Sözler

The Eighth Word

Source: risaleinur multilingual dataset, risale.site source · Risale-Nur multilingual research corpus
Risale reading plan
§1

بِسْمِ اللّٰهِ الرَّحْمٰنِ الرَّحِيمِ اَللّهُ لاَ اِلهَ اِلاَّ هُوَ الْحَىُّ الْقَيُّومُ اِنَّ الدِّينَ عِنْدَ اللّهِ اْلاِسْلاَمُ Kama unataka kuifahamu dunia hii, na roho ya mwanadamu duniani na hali na thamani ya dini kwa mwanadamu, na jinsi dunia ilivyo gereza ikiwa kutakosekana dini ya kweli, tena bila ya dini mwanadamu hugeuka kuwa kiumbe mwenye kutaabika zaidi, na kuwa ni يَا اَللّٰهُ na, لاَ اِلهَ اِلاَّ اللّٰهُ inayoleta ufumbuzi wa zindiko la dunia na kuitoa nafsi ya mwanadamu kutoka gizani, basi sikiliza na uzingatie mfano huu: Zamani, ndugu wawili walikwenda safari ndefu. Waliendelea na safari yao mpaka njia ikafikia njia ya panda. Katika njia ya panda walimwona mtu aliyeonekana kuwa makini na wakamuuliza: “Ipi ndio njia nzuri?” akawajibu: “Katika njia ya upande wa kuume, hulazimika kufuata sheria na utaratibu, lakini licha ya taabu kuna usalama na furaha. Hata hivyo, kwenye njia ya upande wa kushoto kuna uhuru na hakuna kikwazo, lakini katika uhuru wake kuna hasara na umaskini, sasa chaguo ni lenu.” Baada ya kusikiliza hayo, huku akasema, تَوَكَّلْتُ عَلَى اللّٰهِ ndugu mwenye tabia njema alipita njia ya upande wa kuume na akafuata utaratibu na kanuni. Ndugu mwingine, ambaye hakuwa na maadili mema na mvivu, alichagua njia ya upande wa kushoto kwa sababu tu haikuwa na vikwazo. Kwa fikra zetu, tutamfuata huyu mtu kuhusu hali yake, ambayo kijuujuu ilikuwa nyepesi, lakini kiukweli ilikuwa na matatizo. Mtu huyo alipanda milima na kushuka mabonde mpaka akajikuta akiwa katika mwitu wa ukiwa. Ghafla akasikia sauti ya kutisha na kumwona simba mkubwa amekuja kutoka porini na alikuwa amejitayarisha kumshambulia. Akakimbia na kukutana na kisima kirefu cha urefu wa yadi sitini na kisicho na maji, na kwa hofu aliyokuwa nayo, alitumbukia ndani yake. Katikati, mikono yake ilikamata mti na akaning’inia. Mti ulioota kutoka pembeni mwa ukuta ulikuwa na mizizi miwili. Panya wawili, mmoja mweupe na mwingine mweusi, walikuwa wakiishambulia na kuiguguna. Alitizama juu na kumuona simba alikuwa akisubiri juu ya kisima kama askari wa zamu. Akaangalia chini na kuona joka la kutisha. Lilinyanyua kichwa mpaka karibu na mguu wake umbali wa yadi thelathini kutoka chini. Mdomo wake ulikuwa mkubwa kama mdomo wa kisima. Akaangalia kingo za kisima na kuona kulikuwa na nyoka wa sumu wakining’inia na wamemzunguka. Akaangalia mdomoni mwa kisima na kuona mtini. Hata hivyo, haukuwa mti wa kawaida, ulizaa matunda ya miti mingi mingine, kutokea jozi mpaka makomamanga. Kutokana na ukosefu wake wa fikra na upumbavu wake, mtu huyo hakufahamu kuwa hili halikuwa jambo la kawaida, vitu hivi havikutokea hapa kwa bahati tu, na kuwa kulikuwa na siri za kimafumbo zilizofichikana kwa viumbe hawa wa kimkakati, na hakutambua kuwa kulikuwepo na mweye nguvu anayewaongoza. Sasa, ingawa moyo wake, nafsi na akili vilikuwa vinalia kisirisiri na kuhuzunikia hali hii ya kutisha, nafsi yake yenye kuamrisha uovu ilijifanya kuwa hakukuwa na jambo; haikuusikiliza moyo