ya akhera, na pahala pa mapokezi mazuri pa Mwingi wa Rehema. Kisha imani ikanionesha kwa elimu ya yakini kwamba yanayoonekana kwa mtazamo wa kughafilika katika tunda pekee lililopo juu ya mti wa umri kwa umbile la jeneza, kwamba haliko hivyo, bali ni mwondoko wa roho yangu – ambayo ndio maisha ya milele na furaha ya kudumu – kutoka kwenye makazi ya kale kuelekea kwenye peo za nyota kwa ajili ya matembezi na utalii wa mara kwa mara. Kisha imani imebainisha kwa siri zake kwamba mifupa yangu na mabaki yake na mchanga wa chanzo cha kuumbwa kwangu, sio mifupa isiyo na maana na yenye kutoweka inayokanyagwa na miguu, bali mchanga huo ni mlango wa rehema, mapazia na kuta za peponi. Kisha imani imenionesha kwa fadhila za siri za Qur’an Tukufu kwamba hali za kidunia na matukio yake yenye kuporomoka katika giza la kutoweka kwa mtazamo wa kughafilika, hazibiringii namna hii katika viza vya kutoweka – kama ilivyodhaniwa mwanzoni – bali ni namna fulani ya barua za kiungu Mola Mlezi na maandiko ya kiungu Mkusudiwa wa haja, na ni nyaraka zilizonakshiwa majina matukufu ya Allah aliyetakasika yakiwa yamehitimisha jukumu lake, na kunufaisha maana zake. Na ikatoa matokeo yake katika uwepo, na kunifunza kuamini uhalisia wa dunia kwa elimu ya yakini. Kisha kwamba imani imenifafanulia kwa nuru ya Qur’an kwamba kaburi hilo lililonikodolea macho huku likinisubiri sio shimo la kisima bali ni mlango wa ulimwengu wa nuru. Na kwamba njia hiyo inayoelekea kwenye umilele sio njia iliyomalizikia kwenye viza na kutoweka bali ni njia iliyo sawa kuelekea kwenye ulimwengu wa nuru na ulimwengu wa kuwepo na ulimwengu wa furaha ya kudumu.. na kwa namna hii hali hizi ndio zimekuwa dawa kwa gonjwa langu na malhamu yake kiasi kwamba imedhihiri wazi wazi ikanikinaisha kikamilifu. Kisha kwamba imani inaitunuku sehemu finyu ya hiari inayomiliki sehemu ndogo mno ya chumo kielelezo kinachoegemezewa kwenye uwezo usio na mipaka na kunasibishiwa kwenye rehema pana dhidi ya wingi huo uliokithiri wa maadui na giza lililotanda. Bali kwamba imani yenyewe ni kielelezo mkononi mwa sehemu ya hiari. Kisha kwamba sehemu hii ya hiari ambayo ndio silaha ya kiutu hata kama yenyewe ina mapungufu, isipokuwa ikitumiwa kwa jina la Haki (s.w) na kutumiwa katika njia yake na kwa ajili yake – inaweza – kwa mujibu wa imani – kuwa ni njia ya kupata pepo ya milele kwa upana wa miaka mia tano. Mfano wa muumini katika hayo ni kama mfano wa mwanajeshi anapotumia sehemu ya nguvu zake kwa jina la dola basi huwa rahisi kwake kutekeleza majukumu yenye kuzishinda nguvu zake binafsi kwa mara elfu kadhaa. Kama ambavyo imani inaitunuku sehemu ya hiari kielelezo, kwani inaunyakua udhibiti wake kutoka katika mwili ambao hauwezi kufanya jambo katika muda uliopita wala ujao, na inaukabidhi kwa moyo na roho, na kutokana na duara la maisha ya roho na moyo kutofungika katika wakati wa sasa kama ilivyo katika mwili, na kutokana na kuingia miaka kadhaa ya muda uliyopita na miaka kama hiyo ya wakati ujao katika duara la maisha hayo, basi sehemu hiyo ya hiari inaondoka kutoka kwenye usehemu na kupata ujumla. Na kama ambavyo inaingia kwa nguvu ya imani katika kina cha mabonde ya wakati uliyopita ikiteketeza viza la majonzi, pia inapaa ikiambatana na nuru ya imani kuelekea milima ya mbali ya wakati ujao huku ikiondosha fazaa na vitisho vyake. Enyi ndugu zangu wazee wa kike na wa kiume! Na enyi mnaosumbuliwa na uzee kama mimi! Kwa kuwa sisi alhamdulillahi ni waumini, na imani ina hazina tamu zenye nuru na zenye kupendeza kiasi hiki, na kwamba uzee wetu unatusukuma sana kwenda kwenye hazina hizi, basi hatupaswi kulalamika kutokana na uzee, bali inatupasa tutangulize maelfu ya shukurani kwa Allah (s.w) na tumsifu yeye kwa uzee wetu wenye kung’aa imani.

§9

Katika wakati ambapo mvi, alama ya uzee, zilipoanza kujitokeza katika nywele zangu, misukosuko ya Vita vya Kwanza vya Dunia na kukamatwa kwangu na Urusi kama mfungwa wa kivita vilizidisha kwangu usingizi wa kughafilika wa ujana, hayo yakafuatiwa na mapokezi mazuri wakati wa kurejea kwangu mji wa Istanbul sawa kutoka kwa Khalifa, au sheikhul-Islam, au kamanda mkuu wa jeshi hadi wanafunzi wa elimu ya dini na namna nilivyopokelewa kwa heshima zaidi ya ninavyostahili, yote hayo yamezalisha kwangu hali ya kiroho ukiongezea ulevi wa ujana na mghafiliko wake, vilifanya usingizi wa ujana uzidi sana kiasi kwamba niliona dunia kama ya kudumu, nikaiona nafsi yangu kuwa katika hali ya ajabu ya kufungamana nayo kama vile sitokufa. Kisha, siku moja katika Ramadhan, nilikwenda katika Msikiti wa Bayazid kusikiliza wasomaji wenye ikhlasi waliohifadhi Qur'an. Kwa kupitia ndimi za wasomaji hao wa Qur'an ya Ufafanuzi wa Kimiujiza ilikuwa ikitangaza kwa nguvu kuhusu kufa kwa mwanadamu na viumbe hai na kutoweka kwao anuani yake tukufu kabisa ya mbinguni na hiyo ni kwa aya isemayo: كُلُّ نَفْسٍ ذَائِقَةُ الْمَوْتِ Tangazo hilo liliingia sikioni mwangu, likapenya mpaka ndani kabisa ya moyo wangu na kukaa humo; ilivunja usingizi ule uliojikita na kutokujali kule. Nikatoka msikitini. Kwa sababu ya mzubao wa usingizi ambao kwa muda mrefu ulikaa kichwani kwangu, kwa siku nyingi tufani sasa lilikuwa likifanya ghadhabu ndani mwake, na mwenyewe niliona kama ngalawa iliyopotea na mawimbi yanayosongana. Nafsi yangu ilikuwa ikiwaka moto wenye moshi mkubwa, kila nilipoziangalia nywele zangu kwenye kioo, mvi ziliniambia: "Zinduka!" Nikaangalia na kuona kuwa ujana wangu uliyoniteka sana kwa starehe zake ambazo nilizitumainia sana zikiniaga, na kuwa maisha ya kidunia niliyoyapenda sana na niliyojihusisha nayo sana yalikuwa yakianza kuzimika, na kuwa dunia niliyoungana nayo sana na kuipenda ilikuwa ikiniambia: "Safari njema", na ilikuwa ikinionya kuwa nitatoka katika nyumba hii ya wageni. Yenyewe, pia, ilikuwa ikisema "Kwaheri", na ilikuwa ikijiandaa kuondoka. Kutokana na ishara za aya ya Qur'an ya Ufafanuzi wa Kimiujiza, كُلُّ نَفْسٍ ذَائِقَةُ الْمَوْتِ maana ifuatayo ilikuwa ikijikunjua moyoni mwangu: mbari ya kibinaadamu ni kiumbe hai; itakufa ili ifufuliwe. Na tufe la dunia ni kiumbe hai; pia itakufa ili iwe na umbo la milele. Na dunia, pia, ni kiumbe hai; itakufa ili iwe na umbo la Akhera. Hivyo, nikiwa katika hali hii, niliitafakari hali yangu. Niliona kuwa ujana, ambao ni chanzo cha furaha, ulikuwa ukiondoka, na uzee, ambao ni chanzo cha huzuni, ulikuwa unakuja, kwamba uhai, uliokuwa uking’aa sana, ulikuwa unaanza kuondoka, ilhali kifo, ambacho kinatisha na giza dhahiri kilikuwa kikijitayarisha kuwasili, na kuwa dunia inayopendwa, iliyodhaniwa kuwa ya kudumu na ya kupendwa na wasio na mazingatio, ilikuwa ikiharakishia katika kifo chake. Ili nijidanganye na kutumbukiza kichwa changu tena katika kutokujali nilitafakari furaha za msimamo wa kijamii niliofurahia katika Istanbul, uliyokuwa wa juu zaidi kuliko nilivyostahiki, lakini hakukuwa na faida yoyote katika hilo. Fikra, mtizamo, na faraja ingeweza tu kuja mpaka katika mlango wa kaburi; hapo ingezimika. Na kwa kuwa niliiona kama unafiki wa kutaabisha, taabu baridi, na fadhaa ya muda mfupi chini ya stara ya pambo la utukufu na umashuhuri, ambao ni kusudio la kufikirika la wenye kuabudu umashuhuri, nilifahamu kuwa mambo haya yaliyonihadaa tangu wakati huo yasingeweza kunifariji, hakukuwa na nuru yoyote katika hayo. Nikaanza tena kuwasikiliza wasomaji katika Msikiti wa Bayazid ili nisikie mafunzo ya mbinguni ya Qur'an, na kupata uamsho zaidi. Basi kutokana na maelekezo hayo adhimu nilisikia habari njema kwa kudura tukufu za namna yake, وَبَشِّرِ الَّذِين آمَنُواْ Kwa mng’ao wa Qur'an, nilitafuta faraja, matumaini, na nuru, si nje yake, lakini ndani ya nukta nilizotishika, kuhuzunika na kukata tamaa. Shukurani nyingi sana ni kwa Allah (s.w), nikapata tiba ndani ya maradhi yenyewe. Nikapata nuru katika giza lenyewe. Nikapata faraja katika kitisho chenyewe. Mosi, niliangalia katika mkabala wa kifo, ambacho nilidhani ndiyo jambo la kutisha zaidi, na kinamtisha kila mmoja. Kwa nuru ya Qur'an niliona kuwa ingawa stara ya kifo ni nyeusi, yenye kiza na mbaya, kwa waumini sura yake halisi, ni mwanga na nzuri. Na tumethibitisha ukweli huu kimkataa katika sehemu nyingi za Risale-i Nur. Mathalani, kama tulivyoeleza katika Neno la Nane na Barua ya Ishirini kifo si maangamizi, si utengano, badala yake ni mwanzo wa uzima wa milele. Ni mwanzo wake. Ni pumziko kutokana na taabu za majukumu ya maisha, ni ruhusa ya kwenda nyumbani. Ni kubadilisha makazi. Ni kukutana na msafara wa rafiki mmojawapo ambao tayari wamehamia kwenye Dunia ya kati na kati; na kuendelea. Niliona ukweli wa kifo, na uso wake mzuri kwa ukweli kama huu. Niliuangalia uso wa kifo si kwa hofu bali kwa shauku. Nilifahamu maana moja ya kisufi ya 'tafakuri ya mauti'. Halafu nikauangalia ujana - ujana unaoondoka, unaomliza kila mmoja kwa kuondoka kwake, unaowapumbaza na kuwajaza hamu, na kuwasababishia kuutumia katika dhambi na kutokujali. Niliona kuwa pamoja na vazi lake zuri lililotariziwa ulikuwa una sura mbaya, uliyolewa na uso uliopigwa bumbuwazi. Kama sikujua hali yake halisi, basi ungenifanya nilie kwa miaka mia moja kama ningebakia duniani muda huo, baada ya kunilewesha na kunikejeli kwa miaka kadhaa. Kama mtu mmoja alivyolalamika: “Laiti siku moja ujana ungerejea, nikaueleza yaliyofanywa na uzee.” Kwa hakika, wazee kama huyo hapo juu wasiojua hali halisi ya ujana, hufikiria ujana wao wenyewe, na kulia kwa majuto na shauku. Lakini ujana unapokuwa kwa waumini wenye akili nzuri na nyoyo, ni njia ya nguvu zaidi, yenye kukubalika na nzuri ya kufanya kazi njema, na biashara kwa ajili ya Akhera, maadam wanautumia katika ibada, biashara hiyo na kazi hizo njema. Na kwa wenye kujua majukumu yao ya kidini, na hawautumii vibaya ujana wao, ni neema yenye thamani kubwa sana ya kiungu na ya furaha. Usipotumika katika ustawi, unyofu, na kumcha Allah, una hatari nyingi, unaharibu furaha ya milele na maisha ya hapa duniani. Kwa hakika, badala ya furaha ya ujana wa mwaka mmoja au miwili, husababisha miaka mingi ya masikitiko na huzuni uzeeni. Kwa kuwa kwa watu wengi, ujana una madhara, sisi wazee tunapaswa kumshukuru Allah kuwa tumenusuriwa dhidi ya hatari na madhara yake. Kama kila kitu kingine, furaha za ujana huondoka. Kama umetumika katika ibada na kazi njema, matunda ya ujana wa aina hiyo huendelea kubakia katika mahali pao na ni njia za kupata ujana katika maisha ya milele. Baada ya hapo, niliitafakari dunia, ambayo watu wengi wamepumbazika nayo na wameshikamana nayo. Kwa nuru ya Qur'an, niliona kuwa dunia ina nyuso tatu, moja ndani ya mwingine: Kwanza: Hii inaangalia Majina ya Kiungu; ni kioo cha majina hayo. Uso wake wa pili: Hii inaangalia Akhera, na ni shamba lake. Uso wake wa tatu: Hii inaangalia watu wa kidunia; ni uwanja wa michezo wa wasiozingatia. Kwa kuongezea, kila mmoja ana dunia yake pana humu duniani. Kwa wepesi, zipo dunia nyingi mojawapo ndani ya nyingine kwa idadi ya wanaadamu. Nguzo ya dunia binafsi ya kila mmoja ni maisha yake mwenyewe. Wakati wowote mwili wake unapoondoka, dunia yake inaangamia kichwani mwake, huwa ni kiama chake. Kwa kuwa wasiozingatia na wenye kupuuzia hawatambui kuwa dunia yao itaangamia kwa haraka, wanaidhania kuwa ya milele kama dunia ya jumla na wanaiabudu. Nilijifikiria mwenyewe: "Mimi, pia, nina dunia yangu itakayoangamia taratibu na kuvunjika kama dunia za watu wengine. Kuna thamani gani katika dunia hii binafsi, maisha yangu haya mafupi?" Halafu, kwa nuru ya Qur'an niliona kuwa kwa ajili yangu na kila mwingine, dunia ni sehemu ya biashara ya muda mfupi, nyumba ya wageni ambayo kila siku hujaa na kubakia tupu, soko lililo njiani kwa ajili ya wapita njia kuja kununua, daftari lenye kufanywa upya la Mwandishi wa Tangu linaloendelea kuandikwa na kufutwa, na kila majira ya kuchipua huandikwa herufi za dhahabu, na kila kiangazi kimesheheni vyema, chenye namna ya vioo vyenye kuakisi na kuhuisha udhihirisho wa Majina ya Muumbaji (s.w), ni kitalu cha Akhera, kitalu cha maua ya Rehema ya Kiungu, na karakana maalumu ya muda mfupi ya kutengeneza mabango yatakayooneshwa katika dunia ya Umilele. Nilimshukuru sana Muumbaji (s.w) aliyeiumba dunia kwa namna hii. Na ninafahamu kuwa ilhali kupenda sura nzuri za ndani za dunia zinazoangalia Akhera na Majina ya Kiungu kapewa mwanaadamu, kwa kuwa wanaitumia katika uso wake wa mpito, mbaya, wa dhambi na usiozingatia, wanadhihirisha maana ya Hadithi: (Kuipenda dunia ni chanzo cha uchupaji mipaka wote). Na kwa hivyo, enyi wazee! Ninautambua ukweli huu kwa nuru ya Qur'an yenye hekima na maonyo ya uzee na imani kufumbua macho yangu. Na nimeionesha kwa shuhuda mkataa katika sehemu nyingi ndani ya Risale-i Nur. Nikapata faraja ya kweli, matumaini yenye nguvu, na nuru yenye kung’aa. Niliushukuru uzee wangu, na nilifurahi kuwa ujana wangu umeondoka. Nyinyi, pia, msilie, bali mtoe shukurani. Kwa kuwa kuna imani na huo ndio ukweli, waache wasiozingatia walie, waache wapotevu walalamike.

