بِسْمِ اللّهِ الرَّحْمنِ الرَّحِيمِ يَا اَيُّهَا النَّاسُ اعْبُدُوا Faida na furaha ipo ndani ya ibada. Kama mnataka kufahamu namna ibada ilivyo na faida kubwa na furaha, na namna uovu ulivyo na hasara kubwa na maangamizi, sikilizeni na mzingatie kisa kifuatacho kilicho katika namna ya mfano. Wakati fulani, askari wawili walipewa amri kwenda katika mji wa mbali. Walitoka na kusafiri pamoja mpaka njia ilipogawanyika. Kwenye mgawanyiko kulikuwa na mtu aliyewaambia, “Njia ya upande wa kulia haina hasara hata kidogo, na watu tisa kati ya kumi wenye kuifuata hupata faida kubwa na wanapata mazuri makubwa. Njia ya upande wa kushoto haina manufaa yoyote na watu tisa kati ya kumi ya wanayoitumia hupata hasara. Masafa ya kila mojawapo yanalingana, lakini kuna tofauti moja: Wanaotumia njia ya upande wa kushoto, isio na kanuni wala mwenye mamlaka nayo, husafiri bila ya mizigo na silaha. Hujisikia wepesi na urahisi wa uongo. Wanaosafiri kwenye njia ya upande wa kuume, ambayo iko chini ya amri ya kijeshi wanashurutishwa wabebe shanta lililojaa vyakula vya uzito wa wakia nne hivi na bunduki bora ya uzito wa takribani wakia mbili ya kumshinda adui yeyote. Baada ya askari hao wawili kusikiliza maelekezo aliyoyasema mtu huyo, mwenye bahati njema alipita njia ya upande wa kuume. Akabeba mzigo wa wakia kumi mgongoni mwake, lakini moyo wake na roho yake vilinusurika dhidi ya maelfu ya wakia za hofu na hisia ya kuwa na majukumu kwa wengine. Yule mtu askari, asiye na bahati, aliacha jeshi. Hakutaka kufuata amri na akapita upande wa kushoto. Akaachiliwa asibebe mzigo wa uzito wa wakia kumi, lakini hofu yake ilibanwa na maelfu ya wakia za madeni na roho yake ilipondwapondwa na hofu zisizohesabika. Alipita katika njia yake huku akimwomba kila mmoja na kukitetemekea kila kitu na kila tukio mpaka akafika mwisho wake. Huko aliadhibiwa kwa uasi na utoro. Askari aliyependa amri ya jeshi alilinda shanta na bunduki yake na kupita njia ya upande wa kuume, alipita katika njia yake bila ya kumwajibikia yeyote, bila ya kumuogopa yeyote, tena kwa moyo mwepesi na ufahamu mpaka akafika katika mji aliokuwa akienda. Huko alipata zawadi ya thamani ya askari mheshimiwa aliyetekeleza majukumu yake kwa uaminifu. Ewe nafsi yenye kuasi, tambua kuwa askari mmoja anawawakilisha wenye kujisalimisha kwenye sheria za kiungu, ilhali mwingine anawawakilisha waasi na wale wanaofuata matamanio yao. Njia ni njia ya maisha, inayokuja kutoka katika Dunia ya Kiroho, inapita kaburini na kuendelea mpaka akhera. Ama kuhusu shanta na bunduki, ni ibada na uchamungu. Kuna mzigo waziwazi kwenye ibada, lakini kuna urahisi na wepesi katika maana yake ambayo maelezo yake hayana kifani. Kwenye swala za faradhi, mwenye kuswali anasema, اَشْهَدُ اَنْ لاَ اِلهَ اِلاَّ اللّٰهُ. Maana yake, katika kila jambo anakuta mlango wa hazina ya rehema kwa sababu anaamini na kusema “Hakuna Muumbaji na Mtoa Riziki isipokuwa Allah. Madhara na manufaa yapo mkononi mwake. Yeye ni Mwingi wa Hekima; Hafanyi jambo burebure, na Yeye ni Mwingi wa Rehema. Neema na rehema zake ni nyingi mno.” Anagonga mlangoni kwa dua lake. Zaidi ya hayo, anaona kuwa kila kitu kimetiishwa kwenye amri ya Mola wake Mlezi, hivyo anajikinga kwake. Anamtumaini na kumtegemea Yeye, na anakuwa amejiwekea ngome dhidi ya kila janga, imani yake inampa matumaini kamili. Kwa hakika, kama ilivyo kwa kila wema wa kweli, chanzo cha ujasiri ni kumuamini Allah, na ibada. Na kwa kila uovu, chanzo cha uoga ni upotevu. Kwa kweli, kwa mfanya ibada mwenye moyo uliotiwa nuru kiukweli, inawezekana kuwa hata kama tufe la dunia lingegeuka kuwa bomu na kulipuka, lisingemuogopesha. Angeliangalia akistaajabu kwa furaha kama muujiza wa uwezo wa Mmoja Mwenye Kuhitajiwa. Lakini pindi mwanafalsafa mashuhuri aliye mpotovu mwenye akili bora, lakini si moyo atakapoona kimwondo angani, atatetemeka ardhini, na kupiga kelele kwa wasiwasi: “Kwani kimondo hicho hakitaangukia duniani?” (Katika tukio moja, Amerika ilikuwa inakitetemekea kimwondo kama hicho kwa hofu, na watu wengi wakakimbia makazi yao katikati ya usiku.) Ingawa mtu ana haja ya vitu vingi, mtaji wake ni kama haupo, na ingawa ni mwenye kupatwa na majanga yasiyokwisha, uwezo wake ni kama haupo. Kwa kawaida, mtaji na uwezo wake unapatikana pale tu mkono wake unapoweza kufika. Hata hivyo, matumaini yake, utashi, maumivu, na taabu hufika mbali panapoweza kufikiwa na jicho na fikra. Yeyote asiye kipofu kabisa anaweza kufahamu baadaye kuwa ibada, kukiri umoja wa Allah, na kumtegemea Allah na kumnyenyekea ni faida kubwa, furaha na uzuri, na neema kwa ajili ya roho ya mwanadamu, ambayo kwa hivyo haina nguvu na dhaifu, masikini na yenye haja. Ni dhahiri kuwa njia salama huchaguliwa badala ya madhara, hata kama uwezekano wa usalama wake ni moja tu kati ya kumi. Lakini katika njia ya ibada, ambayo ni jambo letu hapa, kuna uwezekano katika tisa kati ya kumi kuwa inaelekea kwenye hazina ya furaha ya milele, kadhalika na kuwa kwake salama. Pia imewekwa na ushahidi wa kweli usiopingika wa mabingwa na mashahidi wasiohesabika kuwa licha ya kutokuwa na manufaa, na hata wapotovu wanakiri jambo hili, njia ya uovu na ufasiki inaishia katika taabu ya milele. Kwa mujibu wa taarifa za wale walioweka wazi mafumbo ya uumbwaji, hili ni hakika kabisa. Kwa ufupi: Kama ilivyo ile ya akhera, furaha ya duniani ipo katika ibada na kuwa askari wa Allah (s.w). Katika hali zote, tunapaswa tuseme: اَلْحَمْدُ لِلّٰهِ عَلَى الطَّاعَةِ وَالتَّوْفِيقِ na tunapaswa tumshukuru kuwa sisi ni Waislamu.
Source text is preserved. When a suitable model is available, translation is displayed separately.
Sözler
The Third Word
Source: risaleinur multilingual dataset, risale.site source · Risale-Nur multilingual research corpus

