Sözler

The Sixth Word

Source: risaleinur multilingual dataset, risale.site source · Risale-Nur multilingual research corpus
Risale reading plan
§1

بِسْمِ اللّٰهِ الرَّحْمٰنِ الرَّحِيمِ اِنَّ اللّٰهَ اشْتَرٰى مِنَ الْمُؤْمِن۪ينَ اَنْفُسَهُمْ وَاَمْوَالَهُمْ بِاَنَّ لَهُمُ الْجَنَّةَ Amana anayopewa Mwanadamu Kama unataka kufahamu biashara ina faida kubwa namna gani, na jinsi hadhi ilivyo na heshima ya mtu kumuuzia Allah nafsi na mali yake, kuwa mtumwa wake na askari wake, basi sikiliza mfano ufuatao. Kuna wakati mfalme aliwapa amana kila mmoja katika watu wake kwa kumpa shamba, likiwa pamoja na karakana zote muhimu, mashine, farasi, silaha na vingine. Lakini kwa kuwa ulikuwa wakati wa ugomvi na vita vingi, hakuna kilichopata utengamano; ama kilipotea au kilibadilika. Mfalme kwa huruma yake kubwa alimtuma mjumbe wake mheshimiwa zaidi kwenda kwa watu hao wawili na kwa njia ya agizo lenye huruma aliwafikishia ujumbe ufuatao: “Niuzieni mali mliyo nayo sasa kama amana, ili nikuhifadhieni, ili isiharibike pasi na malengo yoyote. Baada ya vita kuisha, nitakurejesheeni yakiwa katika hali nzuri kuliko hapo kabla. Nitazingatia amana hizo kama mali yenu na kukulipeni bei kubwa. Kuhusu mashine na vifaa vya katika karakana, vitatumika juu ya jina na benchi langu la umakanika. Lakini bei na malipo ya kuvitumia zitaongezwa mara elfu moja. Mtapata faida zote zinazotokana nazo. Nyinyi ni mafukara na msio na mali, na hamwezi kulipa gharama za shughuli hizi. Basi nitakupeni ruzuku za gharama zote na vifaa, na kukupeni mapato na faida zote. Mtahifadhi mpaka wakati wa uhamasishaji. Basi angalieni namna tano ambazo zitakufaidisheni! Sasa, kama hamtaniuzia mali hizo, mtaona kuwa hakuna atakayeweza kuhifadhi anachokimiliki, nanyi pia mtapoteza mlicho nacho. Yataondoka bila faida, na mtapoteza bei ya juu niliyokupeni. Vifaa laini na vya thamani na mizani, metali za thamani zinazongojea kutumika, pia zitapoteza thamani kabisa. Mtapata matata na hasara ya kusimamia na kuhifadhi, lakini wakati huo huo kuadhibiwa kwa kusaliti amana zenu. Basi angalieni njia tano mnazoweza kupoteza! Zaidi ya hivyo, kama mtaniuzia mali yenu, mtakuwa askari wangu na kutenda kwa jina langu. Badala ya mfungwa wa kawaida au askari mgambo, utakuwa mjumbe aliye huru katika ufalme wa heshima.” Baada ya kusikiliza agizo hili lenye huruma, aliyekuwa na akili zaidi kati ya hao wawili alisema: “Kwa hali zozote, ninajivunia na kufurahia kuuza, ninatoa shukrani nyingi.” Lakini mwingine alikuwa mwenye kiburi, mbinafsi na mbadhirifu, nafsi yake ina kiburi kama Firauni. Kana kwamba angekaa milele katika shamba, alipuuzia matetemeko ya ardhi na misukosuko ya dunia. Akasema: “Hapana! Mfalme ndiye nani? Sitauza mali yangu, wala kuharibu furaha yangu.” Baada ya muda mfupi, mtu wa kwanza alifikia hadhi ya juu sana kiasi cha kila mmoja kuionea wivu hali hiyo. Alipata ukarimu wa mfalme, na akaishi kwa furaha katika kasri la mfalme. Yule mwingine kinyume chake aliangukia katika hali ambayo kila mmoja alimsikitikia, lakini pia alisema kuwa alistahili hivyo. Kutokana na hofu yake, furaha na mali yake vilitoweka, na akapata adhabu na mateso. Ewe nafsi iliyojaa kigeugeu! Angalia upande wa ukweli kwa darubini ya mfano huu. Kuhusu mfalme, ni Mfalme wa milele na wa tangu, Mola wako mlezi na Muumbaji. Mashamba, mashine, vifaa na vipimio ni mali yenu mnapokuwa hai, viwiliwili, roho na moyo katika mali