§10

Nilikuwa mateka kipindi cha Vita vya Kwanza vya Dunia katika mji wa mbali kaskazini mashariki mwa Urusi ulioitwa “Kosturma”. Kulikuwa na msikiti mdogo wa Watatari pembezeni mwa mto maarufu wa “Volga”. Nilikuwa nimedhikika baina ya rafiki zangu askari mateka, nikaona bora kujitenga ila sikuruhusiwa kutembea nje bila ya idhini. Kisha nikaruhusiwa kubaki katika msikiti huo kwa dhamana ya Watatari. Nilikuwa nikilala hapo peke yangu, na majira ya machipuo yalikuwa yameshakaribia na masiku yangu yalikuwa ni marefu sana katika kitongoji hicho nje ya mji. Uchovu ulikuwa ukinipata sana katika masiku hayo meusi totoro yaliyojivika huzuni za upweke, ambapo hapasikiki ila sauti ya huzuni ya mto (Volga) na sauti nyepesi za matone ya mvua, na uchungu wa utengano katika miluzi ya upepo yote hayo yameniamsha – kwa kitambo kifupi - kutokana na usingizi mzito wa mghafala. Na japo sikuwa nikijiona mzee, ila yeyote anayeshuhudia vita ni mzee, kwa kuwa masiku yake yanawazeesha vijana kutokana na fazaa zake, kana kwamba ni siri miongoni mwa siri za aya tukufu: يَجْعَلُ الْوِلْدَانَ شِيبًا Na japo nilikuwa nakaribia miaka arobaini ila nilijikuta kama nina miaka themanini. Katika masiku hayo yenye giza, marefu na yenye huzuni, na katika hali hiyo iliyojaa huzuni za upweke, na kutokana na hali yangu yenye kuumiza, ilitawala katika kifua changu hali nzito ya kukata tamaa upande wa maisha na nchi yangu, kila nilipoyageukia mapungufu yangu na upweke wangu matumaini yangu yalikatika. Lakini msaada ulinijia kutoka katika Qur’an tukufu ulimi wangu ukatamka: حَسْبُنَا اللّهُ وَنِعْمَ الْوَكِيلُ Na moyo wangu ukiwa unalia ukasema: Mimi ni mgeni.. mimi ni mpweke.. mimi ni dhaifu.. mimi ni fakiri.. nataka amani.. nataka msamaha.. nataka msaada.. kwako ewe Mola wangu. Ama roho yangu ambayo imewakumbuka marafiki zangu wa zamani nchini kwangu, na imesawiri kifo changu katika ugeni huu, imejifananisha na ubeti wa Niyaz Al-Masry, unaotafuta rafiki pale aliposema: Nimepitia huzuni za dunia, na nikauachia ubawa wangu kwenye kukosa Naruka nikiwa na shauku, nikipiga kelele kila wakati: Rafiki!.. Rafiki..! Kwa hali yoyote.. “udhaifu” na “kushindwa kwangu” katika usiku wa masiku hayo marefu yaliyojaa simanzi na giza nene la utengano, udhalili na upweke vimekuwa njia mbili za kujikaribisha katika kizingiti cha rehema ya kiungu, na waombezi katika hadhara ya kiungu, hadi kwamba bado nimepatwa na mshangao vipi nimeweza kutoroka baada ya siku chache. Na nikakata masafa yasiyotegemewa ambayo haiwezekani kuyakata kwa miguu kwa mwaka mzima, na sikuwa mjuzi wa lugha ya Kirusi. Nilimalizana na kushikiliwa mateka kwa namna ya maajabu yenye kushangaza, kwa sababu ya uangalizi wa kiungu ambao ulinipata kutokana na kushindwa na udhaifu wangu, na nikafika Istanbul nikipitia Warsaw na Austria. Na kwa namna hii niliokoka na kushikiliwa mateka kwa wepesi wa kushangaza ambapo nilikamilisha matembezi ya kukimbia masafa marefu kwa wepesi mkubwa, kwa namna ambayo watu mashujaa, wenye akili, wajanja na wanaoifahamu lugha ya Kirusi wasingeweza kufanikisha. Lakini hali yangu ndani ya usiku ule katika msikiti wa Volga imenipa ilhamu ya uamuzi huu: “Nitatumia umri wangu uliyobakia katika mapango, nikijitenga na watu, nimetosheka na kuyaingilia mambo yao, na ilivyokuwa mwisho wangu ni kuingia katika kaburi peke yangu, basi ni juu yangu kuchagua upweke na kujitenga na watu kutokea sasa, ili kuizoesha nafsi yangu kwa hilo!.” Naam, hivi ndivyo nilivyoamua, lakini - kwa bahati mbaya – hakika vipenzi vyangu wengi waaminifu wapo Istanbul, na maisha mazuri ya kijamii yapo huko, na hasa yasiyo na maana ndani yake katika kuhudhuria watu, umashuhuri na kutajika, yote hayo yamenisahaulisha uamuzi wangu kwa kipindi kifupi. Kana kwamba usiku huo wa upweke ni weusi wenye kuangaza jicho la uhai wangu, na kana kwamba mchana wenye kufurahisha wa maisha ya Istanbul ni weupe usiyo angaza jicho la uhai wangu. Jicho halikuweza kuona mbali, bali lililifumba la pili kulala katika usingizi mzito, hadi pale Sheikh Al-Kaylany alipolifumbua kwa kitabu chake Futuh Al-Ghaib baada ya miaka miwili. Na kama hivi enyi wazee wa kiume na wa kike! Tambueni kwamba kilichomo ndani ya uzee miongoni mwa udhaifu na kushindwa si vinginevyo ila ni njia mbili za kupata rehema ya kiungu na uangalizi wa kiungu. Mimi ni shahidi wa ukweli huu katika matukio mengi ya maisha yangu, na kudhihiri kwa rehema juu ya mgongo wa ardhi kunadhihirisha hilo kwa namna ya uwazi, kwa sababu wanyama wenye kushindwa na dhaifu zaidi ni wale wadogo, na hali za upole zaidi za rehema nzuri na zenye ladha zaidi zinadhihiri katika wanyama hao wadogo, kushindwa kwa kinda aliye ndani ya kiota juu ya mti mrefu anamtumia - mama yake - kuidhihirisha rehema kana kwamba ni mwanajeshi anayesubiri amri. Basi atahangaika katika mashamba yaliyostawi ili kuleta riziki nyingi kwa kinda lake dogo, lakini pale tu kinda huyo atakaposahau kushindwa kwake - kwa kuota mabawa yake na kupevuka – mama yake humwambia: Ni juu yako kutafuta riziki yako mwenyewe. Na hatomuitikia maombi yake baada ya hapo. Basi kama inavyotembea siri ya rehema kwa namna hii kwa wadogo, inatembea hivyo hivyo kwa upande wa kushindwa na udhaifu kwa upande wa wazee ambao wamekuwa kama watoto. Na uzoefu wangu binafsi umenipa ukinaifu kamili kwamba riziki ya wadogo kama inavyokuja kulingana na udhaifu wao, na rehema ya kiungu inaituma kwao kwa namna ya ajabu, inabubujisha chemchem za maziwa kutoka katika chuchu, basi hakika riziki ya wazee waumini ambao wamepata hifadhi hutumwa kwao kutoka kwa rehema kwa namna ya baraka, na kwamba nguzo za baraka za nyumba yoyote si vinginevyo bali ni hao wazee wanaoishi humo, na kwamba wanaohifadhi nyumba hiyo kutokana na mabalaa na misiba ni hao wazee walioinama wenye kufanya makaazi yao humo. Sehemu ya hadithi tukufu inathibitisha ukweli huu uthibitisho kamili: (Kama si wazee waliyoinama, mngeshushiwa balaa) Na kama hivi maadam udhaifu na kushindwa katika uzee vinakuwa ni mihimili miwili ya kupata rehema pana ya kiungu, na kwamba Qur’an tukufu inawalingania watoto kuwaheshimu na kuwahurumia wazee wawili katika ngazi tano, na kwa mtindo uliyo katika upeo wa muujiza, katika kauli yake (s.w) إِمَّا يَبْلُغَنَّ عِندَكَ الْكِبَرَ أَحَدُهُمَا أَوْ كِلاَهُمَا فَلاَ تَقُل لَّهُمَا أُفٍّ وَلاَ تَنْهَرْهُمَا وَقُل لَّهُمَا قَوْلاً كَرِيمًا*وَاخْفِضْ لَهُمَا جَنَاحَ الذُّلِّ مِنَ الرَّحْمَةِ وَقُل رَّبِّ ارْحَمْهُمَا كَمَا رَبَّيَانِي صَغِيرًا Na maadam Uislamu unaamrisha kuwaheshimu wazee na kuwahurumia, na maumbile ya kibinadamu yanataka kuwaheshimu na kuwarehemu wazee, basi tunapaswa - sisi wazee - kutobadilisha uzee wetu huu kwa zama mia moja katika zama za utoto, kwa sababu tuna vionjo stahiki vya kimaanawi na vya kudumu, badala ya kionjo cha kimaada kinachotokana na muhemko wa ujana, ambapo tunachukua vionjo vya kiroho vinavyotokana na rehema itokayo kwa uangalizi wa kiungu na kutokana na heshima inayotokana na maumbile ya kibinadamu. Naam, nakutulizeni kwamba lau ningepewa miaka kumi ya ujana wa (Said wa zamani) nisingeubadilisha kwa mwaka mmoja wa uzee wa (Said wa sasa). Nimeridhia uzee wangu, nanyi vilevile uridhieni.

§11

Baada ya kurejea kutoka kuzuiwa mateka, kughafilika kulinitawala kwa mara nyingine kwa muda wa miaka miwili ya maisha yangu ndani ya Istanbul, ambapo hali ya kisiasa na makundi yake yamebadilisha mtazamo wangu wa kutafakari katika nafsi yangu, na yamesababisha kuchanganyikiwa kwenye akili yangu na fikra yangu. Siku moja nilipokuwa nimekaa katika makaburi ya Abuu Ayyub Al-Answary (r.a) na nikiwa juu ya bonde lenye kina kirefu, nikiwa nimezama katika kutafakari maeneo yaliyoizunguka Istanbul, tahamaki ninaona kana kwamba dunia yangu pekee inakaribia kufa, hadi nikahisi – kimawazo – kana kwamba roho inatoka katika baadhi ya viungo vyangu. Nikasema: Je maandishi yaliyokuwepo juu ya makaburi haya ndiyo yaliyonipeleka katika mawazo haya?. Nikaangalia kwa makini katika makaburi nikiacha sehemu nyengine za mbali ikanijia moyoni mwangu: (Kwamba makaburi haya yaliyokuzunguka yamekusanya Istanbul mia moja! Ambapo Istanbul imekuwa tupu mara mia moja, hutoachwa wewe peke yako kutokana na hukumu ya Mwenye kuhukumu Mweza ambaye amewaondoa watu wote wa Istanbul hapa, basi si vinginevyo na wewe utaondoka kama wao!). Nikaondoka makaburini nikiwa nimebeba mawazo haya yenye kutisha, nikaingia katika chumba kidogo katika msikiti wa Abuu Ayyub Al-Answary (r.a) na ambacho nilikuwa nikiingia mara kwa mara huko nyuma nikazama katika kuifikiria nafsi yangu: Hakika mimi ni mgeni! Na ni mgeni kwa sura tatu; kwa kuwa mimi ni mgeni katika chumba hiki kidogo, basi mimi vile vile ni mgeni Istanbul, bali mimi ni mgeni duniani na ni mwenye kuiacha vile vile, hivyo ni juu ya msafiri kufikiria njia yake. Naam, kama ambavyo nitatoka katika chumba hiki na kukiacha, basi siku moja nitaiacha Istanbul na kuondoka na nitatoka duniani vile vile. Na namna hii ikatokea katika moyo wangu na fikra yangu nikiwa katika hali hii yenye kuhuzunisha na kuumiza. Si tu kwamba ninawaacha vipenzi vichache peke yao, bali nitaacha maelfu ya vipenzi ndani ya Istanbul, bali nitaiacha Istanbul kipenzi yenyewe na nitatengana na mamia ya maelfu ya vipenzi kama nitakavyotengana na dunia nzuri ambayo tumetahiniwa kwayo. Nikaenda sehemu ile ile iliyoinuka katika makaburi kwa mara nyengine, wakanidhihirikia watu wa Istanbul wakiwa ni majeneza wanatembea wakiwa wamesimama kama wanavyodhihiri wafu wanaotembea katika filamu za sinema, nilikua nikienda huko baadhi ya wakati kwa ajili ya mazingatio! Mawazo yangu yakaniambia: Maadam sehemu ya waliolala katika makaburi haya wanaweza kudhihiri wakiwa wanatembea kama watu wa sinema, basi vile vile fikiria katika watu hawa kwamba wataingia katika makaburi haya bila ya shaka, na zingatia ni wenye kuingia humo kutokea sasa. Na nilipokua nikigeukageuka katika hali hiyo ya huzuni iumizayo tahamaki nuru kutoka katika Qur’an yenye hekima na mwongozo kutoka kwa Sheikh Al-Kilany (Itukuzwe hadhi yake) vinabadilisha hali hiyo ya huzuni kuwa hali ya furaha na yenye ladha, ambapo nuru inayokuja kutoka katika Qur’an tukufu imenikumbusha na kunizindua yafuatayo: Ulikuwa na rafiki wawili katika maaskari mateka ulipokuwa umetekwa ndani ya (Kosturma) kaskazini mashariki mwa Urusi, na ulikuwa unajua fika kwamba watarejea Istanbul. Na laiti mmoja wao akikutaka uchague kwa kusema: Utakwenda Istanbul au utabaki hapa!. Lau kama utakua na chembe ya akili basi bila shaka ungelichagua kwenda Istanbul, kwa furaha ambapo vipenzi laki tisa na tisini na tisa elfu wapo Istanbul sasa hivi, na hapa huna isipokua mmoja au wawili, nao kwa upande wao watasafiri kuelekea huko. Basi kwenda Istanbul kwako wewe sio utengano wa huzuni wala wenye kuumiza. Na haya sasa umeshakuja Istanbul, je hujawa radhi mwenye kushukuru? Umeokoka kutokana na nchi ya maadui, kutokana na masiku yake meusi na marefu, na kutokana na baridi yake kali, na umekuja Istanbul yenye kupendeza, kana kwamba ni pepo ya dunia! Na jambo lipo kama namna hii ambapo watu tisini na tisa katika mia miongoni mwa wale unaowapenda tokea udogoni mwako hadi sasa, wameshaelekea makaburini. Makaburi hayo ambayo kwako yanaonekana ni maeneo ya upweke na ya kutisha na hakubaki miongoni mwao katika dunia hii isipokuwa mmoja au wawili, nao pia wapo njiani kuelekea huko. Hivyo kufa kwako duniani sio utengano, bali ni kuungana na kukutana na vipenzi vyako hivyo vya dhati. Naam, hakika hao (Yaani roho zilizobaki) wameacha mafikio yao na makazi yao yaliyochakaa chini ya ardhi, sehemu kati yao wanaogelea baina ya nyota na sehemu nyengine baina ya matabaka ya ulimwengu wa Barzakh. Na hivi ndivyo nuru hiyo ya ki-Qur’an ilivyonikumbusha. Na kwa hakika Qur’an tukufu na imani vyote vimethibitisha ukweli huu kinaganaga, kwa namna ambayo ambaye hajapoteza roho yake na moyo wake au hakuzama katika upotovu ni lazima auamini kana kwamba anauona, hiyo ni kwa sababu yule ambaye ameupamba ulimwengu huu kwa aina za mazuri yake yasiyo na mpaka na kwa aina za neema zake zisizo na idadi anadhihirisha kwazo Uungu wake Mtukufu Bwana Mlezi mwenye huruma, mwenye kuhifadhi hadi vitu vidogo sana vya kisehemu - kama mbegu - basi Mtengenezaji huyo Mkarimu Mwenye Huruma, ni lazima - kiakili - asimwondoshe mwanadamu huyo ambaye ndiye kiumbe aliyekamilika zaidi, aliyekirimiwa zaidi, mwenye sifa nyingi zaidi, muhimu zaidi na anayempenda zaidi baina ya viumbe vyake, hamwondoi moja kwa moja, bila ya rehema na bila ya makazi mengine - kama inavyoonekana wazi wazi – wala hampotezi milele, bali Muumba Mwenye rehema anamweka kiumbe huyo mpendwa chini ya udongo ambao ndio mlango wa mpito wa rehema, ili atoe matunda yake katika maisha mengine, kama mkulima anavyopanda mbegu ardhini . Na baada ya kupokea tanbihi hii ya ki-Qur’an makaburi hayo kwangu yakawa ni yenye kunituliza kuliko Istanbul yenyewe, na kujitenga kwangu kukawa ni ukarimu zaidi kuliko kukutana na watu, jambo ambalo limenipelekea kupata sehemu ya kujitenga katika mji wa Saryer ndani ya Bosphorus. Na Sheikh Al-Kilany (r.a) akawa Ustadhi Daktari na mwongozo wangu kwa kitabu chake (Futuuh Al-Ghaib), Na Imamu Rabbany (r.a) akawa vile vile Ustadhi rafiki mwenye huruma kwa kitabu chake (Maktuubati), nikawa radhi kabisa na mwenye kushukuru kwa kuingia kwangu uzeeni, na kujitenga kwangu na utamaduni mzuri na starehe yake ya uongo, na kutoka kwangu katika maisha ya kijamii, nikamshukuru sana Allah kwa hilo. Ewe mwenye kuuchungulia uzee kama mimi, na ewe mwenye kuukumbuka mauti kwa onyo la uzee..! Hakika ni juu yetu kuuridhia uzee, mauti na maradhi, na tuone ni uzuri kwa nuru ya imani ambayo Qur’an tukufu imekuja nayo, bali ni juu yetu kuupenda - kwa upande mmoja - maadam tunamiliki imani ambayo ni neema kubwa, basi kwa hivyo uzee ni jambo zuri, maradhi ni jambo zuri na mauti ni jambo zuri pia. Na hakika hakuna kitu kibaya kabisa isipokuwa dhambi, ujinga, bidaa na upotovu.

