Yirmi Beşinci Lem’a’nın Zeyli MAOMBOLEZO KWA MTOTO بِاس۟مِهٖ وَ اِن۟ مِن۟ شَى۟ءٍ اِلَّا يُسَبِّحُ بِحَم۟دِهٖ Bwana Mwenye kuhifadhi “Khalid”, ewe kaka yangu mpendwa wa Akhera! وَبَشِّرِ الصَّابِرٖينَ اَلَّذٖينَ اِذَٓا اَصَابَت۟هُم۟ مُصٖيبَةٌ قَالُٓوا اِنَّا لِلّٰهِ وَاِنَّٓا اِلَي۟هِ رَاجِعُونَ Ewe ndugu yangu! Hakika nimeumizwa sana na habari ya kifo cha mtoto wenu, lakini: Hukumu ni ya Allah, na kuridhia maamuzi na kadari yake ni katika alama za Uislamu. Namuomba Allah (s.w) akuruzukuni subira njema, na akujaalieni marehemu kuwa ni hazina huko Akhera, na mwombezi siku ya kiama. Na tutakubainishieni na waumini wengine wachamungu mfano wa nyinyi “Nukta Tano” zenye kueneza bishara njema na kudondosha matone ya maliwazo ya kweli kwenu.
Source text is preserved. When a suitable model is available, translation is displayed separately.
Mektubat
The Seventeenth Letter
Hakika maana ya aya tukufu: "وِلْدَانٌ مُّخَلَّدُونَ" na siri yake ni kama ifuatavyo: Hakika watoto wa waumini waliokufa kabla ya kubaleghe watadumishwa peponi wakiwa ni watoto wapendwa kwa namna inayoendana na pepo. Na watakuwa chimbuko la furaha kwa baba na mama zao ambao wameenda peponi. Na watakuwa ni kituo cha kupata vionjo vya milele vizuri zaidi kwa wazazi wao ambavyo ni kupenda watoto na kucheza nao. Na kwa kuwa kila kitu kitamu kipo peponi, hakuna usahihi wa kauli ya anayesema: “Hakuna mapenzi ya watoto na kucheza nao peponi kwa sababu ya kukosekana humo kuzaana”. Bali huko kuna ushindi mkubwa katika kuwapenda watoto na kucheza nao kwa usafi na ladha kamili kipindi chote cha mamilioni ya miaka, bila ya kuchanganyika na maumivu au huzuni, badala ya kuwapenda na kucheza nao katika miaka kumi mifupi ya dunia yenye kutoweka na yenye kuchanganyika na maumivu. Yote haya yanahakikishwa na aya tukufu kwa sentensi وِلْدَانٌ) (مُّخَلَّدُونَ na kuwa ni sehemu kuu ya furaha ya waumini na kutoa bishara njema kwao.
Siku moja alikuwepo mtu mmoja mkarimu jela, mwanawe pia akaletwa hapo baada yake. Akawa anaumia sana kwa taabu za kushindwa kumweka salama mwanawe ukiachilia mbali kuteseka na maumivu yake binafsi. Mtawala mwenye huruma akamtuma mtu kumfikishia: “Kwamba mtoto huyo hata kama ni mwanao ila ni mmoja wa wananchi wangu, nitamchukua ili nimlee katika kasri zuri kubwa”. Yule bwana akaanza kulia na kuvunjika moyo na akasema: “Hapana. Hapana, simtoi mtoto wangu kwani ni sehemu ya faraja yangu”. Rafiki zake wakapingana naye jela: Eh bwana wee! Hakuna haja ya kuhuzunika wala maana ya kuumia kwako. Kama unaumia kwa ajili ya mtoto, basi ataenda katika kasri pana badala ya jela hii chafu yenye harufu mbaya na finyu. Na kama unaumia kwa ajili ya nafsi yako, na kutafuta manufaa yako binafsi, basi hakika ya mtoto huyo atateseka na mashaka mengi pamoja na maumivu makali ikiwa atabakia hapa kwa ajili ya wewe kupata manufaa ya muda mfupi na yenye shaka! Ama akienda huko atakuwa ni njia ya manufaa elfu moja kwako, hiyo ni kwa