uliokuwa unalia, na kujihadaa, akaanza kula matunda ya mti huo kana kwamba ilikuwa bustani. Lakini baadhi ya matunda yalikuwa na sumu na madhara. Allah (s.w) anasema katika Hadithi Qudusi, “Mimi niko kama mja anavyonidhania.” Kutokana na upumbavu na ukosefu wa kuelewa hilo, mtu huyu asiye na furaha alidhania alichokiona kilikuwa ukweli wa kawaida na halisi. Basi hivyo ndivyo alivyofanyiwa, na atakavyofanyiwa. Hatakufa ili anusurike, wala hatakuwa hai, yuko katika adhabu hiyo. Sasa tutamwacha mtu huyu mwenye mkosi akiwa katika adhabu yake na turejee kuangalia hali ya ndugu mwingine. Mtu huyu mwenye bahati na akili alisonga mbele na safari yake lakini hakupata taabu kama nduguye kwa kufanya tabia zake njema, alifikiria mambo mema na kuwa na fikra ya mambo mazuri. Kila kitu kilikuwa rafiki na kinachofahamika kwake. Hakupata taabu na ugumu aliokumbana nao nduguye, kwakuwa alijua utaratibu na akaufuata. Alipata wepesi. Alisonga mbele kwa uhuru na amani na usalama. Halafu akakuta bustani ambamo kulikuwa na maua na matunda mazuri, na kwa kuwa haikutunzwa, ilikuwa ikioza na vitu vichafu. Ndugu yake aliingia kwenye bustani hiyo, lakini aliona na kujishughulisha na mambo machafu na yakaharibu tumbo lake, basi akaiacha na kusonga mbele bila ya kuweza kujipumzisha. Lakini mtu huyu alifanya kwa mujibu wa kanuni, “Angalia upande mzuri wa mambo,” na akapuuzia mambo yaliyooza. Alinufaika sana kutokana na mambo mazuri na kupumzika vyema, ameondoka na kusonga mbele. Baadaye, pia kama ndugu wa kwanza, aliingia katika jangwa na ghafla akasikia mngurumo simba aliyekuwa akimshambulia. Aliogopa, lakini si sana kama ndugu yake, ni kwa sababu ya fikra zake njema na mtizamo chanya, akawaza: “Jangwa hili lina mtawala, na inawezekana kuwa huyu ni mtumishi aliyeamrishwa na mtawala,” na akafarijika. Lakini alikimbia mpaka akakuta kisima kisicho na maji chenye kina cha yadi sitini. Akatumbukia humo. Kama nduguye, mkono wake ulikamata mti kabla hajafika mwisho, akabakia ananing’inia. Aliangalia na kuona wanyama wawili wakiguguna mizizi miwili ya mti alioshikilia. Akaangalia juu, akamuona yule simba, akaangalia chini na akaona joka. Kama alivyokuwa nduguye, alijikuta akiwa katika hali ngeni kabisa. alitishika kama nduguye, lakini kutishika kwake kulikuwa pungufu mno kukilinganishwa na nduguye. Ni kwa sababu maadili yake mema yamempa fikra njema, na fikra njema huonesha upande mwema wa kila jambo, basi kwa sababu hii alifikiria yafuatayo: “Yuko mwenye kuhusika na matukio haya mageni. Pia inaonekana kuwa yanatokea kwa mujibu wa amri. Kwa hali yoyote, mambo haya yana zinguo. Ndiyo, kila kitu kinafanyika kwa amri ya mtawala aliyefichikana. Kwa hivyo, sipo peke yangu, mtawala huyo aliyefichikana ananitazama, ananipa mtihani, ananilazimisha kwenda mahali kwa lengo fulani, na ananiita huko. Udadisi unaotokana na hofu na fikra hizi zenye kukubalika zinanishawishi kusema: Ninashangaa ni nani huyo anayenipa mtihani, anayetaka kujitambulisha, na ananichochea kwa ajili ya lengo fulani. Kumpenda mmiliki wa zinguo kulitokana na utashi wa kumjua, na kutokana na kumpenda kuliibuka utashi wa kupata ufumbuzi wa zinguo, na