§12

Niliporejea kutoka kushikiliwa mateka, nilikuwa nikiishi na mtoto wa kaka yangu (AbdulRahman) katika kasri juu ya mlima wa Çamlica Istanbul. Na maisha haya yanaweza kuzingatiwa kuwa ni maisha ya kupigiwa mfano duniani kwa watu kama sisi, hiyo ni kwa sababu nimeokoka kutokana na kushikiliwa mateka na vyombo vya habari vilikuwa wazi mbele yangu katika (Darul Hikma Al-Islamiya) , na kwa kile kinachonasibiana na kazi yangu ya kielimu, na kwamba umaarufu, kutajika na kukubalika kunanizunguka kwa daraja ambayo hainistahiki na mimi naishi katika sehemu nzuri Istanbul (Çamlica), na kila kitu kwangu kinaenda vizuri, ambapo mtoto wa kaka yangu “AbdulRahman” - Allah amrehemu - yuko na mimi, naye ni mwenye akili sana kwani yeye ni mwanafunzi, mwenye kujitolea, mtumishi na mwandishi kwa pamoja, kiasi kwamba nilikuwa nikimzingatia kama ni mtoto wangu wa kimaanawi. Wakati nilipokuwa ninahisi ya kwamba mimi ni mwanadamu mwenye furaha zaidi duniani, niliangalia katika kioo, na nikaona mvi katika nywele na ndevu zangu, tahamaki mzinduko ule wa kiroho ambao niliuhisi katika kushikiliwa kwangu mateka ndani ya msikiti wa (Kosturma) ukaanza kudhihiri. Nikaanza kuangalia na kufikiri kwa makini katika hali nilizokuwa nikiambatana nazo kimoyomoyo, na nilikuwa nikidhani ndio kitovu cha furaha ya kidunia. Hakuna hali au sababu niliyoiangalia kwa makini isipokuwa niliiona ni sababu ya kipuuzi na yenye kuhadaa, haifai kushikamana nayo wala kuambatana nayo. Ukiachilia mbali nilikuta katika kipindi hicho ukosefu wa urafiki wa kweli kutoka kwa rafiki yangu kipenzi, anayezingatiwa kuwa ni katika marafiki zangu wema zaidi, na kwa namna isiyotegemewa na hali isiyofikirika. Yote hayo yamepelekea kukataa na kujitenga na maisha ya dunia, nikasema kuuambia moyo wangu: Je mimi nimehadaika kabisa; nawaona wengi wakiangalia maisha yetu ambayo ni yenye kuonewa huruma kwa upande wa hakika kwa mtazamo wa kuona choyo? Je watu hawa wote wamekuwa wenda wazimu, ama mimi ndio nipo njiani kuelekea katika wazimu, kwa kuwaona wendawazimu hawa waliyohadaika na dunia?! Na kwa vyovyote kuzinduka kwa hali ya juu nilikozinduka kwa kuona mvi kumenifanya nione kwanza: Kutoweka kwa vitu nilivyofungamana navyo vilivyoandaliwa kwa ajili ya kutoweka!! Kisha nikaielekea nafsi yangu nikaiona ipo katika kilele cha kutojiweza, roho yangu ilipopiga ukelele ambayo inaimba kubaki bila ya kutoweka na inashikamana na vitu vyenye kutoweka ikividhania kubaki, ilipiga ukelele: (Maadam ni mwenye kutoweka kimwili ni faida gani ninayoitarajia kwa hivi vyenye kutoweka? Na maadam mimi si mwenye kujiweza basi ni kitu gani ninangojea kutoka kwa wasiojiweza? Basi maradhi yangu hayana dawa isipokuwa kwa Mwenye Kubaki wa milele, kwa Mwenye Uweza wa Tangu) Nikaanza kutafuta na kutafiti.. cha kwanza nilichokirejea ni zile elimu nilizozipata hapo kabla, natafuta ndani yake faraja na tumaini. Lakini – kwa masikitiko – kipindi hicho nilikuwa nikichota kutoka katika elimu za Kiislamu pamoja na elimu za kifalsafa nikidhani - dhana ya makosa sana – kwamba elimu hizo za kifalsafa ndiyo chanzo cha maendeleo, ukamilifu na mhimili wa elimu na kunawirika kwa fikra, wakati ambapo mambo hayo ya kifalsafa yaliyochafua roho yangu sana, bali yamekuwa ni kizuizi mbele ya kukua kwangu kimaanawi. Naam, nilipokuwa katika hali hii, tahamaki hekima ya Qur’an iliyotakasika inanisaidia, ni rehema kutoka kwa Aliye juu Mwenye uweza, na fadhila na ukarimu kutoka kwake (s.w). Ikasafisha takataka za mambo ya kifalsafa, na ikasafisha roho yangu kutokana na mambo hayo - kama ilivyokuwa wazi katika risala nyingi – kwa kuwa giza la kiroho lilitokana na elimu za kifalsafa zilikuwa zikiizamisha roho yangu na kuifuta ndani ya viumbe, kila nilipoelekeza mtazamo wangu katika mambo hayo sikuona nuru wala mwangaza, wala sikuweza kupumua na moyo kukunjuka hadi ilipokuja nuru ya Tawhid yenye kung’aa inayotokana na Qur’an tukufu ambayo inafundisha (Hapana Mola ila yeye) ikachana giza hilo na kuliangamiza. Kifua changu kikafunguka na kupumua kwa raha na utulivu. Lakini nafsi na Shetani wakaelekeza mashambulizi makali kwenye akili na moyo na hiyo ni kwa vile vilivyo chukua miongoni mwa mafundisho na masomo kutoka kwa watu wa upotovu na falsafa. Malumbano ya kinafsi yakaanza katika mashambulizi haya hadi yakamaliza - Shukrani kwa Allah - kwa ushindi wa moyo. Na ilivyokuwa sehemu katika malumbano hayo imekuja katika aghlabu ya risala, basi tunatosheka nayo, ila tutabainisha hapa dalili moja tu miongoni mwa maelfu ya dalili, ili kubainisha ushindi wa moyo dhidi ya nafsi na Shetani, na ili dalili hiyo isafishe roho za wazee ambao wamezichafua roho zao, na wakazipa maradhi nyoyo zao na nafsi zao, hadi zikavuka mipaka yake, mara kwa upotevu na mara nyingine kwa yasiyowahusu miongoni mwa mambo ambayo yanajificha chini ya pazia la elimu za kimagharibi na fani za kitamaduni, na ili viokoke - kwa idhini ya Allah – katika haki ya Tawhid, kutokana na shari za nafsi na Shetani kwa haki ya Tawhid. Na malumbano yalikuwa kama ifuatavyo: Nafsi yangu ilisema ikiuliza kwa jina la elimu za kifalsafa za kimaada: “Hakika vitu vilivyokuwepo ulimwenguni, kwa asili yake vinaingia katika vitu vilivyokuwepo, basi kila kitu ni chenye kutoka na kuelekea katika sababu, basi tunda huchukuliwa kutoka katika mti, na mbegu huhitajiwa na udongo, basi nini maana ya kunyenyekea kwa Allah na kutaka kitu kidogo zaidi kutoka kwake (s.w)?!” Ilidhihiri haraka siri ya Tawhid kwa nuru ya Qur'an tukufu kwa sura ifuatayo: Moyo wangu ukaijibu nafsi yangu yenye mantiki ya kifalsafa: Hakika kitu kidogo zaidi na vingi vyao ni vijisehemu si vinginevyo ila ni kama kitu kikubwa zaidi, kinatokana na uweza wa Muumba wa viumbe moja kwa moja, na kinatoka katika hazina ya Allah. Hivyo hakuna namna nyingine katu, na sababu ni mapazia, hiyo ni kwa sababu kiumbe kidogo zaidi na kisicho na umuhimu - kulingana na dhana yetu kinaweza kuwa kikubwa zaidi kwa upande wa umbile, kutengenezwa na kuundwa vyema kuliko kiumbe kikubwa zaidi. Nzi kwa mfano, kama asingekuwa anapendeza zaidi kwa upande wa kutengenezwa kwake kuliko kuku basi sio kwamba ni duni kuliko kuku huyo. Kwa hiyo haiwezekani kubagua baina ya kidogo na kikubwa kwa upande wa kuumbwa na kutengenezwa, ima uegemezwe uumbwaji wa vyote – kidogo na kikubwa – kwa sababu za kimaada, na ima uegemezwe uumbwaji wa vyote kwa Mmoja wa Pekee. Na kama ilivyokuwa upande wa kwanza ni muhali ndani ya muhali, basi hakika upande wa pili ni wajibu kuitakidi na ni lazima. Kwa sababu elimu ya Allah (s.w) inakizunguka kila kitu na ambaye uwepo wake ni thabiti kwa namna ya kukata shauri, kwa kunadhimika kwa viumbe vyote na hekima zilizo ndani yake, na maadam kila kitu kiwango chake kinabainika ndani ya elimu yake (s.w), na maadam vilivyotengenezwa na kuumbwa – vipo katika ukomo wa kupendeza na kuundwa vyema – vinakuja kwa wepesi mno kwenye uwepo kutoka katika kutokuwepo kila wakati kama inavyoonekana. Na maadam huyo Mweza Mjuzi anamiliki uweza usiyo na mipaka anaweza kukifanya kiwepo kila kitu kwa amri ya كُنْ فَيَكُوْن na kwa mpweso wa jicho, kama tulivyo bainisha hayo katika risala nyingi kwa hoja za uhakika na hasa katika (Andiko la Ishirini) na mwisho wa (Mwale wa ishirini na tatu). Hivyo hapana budi kuwa wepesi usio na mipaka na wenye kuonekana na wenye kuvuka kawaida, si vinginevyo isipokuwa ni kutokana na udhibiti wa kielimu na ukubwa wa uweza huo usio na mpaka. Mathalani: Kama ambavyo ukipitisha mada maalumu ya kikemia juu ya kitabu kilichoandikwa kwa wino wa kikemia usioonekana, basi hakika ya kitabu hicho kikubwa kitadhihiri bayana hadi kumtaka asome kila mwenye kukiangalia, hivyo hivyo kiwango cha kila kitu na namna yake maalumu kinabainika katika elimu yenye kukizunguka ya Mweza wa Tangu. Basi Mweza ambaye nguvu zake hazina mipaka atapitisha – ambayo ni dhihirisho la uweza wake – kwa wepesi kabisa, kama kupitisha kwa mada ile katika mfano, juu ya maandiko yale ya kielimu, anapitisha kwa amri ya كُنْ فَيَكُوْن , na kwa uweza wake ule usio na mpaka, na kwa utashi wake tendaji, basi anakipa (s.w) kitu hicho uwepo wa nje, akikidhihirisha mbele ya wenye kushuhudia, jambo litakalowafanya kusoma yaliyo ndani yake miongoni mwa nakshi za hekima yake. Lakini kama haukuegemezwa uumbaji wa vitu vyote mara moja kwa Mjuzi asiye na mpaka na kwa Mweza wa Azali, basi hakika kuumba kitu kidogo zaidi wakati huo – kama nzi mathalani – inalazimu kukusanya vyote vyenye uhusiano na nzi kutoka kwa aina nyingi za ulimwengu, kuzikusanya kwa mizani maalumu na makini, yaani kukusanya vyote hivyo ndani ya mwili wa nzi, bali inapaswa kila atomu yenye kufanya kazi katika kiwiliwili cha nzi kuwa ni yenye elimu kamili kwa siri ya uumbaji wa nzi na hekima ya uwepo wake, bali inapaswa iwe yenye kutengeneza vyema kwa uzuri ambao upo ndani yake kwa umakini mkubwa na uchambuzi wake wote. Na ilivyokuwa sababu za kiasili haziwezi kuumba kitu kutokana na kutokuwepo kabisa kama walivyoafikiana magwiji; kwa hiyo, hakika ya sababu hizo hata kama zikiweza kukifanya kitu kiwepo basi haziwezi kufanya hivyo isipokuwa kwa kukusanya. Na maadam zitakusanya, na kwamba kiumbe hai - vyovyote awavyo – amekusanya aghlabu ya mifano ya vilivyo ulimwenguni miongoni mwa spishi na aina, kana kwamba ni muhtasari wa viumbe au mbegu ya viumbe hivyo. Basi kwa hiyo hapana budi kukusanya atomu za mbegu kutokana na mti mzima, na kukusanya spishi za kiumbe hai na atomu zake kutoka ulimwenguni kote, na hiyo ni baada ya kuzichuja, kuzipangilia na kuzikadiria kwa umakini na ustadi kulingana na vigezo maalumu. Na kwa kuwa sababu za kimaada za kiasili si zenye utambuzi, basi hazina elimu kabisa ili kukadiria mpango, na kuratibu mfumo, na kufungamanisha faharisi, na ili ifanye kazi pamoja na atomu kwa mujibu wa kalibu za kimaanawi, ikiziyeyusha ndani ya kalibu hizo ili kuzizuia zisifarikiane, kuachana na kuharibu mpangilio. Wakati ambapo muundo wa kila kitu unaweza kuwa ndani ya aina zisizokuwa na mipaka, hivyo kitu kukipa umbo moja maalum kati ya maumbo hayo yasiyo na mipaka, na kukiratibu kitu hicho kwa kiwango maalumu ndani ya viwango hivyo visivyo na idadi, bila ya kufarikiana kwa atomu za spishi zenye kutembea kama kimiminika na kwa nidhamu kamili. Kisha kujenga baadhi yake juu ya nyingine bila ya kalibu maalumu na bila ya kuainisha viwango, kisha kukipa kiumbe hai uwepo ulionadhimika, yote haya ni jambo lililo wazi kwamba liko nje ya mipaka ya uwezekano, bali liko nje ya mipaka ya akili! Basi yule ambaye hajapoteza uoni wake, anaona hilo kwa uwazi! Naam, na kufafanua ukweli huu, imekuja katika Qur'an tukufu: إِنَّ الَّذِينَ تَدْعُونَ مِن دُونِ اللَّهِ لَن يَخْلُقُوا ذُبَابًا وَلَوِ اجْتَمَعُوا لَهُ yaani zinapokusanyika sababu tofauti za kimaada haziwezi kukikusanya na kukiratibu kiwiliwili cha nzi mmoja na viungo vyake kwa mujibu wa vipimo maalumu, hata kama sababu hizo zitapewa utashi na hiari, bali hata zingeweza kukitengeneza kiwiliwili cha nzi na kukikusanya basi haziwezi kukibakisha na kukidumisha kwa kiwango chake maalumu, bali hata zingeweza kumbakisha kwa kiwango maalumu basi zisingeweza kuzifanyisha kazi atomu hizo kwa mpangilio ambazo daima ni zenye kujiunda upya na zinarejeshwa katika uwepo huo ili ziufanyishe kazi ndani yake; kwa hiyo, kiakili, sababu haziwezi kuwa mmiliki wa vitu hivi. Mwenyewe wa kweli si sababu.. Ndiyo, vitu hivyo vina mmiliki na mwenyewe wa kweli ambapo kuhuisha vilivyopo juu ya ardhi miongoni mwa viumbe ni rahisi kwake kama kumhuisha nzi mmoja. Na kuyafanya majira ya machipuo yawepo, kwake ni wepesi kama ilivyo wepesi kwa ua moja kulifanya liwepo. Kama aya tukufu inavyobainisha hilo: مَّا خَلْقُكُمْ وَلَا بَعْثُكُمْ إِلَّا كَنَفْسٍ وَاحِدَةٍ Hiyo ni kwa sababu yeye si muhitaji wa kukusanya, kwa kuwa yeye ni mmiliki wa amri كُنْ فَيَكُوْن na kwa kuwa yeye anaumba kutokana na kutokuwepo ndani ya kila majira ya machipuo hali za vilivyomo ndani ya majira ya machipuo, sifa zake na miundo yake, zisizokuwa spishi zake, na kwa kuwa mpango wa kila kitu, kielelezo chake na faharisi yake vimeainishwa katika elimu yake (s.w). Na kwamba atomu zote hazifanyi kazi isipokuwa katika mzingo wa elimu yake na uweza wake, hivyo anaumba kila kitu na kukifanya kiwepo kwa mpweso wa jicho na kwa ukomo wa wepesi. Na kitu hakiendi upogo kutoka kile kilichopangiwa walau kwa kiwango cha atomu. Basi Sayari zenye kusafiri zinakuwa jeshi lililo pangika lenye kumtii Yeye. Na atomu zinakuwa askari watiifu wa amri yake, na kwa vile wote wanaenda kwa mujibu wa uweza huo wa tangu na kwa mujibu wa desturi za elimu hiyo ya tangu, hivyo hakika ya athari hizi huja katika uwepo kulingana na uweza huo. Basi haziwi ndogo athari hizo kwa mtazamo wa kuzidogesha, wala haziwi zenye kupuuzwa kwa kutozitilia umuhimu, kwa kuwa nzi anayenasibishwa na uweza huo anamuangamiza Namrudi, na sisimizi anaangamiza kasri la Firauni, na mbegu ya Msonobari iliyo katika ukomo wa udogo inabeba juu ya mabega yake uzito wa mti wa Msonobari mkubwa kama mlima. Basi kama tulivyothibitisha ukweli huu katika risala nyingi hapa pia tunasema hayo hayo: Hakika mwanajeshi anayejinasibisha na mfalme kwa uanajeshi anaweza kufanya mambo yanayozidi uweza wake mara elfu moja, kama kumshikilia mateka kiongozi mkubwa wa kiadui kwa kujinasibisha kwake, vile vile hakika kila kitu kwa kujinasibisha kwake kwa uweza huo wa tangu kinakuwa chanzo cha miujiza ya kutengenezwa vyema kwa namna ambayo inazidi sababu zile za kiasili kwa mara mia moja elfu. Muhtasari: Hakika kutengenezwa kila kitu kwa ustadi wa hali ya juu na wepesi usiyo na mpaka katika kukifanya kiwepo, vinaonesha kwa pamoja kwamba kitu hicho ni katika athari za Mwenye uweza wa Azali Mwenye elimu iliyozunguka kila kitu, vinginevyo ni muhali ndani ya muhali mia moja kuja kitu hicho kwenye uwepo, bali - wakati huo - inakuwa nje ya mipaka ya uwezekano na ndani ya duara la kutowezekana, bali nje ya hali ya uwezekano kuelekea hali isiyowezekana, bali haiwezekani kitu kuja katika uwepo kabisa. Na kwa namna hii hakika ya dalili hii mbayo ipo katika ukomo wa uimara na umakini, na ukomo wa kina na uwazi imeinyamazisha nafsi yangu ambayo ilikuwa ni mwanafunzi wa muda wa shetani, na msemaji wa watu wa upotevu na falsafa, hadi imeamini - sifa zote njema kwa Allah - imani thabiti na ikasema: “Naam, inapaswa mimi niwe na Mola Mlezi Muumba ambaye anajua na kusikia fikra ndogo kabisa katika moyo wangu na matumaini na dua za siri zaidi, na ni Mwenye uweza usio na mpaka, basi anazisaidia haja zilizojificha za roho yangu na vilevile anaibadili dunia hii kubwa kwa kuleta dunia nyengine ili anifurahishe furaha ya milele na kuleta Akhera baada ya kuiondoa dunia hii. Kama anavyoumba nzi ndivyo pia anavyoifanya mbingu iwepo. Na kama anavyoupanda uso wa mbingu kwa jicho la jua, amejaalia atomu kuwa ni pambo katika mboni ya jicho langu. Kama sio hivyo hakika ambaye hawezi kuumba nzi basi hawezi kuingia katika fikra za moyo wangu, na hatosikia unyenyekevu wa roho yangu. Na kwamba ambaye hawezi kuumba mbingu basi hawezi kunipa furaha ya milele. Hivyo hakika Mola wangu Mlezi ni yule anayesikia - bali anazitengeneza - fikra za moyo wangu. Basi kama anavyoijaza anga mawingu na kuyaondoa ndani ya saa basi hakika atabadilisha dunia hii kuwa Akhera na kuitengeneza Pepo na kunifungulia milango yake akisema: Ingia!” Enyi ndugu zangu wazee, na enyi mliopoteza sehemu katika umri wenu kwa bahati mbaya ya nafsi na tabu - kama nafsi yangu - katika elimu za kigeni na za kifalsafa zisizo na nuru! Tambueni kwamba yale ambayo Qur'an inayasema kwa kurejea daima kama (لا إله إلاالله) amri hiyo tukufu, ni nguzo ya kiimani yenye nguvu na ya hakika isiyotetereka wala kuvunjika wala kubadilika milele, kwa kuwa inaondosha aina zote za giza na kutibu majeraha ya kimaanawi. Na hakika kuweka tukio hili refu ndani ya milango ya matumaini ya uzee wangu haikuwa kwa hiari yangu, bali sikutaka kuliweka hapa kwa kuepusha kuwachosha, isipokuwa naweza kusema: (Limenakiliwa kutoka kwangu bila ya hiari yangu). Na kwa vyovyote.. turudi katika maudhui yetu: Naam, na kwa namna hii, hali ya kuyakataa maisha hayo mazuri ya kidunia ilinijia nikiwa Istanbul ambayo kwa nje ni yenye ladha, kutokana na kufikiria katika mvi za kichwa changu na ndevu zangu, na kutokana na kukosekana uaminifu kutoka kwa rafiki mwaminifu hadi nafsi ikaanza kutafuta ladha za kimaanawi badala ya kile kilichoitahini miongoni mwa ladha, nikaomba nuru na faraja katika uzee huu ambao unaoneka ni mzito wenye usumbufu na usiyokubalika katika mtazamo wa walioghafilika. Sifa njema zote na shukurani ni kwa Allah (s.w) ambaye ameniwafikisha kupata ladha hizo za kiimani za kweli na za kudumu ndani ya (لا إله إلا الله) na katika nuru ya Tawhid badala ya ladha hizo za kidunia zisizo na ukweli, bali mwisho wake hazina kheri. Na sifa zote njema zimwendee kwa kuniwafikisha vilevile kuuona uzee ni mwepesi naneemeka na uchangamfu wake na nuru yake tofauti na uzito na kupooza wanakokuona walioghafilika. Naam, enyi ndugu zangu! Maadam mnamiliki imani, na maadam mna swala na dua ambavyo vinaangaza imani, bali vinafanya ikue na iwe imara, basi kwa hivyo mnaweza kuuangalia uzee wenu kana kwamba ni ujana wa kudumu, kwa ujana mtakaoupata katika makazi ya kudumu, kwa kuwa ni kupooza hasa, ni mzito, mbaya bali usio na nuru wenye kuumiza kabisa si vinginevyo isipokuwa ni uzee wa watu wa upotevu, bali huenda kipindi cha ujana wao vilevile basi na walie.. na waseme..: Majuto yaliyoje! Ama nyinyi enyi wazee waumini waheshimiwa! Mnapaswa kumshukuru Mola wenu Mlezi kwa furaha na kusema: “sifa zote njema ni kwa Allah kwa kila hali!”.