sababu atakuwa ni sababu ya wewe kupata rehema ya Mtawala, na atakuwa katika hukumu ya mwombezi. Na hapana budi kwamba Mtawala siku moja atataka kumfurahisha kwa kukutana na wewe, na hapana shaka kwamba hatomtuma kwako jela, bali atakuchukua wewe na kukutoa jela na kukupeleka katika kasri lile ili upate bahati ya kukutana na mtoto huyo, ukiwa tu ni mwenye kumtii na kumwamini. Na kupitia mwanga wa mfano huu – Ewe kaka yangu mpendwa – waumini mfano wako wanapaswa kufikiri pale wanapofiwa na watoto wao, na waseme: Hakika mtoto huyu hana hatia, na Muumba wake ni Mwenye rehema Mkarimu, badala ya huruma yangu pungufu kwake, na badala ya malezi yangu pungufu kwake, rehema ya kiungu imemkumbatia, kugubikwa na uangalizi wa kiungu ndani ya hifadhi yake tukufu, na imemtoa katika jela la taabu, mashaka na maumivu ya kidunia na kumpeleka katika vivuli vya pepo ya Firdausi yake tukufu. Basi hongera kwa mtoto huyo! Na nani anatambua nini angelikuwa anafanya na vipi angelikuwa anatenda lau angelibakia duniani? Kwa hiyo mimi si mwenye kuumia kwa ajili yake, bali namwona ni mwenye furaha na mwenye bahati. Ama kuumia kwangu kwa ajili ya nafsi yangu mwenyewe, siumii sana kwa ajili yake, kwa yale yanayohusu kustarehe kwangu. Kwa kuwa kama angelibakia duniani angenipa mapenzi ya watoto na kucheza nao kwa muda mfupi wa miaka kumi ikiwa imechanganyika na maumivu, na huenda lau angelikuwa mwema mwenye kutii, na akawa ni mwenye uwezo katika mambo ya kidunia angeliweza kunisaidia na kushirikiana na mimi, isipokuwa kwa kufa kwake amenihakikishia mapenzi ya watoto na kwa miaka milioni ishirini na katika pepo ya kudumu, na amekuwa ni mwombezi wangu ili kuingia katika furaha ya milele. Basi siwezi kuumia sana kwa ajili yake hata kwa ajili ya nafsi yangu vilevile. Kwa sababu atakayepoteza manufaa ya haraka yenye mashaka, na kufuzu manufaa elfu moja yenye kuchelewa yaliyo na uhakika wa kutokea, hatodhihirisha huzuni zenye kuumiza, na hatolia kwa kukata tamaa abadan!
Kwamba mtoto aliyekufa kwa hakika ni kiumbe cha Muumba Mwenye rehema, na mja wake, na kwa hali zake zote ni mwenye kutengenezwa katika vitengenezwa vyake (s.w) na rafiki aliyetunukiwa kwa wazazi kutoka kwake, ili abaki chini ya uangalizi wao kwa muda fulani. Na Allah (s.w) amewafanya mama na baba yake kuwa ni watumishi waaminifu kwake, na akampa kila mmoja kati yao huruma yenye ladha, ujira wa haraka kwa ule utumishi wanaoufanya. Na sasa, hakika ya Muumba Huyo Mwenye rehema ambaye ndiye Mmiliki wa kweli wa mtoto – na ana sehemu mia tisa na tisini na tisa na moja tu ni ya baba yake – ikiwa atamchukua mtoto huyo kulingana na rehema na hekima yake kutoka kwako akimaliza utumishi wako kwake. Basi haiendani na watu wa Imani kuhuzunika hali ya kukata tamaa na kulia kwa makelele kwa namna ambayo inaashiria kushtaki mbele ya Mola wao wa haki Mwenye sehemu elfu moja, mkabala na sehemu moja. Hii si vinginevyo ila ni hali ya watu wa kughafilika na upotevu.
