Namna Imani Inavyotia Nuru Njia ya Akhera Ukitaka kujua thamani kubwa na uwezo mkubwa wa kutatua matatizo wa maneno, آمَنْتُ بِاللّٰهِ وَ بِالْيَوْمِ اْلآخِرِ ambapo yote mawili yanaleta ufumbuzi wa fumbo tata la uumbwaji kufungua mlango wa furaha kwa ajili ya roho ya mwanadamu, na dawa zenye manufaa na zenye kuponya zilivyo, kumtegemea Muumba wako na kujihifadhi kwake kupitia subira na dua, na kumuomba Mwenye Kukuruzuku kwa shukrani, na umuhimu wa tiketi za thamani kubwa zenye kung’aa kwa ajili ya safari ya akhera – na chakula cha akhera na nuru ya kaburini – ni kusikiliza Qur’an, kutii amri zake, kuswali swala tano, na kuacha dhambi kubwa, basi sikiliza na kuzingatia mfano huu: Kuna wakati askari aliangukia katika hali mbaya sana katika uwanja wa vita na mtihani, na mzunguko wa faida na hasara. Ilikuwa kama ifuatavyo: Askari huyo alipata majeraha mawili makubwa mbavuni mwake, kulia na kushoto na nyuma yake alisimama simba mkubwa sana kama vile akisubiria kumshambulia. Mbele yake kulikuwa na kitanzi kilichokuwa kikiwaua na kuwaangamiza wote aliowapenda, kilikuwa kikimsubiri na yeye pia. Mbali na hayo, mbele yake kulikuwa na safari ndefu ikimsubiri, alikuwa akipelekwa mbali uhamishoni. Askari huyo mwenye mkosi alipofikiria juu ya hali yake mbaya na ya kutisha huku akiwa amekata tamaa, mtu mkarimu aliyeng’aa nuru kama Khidr alitokea. Akamwambia: “Usikate tamaa, nitakupa mazindiko mawili na kukufundisha. Kama utayatumia vyema, simba atageuka kuwa farasi msikivu kwa ajili yako, na vitanzi vitageuka kuwa bembea ya kukufurahisha. Pia nitakupa dawa mbili. Kama utazingatia maelekezo, majeraha hayo mawili yenye usaha yatageuka kuwa maua mawili yenye kunukia yanayoitwa waridi la Muhammad (s.a.w). Pia nitakupa tiketi, utaweza kusafiri mwaka mzima kwa siku moja kama vile kupaa. Kama huniamini, jaribu kidogo, ili uweze kuona kuwa ni kweli.” Askari huyo alijaribu kidogo, na akathibitisha kuwa ilikuwa kweli. Naam, ndivyo hivyo, Said huyu asiye na bahati, alithibitisha hilo pia, kwa sababu nilifanya na nikaona hilo kuwa ni kweli kabisa. Wakati mwingine baadaye, alimwona mtu mwenye kuonekana kuwa ni mdanganyifu na mpotoshaji, mwenye hila kama Shetani kutoka upande wa kushoto akiwa analeta picha na taswira zilizopambwa vizuri sana na kupendezeshwa sana, pamoja na ulevi. Alisimama mbele ya askari huyo na kumuambia: We! Njoo, rafiki yangu! Twende tukanywe na kufurahi. Tutaangalia picha hizi za wasichana warembo, kusikiliza muziki, na kula chakula hiki chenye ladha tamu.” Kisha akamuuliza: “Unasoma nini katika pumzi zako? “Zindiko” alijibu. “Acha upuuzi huo usioeleweka! Hebu tusiharibu raha yetu iliyopo!” Akauliza swali la pili, “Umeshikilia nini mkononi mwako?” “Dawa,” askari alijibu. “Zitupe! Wewe una afya, huna tatizo. Ni muda wa furaha.” Akauliza tena: “Ni kitu gani hiyo karatasi yenye alama tano juu yake?” “Ni tiketi na kadi ya posho.” “Ah, zichane!”, mtu huyo alisema. “Tuna haja gani ya safari katika majira haya mazuri ya kuchipua?” alijaribu kumshawishi kwa kila namna na hila, na maskini askari, alikaribia kushawishika. Ndiyo, mtu anaweza kuhadaika kwa udanganyifu huo wa hila. Ghafla ikaja sauti kutoka upande wa kuume kama radi. “Tahadhari!”, ilisema. “Usidanganyike! Mwambie huyo mwenye hila: “Kama una njia ya kumuua simba aliye nyuma yangu, kuondoa vitanzi mbele yangu, kuondoa mambo yanayojeruhi pande zangu za kulia na kushoto na kuzuia safari iliyo mbele yangu, hebu fanya hivyo basi! Onesha kuwa unaweza na tuone! Halafu useme, njoo, twende tukafurahi. Vinginevyo, nyamaza!’ zungumza vilevile kama mtu aliyefunuliwa na Allah kama Khidr.” Ewe nafsi yangu, iliyocheka katika ujana wake na sasa inakililia kicheko chake! Tambua kuwa askari huyo maskini ni wewe, ambaye ni mtu. Simba ni saa iliyopangwa. Ama kuhusu vitanzi, ni mauti, kuangamia na utengano, ambao katika kubadilika usiku na mchana, marafiki wote huaga na kupotea. Kuhusu majeraha mawili, moja ni udhaifu usio na mipaka na wenye taabu sana wa mwanadamu, na jingine ni umaskini wake wa kuhuzunisha na usio na kikomo. Uhamisho na safari ni safari ndefu ya majaribio inayotokea katika dunia ya roho, hadi kwenye tumbo la uzazi na utoto mpaka uzee; na kupita duniani na kaburini na dunia ya kati na kati, mpaka ufufuo na Daraja la Sirati. Ama kuhusu mazindiko mawili, ni kumuamini Allah (s.w) na akhera. Ndiyo, kupitia zindiko tukufu la pili, kifo kinakuwa katika namna ya farasi stadi, wa kumbeba muumini kutoka jela ya dunia hii na kumpeleka kwenye mabustani ya Peponi na mbele ya Mwingi wa Rehema. Ni kwa sababu hii ambapo mtu mwenye hekima aliyeona uhalisi wa mauti ameyapenda. Wameyataka kabla ya hayajafika. Na kwa zindiko la kumuamini Allah, kupita kwa wakati, ambao ni kuangamia na utengano, mauti na vitanzi, vinachukua namna ya njia ya kuangalia na kutafakari kwa furaha halisi, miujiza ya Mwingi wa Rehema, darizi mbalimbali, zenye rangi nyingi, zenye kufanywa upya daima, na udhihirisho wa rehema Zake. Ndiyo, wakati vioo vinapoakisi rangi za mwanga wa jua, hubadilika na kufanywa upya, na picha za sinema kubadilika kuwa bora zaidi, mandhari mazuri zaidi hutokeza. Kuhusu dawa zile mbili, moja ni kumtumaini Allah na subira, na nyingine ni kutegemea uwezo wa Muumba na kuwa na imani katika hekima Yake. Je ndivyo hivyo? Kwa hakika ndivyo. Mtu anaweza kuwa na hofu gani, ambaye kupitia cheti cha udhaifu wake, anamtegemea Mtawala wa Dunia, mwenye uwezo wa kuamuru: كُنْ فَيَكُونُ kwani anapopatwa na msiba husema, اِنَّا لِلّٰهِ وَاِنَّا اِلَيْهِ رَاجِعُونَ na anaweka matumaini yake kwa Mola Mlezi Mwingi wa Rehema. Mtu anayemjua Allah hupata furaha kutoka katika udhaifu, kutoka katika kumcha Allah. Naam, ipo furaha katika hofu. Kama mtoto wa miezi kumi na mbili angekuwa na akili ya kutosha na akaulizwa: “Ni kipi cha kukufurahisha na kitamu zaidi kwako?” anaweza kusema: “Kutambua udhaifu na kutokujiweza kwangu na kwa kuhofia kofi lisilo kali la mama na wakati huo huo kujihifadhi katika matiti yake matamu.” Lakini huruma za mama wote si jingine, bali ni nuru ya ghafla ya udhihirisho wa rehema ya kiungu. Ni kwa sababu hii ambapo wenye busara wameipata furaha hiyo katika udhaifu na kumhofu Allah, waziwazi huku wakitamka kuwa hawana nguvu na uwezo, na wamejihifadhi kwa Allah katika udhaifu wao. Wamefanya udhaifu na hofu kuwa mwombezi kwa ajili yao. Dawa ya pili ni shukrani na kutosheka, na kufanya maombi na dua, na kutegemea rehema ya Mtoaji riziki Mwenye kurehemu. Ndivyo hivyo? Ndiyo, unawezaje umaskini, utashi na haja kumsababishia maumivu na mzigo kwa mgeni wa Mwingi wa ukarimu anayeufanya uso wote wa