بِسْمِ اللّٰهِ الرَّحْمٰنِ الرَّح۪يمِ اَلَّذٖينَ يُؤ۟مِنُونَ بِال۟غَي۟بِ Namna imani inavyomea mbegu ya peponi na ukafiri kumea mbegu jahanamu. Kama unataka kuifahamu furaha na neema kubwa ni ipi, na fadhila zipi na neema zinazopatikana katika kumuamini Allah, basi sikiliza kisa kinachokujia kwa njia ya mfano: Wakati fulani, watu wawili walikuwa katika safari ya starehe na biashara. Mmoja alitoka kuelekea upande wa kibinafsi na usio mwema, na mwingine katika njia ya kiungu, ya neema. Yule mtu mbinafsi alikuwa mwenye kujiona, mbinafsi, asiye na rajua, akaishia mahali palipoonekana, kwa kukosa kwake rajua, kuwa ilikuwa nchi mbaya zaidi. Aliangalia kila mahali na akawaona watu dhaifu na wasio na bahati njema wakilalamika mikononi mwa mwasi katili wa kutisha, wakilia kwa mateso yao. Popote alipokwenda aliona hali za kuhuzunisha na za kuumiza. Nchi nzima ilionekana kama nyumba ya maombolezo. Mbali na kuwa mlevi, hakupata njia yoyote ya kutoona hali hii ya kuhuzunisha na ya majonzi. Kila mmoja alimwona ni adui na mgeni, na kila mahali palipomzunguka aliona maiti za kutisha na yatima wenye kukata tamaa na kulia. Ufahamu wake ulikuwa katika hali ya adhabu. Yule mtu mwingine alikuwa mtu wa Mungu, mchamungu, mwenye akili njema tena mwenye murua na nchi aliyokwenda ilikuwa bora kwa mtazamo wake. Mtu huyu mwema aliona furaha iliyoenea katika ardhi aliyoingia. Kila mahali kulikuwa na sherehe ya furaha, mahali pa kumkumbuka Allah palipofurika furaha; kila mtu kwake alionekana rafiki na jamaa. Katika nchi nzima alikuta sherehe ya kuondoshewa majukumu kiujumla kulikoambatana na vilio vya sauti za kutakiana mema na shukrani. Pia alisikia sauti ya ngoma na bendi kwa ajili ya kuandikisha askari kwa wito wa furaha wa “Allah ni Mkubwa Kabisa! na “Hapana wa haki kuabudiwa isipokuwa Allah!” Badala ya kuhuzunika kwa mateso yake na ya kila mwingine kama yule mtu wa kwanza mwenye taabu, mtu huyu mwenye bahati, alifurahishwa kwa kufurahi yeye mwenyewe na wakazi wote. Zaidi ya hayo, aliweza kufanya biashara ya faida. Alimshukuru Allah. Baada ya muda alirejea na kukutana na yule mtu mwingine. Alifahamu hali yake na kumuambia: “Ulitokwa na akili, ubaya ulio ndani mwako umeakisiwa kwenye dunia ya nje kiasi kwamba ulidhani kuwa kicheko ni kilio, na kuondoshewa majukumu kuwa ni kufukuzwa kazi na kuporwa. Zinduka na utakase moyo wako barakoa la majanga haya liondolewe machoni mwako na uweze kuona ukweli. Kwa nchi yenye mfalme mwadilifu, mwenye huruma, mkarimu, mwenye uwezo, mpenda utaratibu na mwema hawezi kuwa kama ulivyofikiri, wala nchi iliyoonesha idadi hii ya dalili za waziwazi za mafanikio na maendeleo.” Yule mtu asiye na furaha alizinduka baadaye na kutubu. Akasema: “Ndiyo niliwehushwa na kinywaji. Ninamwomba Allah awe radhi nawe, umeniokoa kutoka katika hali mbaya kabisa.” Ewe nafsi yangu! Tambua kuwa mtu wa kwanza anamwakilisha kafiri, mtu aliyekengeuka au asiye mtiifu. Kwa mtazamo wake, dunia ni nyumba ya maombolezo. Viumbe wote ni yatima wanaolia kwa mapigo ya mauti na utengano. Mwanadamu na wanyama ni wapweke na bila ya mafungamano kuchanwa chanwa na kucha za saa teule. Viumbe vyenye nguvu kama vile milima na bahari vinashabihiana na mizoga ya kutisha isiyo na uhai. Madanganyo mengi ya kutisha kama haya hutokana na ukafiri wake na upotevu, na kumtesa yeye. Ama kuhusu mtu yule mwingine, yeye ni muumini. Anamtambua na kumshuhudia Allah (s.w), kwa mtazamo wake dunia hii ni makazi ambapo majina ya Mmoja Mwingi wa Rehema husomwa bila kukoma, mahali pa maagizo kwa mwanadamu na wanyama, na eneo la mtihani kwa mwanadamu na majini. Vifo vyote vya wanyama na wanadamu ni ruhusa ya kuondoka. Wale waliokamilisha majukumu yao ya maisha huondoka kutoka dunia ya mpito na kwenda nyingine ya furaha isiyo na matata ili kuwaruhusu maafisa wapya waje na kufanya kazi. Kuzaliwa wanyama na wanadamu kunafanya kuorodheshwa kwao jeshini, kuchukuliwa jeshini na kuanza majukumu yao. Kila kiumbe hai ni askari wa kawaida mwenye furaha, afisa mwaminifu, aliyetosheka. Sauti zao zote zitakuwa ni ima zenye kumtukuza Allah na kuutaja utajo wake mwanzoni mwa kutekeleza majukumu yao na shukrani pamoja na furaha wakati wa kumaliza kazi, au ni nyimbo zinazotokana na furaha zao wakiwa kazini. Kwa mujibu wa mtazamo wa muumini viumbe wote ni watumishi wenye amani na urafiki baina yao, pia ni maafisa wa amani, pia ni vitabu vyenye kuwafikiana kutoka kwa Mola wake mkarimu mno na Mmiliki mwingi wa rehema. Nukta nyingi za ukweli, pambanuzi, tukufu, za kufurahisha na nzuri kama hizi zinadhihirika na kujitokeza katika imani yake. Maana yake, kumuamini Allah kunabeba mbegu ya ambacho ni mti wa Tuba wa Peponi, wakati ambapo ukafiri unaficha mbegu ya mti wa Zakkum wa Jahanamu. Hivyo, uokovu na usalama utapatikana kwenye Uislamu na imani tu, ambapo tunapaswa kuendelea kusema: اَلْحَمْدُ لِلّٰهِ عَلَى دِينِ اْلاِسْلاَمِ وَ كَمَالِ اْلاِيمَانِ
Source text is preserved. When a suitable model is available, translation is displayed separately.
Sözler
The Second Word
Source: risaleinur multilingual dataset, risale.site source · Risale-Nur multilingual research corpus