kutoka katika utashi ilipatikana nia ya kupata sifa njema ambazo zingempendeza na kumfurahisha mwenye kumiliki zinguo. Halafu akauangalia mti na kuuona ulikuwa mtini, lakini ulikuwa na matunda ya maelfu ya miti. Basi woga wote ukamtoka, kwa kuwa alifahamu kwa hakika kuwa mtini ulikuwa ni orodha, kielelezo, onesho. Mtawala aliyefichikana lazima atakuwa ameweka sampuli za matunda ya bustani kwenye mti huo kwa njia ya muujiza na pamoja na zinguo, na lazima atakuwa ameupamba mti kwa namna itakayoonesha kila aina ya vyakula alivyowaandalia wageni wake, kwani hakuna namna yoyote ambapo mti mmoja unaweza kuzaa matunda ya miti mingi mingine. Kisha akaanza kuomba kuwa apate msukumo wa ufunguo wa kufungulia zinguo. Akaita: “Ewe mtawala wa mahali hapa! Nimejikuta niko kwako na ninajikinga kwako. Mimi ni mtumishi wako na ninataka kukufurahisha. Ninakutafuta wewe.” Baada ya kufanya maombi hayo, ghafla kuta za kisima zikaachia na mlango ukafungua bustani nzuri sana. Kwa hakika, mdomo wa joka uligeuka kuwa mlango, na huyo joka na simba wakageuka kuwa wahudumu wawili, wakamkaribisha ndani. Simba aligeuka kuwa farasi mtiifu kwake. Ewe nafsi yangu iliyozembea! Na ewe rafiki yangu wa kufikirika! Njoo! Hebu tulinganishe nafasi za ndugu hawa wawili ili tuweze kuona jinsi heri inavyopatikana kwenye heri na shari inavyoletwa na shari. Hebu tuchunguze. Angalia, msafiri asiye na furaha katika njia ya upande wa kushoto kwa muda wote anatetemeka kwa hofu huku akisubiri kuingia mdomoni mwa joka, ilhali mwenye bahati amealikwa katika bustani nzuri iliyochanua maua na kujaa matunda. Na moyo wa yule asiyebahatika ukichakazwa na hofu kubwa na woga mkubwa sana, ilhali mwenye bahati anatazama mambo mageni kama somo la kufurahisha, pamoja na hofu yenye furaha na kupenda elimu. Pia mwenye taabu anataabika na adhabu ya kuwa mpweke, kukata tamaa na ukiwa, ilhali mwenye bahati ana furaha, huku akiwa na matumaini makubwa, shauku na hisia ya kumiliki. Zaidi ya hayo, yule asiyebahatika anajiona kama mfungwa anayekabiliwa na mashambulizi ya wanyama wa mwitu, ilhali aliyebahatika ni mgeni wa heshima aliye na urafiki na akijifurahisha kwa kutumia watumishi wa kigeni wa mwenyeji mkarimu. Pia yule asiye na furaha anaharakisha adhabu zake kwa kujiingiza kwenye matunda ambayo kwa juu juu ni matamu lakini yana sumu kwa hakika. Kwa kuwa matunda ni sampuli, kuna ruhusa ya kuyaonja ili kutafuta ya halisi na kuwa wateja kwa ajili ya matunda hayo, lakini hairuhusiwi kuyala kwa ulafi kama mnyama. Mwenye bahati anayaonja na kulielewa jambo hilo, anaahirisha kuyala na anafurahia kusubiri. Zaidi ya hivyo, yule asiyebahatika anajifanyia ubaya yeye mwenyewe, kwani kutokana na ukosefu wake wa utambuzi, anafanya ukweli na hali ambazo ni dhahiri kama mwangaza wa mchana kuwa giza na hofu kandamizi kuwa madanganyo ya kishetani. Hastahiki huruma, wala hana haki ya kumlalamikia yeyote. Kwa mfano, kama mtu wa dhifa ya kupendeza katika bustani nzuri wakati wa majira ya joto baina ya marafiki anajilewesha kwa ulevi mchafu, halafu anadhania ana njaa na yuko uchi katikati ya majira ya baridi baina ya wanyama na kuanza kupiga kelele na