Sözler

The Fourth Word

Source: risaleinur multilingual dataset, risale.site source · Risale-Nur multilingual research corpus
Risale reading plan
§1

بِسْمِ اللّٰهِ الرَّحْمٰنِ الرَّحِيمِ اَلصَّلَاةُ عِمَادُ الدّٖينِ Maisha ya mpito yanafanywa na swala kuwa ya milele Kama unataka kuufahamu uhakika wa mbili jumlisha mbili sawa na nne, na jinsi gani ilivyo thamani na umuhimu kwa swala za faradhi, tena licha ya udogo wa gharama zake katika kuzitekeleza, na namna alivyo mwendawazimu na anayedharaulika yule anayezipuuzia, basi zingatia kisa kifuatacho kilicho katika namna ya mfano. Wakati fulani, mtawala mwenye nguvu alimpa kila mmoja katika watumishi wake wawili, vipande ishirini na nne vya dhahabu na akawatuma kwenda kuandaa mojawapo ya utajiri wake, mashamba ya kifalme katika umbali wa miezi miwili. “Tumieni pesa hizi kwa ajili ya tiketi zenu,” aliwaamuru, “Na mnunulie nyumba yenu huko.” Kuna kituo katika masafa ya siku moja kutoka shambani, na kuna usafiri wa barabara na reli, na mashua na ndege. Hivyo vinaweza kutumiwa kulingana na mtaji wenu. Baada ya kupata maelekezo haya, watumishi hao wawili waliondoka. Mmoja wao alikuwa mwenye bahati kiasi kuwa alitumia kiasi kidogo cha pesa alipokuwa njiani kuelekea kituoni. Katika matumizi yake kulikuwa na biashara za faida kubwa na za kumfurahisha mkuu wake kiasi cha mtaji wake kuongezeka mara elfu moja. Yule mtumishi mwingine, hakuwa mwenye bahati na hakutaka kufanya kazi na kwa hivyo, akatumia vipande ishirini na tatu vya dhahabu njiani akielekea kituoni, huku akiipoteza kwenye kamari na burudani. Kikabaki kipande kimoja cha dhahabu. Rafiki yake akamwambia: “Kipande hiki kilichobakia kitumie kununulia tiketi ili usilazimike kutembea masafa marefu na kushinda na njaa. Zaidi ya hayo, mkuu wetu ni mkarimu, huenda atakuhurumia na kukusamehe makosa yako na kukuweka pia kwenye ndege. Halafu tutafika tunakokwenda kuishi kwa siku moja. La sivyo, utalazimika kutembea kwa miguu peke yako huku ukiwa na njaa kukatisha jangwa ambalo huchukua miezi miwili.” Mtu asiye na akili kabisa anaweza kufahamu jinsi ambavyo angekuwa mpumbavu, mwenye madhara na mpuuzi kama kwa ukaidi asingetumia kipande kile kimoja kwa tiketi, kinachoshabihiana na ufunguo wa hazina, na badala yake kutumia katika uovu kwa kufanya starehe. Je sivyo? Enyi msioswali swala za faradhi! Na ewe nafsi yangu, usiyetaka kuswali! Mtawala katika mfano ni Mola wetu Mlezi, Muumba wetu. Kuhusu wasafiri hao wawili, mmoja anawakilisha wachamungu wanaoswali swala zao kwa bidii, na mwingine si msikivu anayezipuuzia. Vipande ishirini na nne vya dhahabu vinawakilisha maisha tunayopitisha katika kila siku ya saa ishirini na nne. Na uwanja wa kifalme ni Pepo. Ama kuhusu kituo, ni kaburi. Safari ni mapito ya mwanadamu mpaka kaburini na mpaka ufufuo na kwenda akhera. Watu hupita safari hiyo ndefu kwa kuwiana na vitendo vyao na nguvu ya hofu yao kwa Allah. Baadhi ya wachamungu wamepita umbali wa miaka elfu moja katika siku moja kama umeme, na wengine wamepita masafa ya miaka elfu hamsini kwa siku moja kwa kasi ya fikra. Qur’an ya Allah (s.w) inadokezea ukweli huu kwa aya zake mbili. Tiketi katika mfano inawakilisha swala za faradhi. Saa moja kwa siku inatosheleza kwa swala tano pamoja na kuchukua udhu. Hivyo, hasara gani anayopata mtu kama atatumia saa ishirini na tatu juu ya maisha haya ya mpito ya kidunia na anashindwa kutumia saa moja kwenye maisha marefu ya akhera; namna gani anavyojifanyia makosa; namna gani anavyotenda bila kutumia akili. Kwa yeyote anayejizingatia kuwa ni mwenye akili atafahamu namna ilivyo tofauti na mantiki na busara kuona tabia ya mtu wa aina hiyo na namna gani alivyo mbali na mantiki kama anadhani kuwa ni mantiki, anatumia nusu ya mali yake katika kamari ambayo watu elfu moja wanashiriki na uwezekano wa kushinda ni moja katika elfu moja, na hatumii moja ya saa ishirini na nne kwenye hazina ya milele ambapo uwezekano wa kushinda ni asilimia tisini na tisa, katika mia moja. Zaidi ya hayo, nafsi ya mwanadamu, moyo na akili, hupata utulivu katika swala, na si jambo lenye kuchosha kwa kimwili. Tena, kwa makusudio sahihi matendo yote mengine ya mtu anayeswali swala za faradhi yanakuwa ibada. Anaweza akayafanya mtaji wa maisha yake yote kuwa ni akhera kwa njia hii. Anaweza kuyafanya maisha yake ya mpito kuwa ya daima.

Private reading note

This note stays on this device and is never uploaded to a server.

Up to 1,200 characters