hiyo, na hisia zenu za nje na za ndani kama vile jicho na ulimi, akili na fikra. Mjumbe mheshimiwa zaidi ni Mtume wetu Muhammad (s.a.w) na agizo lenye hekima zaidi ni Qur’an yenye hekima, inayoeleza biashara tunayozungumzia katika aya hii: اِنَّ اللّٰهَ اشْتَرٰى مِنَ الْمُؤْمِن۪ينَ اَنْفُسَهُمْ وَاَمْوَالَهُمْ بِاَنَّ لَهُمُ الْجَنَّةَ Uwanja wa vita wenye misukosuko na vita ni dunia yenye ugomvi mwingi na mabadiliko yasiyokoma, yanambadilisha mtu na kumfanya ajiulize: “Vyote tulivyo navyo havitadumu na kusalia mikononi mwetu, bali vitakwisha na kupotea, je hakuna namna yoyote ya kutatua hili? Je hakuna njia ya kuvibadili viwe vya kudumu na kuvitunza? Huku akiwa katika fikra hizi, ghafla anasikia sauti ya Qur’an mbinguni ikisema: “Kwa hakika ipo njia nzuri na nyepesi yenye faida tano: Ni njia gani hiyo? Jibu ni kumuuzia mwenyewe amana yake. Uuzaji huo unaleta faida mara tano. Faida ya Kwanza: Mali ya mpito yanageuka kuwa ya kudumu. Kwa kuwa maisha haya yenye kuondoka anapopewa aliye hai daima na Mwenye kuwepo milele na kutumika katika njia yake (s.w), yatageuka kuwa ya milele. Wakati huo yatazaa matunda ya kudumu. Muda wa maisha ya mtu utapotea waziwazi na kuoza kama viini na matunda. Lakini wakati huo, maua yenye faida na fadhila yatachanua katika ulimwengu wa milele, na kila moja pia litaleta kipengele chenye kutoa nuru na uthibitisho katika Ulimwengu wa kati na kati. Faida ya Pili: Thamani kubwa ya pepo ndio malipo. Faida ya Tatu: Thamani ya kila kiungo na kila hisia huzidishwa hata mara elfu moja. Akili mathalani, ni kama kifaa. Kama humuuzii Allah (s.w), na badala yake kuitumia kwa ajili ya matamanio na nafsi, itakuwa kifaa cha kulaumiwa, kibaya, dhaifu na cha maangamizi kitakachoibebesha nafsi yako dhaifu mizigo ya huzuni zote zilizopita na hofu kubwa za hapo baadaye, itashuka chini mpaka kuwa kifaa cha nuksi na maangamizi. Ni kwa sababu hii ndipo mtenda dhambi atakimbilia kila mara kwenye ulevi au starehe za kipuuzi ili kuepuka maudhi na majeraha ya akili yake. Lakini kama akili yako utamuuzia Allah na kuitumia kwa ajili Yake na ndani ya mipaka aliyoweka, basi akili itakuwa kama ufunguo unaofaa, ikifungua hazina zisizo na mipaka za rehema na maghala ya hekima zilizo katika uumbaji. Mfano mwingine, jicho ni mojawapo kati ya viungo vya hisia, dirisha ambalo roho hutumia kuangalia duniani. Kama humuuzii Allah (s.w), bali unalitumia kwa ajili ya nafsi kwa kuangalia mandhari machache ya mpito na ya kuondoka, litadidimia mpaka katika kiwango cha kuishawishi nafsi yenye tamaa na ashiki. Lakini kama jicho lako utamuuzia Muumbaji wake Mwenye kuona yote na kulitumia kwa ajili Yake na ndani ya mipaka Aliyoiweka, basi jicho lako litapanda mpaka katika hadhi ya mwenye kusoma kitabu kikubwa cha ulimwengu, na kushuhudia muujiza wa ufundi wa kiungu, kama vile nyuki mbarikiwa akinyonya baina ya maua ya rehema katika bustani ya dunia hii. Mfano mwingine ni ulimi na hisia ya kuonja. Kama humuuzii Muumbaji wake Mwenye hekima, lakini badala yake kuutumia kwa ajili ya nafsi na kwa ajili ya tumbo, inazama na kuporomoka mpaka kuwa kama bawabu wa zizi la tumbo, mlinzi wa kiwanda chake. Lakini kama utamuuzia Mtoaji riziki, basi hisia ya kuonja iliyo katika ulimi itapanda mpaka kufikia daraja la msimamizi mahiri mekoni mwa nguvu za milele za Allah. Basi angalia vyema, ewe akili! Ona tofauti baina ya kifaa cha maangamizi na ufunguo wa hazina za