kulia, hastahiki kuhurumiwa, anajifanyia makosa yeye mwenyewe na anawatukana rafiki zake kwa kuwafikiria kuwa ni wanyama wa mwituni. Ndugu yule mwenye mikosi yuko kama hivyo, ilhali aliyebahatika anaona ukweli. Na ukweli ni mzuri. Kwa kuutambua uzuri wa ukweli, ndugu yule mwenye bahati anaheshimika kwa mwenye kumiliki ukweli, basi anastahiki kupata huruma zake. Hivyo, maana ya agizo la Qur’an, “Jua kuwa shari inatokana na wewe mwenyewe na heri inatokana na wewe mwenyewe,” inadhihirika. Kama unalinganisha tofauti nyinginezo kwa namna hiyohiyo, utafahamu kuwa nafsi yenye kuamrisha maovu ya ndugu wa kwanza imemuandalia namna ya jahanamu, ilhali nia njema, tabia njema na fikra njema za huyo mwingine vimemruhusu kupata neema nyingi, uzoefu, furaha ya kweli na mafanikio; na kutenda kulingana nayo. Ewe nafsi yangu! Na ewe unayesikiliza kisa hiki pamoja na nafsi yangu! Kama hutaki kuwa ndugu mkosa bahati na unataka uwe yule aliyebahatika, sikiliza Qur’an, tii maagizo yake, yang’ang’anie na utende kulingana nayo. Kama umeelewa ukweli katika mlinganisho huu, utaweza kuyafanya hayo yaendane na ukweli wa dini, dunia, mwanadamu na kumuamini Allah. Nitayasema yaliyo muhimu, halafu utachimbua mwenyewe nukta ndogo ndogo. Basi angalia, kati ya ndugu hao wawili, mmoja ni roho yenye kuamini na moyo ulioongoka, mwingine ni roho ya kikafiri na moyo uliokengeuka. Kuhusu njia hizo mbili, ile ya kulia ni njia ya Qur’an na kumuamini Allah, ilhali ile ya kushoto ni njia ya uasi na ukanushaji. Bustani iliyo njiani ni maisha ya mpito ya mwanadamu katika jamii na ustawi wa mwanadamu, ambapo heri na shari, na mambo mema na mabaya, masafi na machafu yanapatikana kwa pamoja. Mtu mwenye akili ni yule anayetenda kwa kufuata kanuni: “Chukua chema na kisafi na uache kibaya na kichafu,” na anasonga mbele huku akiwa na moyo mtulivu. Ama kuhusu jangwa, ni dunia na ulimwengu huu. Simba ni mauti na saa iliyopangwa. Kisima ni mwili wa mwanadamu na muda wa uhai wake, ilhali yadi zake sitini zinaashiria muda wa kawaida wa uhai wa miaka sitini. Mti ni kipindi cha uhai na nguvu ya uhai. wanyama wawili hao, mmoja mweupe na mwingine mweusi ni usiku na mchana. Joka ni njia ya kwenda kwenye ulimwengu wa Kati na Kati na banda la maonesho ya akhera, ambalo mdomo wake ni kaburi. Lakini kwa muumini, mdomo huo ni mlango wa kutoka gerezani na kuingia bustanini. Nyoka wenye sumu ni majanga ya duniani. Kwa muumini, hayo ni kama maonyo ya upole ya Allah na fadhila za Mwingi wa Rehema ili kumzuia asiteleze na kutumbukia kwenye usingizi wa kughafilika. Matunda ya kwenye mti ni neema za duniani ambazo Mwingi wa Ukarimu ameyaweka katika namna ya orodha ya neema za akhera, nayo pia ni mifano na maonyo, na pia ni sampuli zenye kuwaita wateja kwenye matunda ya Peponi. Mti unaozaa matunda mengi ya aina mbalimbali licha ya kuwa ni mti mmoja unaashiria mhuri wa umiliki wa kiungu na mamlaka. Kwani ili “kufanya vitu vyote kutokana na jambo moja,” yaani, kufanya mimea na matunda yote kutokana na udongo, na kuwaumba wanyama wote kutokana na kimiminika, na kuumba mikono na miguu na viungo vyote vya wanyama kutokana na chakula cha kawaida, pamoja