§13

Nilipokuwa peke yangu bila ya msaidizi huko (Barla) upande uliopo katika mkoa wa (Isparta) nikisumbuliwa na kushikiliwa mateka kwenye mateso kunakoitwa uhamishoni, nikiwa nimezuiwa kuchanganyika na watu, bali hata kutumiana ujumbe na yeyote, ukiachilia mbali maradhi niliyokuwa nayo, uzee na ugeni. Wakati nikisumbuliwa na hali hii na machungu ya huzuni, tahamaki nuru yenye kufariji inaangaza kutoka katika siri nzuri za Qur'an tukufu na nukta zake za kina, Allah (s.w) amenipa kwa rehema yake kamili iliyo pana, nikawa nafanya kazi kwa bidii kwa nuru hio ili kusahau hali ya kuumiza na ya huzuni niliyokuwa nayo, hadi nikaweza kusahau nchi yangu, vipenzi vyangu na jamaa zangu. Lakini hasara iliyoje sikuweza kumsahau mmoja kati yao ambaye ni mtoto wa kaka yangu, bali ni mwanangu wa kimaanawi, mwanafunzi wangu mwaminifu na rafiki yangu shujaa (Abdul Rahman) Allah amrehemu. Ambaye nimetengana naye kabla ya takribani miaka saba, wala sifahamu hali yake ili niwasiliane naye, kuongea naye na kushirikiana naye katika maumivu, wala yeye hafahamu nilipo ili aje kunihudumia na kunifariji. Naam, nilikuwa katika haja kubwa - hasa katika uzee wangu huu – ya mtu mwaminifu mkweli kama (Abdul Rahman). Na siku moja ghafla mtu mmoja alinikabidhi barua nilipoifungua tu ikanibainikia kwamba ni barua yenye kudhihirisha haiba ya (Abdul Rahman) kikamilifu na katika barua hiyo kumeambatanishwa sehemu ya aya za (Andiko la Ishirini na Saba) ambalo linadhihirisha karama tatu za miujiza. Kwa hakika barua hiyo iliniliza sana na bado inaendelea kuniliza, ambapo ndani yake (Abdul Rahman) anabainisha kwa ukweli wote kwamba yeye amejitenga kikamilifu na vionjo vya kidunia na ladha zake, na kwamba anachokitamani zaidi ni kufika kwangu ili anitunze katika uzee wangu huu kama nilivyokuwa nikimlea udogoni kwake na kunisaidia kwa kalamu yake katika wadhifa na kazi yangu ya kweli duniani, nayo ni kusambaza siri za Qur'an tukufu, hata alikuwa anasema katika barua yake: Nitumie barua zinazokaribia thelathini ili niandike kutokana na kila moja nakala thelathini. Kwa hakika barua hii imenivuta katika dunia kwa tumaini lenye nguvu, nikasema kuiambia nafsi yangu: Sasa hivi nimempata mwanafunzi wangu mtiifu na shujaa, mwenye akili isiyo ya kawaida, na mwenye uaminifu wa kweli, na mafungamano thabiti ambayo yanavuka uaminifu wa mtoto wa kweli kwa mafungamano yake na mzazi wake. Basi kwa - idhini ya Allah – atanitunza na kunihudumia bali hata nimesahau hali niliyokuwa nayo ya kifungo chenye kuumiza na kutokuwa na msaidizi, bali nilisahau hata ugeni na uzee! Kana kwamba (Abdul Rahman) ameandika barua hiyo kwa imani ya upeo wa nguvu na kung’aa akisubiri muda wake, kwa kuwa ameweza kupata nakala iliyochapishwa ya (Neno la Kumi) nililolichapisha likielezea kuamini Akhera. Basi barua hiyo ikawa dawa yenye kumponya ambapo ilitibu majeraha yake ya kimaanawi ambayo aliugua kwa miaka saba iliyopita. Na baada ya kupita takriban miezi miwili nikiwa ninaishi katika tumaini hilo ili tuweze kuishi maisha ya furaha duniani, tahamaki ninashtukizwa na habari ya kufa kwake, basi huzuni iliyoje.. na masikitiko yaliyoje.. kwa hakika habari hii ilinitikisa sana kiasi cha kuwa bado nipo katika taathira yake tangu miaka mitano na imenipa huzuni kubwa na maumivu makali kwa utengano wenye kuumiza, yanavuka maumivu niliyokuwa nikiyapata kutokana na kushikiliwa mateka yenye mateso na maumivu ya upweke, ugeni, maumivu ya uzee na maradhi. Nilikuwa nikisema: Hakika nusu ya dunia yangu binafsi imekufa kwa kufa mama yangu na nimeona nusu ya pili imekufa pia kwa kufa (Abdul Rahman), kwa hiyo hayajabaki kwangu mafungamano na dunia. Naam, lau (Abdul Rahman) angelibaki pamoja nami duniani angelikuwa msaada mkubwa katika wadhifa wangu wa kiakhera duniani na angelikuwa mrithi wangu bora, na angelichukua nafasi yangu baada yangu, na angelikuwa rafiki mwaminifu bali sehemu ya faraja kwangu, na angelikuwa mwanafunzi hodari wa Risale-i Nur, na mwaminiwa mwenye ikhlasi na mwenye kuihifadhi. Basi hasara kama hii – kwa kuzingatia kibinaadamu – ni hasara yenye kuunguza iumizayo kwa watu kama mimi. Na japo nilikua ninajitahidi kusubiri na kuvumilia maumivu niliyokuwa nikiyapata isipokuwa kulikuwa na kimbunga kikali sana kinavuma katika pande za roho yangu. Basi lau kama si liwazo hilo linalotokana na nuru ya Qur'an tukufu linalomiminika kwangu baadhi ya nyakati mtu kama mimi asingeliweza kuvumilia na kuthibiti. Nilikuwa nikienda na kutafakari katika mabonde ya (Barla) na nikizunguka kwenye milima yake nikiwa mpweke na kukaa katika sehemu tupu nikijitenga, nikiwa nimebeba huzuni na maumivu, ikawa mbele yangu yanapita mabango ya maisha ya furaha na mandhari zake nzuri ambayo nilikuwa nimeyaishi pamoja na wanafunzi wangu mfano wa - (Abdul Rahman) – kama filamu ya sinema. Kila mabango hayo yalipopita mbele ya mawazo yangu, inapora kutokana na ukali wa kujizuia kwangu na udhaifu wangu na uharaka wa kuathiri unaotokana na uzee na ugeni. Lakini ghafla ikadhihiri siri ya aya tukufu: ﴿كُلُّ شَيْءٍ هَالِكٌ إِلَّا وَجْهَهُ لَهُ الْحُكْمُ وَإِلَيْهِ تُرْجَعُونَ ﴾ Ilidhihiri kwa uwazi kiasi cha kunifanya nirudierudie: (يا باقي انت الباقي), na kutokana na hilo nimepata liwazo la kweli. Naam, nimeiona nafsi yangu kwa siri ya aya hii tukufu, nikavuka mabonde hayo matupu pamoja na hali ile iumizayo, nimeiona kichwani ikiwa ni majeneza matatu makubwa kama nilivyoyaashiria katika Risala (Ngazi ya Sunna): Kwanza: Nimeiona nafsi kama shahidi wa kaburi likusanyalo Saidi hamsini na tano wamekufa na wamezikwa katika maisha yangu, na ndani ya umri wangu unaokaribia miaka hamsini na tano. Pili: Nimeiona nafsi yangu kama kiumbe hai mdogo sana - kama sisimizi – akitembea juu ya uso wa zama hizi ambazo ni kama shahidi wa kaburi la jeneza kuu kwa ambao ni watu wa jinsi na aina yangu, ambao wamezikwa katika kaburi la muda uliopita tangu zama za Adam (a.s). Ama Tatu: Kufa kwa dunia hii kubwa kumekuja mbele ya mawazo yangu – kwa siri ya aya tukufu – kama mfano dunia yenye kutembea inavyokufa kutoka katika uso wa dunia kila mwaka kama anavyokufa mwanaadamu, na hivi ndivyo maana ya kiishara ya aya tukufu imeniokoa: فَاِن۟ تَوَلَّو۟ا فَقُل۟ حَس۟بِىَ اللّٰهُ لَٓا اِلٰهَ اِلَّا هُوَ عَلَي۟هِ تَوَكَّل۟تُ وَهُوَ رَبُّ ال۟عَر۟شِ ال۟عَظٖيمِ na ikanipa nuru isiyozimika, ikaangamiza huzuni niliyokuwa nikiipata kutokana na kufa kwa (Abdul-Rahman) ikinitunukia maliwazo ya kweli. Naam, aya hii tukufu imenifundisha kwamba maadam (s.w) yupo basi yeye ndio mbadala wa kila kitu, na maadam ni mwenye kubaki basi ni mwenye kumtosheleza mja wake, kwa kuwa dhihirisho moja katika madhihirisho ya uangalizi wake (s.w) ni sawa na ulimwengu wote, na udhihirisho miongoni mwa madhihirisho ya nuru yake yenye kukusanya unayapa majeneza hayo matatu maisha ya kimaanawi, ambapo hudhihiri kwamba si majeneza, bali ni miongoni mwa waliomaliza majukumu yao na kazi zao juu ya ardhi hii na kusafiri kuelekea ulimwengu mwingine. Na kwa vile siri na hekima hii tumeshaiweka wazi katika (Mng’ao wa Tatu) unanionesha kuwa sina haja ya kuweka wazi zaidi, ila ninasema: Hakika kilichoniokoa kutokana na hali hiyo ya huzuni yenye kuumiza, ni kukariri kwangu ya (يا باقي انت الباقي) mara mbili ambayo ndio maana ya aya tukufu: كُلُّ شَئٍ هَالِكٌ إِلاَّ وَجْهَه Na ubainifu wa hilo ni: Kwamba niliposema: (يا باقي انت الباقي) kwa mara ya kwanza, tiba na maponyo ikaanza kwa kinachofanana na upasuaji kwenye majeraha hayo ya kimaanawi yasiyokuwa na mpaka yanayotokana na kutoweka kwa dunia na kutoweka walio ndani yake miongoni mwa vipenzi – mfano wa (Abdul Rahman) – na yanayotokana na wingi wa mafungamano ninayofungamana nayo. Ama mara ya pili maneno (يا باقي انت الباقي) yamekuwa ni malhamu yenye kuponya kwa majeraha yote hayo ya kimaanawi, na hiyo ni kwa kuzingatia maana ifuatayo: Ewe Mola wangu na aondoke aondokaye, Wewe ndiye Mwenye kubaki na Wewe ndiye Mwenye kutosha, na maadam Wewe ni Mwenye kubaki basi udhihirisho miongoni mwa madhihirisho ya rehema yako ni wenye kutosha kwa kila chenye kutoweka. Na maadam upo basi kila kitu kipo kwa anayediriki maana ya kujinasibisha kwake kwako kwa kuamini uwepo wako na anatembea kwa mujibu wa kujinasibisha kwa siri ya Uislamu. Basi kutoweka, kuondoka, mauti na kukosekana si chochote ila ni mapazia ya kufanywa upya, na si chochote ila ni kutembea katika vituo tofauti, kwa fikira hii hali ile ya huzuni ya kiroho yenye kuunguza ikabadilika, na ile hali ya giza na ya kutisha ikabadilika kuwa hali ya kufurahisha na nzuri, na hali yenye nuru yenye kupendwa na yenye kutuliza. Ulimi wangu na moyo wangu bali kila atomi katika atomi za mwili wangu ikawa vinarudiarudia kwa ulimi wa hali vikisema: Alhamdulillahi. Na kwa hakika sehemu katika sehemu elfu moja imedhihiri kutokana na madhihirisho hayo ya rehema kwa namna hii: Niliporejea kutoka katika huzuni yangu, kutoka katika mabonde kuelekea (Barla) nikiwa nimebeba huzuni hizo, nilimwona kijana aliyeitwa “Kuleönlü Mustafa” amenijia akitaka ufafanuzi wa baadhi ya masuala yanayomshughulisha ya Fiqhi, udhu na sala. Japo sikuwa nikiwapokea wageni katika kipindi hicho isipokuwa kana kwamba roho yangu ilisoma Ikhlasi iliyomo katika roho ya kijana huyo, na kana kwamba ilihisi – kwa hisia ya kabla ya kutokea – atakachokifanya kijana huyu katika kuhudumia Risale-i Nur kwenye mustakabali, hivyo sikumrejesha na nilimkubali awe mgeni, kisha ikanibainikia kwamba Allah (s.w) amenipa kijana huyu akiwa ni mbadala wa (Abdul-Rahman) ambaye ni mrithi wangu bora na anatekeleza jukumu la mrithi wa kweli katika kuhudumia Risala ya Nuru. Na Allah (s.w) ameniletea (Mustafa) kana kwamba anasema: Nimemchukua kutoka kwako Abdul-Rahman mmoja na nitakupa mbadala wake Abdul-Rahman thelathini kama mfano wa kijana huyu Mustafa ambao watafanya juhudi katika wadhifa huo wa kidini, na watakuwa ni wanafunzi wako waaminifu, watoto wa kaka wakarimu, Watoto wa kimaanawi, ndugu wema na marafiki wenye kujitolea. Naam, - shukrani kwa Allah – hakika amenitunuku Allah Muumba (s.w) Abdul-Rahman thelathini, na hapo nikaongea na moyo wangu: Maadam ewe moyo wangu wenye kulia na wenye jeraha umeona kielelezo na mfano huu na umepoa majeraha muhimu miongoni mwa majeraha hayo ya kimaanawi, basi ni juu yako kutulizana kuwa Allah (s.w) ataponya majeraha yaliyobakia ambayo yana kuhuzunisha na kukupa maumivu. Enyi ndugu wazee wa kiume na wa kike, na enyi mliopoteza mwana mpendwa zaidi wakati wa uzee au mmoja wa watu wake wa karibu amemuacha kama mimi, na ewe mwenye kubeba uzito wa uzee na kubeba juu ya kichwa chake ghamu nzito zinazotokana na utengano! Kwa hakika mmetambua hali yangu kwani pamoja na ugumu wake mara dufu ya hali zenu, isipokuwa aya hii tukufu imeponya na kutibu kwa idhini ya Allah (s.w), hapana shaka kuwa katika famasia ya Qur’an tukufu kumejaa dawa ya kila maradhi katika maradhi yenu. Mkiweza kuirejea kwa Imani, na mkajitibu kwa ibada, hapana budi kupungua mizigo mliyoibeba miongoni mwa mizigo ya uzee na ghamu zenye kuleta uzito katika vichwa vyenu. Hivyo basi, hakika sababu ya kuandika somo hili kwa urefu ni kwa kutaraji kukithirisha ombi la dua kwa (Abdul-Rahman). Basi msichoke wala kupatwa na uchovu kutokana na urefu wake. Na hakika kusudio langu la kudhihirisha jeraha langu la kutisha kwa sura hii yenye kuumiza, nanyi kupata maumivu zaidi na kuhuzunika kiasi kwamba inaweza kupelekea kuzidi maumivu na huzuni zenu na hatimaye kuikataa, si chengine ila ni kwa kubainisha kilicho ndani ya tiba ya Qur’an tukufu miongoni mwa ponyo thabiti na nuru yenye kung’aa.