viumbe. Ewe jicho nawe! Kuwa mwangalifu, angalia tofauti baina ya ushawishi wa kuchukiza na usimamizi wake wa kisomi wa maktaba ya kiungu! Na, onja vyema, ewe ulimi! Ona tofauti baina ya bawabu imara au mlinzi wa kiwanda na mwangalizi wa hazina ya rehema ya Allah! Linganisha vifaa vyote vingine na viungo vyake, kisha utaelewa kuwa kwa hakika, muumini anapata hali inayostahiki Pepo na kafiri anapata hali inayoendana na Jahanamu. Sababu ya kila mmoja kupata thamani yake inayomhusu ni kuwa, muumini, kwa fadhila ya imani yake, anatumia amana ya Muumba wake kwa ajili yake na katika mipaka aliyoiweka Yeye Mwenyewe, ilhali kafiri anasaliti amana na anaitumia kwa ajili ya tamaa za nafsi yake yenye kuamrisha uovu. Faida ya Nne: Mwanadamu hajiwezi na yuko katika kupatwa na majanga mengi. Yeye ni fukara, na haja zake ni nyingi. Ni dhaifu, na mzigo wa kimaisha ni mzito mno. Kama hamtegemei (s.w) Mwenye uwezo wote, kumtumainia Yeye na jambo lake kumuachia Yeye, mara zote dhamiri zake zitatatizika. Mateso yasiyo na faida, maumivu na majuto yatamsonga, au kumgeuza mnyama. Faida ya Tano: Wale waliopata nuru na wamefunukiwa na ukweli wa mambo, wateule walioshuhudia ukweli, wote wameafikiana kuwa malipo mema kwa ibada na kumtukuza Allah kulikofanywa na viungo na vifaa mtalipwa katika wakati wa haja kubwa zaidi, kwa njia ya matunda ya Peponi. Kama mtadharau biashara hii pamoja na faida yake mara tano, zaidi ya kunyimwa faida zake, mtapata hasara mara tano zaidi. Hasara ya Kwanza: Mali na watoto mnavyohusiana navyo, nafsi na kigeugeu chake mnavyoabudu, ujana na maisha mnayopumbazwa nayo, vyote vitatoweka na kupotea; mikono yenu itakuwa mitupu. Lakini itaacha dhambi na maumivu nyuma yake, vimefungwa shingoni mwenu kama nira. Hasara ya Pili: Mtapata adhabu kutokana na usaliti wa amana. Mtakuwa mmejikosea wenyewe kwa kutumia vifaa vya thamani kubwa sana katika vitu visivyofaa kabisa. Hasara ya Tatu: Kwa kuushusha nyenzo zote wa thamani za mwanadamu mpaka katika daraja ya chini zaidi kuliko wanyama, utakuwa umetusi na umekiuka hekima ya Allah. Hasara ya Nne: Katika udhaifu na umaskini wako, utakuwa umejibebesha begani mzigo mzito wa maisha, na daima utagumia na kusikitika chini ya mapigo ya muda mfupi na utengano. Hasara ya Tano: Zawadi nzuri za Mwingi wa Rehema kama vile akili, moyo, jicho na ulimi, ulizopewa ili ufanyie matayarisho kwa ajili ya msingi wa uzima wa kudumu na furaha ya milele katika akhera, utazivaa katika namna mbaya, inayotosha kufungua milango ya Jahanamu mbele yako. Sasa ni vigumu sana kuuza amana? Ni mzigo mzito ambao watu wengi wanaepuka muamala huo? Hasha! Hakuna taabu wala uzito hata kidogo. Kwa sababu mipaka ya halali ni mipana, na inatosha utashi wa mwanadamu, hakuna haja ya kuvuka mipaka iliyokatazwa. Majukumu yaliyowekwa na Allah ni mepesi na machache. Kuwa mja na askari wa Allah ni heshima kubwa isiyoelezeka. Jukumu la mtu ni kutenda na kuingia kwenye mambo yote kwa jina la Allah, kama askari, kuchukua na kutoa kwa ajili ya Allah; kwenda na kubakia katika hali inayoendana na ruhusa na sheria Yake. Kama kutakuwa na dosari, basi aombe msamaha kwa kusema: “Ewe Mola wangu! Tusamehe makosa yetu, na utukubali kama waja wako. Utujaalie wenye kutunza amana Yako mpaka ufike wakati wa kuchukuliwa kutoka kwetu, Amin.”

Private reading note

This note stays on this device and is never uploaded to a server.

Up to 1,200 characters