بِسْمِ اللّٰهِ الرَّحْمٰنِ الرَّحِيمِ اِنَّ اللّٰهَ مَعَ الَّذ۪ينَ اتَّقَوْا وَالَّذ۪ينَ هُمْ مُحْسِنُونَ Jukumu Letu Kuu ni: Ibada Kama unataka kuona ni lipi jukumu la kweli kwa mwanadamu na maumbile yake, pamoja na malipo yanayowafikiana na kuumbwa kwake ni kutokana na kusimamisha swala na kuacha dhambi kubwa, basi sikiliza na zingatia mifano hii inayofuata: Wakati fulani katika muda wa uhamasishaji wa ujumla, askari wawili walijikuta wakiwa pamoja katika kikosi kimoja. Mmoja alikuwa na elimu ya kutosha na mwangalifu sana, mwingine alikuwa kuruta na mwenye kujipenda. Askari mwangalifu alizingatia mafunzo na vita, kwa kuwa alijua kuwa lilikuwa ni jukumu la taifa kumlisha na kumpa zana, kumtibu anapougua na hata kumwekea chakula mdomoni inapotokea haja hiyo. Alijua kuwa jukumu lake kuu lilikuwa mafunzo na kupigana, lakini pia alikuwa akipata baadhi ya posho na vifaa kama sehemu ya kazi yake. Alikuwa akichemsha masufuria, kuosha vyombo vya kulia chakula na kuvileta. Alipoulizwa: “Unafanya nini?” alikuwa akijibu: “Ninajitolea kufanya kazi za ziada kwa ajili ya taifa.” Alikuwa hasemi: “Ninafanya kazi ili kutafuta mambo ya kuendesha maisha. Kuruta hata hivyo, alikuwa akilipenda sana tumbo lake na hakujali mafunzo na vita. Hayo ni mambo ya taifa, yananihusu nini?” ndivyo alivyokuwa akisema. Alidumu katika kufikiria maisha yake na katika kuyafuatilia na akitoka kikosini na kwenda sokoni kufanya manunuzi. Siku moja, rafiki yake aliyekuwa na mafunzo vyema alimwambia: “Ndugu yangu, jukumu lako kuu ni mafunzo na mapigano, umeletwa hapa kwa ajili ya hayo. Mtumaini mfalme; hatakuacha na njaa. Huo ni wajibu wake. Vyovyote, wewe ni dhaifu na mwenye haja, hutaweza kujilisha kila mahali. Huu ni wakati wa uhamasishaji na vita; atakwambia kuwa wewe ni mwasi na atakuadhibu. Ndiyo, kuna majukumu mawili yanayotuhusu. Moja ni wajibu wa mfalme: wakati mwingine huwa tunajitolea kufanya kazi zake zisizo za kijeshi na yeye anatupatia chakula kwa ajili hiyo. Lingine ni jukumu letu, ambalo ni mafunzo na kupigana, na wakati mwingine mfalme hutusaidia katika hayo.” Bila shaka kwa kweli utafahamu hatari ya huyo askari asiyetaka kufanya kazi itakuwaje kama hakumzingatia yule mwenye jitihada na aliyepata mafunzo vyema. Ewe nafsi yangu yenye uvivu! Mahali hapo penye zahama ya vita ni maisha haya ya kidunia yenye dhoruba, na jeshi lililogawanyika katika vikosi vya kijeshi, ni vizazi vya kibinadamu. Kikosi katika mfano huo ni jamii ya Kiislamu katika karne hii. Askari mmoja ni Mwislamu mchamungu anayejua majukumu ya dini yake na kuyatimiza, na anapambana na Shetani na roho yake ili asifanye makosa na dhambi. Mwingine ni mtenda dhambi aliyepotoka aliyejitumbukiza sana katika kutafuta mambo ya kimaisha na anamtupia lawama Mtoaji riziki wa kweli, anaacha majukumu yake ya kidini, na anafanya dhambi zote zinazomjia wakati anapotafuta mambo ya kimaisha. Kuhusu mafunzo na maelekezo, kwanza kabisa ni swala za faradhi na ibada. Vita ni mapambano dhidi ya nafsi na matamanio yake, na dhidi ya mashetani baina ya majini na watu, kuwatoa kutoka katika dhambi na mwenendo mbaya, na kuuokoa moyo na roho dhidi ya kuangamia daima. Jukumu la kwanza kati ya mawili hayo ni kuhuisha na kuuchunga uhai huo na kumwomba Mwenye kuleta uhai na kuuchunga. Ni kumtumaini Yeye na kumtegemea. Kwa hakika, aliyewapa viumbe uhai, ambao ni muujiza mng’aavu zaidi wa ufundi wa Mwenye kukusudiwa milele kwa haja na maajabu ya hekima ya mtawala, ndiye anayeuchunga na kuudumisha kwa njia ya riziki. Haiwezekani kuwa vinginevyo. Unataka ushahidi? Wanyama dhaifu na wapumbavu zaidi ndio wenye kupewa lishe nzuri zaidi; kama vile samaki, na minyoo katika tunda. Pia ni wanyama wasiojiweza na laini kabisa ndio walio na chakula kizuri zaidi; kama vile watoto wachanga na watoto wa aina zote za wanyama. Kwa hakika, inatosha kabisa kulinganisha samaki na mbweha, wanyama wachanga waliozaliwa na wanyama mwitu, na miti na wanyama ili kufahamu kuwa chakula halali hupatikana si kwa uwezo na utashi, bali kupitia udhaifu na kutojiweza. Maana yake, mtu anayeacha kuswali swala za faradhi kwa sababu ya kuhangaikia maisha anafanana na askari aliyeacha mafunzo na handaki lake na akaenda kuomba sokoni. Lakini mtu kutafuta posho katika hazina ya rehema za Mpaji Mwingi wa ukarimu baada ya kuswali, na mtu kwenda mwenyewe ili asiwe mzigo kwa wengine ni vizuri na ujanadume. Hiyo pia ni namna ya ibada. Zaidi ya hayo, asili ya mwanadamu na zana za kiroho zinaonesha kuwa aliumbwa kwa ajili ya ibada. Kuhusu uwezo na matendo yaliyo lazima kwa ajili ya uhai wa dunia hii, hawezi kushindana na shorewanda dhalili kabisa. Ilhali kulingana na elimu na haja, ibada na dua, ambavyo ni vya lazima kwa ajili ya uzima wa kiroho na uzima katika maisha ya akhera, yeye ni kama mfalme na mkuu wa wanyama. Ewe nafsi yangu! Kama utafanya maisha ya dunia hii ndio lengo na kufanya kazi daima kwa ajili hiyo, utakuwa kama shorewanda dhalili kabisa. Lakini kama utafanya uzima wa akhera ndio lengo na mwisho, na kuyafanya maisha ya dunia kama njia ya kuyafikia na shamba lake, na kufanya bidii kuiendea, basi utakuwa kama mkuu wa viumbe, mja mtukufu mbele ya Allah (s.w), na mgeni Wake wa kuheshimika. Hizo ni njia mbili zilizo wazi kwako! Unaweza kuchagua yoyote uitakayo; basi omba uongofu na kufaulu kutoka kwa Mwingi wa rehema kuliko wote.
Source text is preserved. When a suitable model is available, translation is displayed separately.
Sözler
The Fifth Word
Source: risaleinur multilingual dataset, risale.site source · Risale-Nur multilingual research corpus