§14

Nitaangalia katika tumaini hili bango muhimu katika mabango ya matukio ya maisha yangu, naomba msichoshwe na urefu wake. Baada ya kuokoka kutokana na kushikiliwa mateka na Urusi katika Vita vya Kwanza vya Dunia, nilikaa Istanbul ili kuhudumia dini katika (Daru Al-Hikma Islamia) takribani miaka mitatu. Lakini kwa mwongozo wa Quran tukufu na kwa hima ya Sheikh Al-Kylani, na kwa kuzinduka kwangu kwa sababu ya uzee, kumenipelekea kuchoshwa na maisha ya kimji ya Istanbul, nikawa ninayakataa maisha yake mazuri ya kijamii, shauku na upendo vinavyoitwa (Maradhi ya ugeni) vilinisukuma kuelekea katika mji wangu, kwani nilikuwa nikisema: Maadam nitakufa basi nife katika mji wangu, nikaielekea katika mji wa (Van). Na huko kabla ya kitu chochote nilienda kuitembelea madrasa yangu ya (Horhor) nikaona kuwa Waarmenia wameichoma moto kama walivyochoma moto baki ya nyumba nyengine zilizokuwepo katika mji wa (Van) wakati wa ukoloni wa Urusi. Nikapanda katika ngome mashuhuri kwenye mji wa (Van) nalo ni rundo la mawe magumu chini yake imeambatana kikamilifu na madrasa yangu, na mbele yangu ilikuwa ikipita mizimu ya wale marafiki zangu wa kweli na ndugu wenye kuliwaza miongoni mwa wanafunzi wangu katika madrasa yangu ambao nilitengana nao kwa takribani ya miaka saba iliyopita. Kwa sababu ya janga hili sehemu ya marafiki hao wa kweli na wenye kujitoa wamekuwa mashahidi wa kweli na wengine ni mashahidi wa kimaanawi, sikuweza kujizuia kulia. Nikapanda katika kilele cha ngome nayo ni kwa urefu wa minara miwili na madrasa yangu ikiwa chini yake. Nikakaa hapo nikitafakari. Mawazo yakanipeleka katika takribani miaka minane iliyopita na yakanitembeza katika muda huo, kutokana na nguvu ya mawazo yangu na kutokuwepo kizuizi chenye kunizuia na mawazo hayo na kuniondoa katika muda huo kwani nilikuwa peke yangu. Nilishuhudia mabadiliko makubwa sana yametokea ndani ya miaka minane kiasi kwamba kila nilipokuwa nikifumbua jicho langu ninaona kana kwamba zama zimepita na matukio yake. Niliona kuwa kituo cha mji kilichoizunguka madrasa yangu – ambayo ipo pembezoni mwa ngome – kimeunguzwa na kuangamizwa kabisa. Nikaangalia mandhari hiyo kwa huzuni na masikitiko, kwani nilikuwa nikihisi tofauti kubwa kati ya nilichokuwa ndani yake na ninachokiona sasa hivi, na kana kwamba miaka mia mbili imepita katika mji huu. Wengi wa waliokuwa wakiishi katika nyumba hizi zilizoangamizwa walikuwa ni marafiki zangu, na vipenzi vyangu. Sehemu kati yao wamekufa kwa kuhama kutoka katika mji na wameonja shida zake, Allah awarehemu. Ambapo nyumba za Waislamu ziliangamizwa kabisa kwenye mji na haikubaki isipokuwa mahala pa Waarmenia, nikaumia ndani ya nafsi na kuhuzunika huzuni kubwa kiasi kwamba lau ningelikuwa na macho elfu moja yote yangebubujikwa na machozi. Nilidhani kwamba nimeokoka kutokana na ugeni kwa kurejea katika mji wangu, lakini – kwa bahati mbaya – niliuona ugeni wenye kuumiza zaidi katika mji wangu, ambapo niliona mamia ya wanafunzi wangu na vipenzi vyangu ambao nafungamana nao kiroho – kama Abdul-Rahman aliyetanguliwa kutajwa katika Tumaini la Kumi na Mbili – nimewaona wamegubikwa na mchanga na vifusi na makazi yao yamekuwa athari baada ya kuwa kitu, na mbele ya bango hili lenye kuhuzunisha maana ya kipengele hiki ilichukua muundo wa mwili wa mmoja wao na ambayo ilikuwa katika kumbukumbu yangu kwa muda mrefu ila sikuwa nikifahamu maana yake kikamilifu: Kama si kutengana na vipenzi mauti usingepata njia kwenye roho zetu Yaani kikubwa kinachomwangamiza mwanadamu si kingine ila ni kutengana na vipenzi. Naam, hakuna kitu kimeniumiza na kuniliza kama tukio hili, na lau kama nisingepata msaada kutoka katika Qur'an tukufu na kutoka katika Imani basi huzuni na ghamu hiyo ingeliniathiri kwa kiasi cha kutosha cha kuitoa roho yangu. Hakika washairi hapo zamani walikuwa wakiyalilia makaazi ya vipenzi vyao wanapopita katika magofu yake, basi nikaona kwa macho yangu bango hili la utengano wenye kuhuzunisha, roho yangu, moyo wangu pamoja na jicho langu vikalia kwa huzuni kubwa kama anayepita katika makaazi ya vipenzi vyake na magofu yake baada ya miaka mia mbili. Na hapo kurasa nzuri na tamu za maisha yangu zikapita mbele ya macho na mawazo yangu ukurasa mmoja baada ya mwingine kwa uchangamfu kama vipande vya matukio ya filamu. Maisha yale ya furaha niliyoyatumia kuwafundisha wanafunzi wangu wema kwa takriban miaka ishirini, na katika maeneo haya ambayo yalikuwa na uhai na furaha, sasa yamekuwa ni magofu. Nimetumia muda mwingi mbele ya mabango haya ya maisha yangu. Na hapo nikaanza kushangazwa na hali za watu wa dunia, vipi wanazihadaa nafsi zao, hali inaonesha wazi kuwa dunia hapana namna ni yenye kutoweka, na mwanadamu ni mpita njia tu na mgeni mwenye kuondoka. Na nikashuhudia kwa macho yangu kiasi cha ukweli wanaousema watu wa ukweli: (Msirubunike na dunia kwani ni yenye kuondoka, yenye vitimbi, yenye kutoweka). Na nikaona kuwa mwanadamu ana uhusiano na mji wake, nchi yake, bali na dunia yake kama alivyo na uhusiano na mwili wake na nyumba yake. Nilipokuwa nataka kulia kwa ajili ya uzee wangu - kwa kuzingatia uwepo wangu – nilitaka kulia kwa macho kumi si tu kwa ukongwe wa madrasa yangu, bali kwa kufa kwake, bali nilikuwa nikihisi haja ya kulia kwa macho mia kwa ajili ya mji wangu mzuri uliofanana na maiti. Kwa hakika imekuja katika hadithi tukufu kwamba Malaika ananadi kila asubuhi: (Zaeni kwa ajili ya mauti na jengeni kwa ajili ya kubomoka . Nilikuwa nikisikia ukweli huu, niliusikia kwa macho yangu mawili na si kwa masikio yangu, na kama hali yangu ilivyoniliza wakati huo, basi mawazo yangu tokea miaka ishirini yanachuruzikwa na machozi pia kila yanapopita katika hali hio. Naam, hakika kuteketea kwa nyumba hizo juu ya kilele cha ngome ambayo imejengwa maelfu ya miaka, na kuzeeka kwa mji ulio chini yake kwa muda wa miaka minane, mpaka umekuwa kama umepitiwa na miaka mia nane. Na kufa kwa madrasa yangu - chini ya ngome - iliyokuwa na uhai na ambayo ilikuwa makutano ya vipenzi, inaashiria kufa kwa madrasa zote za kidini ndani ya dola ya kiothmani na inabainisha utukufu wa kimaanawi wa jeneza lake kuu, kana kwamba ngome ambayo ni jabali moja gumu imekuwa shahidi wa kaburi lake. Na niliona kuwa wanafunzi wangu - Allah awarehemu wote - waliokuwa pamoja nami katika madrasa hio - kabla ya miaka minane - wakiwa wamelala katika makaburi yao, niliwaona kana kwamba wanalia pamoja nami, bali hata nyumba za mji ulioteketezwa zinashirikiana nami katika kulia na kuhuzunika, bali hata kuta zake zilizoanguka na mawe yake yaliyotawanyika. Naam, hakika nimekiona kila kitu kana kwamba kinalia, na hapo nikaelewa kuwa siwezi kuvumilia ugeni huu ndani ya mji wangu, nikafikiria kwamba ima niende kwenye makaburi yao au nijitenge kwenye pango katika mlima nikisubiri kifo changu, nikasema maadam duniani kuna mfano wa kiasi hiki cha utengano ambao hauwezi kuvumiliwa, wala kuzuiwa, nao ni wenye kuumiza na kuunguza kwa kiasi hiki, hapana shaka kuwa mauti ni bora kuliko uhai huu, na ni bora kuliko hali hizi zisizovumilika. Hivyo nimeelekeza uso wangu nikitazama kwenye pande sita. Sikuona ndani yake ila giza totoro. Mghafala unaotokana na maumivu hayo makali na kuathirika kwa kina vimenionyesha dunia ni yenye kutisha yenye kuogofya, na kuwa ni tupu kana kwamba itanidondokea juu ya kichwa changu. Roho yangu ilikua ikitafuta nukta ya kuegemea na nguzo imara mbele ya mabalaa na misiba isio na mipaka ambayo imechukua sura ya maadui wabaya. Na pia ilikuwa ikitafuta nukta ya msaada mbele ya matakwa yake yaliyojifichwa yasiyo na mipaka na yenye kuelekea milele. Wakati ambapo roho yangu inatafuta nukta ya kuegemea na inatafuta nukta ya msaada na inasubiri faraja kutokana na ghamu na huzuni zinazotokana na utengano usio na mipaka, uharibifu na vifo vikubwa, tahamaki ukweli wa aya moja ya Qur’an tukufu ya miujiza ambayo ni: سَبَّحَ لِلَّهِ مَا فِي السَّمَاوَاتِ وَالْأَرْضِ وَهُوَ الْعَزِيزُ الْحَكِيمُ ۞ لَهُ مُلْكُ السَّمَاوَاتِ وَالْأَرْضِ يُحْيِي وَيُمِيتُ وَهُوَ عَلَى كُلِّ شَيْءٍ قَدِيرٌ inadhihiri mbele yangu kwa uwazi na kuniokoa kutokana na mawazo hayo yenye kuumiza na yenye kutisha, na inaniokoa kutokana na maumivu ya utengano ikifungua macho yangu na uoni wangu. Nikayaelekea matunda yanayoning’inia juu ya miti yenye kutoa matunda nayo yakiwa yananiangalia kwa tabasamu tamu na yakiniambia: “Usielekeze mtazamo wako kwenye uharibifu pekee, tutazame na sisi kwa makini..” Naam, hakika ya ukweli wa aya hii tukufu unatanabahisha kwa nguvu ukikumbusha na unasema: Kwa nini inakuhuzunisha kiasi hiki kuanguka kwa utume uliosimamishwa na mwanadamu dhaifu juu ya ukurasa wa jangwa la (Van), mpaka ikachukua sura ya mji wenye kukalika? Kwa nini unahuzunika kutokana na kuporomoka kwake katika mkondo wenye kutisha unaoitwa ukoloni wa kirusi ambao umeondoa athari yake na maandiko yake? Nyanyua uoni wako kwa Al-Bari (Muumbaji) Mwenye kutia sura naye ni Mola Mlezi wa kila kitu na mmiliki wake wa kweli, kila kitu kipo mkononi mwake, na hakika maandiko yake (s.w) juu ya ukurasa wa (Van) yataandikwa upya kwa kuendelea kwa ukamilifu wa furaha, na hakika ulichokishuhudia katika hali za muda uliopita na kilio kwa kutokuwepo kitu katika maeneo hayo na kuteketea kwake na kubaki kwake patupu ni kutokana na mghafala kwa Mmiliki wake wa kweli, na kudhania kwa mwanadamu – kwa makosa – kuwa yeye ndiye mmiliki wake, na kutofikiria kuwa yeye ni mpita njia na mgeni na si vinginevyo.. Ukafunguka mlango wa ukweli mkubwa kutokana na hali hiyo yenye kuunguza, na kutokana na kosa hilo katika kufikiria, na nafsi ikajiandaa kuukubali – kama chuma kinachoingizwa motoni ili kilainike na kukipa muundo maalumu wenye manufaa – kwani hali hiyo ya kuhuzunisha na ya kuumiza ikawa ni moto wenye kuwaka ukalainisha nafsi. Qur’an tukufu ikaidhihirishia kweli nyingi za kiimani kwa uwazi kamili kupitia ukweli wa aya iliyotajwa mpaka ikaifanya ikubali. Naam, kama tulivyothibitisha katika (Andiko la Ishirini) na mfano wake katika risala, hakika ukweli wa aya hii tukufu –Shukrani kwa Allah – umetoa kwa baraka ya Imani nukta kubwa ya kuegemea, imetoa kwa roho na kwa moyo – kila moja kwa mujibu wa kinachodhihirika kwake miongoni mwa nguvu ya Imani inayoimiliki – ambapo inaweza kupambana na misiba hiyo na hali za kutisha hata zikiwa mara mia moja. Hiyo ni kwa sababu imekumbushwa kuwa kila kitu kimedhalilishwa kwa amri ya Muumba wako ambaye ni Mmiliki wa kweli wa mamlaka hii, funguo za kila kitu zipo mikononi mwake, na inakutosha kujinasibisha kwake (s.w). Baada ya kumtambua Muumba wangu, na kumtegemea, kila kitu kikaacha uadui unaouficha kwangu hata zile hali zilizokuwa zikinihuzunisha na kuniumiza, sasa zimeanza kunifurahisha. Na kama tulivyothibitisha katika risala nyingi kwa dalili za kukata shauri, hakika nuru inayokuja kutoka katika (Imani ya Akhera), vilevile imetoa “Nukta ya msaada” mkubwa sana mbele ya matumaini na matakwa yasiyo na mpaka, ambapo inaitosha nguvu hio si kwa matakwa hayo madogo ya muda na mafupi na wala si kwa mafungamano hayo na vipenzi vyangu duniani tu, bali inatosha pia kwa matakwa yangu yasiyo na mwisho katika nyumba ya milele na ulimwengu wa kubakia na katika furaha ya kudumu. Hiyo ni kwa sababu kwa udhihirisho mmoja katika madhihirisho ya rehema ya (Ar-RahmanAr-Rahim) husambazwa kwenye meza ya majira ya machipuo zisizokuwa na idadi miongoni mwa neema tamu juu ya mgongo wa ardhi ambayo ni nyumba miongoni mwa nyumba za ugeni wa dunia ya muda. Basi (s.w) huwapa katika kila majira ya machipuo wageni hao, na kuwaneemesha, ili aingize nyoyoni mwao furaha kwa masaa kadhaa, kana kwamba anawalisha chakula cha asubuhi, kisha anawachukua kuelekea nyumba zao za kudumu katika pepo nane za milele zilizojaa neema zisizo na mpaka kwa muda usio na mpaka ambazo ameziandaa kwa waja wake. Basi hapana shaka kuwa anayeamini rehema hii ya (Ar-RahmanAr-Rahim) na kuwa na utulivu kwayo akitambua kujiegemeza kwake kwa Allah (s.w), hapana budi atapata nukta ya msaada mkubwa ambapo daraja zake za chini zaidi zina matumaini yasiyo na mpaka na kuzidumisha. Na hakika ya nuru inayotokana na mwanga wa Imani – kwa ukweli wa aya hiyo – imedhihiri pia kwa udhihirisho wa wazi mpaka umeangaza pande hizo sita zenye giza kuwa kama mchana, na umeangaza vya kutosha hali yangu yenye kuhuzunisha na kuliza juu ya madrasa yangu hii na wanafunzi wangu, na vipenzi vyangu walioondoka ambapo imenizindua kuwa ulimwengu wanaokwenda vipenzi si ulimwengu wenye giza, bali wamebadilisha sehemu si vinginevyo, mtakutana na kukusanyika pamoja. Na kwa hivyo ikakata kilio moja kwa moja, na kunifahamisha kuwa nitapata mfano wa wao watakaochukua nafasi zao. Shukrani kwa Allah ambaye amehuisha madrasa ya Isparta mbadala wa madrasa ya (Van) iliyokufa na kuwa gofu, na kuhuisha vipenzi hivyo kimaana kwa walio wengi na bora miongoni mwa wanafunzi wema na vipenzi wakarimu. Na amenifundisha pia kuwa dunia si tupu iliyo wazi, na kuwa si mji ulioharibika na kuteketea, kama nilivyoidhania bali Mmiliki wa kweli - kama hekima yake inavyotaka – anabadilisha mabango ya muda na yaliyotengenezwa na mwanadamu kwa kuleta mabango mengine na kufanya upya risala zake. Basi kama matunda mapya yanavyochukua nafasi ya matunda yaliyochumwa basi vilevile kuondoka na utengano kwa wanadamu ni kuwa upya na kufanywa upya. Hivyo hakuleti huzuni yenye kuumiza kabisa kwa kukosekana vipenzi, bali inaleta kwa upande wa Imani huzuni yenye ladha tamu inayotokana na utengano kwa ajili ya kukutana katika nyumba nyingine ya furaha. Na pia imeangaza hali ya mshangao niliyokuwa nayo, na kuangaza kinachoonekana kwangu miongoni mwa uso wenye giza kwa vyote vilivyopo ulimwenguni, nikataka kuonesha himidi na shukrani kwa hali hiyo yenye kuangaza katika wakati wake kikanijia kipengele kifuatacho kwa lugha ya Kiarabu kikisawiri ukweli huo kikamilifu: (Alhamdulillahi kwa nuru ya Imani yenye kujengewa taswira ya yale yanayodhaniwa ni mageni, maadui, wafu, yasiozoeleka, mayatima, yenye kulia, kuwa ni vipenzi, ndugu, wenye uhai, wenye kuliwaza, wenye kuwepesisha mambo, wenye furaha, wenye kumtaja Allah na wenye kumsabih Allah). Inamaanisha kuwa: Ninatanguliza kwa Muumba mwenye utukufu himidi isiyo na mwisho, kwa kile alichonipa miongoni mwa nuru ya Imani ambayo ndio chimbuko la neema hizi zote za kiungu zisizo na mpaka, kwa kulibadilisha bango lile lenye kutisha ambalo lilidhihirishwa kwa nafsi yangu iliyoghafilika, mghafala – uliyotokana na ukali wa kuathirika na hali hiyo iumizayo – likaifanya idhanie kuwa sehemu ya vilivyomo ulimwenguni ni maadui au wageni na sehemu nyingine ni majeneza yenye kufazaisha yenye kushangaza, na sehemu nyingine ni mayatima wenye kulia ambapo hawana msaidizi wala mlezi. Nuru hiyo ilibadilisha kila kitu mpaka nikashuhudia kwa jicho la yakini kuwa wale walioonekana ni wageni, maadui; si vinginevyo ila ni ndugu na marafiki. Na yale yaliyokuwa yakidhihiri kama majeneza yenye kutisha; sehemu kati yake ni yenye uhai na yenye kutuliza, au ni kati ya waliomaliza wadhifa na majukumu yao. Na kuwa kinachodhaniwa kuwa ni vilio vya mayatima wenye kulia, ni sauti za dhikiri na visomo vya tasbihi. Yaani ninatanguliza himidi kwa Allah pamoja na vilivyomo vyote vyenye kuijaza dunia yangu binafsi ambayo inaenea dunia nzima. Ninavishirikisha pamoja nami katika himidi na tasbihi kwa Allah (s.w) kwa nia na kimawazo. Ambapo nina haki katika hilo, tunasema kwa pamoja kwa ulimi wa hali kila mmoja katika vilivyomo na kwa ulimi wa wote pia: (Alhamdulillahi kwa nuru ya Imani). Kisha hakika ladha za maisha na vionjo vyake ambavyo vilipotea kutokana na hali hiyo yenye kushangaza isababishayo mghafala, na matumaini yaliyojitoa moja kwa moja, kufifia na kuisha msaidizi wake, na neema na ladha zangu binafsi ambazo zimebaki katika duara dogo sana na huenda zimetoweka, zote hizo zimebadilika kwa nuru ya Imani – kama tulivyothibitisha hayo ndani ya Risala nyinginezo - . Nuru hiyo ikatanua duara hilo finyu pembezoni mwa moyo na kuwa ni duara pana sana mpaka ulimwengu wote ukaingia humo, na kujaalia nyumba ya dunia na ya akhera ni meza mbili zilizojaa neema, na kuzibadilisha kuwa meza mbili zenye rehema, badala ya neema hizo zilizoganda na kupoteza ladha yake katika bustani ya (Horhor). Hakutosheka na hayo tu bali amejaalia jicho, sikio, moyo na mfano wake wa viungo vya hisia bali viungo mia vya mwanadamu, kuwa ni mkono uliokunjuka kwa mujibu wa daraja za muumini kwenye meza mbili zilizojaa neema ambapo unaweza kuchukua neema na kuziokota kutoka sehemu zake zote. Hivyo nikasema yafuatayo mbele ya ukweli huu mkuu; shukrani kwa Allah kwa neema hizo zisizo na mpaka: (Alhamdulillahi kwa nuru ya Imani yenye kutoa taswira ya nyumba mbili zilizojaa neema na rehema, kila muumini ana haki ya kufaidika nazo kwa hisia zake nyingi zenye kudhihiri kwa idhini ya Muumba wake). Na hii inamaanisha kuwa: Alhamdulillahi kwa ambaye amenitunuku imani ambayo inaonekana kwa neema ya nuru yake kuwa dunia na akhera zimejaa neema na rehema, na inadhamini kufaidika na meza mbili hizo kubwa kwa mikono ya hisia zote zenye kudhihiri kwa nuru ya imani na zenye kukunjuka kwa nuru ya Uislamu kwa waumini wa kweli. Basi lau kama ningeweza kutanguliza himidi na shukrani kwa Allah Muumba wangu mbele ya Imani hiyo kwa chembe zangu ndogo zote za uwepo wangu na kwa ujazo wa dunia na akhera ningefanya. Maadam Imani inafanya katika ulimwengu huu mfano wa matokeo haya makubwa, basi hapana budi katika nyumba ya kubaki na ya milele ina matunda makubwa zaidi na nyongeza zilizo pana zaidi, kwa namna ambayo akili zetu za kidunia haziwezi kuelewa na kuzifahamu. Enyi ndugu zangu wazee wa kiume na wa kike, na enyi wenye kupata maumivu machungu kama mimi kwa kufarikiana na vipenzi wengi kwa sababu ya uzee! Mimi naichukulia nafsi yangu ni mzee zaidi yenu kimaana, hata kama inaonekana kuwa kati yenu yupo ambaye ni mkubwa zaidi kiumri kuliko mimi, hiyo ni kwa kuwa mimi ninapata – ukiachilia mbali maumivu yangu – maumivu ya maelfu ya ndugu zangu, kwa kile ninachobeba katika maumbile yangu miongoni mwa upole na huruma zilizozidi kwa watu wa jinsi yangu. Ninaumia kana kwamba ni mzee anayekaribia mamia ya miaka. Ama nyinyi vyovyote mtakavyopata maumivu ya utengano hamkupata kiasi cha niliyoyapata miongoni mwa mabalaa na misiba! Sina mtoto ninayemfikiria, isipokuwa ninahisi upole na maumivu – kwa siri ya huruma iliyojificha ndani yangu – kuelekea kwenye maumivu na misiba ya maelfu ya watoto wa Kiislamu bali ninahisi hata kwa maumivu ya wanyama wasio na hatia. Ongezea juu ya hilo kuwa ninaiona nafsi yangu - kwa upande wa wivu na Uislamu – imefungamana na nchi hizi bali na ulimwengu wa Kiislamu, na ninafungamana navyo kana kwamba ni nyumba yangu, japo similiki nyumba yangu binafsi hata niifungamanishe akili yangu nayo. Hivyo kwa hakika ninaumia kwa maumivu ya waumini ambao wapo katika nyumba hizi mbili na kuhuzunika sana kwa kuondoka kwao. Na ilivyokuwa nuru ya Imani imenitosheleza kikamilifu na taathira zangu zote zinazotokana na uzee wangu wote na mabalaa ya utengano zimenijia na kunipa tumaini lisilokatisha tamaa na mwanga usiozimika, na faraja isiyoisha. Hivyo hapana budi kuwa Imani pia itakutosheni mbele ya viza vinavyotokana na uzee, na mghafala unaokuja kutokana na viza hivyo, na kuathirika na kuumia kunakotokana nayo. Ni kweli hakika uzee mbaya zaidi ni uzee wa watu wa upotevu na ujinga, na utengano wenye maumivu zaidi ni utengano na maumivu yao!! Naam, hakika kuonja Imani inayoleta matumaini na kusambaza nuru na faraja, na hakika kuhisi faraja na ladha yake ni katika kuwa na hisia za kuabudu zenye kufaa kwa uzee na kuafikiana na Uislamu, na si kwa kuusahau uzee na kujifananisha na vijana na kuvamia mghafala wao wenye kulevya. Fikirieni daima na mzingatie hadithi tukufu: (Bora ya vijana wenu ni wale wenye kujifananisha na wazee wenu na shari ya wazee wenu ni wale wenye kujifananisha na vijana wenu) au kama alivyosema Mtume (s.a.w), yaani bora ya vijana wenu ni wale wenye kujifananisha na wazee katika kuwa makini, kuwa na heshima na kujiepusha na uovu, na shari ya wazee wenu ni wale wenye kujifananisha na vijana katika uovu na kuzama kwenye mghafala. Basi enyi ndugu zangu wazee wa kike na wa kiume! Imekuja katika hadithi tukufu ambayo maana yake ni (Rehema ya kiungu inaona aibu kuurejesha mkono wenye kunyenyekea kutoka kwa mzee muumini wa kiume au wa kike). Maadam rehema ya kiungu inakuheshimuni namna hii, basi iadhimisheni heshima yake kwa uja wenu kwa Allah (s.w).