Lau dunia ingelikuwa ya milele na milele, na mwanadamu humo angelikuwa wa milele na milele, au lau utengano ungelikuwa wa milele, basi huzuni ya kuumiza na kukata tamaa kungelikuwa na maana fulani. Lakini maadamu dunia ni nyumba ya ugeni basi popote alipoenda mtoto aliyekufa basi sote - sisi na nyinyi - pia tunaelekea huko hakuna namna. Kisha hakika ya umauti huu si maalumu kwake pekee, bali ni njia ambayo watu wote wataipita. Na kwa vile utengano si wa milele vilevile, bali kukutana kutatimia katika masiku yajayo katika Barzakh na peponi, hivyo tunapaswa kusema: Hukumu ni ya Allah, hakika ni cha Allah akichukuacho na akitoacho, pamoja na kutaraji, kuwa na subira njema, na kushukuru tukisema: Sifa zote njema ni za Allah kwa kila hali.
Hakika ya huruma ambayo ni dhihirisho zuri zaidi miongoni mwa madhihirisho ya rehema ya kiungu, ni iksiru (ufumbuzi) yenye nuru. Nayo ni tendaji zaidi ya upendo, nayo ni njia ya haraka zaidi ya kufika kwa Al-Hakki (s.w). Naam, kama ilivyo ashiki ya kisitiari na ashiki ya kidunia, kwa matatizo mengi sana, inageuka kuwa “ashiki ya kweli”, mwenye kuwa nayo anampata Allah (s.w). Vilevile huruma, lakini bila ya matatizo, inaifungamanisha moyo na Allah (s.w) ili kumfikisha mwenye huruma hiyo kwa Allah (s.w) kwa njia fupi zaidi na kwa namna safi. Na mzazi wa kiume na wa kike ni sawa, wote wanampenda mtoto wao penzi la ujazo wa dunia yote, anapochukuliwa mtoto kwa yeyote kati yao basi hakika yeye - kama ni mwenye furaha na ni katika watu wa Imani – atageuza uso wake mbali na dunia na kuipa mgongo na kumpata Mneemeshaji wa kweli amehudhuria atasema: Maadamu dunia ni yenye kutoweka, haistahiki kuufungamanisha moyo nayo, anapata kupitia yale aliyopitia mtoto wake uhusiano thabiti na kufuzu hali ya kimaanawi ya hadhi ya juu. Hakika watu wa kughafilika na upotevu wamezuiwa kupata furaha ya hakika hizi tano na bishara zake. Basi pimeni katika yajayo upeo wa hali yao yenye kuumiza; mama mzee anapomshuhudia mtoto wake wa pekee ambaye anampenda penzi la kweli, akigeuka-geuka katika hali za sakarati, fikra zake haraka zinaelekea katika kulazwa kwake ndani ya udongo wa kaburi badala ya kitanda chake laini chenye kustarehesha, kwa kule kusawiri kwake umauti kuwa ni kutoweka na utengano wa milele, kwa kudhania kwake kudumu duniani na matokeo ya mghafala na upotevu, kwa hiyo haipiti katika akili yake rehema ya Mwingi wa rehema Mwenye kurehemu wala pepo yake wala neema ya Firdausi yake ya kudumu... Basi wewe unaweza kupima kutokana na hayo kiasi cha wanachougua watu wa upotevu na mghafala miongoni mwa maumivu na huzuni yenye kukata tamaa bila ya mng’ao wa tumaini. Wakati ambapo Imani na Uislamu nazo ni njia mbili za furaha ya nyumba mbili zinamwambia muumini: Hakika ya mtoto huyu ambaye anataabika na sakarati za umauti Muumba wake atampeleka katika pepo yake tukufu baada ya kumtoa katika dunia hii mbaya, ongeza juu ya hilo kuwa atamfanya mwombezi wako, kama atakavyomfanya pia kuwa ni mtoto wako wa milele... Kwa hiyo usijali wala kuhuzunika. Utengano ni wa muda mfupi tu. Basi subiri ukisema: Hukumu ni ya Allah. اَل۟حُك۟مُ لِلّٰهِ اِنَّا لِلّٰهِ وَاِنَّٓا اِلَي۟هِ رَاجِعُونَ اَل۟بَاقٖى هُوَ ال۟بَاقٖى Mwenye kubaki, Ndiye Mwenye kubaki! Said Nursî