dunia kuwa meza ya neema na majira ya kuchipua kuwa kicha cha maua, na ambaye huweka maua juu ya meza na kuyatandaza juu yake? Umaskini na haja hufanya namna ya hamu nzuri sana. Mgeni anajaribu kuzidisha umaskini wake kwa namna ileile anavyofanya kwa hamu yake. Ni kwa sababu hii kuwa wenye busara wamefanya fahari katika uhitaji na umaskini. Lakini, tahadharini, msilielewe hili vibaya! Maana yake ni mtu kuujua umaskini wake mbele ya Allah na kumwomba Yeye, sio kuwaonesha watu na kuwa ombaomba. Ama kuhusu tiketi na stakabadhi, ni kutimiza majukumu ya kidini na la kwanza kabisa ni swala za faradhi, na kuacha dhambi kubwa. Je, ni hivyo? Naam, ndivyo, kwani kwa mujibu wa muafaka wa wanaoangalia na wenye ujuzi wa ghaibu na wenye kufumbua mafumbo ya uumbwaji, riziki, nuru, na kufanya haraka kwa ajili ya njia ndefu na yenye giza kwenda akhera inaweza tu kupatikana kwa kushikamana na amri za Qur’an na kuacha inayoyakataza. Sayansi, falsafa, na sanaa hayana thamani yoyote katika njia hiyo. Mwangaza wake unaishia katika mlango wa kaburi tu. Ewe nafsi yangu yenye uvivu! Urahisi na wepesi ulioje wa kuswali swala tano na kuacha dhambi saba zenye kuangamiza! Kama utakuwa na akili ya utambuzi utafahamu namna matokeo, matunda na faida zilivyo muhimu na pana. Mwambie shetani na yule mtu aliyekuwa akikuhimiza ujiingize kwenye uovu na ubadhirifu. Kama una njia ya kuyaondosha mauti duniani, na maangamizi na mpito, na kuondoa umaskini na udhaifu wa mwanadamu na kufunga mlango wa kaburi, basi tuambie na hebu tusikie hilo! Vinginevyo, nyamaza! Qur’an inausoma ulimwengu katika msikiti mkubwa wa uumbaji. Hebu tuisikilize, hebu tupate nuru hiyo. Hebu tufuate uongofu wake. Tuwe tunaisoma daima. Naam, Qur’an ndio neno. Ndivyo wanavyoielezea. Ni Qur’an ambayo ni kweli na inatoka kwa Mkweli na inasema ukweli na inaonesha ukweli na inaeneza hekima yenye nuru.” اَللّٰهُمَّ نَوِّرْ قُلُوبَنَا بِنُورِ الْاِيمَانِ وَالْقُرْآنِ اَللّٰهُمَّ اَغْنِنَا بِالْاِفْتِقَارِ اِلَيْكَ وَلَاتُفْقِرْنَا بِالْاِسْتِغْنَاءِ عَنْكَ تَبَرَّاْنَا اِلَيْكَ مِنْ حَوْلِنَا وَقُوَّتِنَا وَالْتَجَئْنَا اِلٰى حَوْلِكَ وَقُوَّتِكَ فَاجْعَلْنَا مِنَ الْمُتَوَكِّلِينَ عَلَيْكَ وَلَا تَكِلْنَا اِلٰى اَنْفُسِنَا وَاحْفَظْنَا بِحِفْظِكَ وَارْحَمْنَا وَارْحَمِ الْمُؤْمِنِينَ وَالْمُؤْمِنَاتِ وَصَلِّ وَسَلِّمْ عَلٰى سَيِّدِنَا مُحَمَّدٍ عَبْدِكَ وَنَبِيِّكَ وَصَفِيِّكَ وَخَلِيلِكَ وَجَمَالِ مُلْكِكَ وَمَلِيكِ صُنْعِكَ وَعَيْنِ عِنَايَتِكَ وَشَمْسِ هِدَايَتِكَ وَلِسَانِ حُجَّتِكَ وَمِثَالِ رَحْمَتِكَ وَنُورِ خَلْقِكَ وَشَرَفِ مَوْجُودَاتِكَ وَسِرَاجِ وَحْدَتِكَ فِي كَثْرَةِ مَخْلُوقَاتِكَ وَكَاشِفِ طِلْسِمِ كَائِنَاتِكَ وَدَلَّالِ سَلْطَنَةِ رُبُوبِيَّتِكَ وَمُبَلِّغِ مَرْضِيَّاتِكَ وَمُعَرِّفِ كُنُوزِ اَسْمَائِكَ وَمُعَلِّمِ عِبَادِكَ وَتَرْجُمَانِ آيَاتِكَ وَمِرْآةِ جَمَالِ رُبُوبِيَّتِكَ وَمَدَارِ شُهُودِكَ وَاِشْهَادِكَ وَحَبِيبِكَ وَرَسُولِكَ الَّذِي اَرْسَلْتَهُ رَحْمَةً لِلْعَالَمِينَ وَعَلٰى آلِهِ وَصَحْبِهِ اَجْمَعِينَ وَعَلٰى اِخْوَانِهِ مِنَ النَّبِيِّينَ وَالْمُرْسَلِينَ وَعَلٰى مَلٰئِكَتِكَ الْمُقَرَّبِينَ وَعَلٰى عِبَادِكَ الصَّالِحِينَ آمِينَ
Source text is preserved. When a suitable model is available, translation is displayed separately.
Sözler
The Seventh Word
Source: risaleinur multilingual dataset, risale.site source · Risale-Nur multilingual research corpus