§15

Mwanzoni mwa mwale wa nne ambao ni tafsiri ya aya tukufu: حَسْبُنَا اللّهُ وَنِعْمَ الْوَكِيلُ yamekuja yafuatayo kwa ufupi: Watu wa dunia waliponiweka mbali na kila kitu, nilijikuta katika aina tano za ugeni na wala sikuangalia kilicho ndani ya “Risale-i Nur” miongoni mwa nuru zenye kutoa faraja kutokana na mghafala uliosababishwa na uchovu na dhiki, moja kwa moja niliangalia moyo wangu na kufuatilia roho yangu, nikaiona kuwa ashiki yenye nguvu kabisa ya kutaka kubakia inanitawala na mapenzi makali ya kutaka kuwepo yalinidhibiti, na shauku kubwa ya kuishi inaniongoza.. pamoja na kilicho ndani yangu miongoni mwa kushindwa na ufakiri usio na mwisho. Ila kutoweka kunakotisha na kushangaza kuna zima kubakia huko. Nikasema kama alivyosema Mshairi anayeungulika moyoni: Hekima ya Mungu inahitaji kutoweka kwa mwili Na moyo ni wenye kupenda kuishi milele Nafsi yangu inahuzunika kutokana na balaa na majonzi Hata Luqman asingeweza kuipatia tiba Nikainamisha kichwa changu kwa kukata tamaa, tahamaki aya tukufu: inaniokoa ikisema: حَسْبُنَا اللّهُ وَنِعْمَ الْوَكِيلُ nisome vizuri kwa umakini na mazingatio, nikaisoma mara mia tano kila siku, kila nilipokuwa nikiisoma baadhi ya nuru na kheri zake nyingi zilikuwa zikidhihiri, nikaona kwa jicho la yakini - na si kwa elimu ya yakini - ngazi tisa za maana za hasbiya: Ngazi Ya Kwanza Ya Nuru Ya Hasbiyya: Hakika kilicho ndani yangu miongoni mwa kupenda kubaki, hakuelekei katika kubaki kwangu mimi bali katika kubaki kwa yule Mkamilifu asiye na mpaka na katika ukamilifu wake na kubaki kwake. Na hiyo ni kwa kuwepo kivuli cha dhihirisho katika madhihirisho ya jina katika majina yake matukufu na mazuri yasiyo na mpaka mwenye ukamilifu usio na mpaka. Naye ni mwenye kupendwa kwa dhati yake - yaani bila ya kuhitajia sababu - ndani yangu ila mapenzi haya ya kimaumbile yamepotea njia kwa sababu ya mghafala, na kushikamana na kivuli na nikapenda kubaki kwa kioo. Lakini haikuja aya: حَسْبُنَا اللّهُ وَنِعْمَ الْوَكِيلُ mpaka ikaondosha pazia. Nikahisi na kushuhudia, na nikaonja kwa haki ya yakini kuwa ladha ya kubaki na furaha yake ipo yenyewe, bali iliyo bora na kamilifu kuliko hiyo katika imani yangu na kujisalimisha kwangu na kuwa na yakini ya kubaki kwa Mwenye kubakia Mwenye ukamilifu, na kuwa yeye ni Mola wangu na Mungu wangu. Na hakika dalili za hili nimeziweka wazi kwa kina sana katika risala ya (Hasbiyya) katika nukta kumi na mbili “hivi.. na hivi.. na hivi...” na nikabainisha kuhisi kwa imani kunakomfanya kila mwenye hisia kuthamini na kupendezwa! Ngazi Ya Pili Ya Nuru Ya Hasbiyya: Hakika pamoja na kushindwa kwangu kusiko na mpaka kulikojificha ndani ya maumbile yangu, na uzee uliyo ndani yangu, na ugeni ule uliyonizungusha, na kutokuwepo msaidizi, na nimewekwa mbali na kila kitu na watu wa dunia wananishambulia kwa uadui wao na wapelelezi wao.. Katika wakati huu hasa niliongea na moyo wangu kwa kusema: (Hakika majeshi ni wengi wanamshambulia mtu mmoja dhaifu na mgonjwa aliyefungwa mikono au hana - yaani sina - sehemu ya kuegemea?). Na nikairejea aya: حَسْبُنَا اللّهُ وَنِعْمَ الْوَكِيلُ ikanifundisha: Kwamba unajiegemeza kupitia utambulisho wa imani kwa Mfalme Mkuu Mwenye uweza usio na mpaka, ambapo anaandaa kwa nidhamu kamili wakati wa machipuo nyenzo zote wanazozihitajia majeshi ya mimea na wanyama walioenea juu ya mgongo wa ardhi. Basi huwapa majeshi hayo yote yanayoundwa na aina laki nne za viumbe tofauti, na kugawa riziki zote za jeshi kubwa la viumbe hai - wakiongozwa na mwanadamu - si kwa namna alivyogundua mwanadamu katika kipindi cha karibuni miongoni mwa nyama na sukari zilizotengwa na vinginevyo, bali kwa namna kamilifu na bora zaidi bali zinaishinda mara mia moja. Hayo ni yaliyochaguliwa maalumu yanayokusanya aina zote za vyakula. Bali ni yenye rehema zile ambazo huitwa mbegu na viini, ukiongezea kuwa huyafunika hayo yaliyochaguliwa kwa funiko za kikadari zenye kuendana na kuiva kwake kukunjuka kwake na kukua kwake, na kuyahifadhi katika maganda na visanduku vidogo sana. Na visanduku hivi pia hutengenezwa kwa haraka sana, na kwa wepesi mno, na kwa wingi sana na hiyo ni katika maabara ya Kaaf na Nuun iliyo katika amri Kun, hata Qur’an tukufu inasema: فَإِنَّمَا يَقُولُ لَهُ كُن فَيَكُونُ Maadam umepata sehemu ya kuegemea mfano wa utambulisho huu wa imani, unaweza basi kuegemea na kutulizana kwa nguvu kubwa na uweza usio na mpaka. Na ni kweli nilikuwa nikihisi nguvu kubwa ya kimaanawi kila nilipokuwa nikipata somo hilo kutoka katika aya hiyo tukufu, nilikuwa nikihisi kuwa namiliki nguvu ambayo naweza kushindana na maadui zangu wote ulimwenguni na si tu waliyo mbele yangu. Hivyo nilirudia kutoka katika kina cha roho yangu: حَسْبُنَا اللّهُ وَنِعْمَ الْوَكِيلُ Ngazi Ya Tatu Ya Nuru Ya Hasbiyya: Maradhi, aina za ugeni, na dhulma tofauti zilipozidi niliona mahusiano yangu na dunia yakikatika, na imani iliniongoza kuwa wewe umeandaliwa kwa ajili ya dunia nyingine ya kudumu na una vigezo kwa ajili ya mamlaka ya kubaki na furaha ya kudumu. Katika wakati huu niliacha kila kitu chenye kuleta majuto na kunifanya nilie na nichoshwe, na nikayabadilisha kwa kila chenye kubashiria heri na furaha na kunifanya niwe katika shukrani daima. Lakini vipi lengo hili linaweza kutimia – ilhali ni lengo la kimawazo, roho, na matokeo ya maumbile – isipokuwa kwa uweza wa Mwenye uweza usio na mpaka ambaye anatambua harakati na kutulia kwa viumbe wake wote kwa kauli na vitendo bali anatambua hali na matendo yao na kuyasajili katika hali hiyo. Na vipi inaweza kutokea kwa mwanadamu huyu dhaifu mwenye kushindwa ila kwa uangalizi wake usio na mpaka hata amemkirimu, na kumfanya rafiki msemeshwa, akimtunukia daraja ya juu kati ya viumbe vyake. Naam, nilipokuwa nikifikiria nukta hizi mbili, yaani katika utendaji wa uweza huu usio na mpaka, na katika umuhimu wa kweli ambao Allah Muumba (s.w) amempa mwanaadamu anayeonekana ni duni, nilitaka kubainisha katika nukta mbili hizi ubainifu utakaodhihirisha imani na kuutuliza moyo. Basi kwa upande wangu nikairejea aya hiyo pia, ikaniambia: (Tazama kwa makini katika herufi ya “نا” kwenye neno “حسبنا”, na tazama ni kina nani hao wanaotamka neno hilo la “حسبنا” pamoja na wewe, iwe wanatamka kwa ulimi wa hali, au kwa kauli, wasikilize). Naam, aya imeniamrisha kama hivi ndivyo ilivyoniamrisha aya! Nami nikatazama, tahamaki nikaona ndege wengi mno, na wadudu wenye kuruka wadogo sana kama nzi kwa idadi isiyodhibitika, na wanyama wasiohesabika na mimea isiyoisha na miti isiyo na mwanzo wala mwisho vyote hivyo vinakariri kama mimi kwa ulimi wa hali maana ya حَسْبُنَا اللّهُ وَنِعْمَ الْوَكِيلُ Bali vinawakumbusha wengine kufanya hivyo.. kuwa wana wakili mzuri aliyoje anayesimamia maisha yao yote, hata anaumba kutokana na mayai yenye kufanana na yenye kuundwa kwa maada hizo hizo, anaumba kutokana na matone yenye kufanana, anaumba kutokana na nafaka ambazo zina kiini kimoja, anaumba kutokana na mbegu zenye kufanana aina laki moja za wanyama, na aina laki moja za ndege, na aina laki moja za mimea, na aina laki moja za miti, anaviumba bila ya kukosea, bila ya kasoro wala kuchanganya, anaviumba kwa mapambo ya kupendeza na vipimo na kwa nidhamu, pamoja na kutofautiana vyenyewe kwa vyenyewe, anaviumba kwa kuendelea hasa siku za msimu wa machipuo mbele ya macho yetu kwa wingi wa hali ya juu, na kwa wepesi mkubwa na kwa wingi. Basi kuumba viumbe vyote hivi vikiwa ni vyenye kufanana, kuingiliana, na kukusanyana kwa namna ile ile ndani ya ukubwa wa uweza huu usio na mpaka na hadhi yake, kunatudhihirishia kwa uwazi upekee wake (s.w) na upweke wake. Na aya imenifahamisha kuwa haiwezekani kuingilia kati kamwe katika matendo kama haya ya kiungu ya Bwana Mlezi yasiyo na mpaka na katika kusarifu kwa uumbaji huu, ambavyo vinaonesha miujiza hii isiyo na mpaka na kuisambaza. Kwa wale wanaotaka kufahamu utambulisho wangu binafsi na wa kiutu kama ilivyo kwa kila muumini.. na kwa wale wanaotaka kuwa kama mimi, ni juu yao kuangalia tafsiri ya nafsi yangu (أنا) katika wingi wa neno (نا) ndani ya aya tukufu na kuzingatia namna ya hali yake katika wingi huo. Na wafahamu ni nini uwepo wangu na mwili wangu unaoonekana finyu na fakiri hauna umuhimu wowote - ni kama uwepo wa kila muumini -?! Na watambue uhai wenyewe ni nini bali ubinaadamu ni nini?! Na nini Uislamu? Na nini imani ya kweli? Na nini kumjua Allah? Na vipi mapenzi ya Allah yanapatikana? Basi na wafahamu na wapate somo kwenye mambo hayo! Ngazi Ya Nne Ya Nuru Ya Hasbiyya Mambo yenye kutetemesha uwepo wangu mfano wa uzee, ugeni na maradhi na kushindwa kwangu, yamewafikiana na kipindi changu cha mghafala, kana kwamba uwepo wangu ambao ninashikamana nao kwa nguvu unaelekea katika kutokuwepo, bali uwepo wa viumbe vyote unatoweka na kuondoka. Kutoweka kwa vyote hivyo kumenisababishia wasiwasi mkubwa na mgongano wenye maumivu makali, nikairejea aya tukufu pia: حَسْبُنَا اللّهُ وَنِعْمَ الْوَكِيلُ Ikaniambia: (Zingatia maana yangu, na uiangalie kwa darubini ya imani) nami kwa upande wangu nikaiangalia maana yake kwa jicho la imani nikaona: Kuwa uwepo wangu ambao ni chembe ndogo sana - kama uwepo wa kila muumini – ni kioo cha uwepo usio na mpaka, na ni njia yakupata aina za uwepo usio na mpaka kwa ukunjufu usio na mwisho. Nao ni mfano wa neno la hekima linalotoa aina nyingi za uwepo zenye kubaki ambazo zina thamani zaidi ya uwepo wangu hadi kwamba muda mdogo wa uhai wake kwa upande wa kujinasibisha kwake na imani ni wa thamani sana, na una hadhi ya juu kama hadhi ya uwepo wa kudumu. Nikatambua yote hayo kwa elimu ya yakini, kwa sababu maarifa yangu ya hisia ya kiimani kuwa uwepo wangu huu ni athari katika athari za aliye wajibu kuwepo na ni ufundi katika ufundi wake na dhihirisho katika madhihirisho yake yamenifanya niokoke kutokana na giza lisilo na mpaka linaloletwa na dhana batili za kutisha, na kuondokana na maumivu yasiyo na mpaka yanayotokana na utengano usio na mwisho, na yamenisukuma kuweka mafungamano ya undugu thabiti kwa vilivyomo vyote na hasa kwa vilivyo na uhai, mafungamano kwa idadi ya matendo na majina ya kiungu yanayofungamana na vilivyopo. Na nikatambua kuwa kuna muungano wa kudumu kwa mafungamano haya na wote niwapendao katika vilivyopo kupitia utengano wa muda. Na kwa namna hii, hakika ya uwepo wangu ni kama uwepo wa kila muumini, amepata imani na kujiegemeza ambako ndani yake kuna nuru za aina za uwepo usio na mpaka hakuna utengano ndani yake. Hata kama uwepo wangu, hakika kubaki kwa aina hizo za uwepo baada yake kunatuliza uwepo wangu kana kwamba umebaki wenyewe kamili. Muhtasari: Kuwa mauti si utengano bali ni muungano na kubadili pahala na kuzalisha tunda lenye kubaki. Ngazi Ya Tano Ya Nuru Ya Hasbiyya Wakati fulani maisha yangu yalitikiswa na hali ngumu sana, mpaka yakaelekeza mtazamo wangu kwenye umri, na maisha, nikaona kuwa umri wangu unakwenda kwa kasi Akhera, na kuwa maisha yangu yenye kukaribia Akhera yanaelekea kuzimika chini ya dhiki kadhaa, lakini majukumu muhimu ya maisha na sifa zake nzuri na faida zake za thamani haziendani na kuzimika huku kwa haraka, bali kunaendana na maisha marefu, nikafikiria hili kwa maumivu na huzuni, nikarejea kwa ustadhi wangu aya tukufu: حَسْبُنَا اللّهُ وَنِعْمَ الْوَكِيلُ Ikaniambia: Angalia uhai kwa upande wa (Aliye hai, Msimamizi) ambaye amekutunuku uhai. Nikauangalia kwa darubini hii na nikaona kuwa: kama uhai una sura moja inayonielekea mimi, basi una sura mia moja zinazoelekea kwa (Aliye hai Mwenye kuhuisha), na kama una matokeo mamoja yanayorejea kwangu, basi una matokeo elfu moja yanayorejea kwa Muumba wangu; hivyo hakika kipindi kichache tu cha uhai, ndani ya upande huu unatosha sana, hapana haja ya muda mrefu. Ukweli huu unabainika kwa masuala manne; basi na watafute wale ambao wanataka kuishi au ambao si wafu, watafute ainisho la uhai, ukweli wake na haki zake za kweli ndani ya masuala hayo manne, wayapate na waishi. Na muhtasari ni kuwa uhai kila unapoelekea kwa Aliye hai, Msimamizi na kila imani inavyokuwa ni uhai wa uhai na roho yake unapata kubaki bali unatoa matunda yenye kubaki vilevile, bali unapanda daraja na kuwa juu kwa kiasi cha kupata udhihirisho wa umilele, na hapo hautazamwi ufupi wa umri na urefu wake. Ngazi Ya Sita Ya Nuru Ya Hasbiyya Kupitia mvi ambazo zinakumbusha utengano wangu binafsi, na kupitia matukio ya zama za mwisho ambayo yanajulisha kuteketea kwa dunia ndani ya utengano wa jumla wenye kukusanya na kupitia kudhihiri kusiko kwa kawaida mwishoni mwa umri wangu kwa hisia za uzuri na kuupenda na kupendezwa na makamilifu yaliyo ndani ya maumbile yangu. Kupitia yote haya nimeona kuwa kuondoka na kutoweka ambavyo daima huteketeza, na kuwa mauti na kutokuwepo ambavyo hutenganisha kwa kuendelea, viwili hivyo nimeviona vinaharibu kwa namna ya kutisha uzuri wa dunia hii tamu na kuharibu sura yake kwa kuivunjavunja, na kuharibu uzuri wa viumbe hivi. Nikaumia sana kwa niliyoyaona. Ashiki ya majazi ikachemka sana ndani ya maumbile yangu, ikaanza kushamiri kwa kukataa na uasi mbele ya hali hii iumizayo, sikuwa na budi ila kuirejea aya tukufu pia ili nipate kupumua na faraja, ikasema: “Nisome vizuri, na zingatia maana zangu” nami kwa upande wangu nikaingia kituo cha uchunguzi cha aya ya surat An-Nur: اللَّهُ نُورُ السَّمَاوَاتِ وَالْأَرْضِ Nikaangalia kutoka huko kwa darubini ya imani tabaka za mbali za aya ya Hasbiya na wakati huo huo nikaangalia kwa darubini ya hisia ya kiimani kwenye siri zake za ndani. Nikaona kuwa kama vioo, chupa, na vitu vyenye kuonesha na hata mapovu ya bahari vinavyodhihirisha uzuri anuai wa mwanga wa jua uliojificha, kila moja kati yao inadhihirisha uzuri tofauti wa rangi saba za mwanga huo. Na kila uzuri huo unapokuwa mpya kwa kufanyika upya kwa vitu hivyo na harakati zake na kwa mujibu wa ukubalifu wake tofauti na kwa mujibu wa kuvunjika kwake kwa namna tofauti, yaani kama inavyoonesha uzuri uliojificha wa jua na mwanga wake na rangi zake saba – kwa namna nzuri yenye kuvutia – vilevile kwa viumbe hivi vizuri na vilivyopo ambavyo vinachukua nafasi ya vioo vyenye kuakisi uzuri huo uliotakasika wa Mzuri Mwenye utukufu ambaye ni (Nuru ya Azali na Milele). Basi viumbe hivi huondoka bila ya kusimama vikifanya upya madhihirisho ya majina yake mazuri (s.w). Uzuri wa dhahiri kwa viumbe hivi sio milki ya dhati yake, bali ni ishara za uzuri mtukufu wa milele ambao unataka kudhihiri, na alama, ishara na madhihirisho ya uzuri huo uliotakasika wenye kudhihiri daima na ambao unataka kushuhudiwa na kushuhudisha. Na dalili za haya zimeelezwa kwa mapana ndani ya “Risale-i Nur” hasa risala ile inayoanza kwa “Hapa tutataja hoja tatu kwa ufupi sana na zenye kuingia akilini” . Mwanadamu yeyote atakayeitazama risala hii kati ya wenye kionjo kilichosalimika hawezi kujizuia bila ya kushangazwa na kuthamini bali ataona ni juu yake kuwanufaisha wengine baada ya kuifaidisha nafsi yake, na hasa nukta tano zilizotajwa ndani ya hoja ya pili. Hapana budi kwamba ambaye akili yake haijaharibika na moyo wake haukupatwa na kutu atasema kwa kukubali na kwa kufaa: Masha Allah.. Baraka Allah.. Na kuufanya uwepo wake ambao unadhihiri ukiwa ni fakiri na duni kuwa na hadhi ya juu na ataelewa kwa kusadiki kuwa: Ni muujiza uliofurutu kweli.