na “kufanya vitu vyote kuwa kimoja,” yaani, ufundi kama vile kufuma ngozi ya kawaida na kufanya minofu mahususi kwa kila mnyama kutokana na aina nyingi sana za vyakula wanavyokula wanyama, ni mhuri usioigika na wa kipekee wa Mmiliki wa tangu na tangu na wa milele, Mmoja, Mwenye Kutegemewa Milele. Kwa hakika, ili kitu kimoja kukifanya kuwa vitu vyote na vitu vyote kuvifanya viwe kimoja ni dalili, alama, ya kipekee kwa Muumbaji wa vitu vyote, Mwenye uwezo wa kila kitu. Kuhusu zinguo, ni fumbo la lengo la kuumbwa ambalo hupatiwa ufumbuzi kwa fumbo la imani. Ufunguo ni “Hakuna wa haki kuabudiwa isipokuwa Allah,” na “Allah, hakuna wa haki kuabudiwa isipokuwa Yeye, wa milele, Mwenye Kujitosha.” Mdomo wa joka kubadilika na kuwa mlango wa kuingia katika bustani ni dalili kuwa, ingawa kwa wapotovu na waasi, kaburi ni mlango wenye kufunguka, katika ukiwa na kusahauliwa, kuelekea kaburi kama gereza la chini ya ardhi na jembamba kama tumbo la joka, lakini kwa watu wa Qur’an na imani, ni mlango unaofunguka kutoka mahali pa mtihani na kwenda kuelekea mabustani ya Peponi, na kutoka katika taabu za maisha hadi kwenye rehema za Mwingi wa Rehema. Simba katili kubadilika kuwa mtumishi rafiki na kipando kitiifu ni dalili kuwa, ingawa kwa wapotovu, kifo ni kichungu, kuachana milele na wapenzi wao wote, na utolewaji kutoka katika pepo ya ulaghai ya duniani na katika kuingia katika majonzi na ukiwa na kuingia katika gereza la chini ya ardhi la kaburi, kwa watu wa Qur’an na uongofu ni njia ya kuwakutanisha marafiki wote wa zamani na wapenzi ambao tayari wameshakwenda akhera, na njia ya kuingia makazi yao ya kweli na mahali pa furaha ya milele. Ni mwaliko wa kwenye malisho ya peponi kutoka gereza la dunia, na wakati wa kupokea malipo yaliyotolewa kwa ukarimu wa Mwingi wa Rehema Mwenye Kurehemu kwa huduma kutokana na huduma alizofanyiwa na kuondolewa kutoka katika taabu za majukumu ya kimaisha, na mapumziko kutoka katika ugumu na maagizo ya ibada na mtihani. Kwa Ufupi: Mwenye kuyafanya maisha haya ya mpito kuwa ndio lengo lake kwa hakika yupo Jahanamu hata kama kwa juu juu atajiona yuko Peponi, na mwenye kugeukia kwa umakini wote kwenye uzima wa milele atapata furaha ya sehemu zote mbili, duniani na akhera. Vyovyote ilivyo ngumu na ya dhiki, dunia hii ni kwa ajili yake, kwa kuwa anaiona kama chumba cha kusubiria kwa ajili ya Pepo, anaivumilia na kushukuru katika hali ya subira. اَللّٰهُمَّ اجْعَلْنَا مِنْ اَهْلِ السَّعَادَةِ وَالسَّلَامَةِ وَالْقُرْآنِ وَالْاِيمَانِ آمِينَ ❀ اَللّٰهُمَّ صَلِّ وَسَلِّمْ عَلٰى سَيِّدِنَا مُحَمَّدٍ وَعَلٰى آلِهِ وَصَحْبِهِ بِعَدَدِ جَمِيعِ الْحُرُوفَاتِ الْمُتَشَكِّلَةِ فِي جَمِيعِ الْكَلِمَاتِ الْمُتَمَثِّلَةِ بِاِذْنِ الرَحْمٰنِ فِي مَرَايَا تَمَوُّجَاتِ الْهَوَاءِ عِنْدَ قِرَائَةِ كُلِّ كَلِمَةٍ مِنَ الْقُرْآنِ مِنْ كُلِّ قَارِئٍ مِنْ اَوَّلِ النُّزُولِ اِلٰى آخِرِ الزَّمَانِ وَارْحَمْنَا وَوَالِدَيْنَا وَارْحَمِ الْمُؤْمِنِينَ وَالْمُؤْمِنَاتِ بِعَدَدِهَا بِرَحْمَتِكَ يَا اَرْحَمَ الرَّاحِمِينَ ❀ آمِينَ وَالْحَمْدُ لِلّٰهِ رَبِّ الْعَالَمِينَ

Private reading note

This note stays on this device and is never uploaded to a server.

Up to 1,200 characters