§16

Nilipokuwa chumbani Emirdağ mpweke katika kifungo cha lazima, macho ya upelelezi yalikuwa yakinifuatilia na kunisumbua muda wote, nilikuwa naadhibika sana na hali hiyo, mpaka nikachoshwa na maisha yenyewe na nikasikitika kwa kutoka kwangu jela, bali nilitamani kwa moyo wangu wote kurudi jela ya Denizli au kuingia kaburini, ambapo jela au kaburi ni bora zaidi kuliko aina hii ya maisha. Uangalizi wa kiungu ukanijia kuniokoa, ambapo mashine ya kunakili iliyodhihiri karibuni kwa wanafunzi wa Madrasatul Az-Zaharaa ambao wanabeba kalamu za almasi kama mashine ya kunakili. Risale-i Nur ikawa inadhihiri kwa nakala mia tano kwa kalamu moja. Ushindi huo ulioandaliwa na uangalizi wa kiungu kwa Risale-i Nur umenifanya nipende maisha hayo yenye tabu, bali umenifanya kukariri maelfu ya shukrani kwa Allah Muumba (s.w). Lakini baada ya kupita kipindi kifupi maadui waliojificha wa Risale-i Nur hawakuweza kuhimili ushindi huo wa kinuru, wakawazindua viongozi wa nchi dhidi yetu na kuwachochea dhidi yetu, na maisha - kwa mara nyingine tena -yakawa mazito yenye kuchosha, isipokuwa uangalizi wa kiungu ghafla ukadhihiri, ambapo viongozi wenyewe – ambao ni wenye kuhitaji zaidi Risale-i Nur – wakaanza kuisoma Risale-i Nur kwa shauku na kuitilia maanani, na hiyo ni kwa sababu ya wadhifa wao. Risala hizo kwa fadhila za Allah zikaweza kulainisha nyoyo zao na kuzifanya zizipende. Na kwa hiyo wigo wa madrasa za nuru ukaongezeka, ambapo walianza kuzipenda na kushangazwa nazo badala ya kuzikosoa. Matokeo haya yakatupa manufaa makubwa, kwani ni bora mara mia zaidi kuliko madhara ya kimaada tuliyokuwa nayo, na kuondosha hali ya wasiwasi na mkanganyo tuliokuwa nayo. Lakini hakikupita kipindi kirefu wanafiki – ambao ni maadui waliojificha - wakabadilisha mtazamo wa serikali kwenye haiba yangu, na kuelekeza mtazamo wao kwenye maisha yangu ya kisiasa yaliyopita, wakachochea dhana mbaya na mashaka, na wakaeneza hofu pembezoni mwangu katika Nyanja za mahakama, mamlaka za elimu (malezi), usalama, na wizara ya mambo ya ndani. Jambo lililowaongezea hofu hiyo ni kile kinachojiri miongoni mwa mapambano ya vyama vya kisiasa, na yanayochochewa na wafanya fujo na magaidi – ambao ni safu ya mbele ya wakomunisti – mpaka serikali ikaanzisha kampeni za kutuzuia na kutupa dhiki sana, ikazuia risala ilizoweza kupata, na hivyo harakati za wanafunzi wa nuru zikasimama. Na japokuwa baadhi ya maofisa walieneza propaganda za dhulma za ajabu ili kunijeruhi mimi na kunishutumu – kitu kisichoweza kusadikiwa na yeyote – isipokuwa hawakuweza kumkinaisha yeyote kwazo. Pamoja na hivyo waliniweka kituoni kwa muda wa siku mbili kwa hoja dhaifu na za kipuuzi sana, na kuniweka katika ukumbi mkubwa sana peke yangu katika masiku yenye baridi kali kama zamhariri, kwa kutambua kuwa sikuwa ni mwenye kuhimili baridi nyumbani kwangu ila kwa tabu na nilikuwa nikipambana nayo kwa kuwasha moto muda wote na kuwasha kitoajoto mara kadhaa kwa siku, na hiyo ni kwa sababu ya maradhi na udhaifu nilionao. Nilipokuwa nikigeukageuka kutokana na ukali wa homa iliyotokana na baridi, na kufurukuta kutokana na hali yangu ya kisaikolojia iliyodhikika sana, ikadhihiri katika nafsi yangu ukweli wa uangalizi wa kiungu na nikazinduliwa yafuatayo: Wewe umeipa jela jina la (Madrasa ya Yusuf), na (Jela ya Denizli) imekutunukieni faida na matokeo maradufu ya maradufu kuliko ilichokuonjesheni miongoni mwa dhiki na tabu, imekupeni furaha kubwa na faida nyingi za kimaanawi: Kupata faida kwa wafungwa wakiwa nanyi kutokana na Risale-i Nur, kusomwa kwa Risale-i Nur katika maeneo rasmi ya juu na faida nyingine kama hizo, mpaka ikakufanyeni kushukuru daima badala ya kulalama na kuteseka ikibadilisha kila saa katika masaa ya jela na dhiki kuwa masaa kumi ya ibada, na kuzidumisha saa hizo zilizotoweka. Madrasa hii ya tatu ya Yussuf pia - kwa idhini ya Allah - itatoa joto la kutosha kupambana na baridi hii kali, na itatunuku furaha itakayoondoa tabu hii nzito, kwa kufaidika watu wa masaibu na mabalaa pamoja nanyi kutokana na Risale-i Nur na nyoyo zao kupata faraja ndani yake. Ama wale uliowakasirikia, ikiwa ni kati ya waliohadaika na kudanganywa basi hawastahiki hasira, kwa kuwa wanakudhulumu bila ya kujua wala kuhisi, na ikiwa wanakuadhibu na kukazia ugomvi ilhali wanafanya hivyo kwa kujua na kwa chuki iliyojificha ili kuwaridhisha watu wa upotovu, basi na wao wataadhibiwa karibuni na mauti ambayo wanadhania ni kutoweka kwa milele, na wataiona dhiki kali ya kudumu katika jela ya upweke nayo ni kaburi. Na wewe kwa upande wako utapata thawabu kubwa – kutokana na dhulma yao – na utapata ushindi wa kudumu kwa saa zako zilizotoweka, na utapata ladha za kiroho ukiongezea na kutekeleza jukumu lako la kielimu na la kidini kwa ikhlasi. Hivi ndivyo maana hii ilivyokuja kwenye roho yangu nikasema kwa nguvu zote: (Alhamdulillahi). Na nikawaonea huruma madhalimu hao kwa uanadamu wangu na nikaomba: Ewe Mola wangu warekebishe.. Na kwa hakika nimethibiti katika kauli yangu niliyoiandika kwa wizara ya mambo ya ndani: Kuwa tukio hili jipya si la kisheria, na nikalithibitisha kwa namna kumi, bali madhalimu hawa wanaovunja sheria kwa jina la sheria wao ndio wahalifu hasa, ambapo wameanza kutafuta hoja dhaifu sana na kufuatishia uzushi wa kutengenezwa kiasi cha kuwasababisha wenye kusikia kuwadhihaki na kuwaliza watu wa haki waadilifu, na wakawadhihirishia waadilifu kuwa hawapati kwa jina la sheria na haki uthibitisho wowote wa kuzuia Risale-i Nur na kuwadhuru wanafunzi wake, hivyo wanaotea katika ujinga na wazimu. Mfano wa hilo: Wapelelezi ambao wamekuwa wakitufuatilia kwa muda wa mwezi hawakupata chochote dhidi yetu, hivyo wakatengeneza ripoti ifuatayo: (Mtumishi wa Saidi amemnunulia pombe kutoka dukani). Isipokuwa hawakuweza kupata yeyote wa kusadiki ripoti hii, isipokuwa mtu wa ajabu na mlevi wakati huo huo, wakamtaka yule mtumishi – kwa nguvu na kumtisha – asadikishe ripoti hiyo, akawajibu: Namuomba msamaha Allah nani awezaye kusadikisha uongo huu wa ajabu wakalazimika kufuta ripoti hiyo. Mfano mwingine: Kutokana na kuhitaji kwangu sana hewa safi na kutokana na maradhi yangu, mtu mmoja nisiyemjua – na sikuweza kumjua mpaka sasa - aliniazima rikwama lenye farasi, ili nitembee nayo nje ya mji, nilikuwa nikitumia saa au masaa mawili katika matembezi haya, na nilikuwa nimemuahidi mwenye rikwama na farasi kumlipa ujira wake vitabu vyenye thamani ya lira hamsini, ili nisiende kinyume na kanuni yangu niliyojiwekea, na ili nisiingie katika malalamiko na kumuudhi mtu yeyote, je kuna uwezekano wowote kupatikana madhara yoyote kutokana na jambo hili?! Isipokuwa polisi, mahakama, usalama wa ndani na hata mkuu wa mkoa mwenyewe waliniuliza zaidi ya mara hamsini: Farasi huyu ni wa nani? Na rikwama hili ni la nani? Kana kwamba limetokea tukio la kisiasa la hatari la kuvunja Amani na utawala! Jambo lililopelekea mtu mmoja kujitolea kudai kuwa farasi ni mali yake na mwingine akadai kuwa gari ni lake ili kumaliza maswali ya kipuuzi yenye kufuatana, ikatoka amri ya kukamatwa wawili hao na wakapelekwa pamoja nami jela. Kwa mifano kama hii tumekuwa tukiangalia michezo ya watoto na midoli yao, tukalia kwa kicheko na tukahuzunika kwa dhihaka, na tukaelewa kuwa kila anayezuia Risale-i Nur na wanafunzi wake anakuwa ni kichekesho na sehemu ya mzaha na dhihaka. Na moja ya mifano hiyo ni maongezi haya hapa: Nilimwambia mwendesha mashtaka mkuu kabla ya kuangalia kilichoandikwa katika kesi ninayotuhumiwa ya kuvunja Amani – nilimwambia: Nilikusema jana nilipomwambia askari mmoja ambaye alinihoji kwa niaba ya mkuu wa usalama: “Aniangamize Allah – mara tatu – ikiwa sijahudumia usalama wa nchi hii zaidi ya wakuu wa usalama elfu moja na zaidi ya waendesha mashtaka wakuu elfu moja..” Kisha katika wakati ambao nilihitaji zaidi kupumzika na kutotilia umuhimu matatizo ya kidunia na kujiweka mbali na baridi moja kwa moja, hakika kuwekwa uhamishoni na hawa - hasa wakati huu wa baridi kali – kutoka mji kwenda mwingine kwa namna inayovuka uvumilivu wangu, na kisha kunishikilia na kunipa dhiki zaidi ya uwezo wangu na kwa namna inayoashiria uwepo wa chuki iliyojificha na jambo la makusudi, yote hayo yamenisababishia chuki isiyo ya kawaida kwa watu hawa. Lakini uangalizi wa kiungu ukaniokoa na kuuzindua moyo kwenye maana hii: Hakika kadari ya kiungu – ambayo ni uadilifu mtupu – ina fungu kubwa sana kwa wanachokufanyia watu hawa miongoni mwa dhulma ya wazi, na kuwa riziki yako huko jela ndio iliyokupelekea kwenda jela, hivyo unapaswa kukabiliana na fungu hili kwa ridhaa na kujisalimisha. Na kwamba hekima ya kiungu na rehema yake pia ina fungu kubwa kama kufungua njia ya nuru na uongofu kwenye nyoyo za wafungwa na kueneza faraja na matumaini kwao, na kwa hiyo nyinyi kupata thawabu; hivyo inapaswa kutoa maelfu ya himidi na shukrani kwa Allah – kupitia subira – mbele ya bahati hii tukufu. Na pia nafsi yako ina fungu lake, ambapo ina kiasi isichotambua cha mapungufu.. hivyo unapaswa kukabiliana na fungu hili pia kwa kuomba msamaha, toba, na kurejea kwa Allah na kuilaumu nafsi kuwa inastahiki pigo hili. Kisha baadhi ya wafanyakazi ambao ni rahisi kurubunika, na woga ambao wanaelekezwa katika dhulma hiyo kwa vitimbi vya maadui waliojificha miongoni mwao wana fungu pia, Risale-i Nur imekulipia kisasi kamili kutoka kwa hawa wanafiki kwa mapigo ya kushangaza ya kimaanawi iliyowashushia. Basi mapigo hayo yanawatosha. Ama fungu la mwisho ni la wale wafanyakazi ambao ni watu wa kati kweli. Lakini kwa kuwa kwao wananufaika bila ya shaka kwa upande wa Imani wakitaka wasitake – wanapoiangalia Risale-i Nur na kuisoma kwao kwa nia ya kuijeruhi au kuikosoa, hakika kuwasamehe kwa mujibu wa kanuni وَالْكَاظِمِينَ الْغَيْظَ وَالْعَافِينَ عَنِ النَّاسِ ni wema na unyofu. Na baada ya kupata tanbihi na tahadhari hii ambayo yote ni haki na hakika, nikaamua kuendelea kusubiri na kushukuru kwa furaha katika madrasa hii mpya ya Yussuf. Bali niliamua kuiadhibu nafsi yangu kwa upungufu usiyo na madhara, nikawasaidia hata wale wanaonitendea vibaya na kunifanyia uadui. Kisha aliyekuwa katika umri kama wangu wa miaka sabini na tano, na mafungamano yake na dunia yameshakatika na hawajabaki katika marafiki zake ila watano katika kila watu sabini. Nakala sabini elfu za Risale-i Nur zinafanya kazi yake kwa uhuru kamili, na ina ndugu na warithi ambao wanatekeleza wadhifa wa imani kwa maelfu ya ndimi badala ya ulimi mmoja, hivyo kaburi kwa mtu kama mimi ni bora mara mia moja kuliko jela hii. Ukiachilia mbali kuwa jela hii ni yenye manufaa na raha zaidi kwa mara mia moja kuliko uhuru wa nje uliofungwa, na kuliko maisha chini ya utawala wa wengine; kwa sababu mtu anastahamili kwa kulazimika pamoja na mamia ya wafungwa kwa utawala wa baadhi ya viongozi; mfano, mkurugenzi na mkuu wa walinzi kutokana na wadhifa wao, na hivyo kupata faraja na ukarimu wa kiundugu kutoka kwa marafiki wengi waliomzunguka, wakati ambapo nje anahimili peke yake kuwadhibiti mamia ya wafanya kazi na viongozi. Na vilevile huruma ya Uislamu na maumbile ya mwanadamu huwa na rehema kwa wazee na hasa walio katika hali hii, na kubadilisha tabu ya jela na adhabu yake kuwa ni rehema pia.. Kwa sababu zote hizo nimeridhia kuwepo jela. Na nilipoletwa katika mahakama hii ya tatu nilikaa juu ya kiti nje ya mlango wa mahakama kwa sababu ya kile nilichokuwa nahisi katika tabu na dhiki ya kusimama kutokana na udhaifu, uzee na maradhi yangu. Na ghafla akaja hakimu na akasema kwa hasira pamoja na dharau: Kwa nini huyu hasubiri akiwa amesimama? Hasira ilichemka ndani yangu kwa kukosekana rehema kwa wazee, nikaangalia pembeni tahamaki kulikuwa na mkusanyiko mkubwa wa Waislamu ukituangalia kwa macho yaliyojaa huruma na nyoyo zilizojaa rehema na undugu, hata hakuweza yeyote kuwaondoa katika mkusanyiko huo, na hapa hakika mbili zikaja kwenye moyo wangu. Ya kwanza: Hakika maadui wangu na maadui wa nuru waliojificha wamewakinaisha baadhi ya wafanya kazi waliyoghafilika na kuwapeleka katika miamala ya kiudhalili kama hii ili waivunjevunje haiba yangu mbele ya macho ya watu, na kuondoa nisichokitaka miongoni mwa kuelekewa na kutazamwa na watu na kunikubali, kwa kudhani kuwa kwa kufanya kwao hivyo wataweza kuweka kizuizi mbele ya kuenea kwa ushindi wa nuru. Kwa udhalilishaji huo unaotokana na mtu mmoja uangalizi wa kiungu kwa ukarimu wake umeelekeza mtazamo wangu kwa hawa “mia moja” kwa ajili ya huduma ya kiimani ambayo Risale-i Nur inaitoa pamoja na wanafunzi wake ikisema: (Watazameni hawa, wamekuja ili wakukaribisheni kwenye huduma yenu hiyo, kwa nyoyo zilizojaa huruma, huzuni, upendo, na mafungamano thabiti). Bali hata katika siku ya pili nilipokuwa nikijibu maswali ya mkuu wa upelelezi; walikusanyika watu elfu moja uwanjani panapokabiliana na madirisha ya sehemu hiyo. Nyuso zao zilikuwa zikieleza hali yao, na zinasema: “Msiwabughudhi hawa”. Na kutokana na mafungamano yao thabiti na sisi, polisi walishindwa kuwatawanya. Na hapo ikaja moyoni mwangu: “Hakika ya watu hawa katika wakati huu mgumu, wanatoa faraja kamili, nuru isiyozimika, imani thabiti, na bishara ya kweli ya furaha ya daima, bali wanaitafuta kwa maumbile yao, na imegonga masikio yao kwamba wanachokitafuta kipo kweli ndani ya Risale-i Nur, hivyo wanaonesha heshima na kuthamini huku kwa mtu kama mimi – ambaye sina umuhimu wowote – kwa kiasi kinachovuka nguvu yangu, kwa kuwa kwangu ni mwenye kuhudumia imani, na huenda ikawa nimefanya chochote katika kuhudumia imani hiyo”. Hakika ya pili: Imekuja moyoni: Kuwa katika kutudhalilisha na kutudharau kwa hoja ya kuvunja usalama wa umma, na katika kuondoa kuelekea kwa watu kwetu kwa miamala duni ambayo watu wenye kuhesabika wenye ghururi ndio wanaofanya hivyo.. kwani hakika kuna makaribisho ya kusisimua na kupewa heshima stahiki kutoka kwa watu wa hakika na watoto wa kizazi kijacho. Naam, katika wakati ambao vurugu na ugaidi vinapamba moto vilivyojificha kwa pazia la ukomunisti kwa kuvunja usalama wa umma, hakika ya wanafunzi wa Risale-i Nur wanazuia uharibifu huo wa kutisha katika pande zote za nchi na kuvunja fitina yake kwa nguvu ya imani ya kusadikisha, na wanafanya juhudi kuweka usalama na nidhamu pahala penye hofu na vurugu. Ndani ya miaka ishirini iliyopita halikudhihiri tukio lolote la kuvunja kwao usalama, licha ya wingi wa wanafunzi wa Nuru na kuenea kwao pande zote za nchi, wakuu wa polisi hawakupata wala kusajili tukio lolote dhidi yao, katika wilaya kumi na katika mahakama nne zenye uhusiano, bali wakuu wa polisi wenye insafu katika wilaya tatu wamesema: “Hakika wanafunzi wa Nuru ni wakuu wa polisi wa kimaanawi kwa usalama katika nchi, wao wanatusaidia katika kulinda usalama na nidhamu kwa kufanya katika kila fikra ya anayesoma Risale-i Nur kwa imani ya hakika kuwa mlinzi, na kwa hivyo wanafanya juhudi ya kulinda usalama. Na jela ya Denizli ni mfano wa wazi na kielelezo kizuri cha maneno haya, hawakuingia wanafunzi wa nuru na risala ya “Matunda” iliyoandikwa kwa ajili ya wafungwa mpaka wakatubia zaidi ya wafungwa mia mbili na kujipamba na utiifu na kutengenea, na hayo ni ndani ya miezi mitatu au zaidi. Kiasi kwamba muuaji wa zaidi ya watu watatu alikuwa anachelea hata kuua kunguni. Hakuwa mwanachama asiye na madhara, bali amekuwa mwenye manufaa na mwenye huruma kwa nchi na watu. Wakuu wakawa wanaiangalia hali hii kwa tahayuri na kustaajabishwa, hadi baadhi ya vijana wakasema kabla ya kupokea maamuzi ya mahakama: “Wanafunzi wa Nuru wakikaa jela tutazihukumu nafsi zetu ili tubaki pamoja nao na kujifunza kutoka kwao na kuzitengeneza nafsi zetu kwa miongozo yao ili tuwe kama wao”. Basi wale ambao wanawatuhumu wanafunzi wa Nuru ambao wana sifa hizi kwa kuvunja usalama hapana shaka wamehadaika kwa namna iumizayo, au wamehadaliwa, au wameghafilika na mihimili ya serikali katika njia ya vurugu na ugaidi – ambapo wakijua au wasijue –hivyo wanafanya juhudi kutuangamiza na kutuadhibu. Basi tunawaambia: “Maadam mauti hayauwawi na kaburi haufungwi mlango wake, na misafara ya wanadamu katika ugeni wa dunia inapotea na kufichika chini ya mchanga kwa haraka mno.. hapana namna tutaachana karibuni, na mtaona malipo ya dhulma yenu malipo ya kutisha, na kwa uchache mtaonja mauti ambao ni ruhusa inayotokana na uhai kwa watu wa imani waliodhulumiwa, mtaonja kutoweka kwenu kwa milele, vionjo vyenye kutoweka mnavyovipata kwa kudhani kwenu kudumu duniani vitabadilika na kuwa maumivu ya kudumu yaumizayo. Hakika ukweli wa Uislamu ambao umma huu wenye dini umeupata na kuuhifadhi kwa damu za mamia ya mamilioni ya mashahidi wake ambao ni katika daraja la mawalii na mapanga ya mashujaa wenye kufanya jihadi ambao leo - kwa masikitiko makubwa - maadui zetu wanafiki waliojificha wanawaita kwa jina la (Madhehebu ya Kisufi) baadhi ya wakati, na kuidhihirisha Madhehebu ya Kisufi ambayo ni mwale mmoja katika myale ya jua hilo lenye kuangaza kana kwamba ni jua lenyewe ili kuharibu sura yake kwa baadhi ya wafanya kazi wa kawaida, wakiwaita wanafunzi wa Nuru ambao wanafanya juhudi na harakati ili kudhihirisha hakika ya Qur’an na hakika za imani jina la (Watu wa njia ya kisufi) au (Jumuiya ya Kisiasa) na hawataki chochote ila kuharibu sura yetu na uchochezi dhidi yetu. Basi tunawaambia hawa na kila anayewasikiliza, kauli yetu ambayo tumeisema mbele ya mahakama ya uadilifu ya Denizli: “Hakika ukweli uliotakasika ambao wameutolea muhanga mamilioni ya vichwa na kichwa chetu pia, lau kama mtaiwasha moto dunia juu ya vichwa vyetu, vichwa hivyo vilivyojitoa mhanga kwa ukweli wa Qur’an havitatii wala kusalimu uongozi kwa wazandiki na wala haitaacha kazi yake tukufu kwa idhini ya Allah”. Na kama hivi, sibadili mwaka mmoja wa uzee wangu ambao matukio yake yameanzisha kukata tamaa na mizigo mizito ambayo imeponywa na faraja safi inayotokana na imani na Qur’an, pamoja na kilicho ndani yake miongoni mwa maumivu na dhiki, kwa miaka kumi ya furaha ya maisha ya ujana wangu. Na hasa inapokuwa kila saa moja miongoni mwa saa za mwenye kutubu mwenye kutekeleza faradhi zake jela kwa hukumu ya saa kumi za ibada, na kuwa kila siku moja inayopita kwa mgonjwa akiwa amedhulumiwa inamfanya apate thawabu za siku kumi za milele, basi kiasi gani maisha kama haya yanakuwa sababu ya shukrani kwa Allah kwa mtu kama mimi ambaye anasubiria zamu yake akiwa mdomoni mwa kaburi. Naam, hili ndilo nililofahamu kutokana na tanbihi hiyo ya kimaanawi, nikasema: Shukrani kwa Allah bila ya ukomo.. Nikafurahia uzee wangu na nikaridhia jela. Ambapo umri hausimami bali unakimbia, basi ukienda kwa ladha na furaha basi huleta huzuni na majuto; Kwa sababu kuondoka kwa ladha kunaleta maumivu, na ukienda kwa mghafala usiyo na shukrani basi unaacha baadhi ya athari za dhambi na kutoweka na kuondoka. Lakini umri ukienda kwa tabu na jela, basi kwa kuondoka maumivu kunaleta ladha ya kimaanawi, na kuwa umri kama huu unazingatiwa ni aina ya ibada; hivyo unaendelea kubaki kwa upande mmoja, na kumfanya mhusika kufuzu umri wa milele wa matunda ya mazuri ya milele, na upande mwingine unakuwa ni kafara ya dhambi zilizopita na utakaso wa makosa yaliyasababisha kwenda jela. Hivyo kwa upande wa mtazamo huu kwa wafungwa ambao wanatekeleza faradhi wamshukuru Allah s.w na kuwa na subira.

§17

Waliponipeleka uhamishoni (Kastamonu) baada ya kukamilisha mwaka mmoja wa kuhukumiwa kwangu katika jela la (Eski Shehir) nami nikiwa ni mzee mkongwe, nilishikiliwa huko katika Kituo cha polisi kwa takribani miezi mitatu. Na ipo wazi kwenu ni kiasi gani cha madhara yanayompata mtu kama mimi katika maeneo haya, na hali ikiwa amejitenga na watu, wala hawezi kubaki hata na rafiki zake watiifu, wala hawezi kubadilisha nguo zake alizozizoea . Wakati ambapo kukata tamaa kulikokuwa kumenizunguka kila upande, tahamaki uangalizi wa kiungu unausaidia uzee wangu, ambapo polisi kituoni hapo wakawa ni marafiki watiifu, kiasi wakawa wananitoa kila nilipotaka kutembea pembezoni mwa mji wakanihudumia kama muhudumu yoyote binafsi, ukiongezea kwamba hawakunilazimisha kuvaa kofia kabisa. Kisha nikaingia katika Madrasa ya Nuru ambayo ilikuwa mkabala na kituo cha polisi huko (Kastamonu) na nikaanza utunzi wa risala, na (Faidhi, Amen, Hilmi, Swadiq, Nadhifu na Swalahuddin) na mfano wao katika mashujaa wa Nuru wakaanza kudumu katika Madrasa hiyo kwa ajili ya kueneza Risala na kuzikithirisha, na wakaonesha katika kumbukumbu zao za kielimu za thamani walizoziandika huko uwezo unaozidi kipindi nilichokitumia wakati wa ujana wangu na wanafunzi wangu waliyopita. Kisha maadui zetu waliojificha wakaanza uchochezi kwa baadhi ya viongozi na baadhi ya wanaojiona waliohadaika miongoni mwa wanazuoni na masheikh wa kisufi, wakawa ni njia ya kutukusanya katika Madrasa ile ya Yusuf (Jela ya Denizli) pamoja na wanafunzi wa Nuru wanaokuja kutoka wilaya kadhaa. Hii, ni kwamba ufafanuzi wa Tumaini hili la Kumi na Sita upo katika risala zile nilizozituma kwa siri kutoka (Kastamonu) na ambazo zimekusanywa katika kitabu (Mulhaq Kastamonu) na katika risala zilizotolewa kwa siri nilizozituma kwa ndugu zangu kutoka jela ya Denizli. Na ufafanuzi wake umekuja katika ‘Utetezi” uliyopelekwa mbele ya mahakama ya Denizli. Ukweli wa Tumaini hili unadhihiri kwa wazi humo tunaelekeza ufafanuzi huo uliyotajwa katika (Mulhaq) na (Utetezi) na hapa tunaashiria ishara fupi: Hakika nilizificha baadhi ya risala maalumu na mikusanyo muhimu na hasa zile zinazoongelea kuhusu Dajjali wa Waislam Sufyani na kuhusu karama za Risale-i Nur, nilizificha chini ya rundo la kuni na mkaa ili zisambazwe baada ya kufa kwangu, au baada ya masikio ya marais kusikia ukweli na kurejea katika usahihi wao. Nilikuwa nina utulivu wa akili katika kazi hii lakini tahamaki wapelelezi na wasaidizi wa mwendesha mashtaka wakaingia nyumbani na wakazitoa zile risala muhimu zilizofichwa chini ya rundo la kuni na mkaa basi wakanipeleka jela la (Isparta), nikiwa nasumbuliwa na maradhi. Na nilipokuwa nikipata maumivu makubwa na nikiwa nimezama katika kufikiria madhara yaliyoisibu Risale-i Nur, tahamaki uangalizi wa kiungu Bwana Mlezi unakuja kutuokoa sote ambapo viongozi ambao walikuwa na haja kubwa ya kuzisoma risala hizo zilizofichwa za thamani wakaanza kuzisoma kwa shauku kubwa, basi mikusanyiko hiyo rasmi ikageuka kuwa kile kinachofanana na madrasa za Nuru, ambapo ukosoaji wao ulibadilika na kuwa mtazamo wa kushangaza na kujali. Hadi kwamba katika jela la (Denizli) wengi wao wawe viongozi au wengineo waliisoma risala ya Al-Ayatul Kubra - bila ya sisi kujua - iliyochapishwa kwa siri kamili, Imani yao ikazidi na kuwa sababu ya msiba wetu kana kwamba haukuwepo. Kisha wakatupeleka katika jela la (Denizli) na kunitupa katika chumba kikubwa chenye harufu na unyevu mkali ukiachilia mbali baridi iliyo humo, ikanipata huzuni na maumivu makali kutokana na kupata majaribu kwa rafiki zangu wasio na hatia kwa sababu yangu, ukiongezea na huzuni iliyotokana na kile kilichoipata (Nuru) katika kusimama na kuzuiliwa pamoja na kile kilichokuwa kinanisumbua katika uzee na maradhi. Vyote hivyo vimenifanya nigugumie kwa huzuni na uchovu.. hadi uangalizi wa kiungu wa Bwana Mlezi ukaniokoa na ukaligeuza jela hilo la kutisha kuwa Madrasa ya (Nuru). Ni kweli hakika ya jela ni Madrasa ya Yusuf, na Risale-i Nur ikaanza kuenea ambapo mashujaa wa (Madrasa Az-Zahara) walianza kuandika risala hizo kwa karamu zao za almasi. Hadi kwamba Shujaa wa Nuru amenakili nakala zaidi ya ishirini kutokana na risala mbili za (Tunda) na (Ulinzi) katika kipindi kisichozidi miezi minne, pamoja na hali hiyo ya kikatili iliyomzunguka. Basi nakala hizo zikawa sababu ya ushindi ndani na nje ya jela. Ukabadilisha madhara yetu kuwa manufaa na kuibadilisha huzuni yetu kuwa furaha, akidhihirisha kwa mara nyengine siri miongoni mwa siri za Aya tukufu: وَعَسَى أَن تَكْرَهُواْ شَيْئًا وَهُوَ خَيْرٌ لَّكُمْ Kisha ikavumishwa taarifa kali dhidi yetu kutokana na ripoti ya juu juu ya kimakosa iliyopelekwa na (Wataalamu wa mwanzo) na waziri wa malezi akaelekeza mashambulizi makali dhidi yetu, kitu kilichopeleka baadhi kutaka sisi tunyongwe bali walifanya juhudi katika jambo hilo. Na katika wakati huu mgumu hasa, uangalizi wa kiungu wa Bwana Mlezi ulitujia na kututuliza pia, ambapo tulipokuwa tukisubiri ukosoaji mbaya kutoka kwa (Wataalamu wa Ankara) tahamaki zikaja ripoti zao zikiwa zimeambatana na kustaajabishwa na kuijali Risale-i Nur, na tahamaki hawakupata katika mkusanyiko wote wa masanduku matano ya Risale-i Nur isipokuwa makosa machache yasiyozidi kumi. Na kwa hakika tumebainisha mbele ya mahakama na tukathibitisha kuwa makosa haya waliyoyaleta sio makosa, bali ndiyo ukweli wenyewe na kwamba wataalamu wenyewe ndiyo wapo kwenye makosa kwa yale wanayoyadai na kukabainisha kuwa katika ripoti yao yenye karatasi tano takribani mna makosa kumi. Na tulipokuwa tukisubiri kitisho na amri kali kutoka ngazi saba rasmi ambazo zilitumiwa risala mbili ya (Tunda) na (Ulinzi) kama zilivyotumwa risala zote kwa Mamlaka ya Mahakama, na hasa zile risala maalumu zilizokusanya vipigo vikali na kuwazungumzia watu wa upotovu.. Ndiyo, wakati tukisubiri kitisho kikali kutoka kwao, tahamaki ikaja ripoti yao yenye kuliwaza ikiwa katika upole na ulaini ikifanana na risala zile alizotutumia waziri mkuu kana kwamba wanaonesha kutaka mapatano nasi. Yote haya - yakathibitisha kwa kukata shauri kuwa ukweli wa Risale-i Nur kwa fadhila za uangalizi wa kiungu na karama zake zimewashinda mpaka zikawafanya kuzisoma na kupata mwongozo kwazo, na kubadilisha mamlaka hizi rasmi pana kuwa kile kinachofanana na Madrasa za Nuru, na kuwaokoa wengi kati ya waliyotahayari na wenye kusita na kuimarisha imani yao, kitu kilichotupa faraja na furaha ni maradufu ya maradufu ya kile tulichokuwa tunasumbuka nacho katika dhiki na huzuni. Kisha maadui waliojificha wakaweka sumu kwenye chakula changu, akachukuliwa shujaa wa Nuru shahidi (Al-Hafidh Ally) kutokana na tukio hilo kuelekea hospitali badala ya yangu, na hivyo akaelekea katika ulimwengu wa Barzakh pia badala yangu, kitu kilichotupelekea kuhuzunika saana na kumlilia kilio kizito. Kwa hakika - siku moja kabla ya kututeremkia msiba huu - nilisema nikiwa katika mlima wa Kastamonu, bali nilipiga kelele mara kwa mara: enye ndugu zangu “Msitupe nyama mbele ya farasi wala majani mbele ya simba” kwa maana: Msitoe risala yoyote vyovyote iwavyo kwa kuhofia wasije kutufanyia ubaya. Kana kwamba ndugu (Al-Hafidh Ally) amesikia kwa simu yake ya kimaanawi maneno yangu haya akiwa umbali wa mwendo wa siku saba. Akaniandikia katika wakati huo huo akisema: “Naam ewe mwalimu wangu.. hiyo ni moja ya karama za Risale-i Nur na sifa zake za kipekee ya kwamba haimpi farasi nyama wala simba majani bali inampa farasi majani na simba nyama!” mpaka akampa msomi huyo risala ya (Ikhlasi), na baada ya siku saba tukapokea risala yake hii, tukaanza kuhisabu tukatambua kuwa ameandika ibara hiyo hiyo ya ajabu katika wakati niliyokuwa nikikariri juu ya mlima wa (Kastamonu). Basi kufa kwa shujaa wa kimaanawi mfano wa shujaa huyu miongoni mwa mashujaa wa Nuru, na wanafiki wanafanya juhudi ili watuteremshie adhabu ukiongezea wasi wasi wangu wenye kuendelea wa kunichukua kwa amri rasmi kuelekea hospitali kutokana na maradhi yangu yanayotokana na kupewa sumu.. Katika wakati huu na dhiki hizi zote zinazotuzunguka, tahamaki uangalizi wa kiungu unakuja kutusaidia, hakika dua safi iliyonyanyuliwa na ndugu zangu wema iliondoa hatari ya sumu. Na kuna alama nyingi zenye nguvu sana zinajulisha kuwa shujaa huyo Shahidi ameshughulika na Risale-i Nur kaburini mwake, na kwamba kwa risala hizo anayajibu maswali ya malaika. Na kwamba shujaa wa Denizli (Hassan Faidhi) - Allah amrehemu - na rafiki zake watiifu watachukua nafasi yake na kutekeleza jukumu lake katika kuihudumia Nuru kwa siri.. na kwamba maadui zetu wamekusanyika katika rai inayosema ulazima wa kutolewa kwetu jela kwa kuhofia kuenea kwa risala kati ya wafungwa na mwitikio wao wa haraka ili waweke kipingamizi baina yetu na wafungwa, na kwa hakika wanafunzi wa Nuru wamebadilisha faragha hiyo yenye kuchukiza kuwa mfano wa pango la watu wa pangoni, wale vijana waumini, au mfano wa mapango ya wenye kujitenga katika watu wa zuhdi, na wakafanya juhudi kwa utulivu kamili katika kuandika risala na kuzisambaza.. yote hayo yanathibitisha kuwa uangalizi wa kiungu ulikuwa ukitusaidia na kutuokoa. Na kwa hakika imekuja katika moyo: Maadam imamu mkuu (Abou Hanifa An-Numani) na mfano wake miongoni mwa maimamu Mujitahidina waliudhiwa kwa kuingizwa jela na wakavumilia mateso yake, na kuwa imamu (Ahmad Ibn Hambali) na mfano wake miongoni mwa Mujtahidina wakubwa wameadhibiwa mno kwa ajili ya suala moja miongoni mwa masuala ya Qur’an tukufu. Na wote walithibiti mbele ya mitihani hiyo mizito na walikuwa katika kilele cha uvumilivu, hakuna kati yao aliyeonesha huzuni na kulalamika, na hakuachana na suala lake alilolisema. Na vilevile wanazuoni wakubwa wengi na maimamu kadhaa hawakutetereka katu mbele ya maumivu na maudhi yaliyowashukia, bali walisubiri hali ya kumshukuru Allah (s.w), pamoja na kuwa balaa lililowashukia lilikuwa kubwa zaidi kuliko lililokushukieni nyinyi. Basi hapana budi kuwa mna deni la kumshukuru Allah (s.w) shukurani kubwa kwa mnayoyavumilia miongoni mwa adhabu chache na mashaka mepesi yaliyokushukieni katika njia ya hakika kadhaa za Qur’an tukufu pamoja na thawabu kubwa na ujira uliyoenea. Na nitabainisha hapa kwa ufupi moja ya madhihirisho ya uangalizi wa kiungu wa Bwana Mlezi kupitia dhulma waifanyao binadamu: Nikiwa na umri wa miaka ishirini nilikuwa nikisema kwa kukariri: Nitajitenga katika pango mwishoni wa maisha yangu, nikijitenga na maisha ya kijamii kama walivyokuwa wakijitenga wachamungu milimani. Vilevile niliamua nilipokuwa nimeshikiliwa mateka kaskazini mashariki mwa Urusi katika Vita ya Kwanza ya Dunia kutumia siku zilizobakia katika umri wangu katika mapango nikijitenga na maisha ya kijamii na kisiasa. Kumenitosha kuingilia kati ya mambo hayo.. Basi uangalizi wa kiungu wa Bwana Mlezi na uadilifu wa kadari – rehema kwa uzee wangu - vikadhihiri na vikabadilisha mapango hayo niliyokuwa nikiyajengea taswira kuwa ni kilicho bora zaidi ya hayo, na kwa namna inayozidi sana hitajio na uamuzi wangu.. vikayabadilisha na kuwa ni jela za kujitenga na upweke, na vikanipa (Madrasa za Yusuf) badala ya mapango hayo milimani kwa watu wenye kujitenga na watu wa mazoezi ya kiroho, ili wakati wetu usipotee bure kwa kuwa katika mapango hayo kuna faida za kiahera na zaidi kilicho ndani yake miongoni mwa kutekeleza jukumu la jihadi kwa ajili ya Qur’an na hakika za kiimani. Mpaka nikaazimia - baada ya kuachiliwa kwa ndugu zangu – kudhihirisha kitu kinachonibakisha katika chumba cha jela pamoja na (Husrev na Faidhi) na mfano wao miongoni mwa wajahidina wenye ikhlasi waliojitolea kwa ajili ya kuihudumia dini ili niifanye iwe hoja inayonitosheleza kutokana na kuchanganyika na watu na ili nisipoteze chochote katika wakati wangu kwenye mambo yasiyonihusu na kutengeneza na kupenda kuonekana, ambapo kubaki katika kizimba cha jela ni bora, isipokuwa kadari ya kiungu na riziki aliyoigawa Allah kwetu vimenipeleka katika sehemu nyengine ya kujitenga. Kulingana na madhumuni: (Kheri ipo katika kile alichokichagua Allah) na kwa siri ya aya tukufu: وَعَسَى أَن تَكْرَهُواْ شَيْئًا وَهُوَ خَيْرٌ لَّكُمْ na rehema kwa uzee wangu, na kwa ajili ya kufanya juhudi kwa shauku zaidi katika huduma ya kiimani, tumepewa jukumu na wadhifa, upo nje ya matakwa yetu na uwezo wetu katika hii (Madrasa ya Tatu ya Yusuf ). Naam, hakika katika kubadilisha uangalizi wa kiungu mapango ya kipindi cha ujana ambayo hayakuwa na maadui wakali, kuwa vizimba vya jela vyenye upweke, kuna hikima tatu na faida tatu muhimu kwa huduma ya Nuru: Hekima na faida ya kwanza: Kukusanyika kwa wanafunzi wa Nuru katika wakati huu bila ya yoyote kati yao kupata madhara huwa katika (Madrasa ya Yusuf) tu. Kwa kuwa kukutana kati yao nje kunaweza kuleta utata na kunahitajia matumizi, ambapo baadhi yao walikuwa wakitumia kiasi cha lira hamsini kwa ajili ya kukutana na mimi kwa muda usiozidi dakika ishirini, au walikuwa wakirejea bila ya kuweza kukutana na mimi. Hiyo ninavumilia dhiki za jela bali ninazikubali kwa furaha ili kukutana kwa karibu na baadhi ya ndugu zangu watiifu, basi jela kwa upande wetu ni neema na rehema. Hekima na faida ya pili: Ni kwamba hapana budi kutangaza na kulingania katika kila upande katika wakati wetu huu kuhusu kutoa huduma ya Imani kwa Risale-i Nur, na kuelekeza mitazamo ya wenye kuhitajia katika kila sehemu. Basi kuingia kwetu jela kunaelekeza mitazamo kwenye risala, na hivyo huwa kama kunazitangaza na hatimaye wakaidi na wenye kuhitaji kuzipata na kuvunja nguvu ya ukaidi wao na kuokoa Imani yao kutokana na risala hizo na kuokoka kutokana na kuangamia na kuenea kwa wigo wa Madrasa za Nuru. Hikima na faida ya tatu: Hakika wanafunzi wa nuru waliyoingia jela kila mmoja kati yao anatambua hali za mwingine, na kila mmoja kati yao anajifunza tabia njema, ikhlasi na kujitoa, hawajali baada ya hapo manufaa ya kidunia katika kuihudumia Nuru. Naam, hakika wao hupata taufiki ya kuwa na ikhlasi kamili kwa kile wanachokipata miongoni mwa alama nyingi zinazojulisha kuwa kila dhiki na mashaka ndani ya (Madrasa ya Yusuf) ina faida za kimaanawi na kimaada mara kumi yake, na matokeo mazuri na huduma pana safi za kiimani, bali huenda zikafikia mara mia moja zaidi, na hapo hawashuki kwa ajili ya kupata manufaa binafsi ya kisehemu. Kwa upande wangu, hakika sehemu za kujitenga na kupiga kambi kuna wema wa kuhuzunisha isipokuwa ni mtamu nao ni kama ifuatavyo: Mimi ninapata hapa hali nilizokuwa nikizipata siku za ujana katika kitongoji changu na Madrasa yangu ya zamani, ambapo chakula cha baadhi ya wanafunzi wa Madrasa - kwa mujibu wa taratibu za wilaya za mashariki - kinawajia kutoka nje ya madrasa na sehemu nyengine wanakipika kati yao ndani ya madrasa. Hivyo kila ninapotazama hapa - pamoja na hali nyengine zenye kufanana - ninakumbuka hali ile ya siku za ujana wangu kupitia majuto matamu hivyo ninakwenda kimawazo kwenye siku hizo, na ninasahau hali za uzee wangu. Andiko la Ishirini na Moja

Private reading note

This note stays on this device and is never uploaded to a server.

Up to 1,200 characters