Dalili za Kiama Masuala ya “Kizuizi cha Dhul Karnaini”, “Yajuja na Majuja” na “Dalili nyingine za Kiama” tumezitafiti katika kitabu chetu kilichochapishwa “Al-Muhaakamaat” kilichotungwa kabla ya miaka thelathini (Unakusudiwa mwaka 1911) na tumeweka masuala ishirini yanayohusu tafiti hizo ili yawe ni ukamilisho wake – sehemu ya muswada wake imeandikwa kabla ya miaka kumi na mitatu – isipokuwa imerekebishwa kwa kuitikia matakwa ya rafiki kipenzi na ikawa ni Mwale wa tano. Otuz Birinci Mektup’tan Otuz Birinci Lem’a’nın Beşinci Şuâ’ıdır. Tanbihi: Kwanza yasomwe masuala yanayokuja baada ya utangulizi ili lifahamike kusudio la utangulizi. بِسْمِ اللّٰهِ الرَّحْمٰنِ الرَّحِيمِ Hakika imeandikwa nukta nzuri katika nukta za aya tukufu: فَقَدْ جَاء أَشْرَاطُهَا katika wakati wa sasa na hiyo ni kwa kuilinda akida ya waumini wa kawaida, na kuihifadhi kutokana na utata. Na kwa vile sehemu ya Hadithi za Mtume zenye kueleza kuhusu matukio yatakayotokea zama za mwisho zinabeba maana ya kina sana, kama (Mutashabih) za Qur’an; hazifasiriwi kama (Muhkamaat), na si kila mtu anaweza kuzielewa, bali huenda wanazuoni wakazifafanua badala ya kuzifasiri, Na fafanuzi zake hufahamika baada ya kutokea kwa tukio, na hapo muradi wake hufahamika, kwa madhumuni ya aya tukufu: وَمَا يَعْلَمُ تَأْوِيلَهُ إِلاَّ اللّهُ وَالرَّاسِخُونَ فِي الْعِلْمِ Na hakika hizo hubainishwa na waliobobea katika elimu na wanasema: آمَنَّا بِهِ كُلٌّ مِّنْ عِندِ رَبِّنَا Hakika “Mwale huu wa Tano” una utangulizi na masuala ishirini na tatu.
Source text is preserved. When a suitable model is available, translation is displayed separately.
Şualar
The Fifth Ray
Ni ibara ya nukta tano:
Hakika ya Imani na taklifu, ni mtihani, jaribio na ushindani ndani ya duara la hiari, basi masuala yake hayatakuwa ni ya kinadharia yasiyofahamika na yasiyokuwa ya wazi na ya kina na ambayo yapo katika haja ya jaribio na kuzingatia sana, yapo wazi uwazi wa kubainika, kiasi ambacho kila mmoja anayasadikisha atake asitake; Ili ibainike imani ya Abubakar na ukafiri wa Abu Jahali, ili waumini wawe juu ya waliokuwa juu na waporomoke Makafiri kwenda chini ya waliokuwa chini, kwani hakuna taklifu bila ya hiari. Na kwa ajili ya hekima hii miujiza inakuja kwa njia tofauti na kwa sura iliyokuwa nadra. Kisha hakika katika nyumba ya taklifu na mtihani kunakuwa na alama za Kiama na dalili zake ambazo inawezekana kuzishuhudia kwa macho, zisizofahamika na zisizokuwa wazi na zenye kubeba ufafanuzi – kama baadhi za mutashaabihaati za ki-Qur'an – isipokuwa “Alama ya kuchomoza kwa jua kutokea magharibi” hiyo ipo wazi uwazi wa kubainika bila ya hoja, hadi hakika yake inawapeleka wote kwenye kuamini bila ya hiari, na kwa hiyo mlango wa toba wakati huo utajifunga, basi hakutakuwa na thamani ya kuamini wala hakutakuwa na faida ya kufanya toba. Ambapo huwa sawa katika kusadikisha yule anayemiliki Imani kama Abubakar na yule kafiri mkubwa kama Abu Jahali. Bali hata kushuka kwa Issa (a.s) , na kujua kuwa yeye ni Issa (a.s) na si mtu mwingine, hakika hujulikana kwa nuru ya Imani yenye nguvu, na kwamba si kila mmoja anaweza kulijua hilo. Bali hata “Dajjali” na “Sufyani” ni katika wenye kutisha ambao watadhihiri pamoja na dalili za kiama, mwanzo hawatajijua kama wao ndio “Dajjali” na “Sufyani”.
Hakika mambo ya ghaibu ambayo amejulishwa Mtume (s.a.w) hayalingani, sehemu miongoni mwa hayo amejulishwa kwa upambanuzi, basi kwenye sehemu hii hakuna kufanya jambo wala kuingilia kati katu, kama Qur'an tukufu na Muhkamu za Hadithi Qudsi. Na sehemu nyingine kwa hakika amejulishwa kwa ujumla, na jambo la kuzijengea taswira na kuzipambanua likaachwa kwenye Ijtihadi yake (s.a.w) kama Hadithi ambazo zinazungumzia matukio ya kiulimwengu na matukio ya mustakabali ambayo si katika misingi ya Imani. Basi Mtume (s.a.w) ndiye anayesawiri na kupambanua kwa balagha yake – kwa mitindo ya tashbihi na tamthili – mambo hayo kwa kuwafikiana na hekima ya taklifu. Mfano: Ulisikika mshindo katika majilisi ya Mtume (s.a.w) akasema: Hakika hiyo ni sauti ya jiwe limekuwa likibiringia kuelekea Jahanamu tangu miaka sabini, hivi sasa limeshafika kwenye kina chake. Na baada ya kupita dakika chache juu ya tukio hili lenye kusisimua akaja mmoja wao na kumwambia Mtume (s.a.w): Hakika Mnafiki fulani anayekurubia miaka sabini amekufa na ameelekea Jahanamu na ndio mafikio mabaya. Akadhihirisha ufafanuzi wa balagha ya hali ya juu ya maneno ya Mtume (s.a.w). Tanbihi: Haupelekei mtazamo wa Utume kuyatilia umuhimu baadhi ya matukio ya mustakabali ambayo hayaingii kwenye dhumuni la hakika za kiimani.
Nayo ni ibara ya nukta mbili: Ya kwanza: Hakika sehemu katika Hadithi zenye kupokewa katika sura ya tashbihi na tamthili wamepokea watu wa kawaida hakika za kimaada kwa kupita muda, hivyo haionekani kuwa mtazamo wao unaendana na uhalisia, licha ya kuwa ni uhakika uliothibiti. Mfano: Hakika Malaika wawili ambao ni wenye kuibeba ardhi – kama ambavyo Arshi ina wabebaji wake – ambao wapo katika sura ya “Ng’ombe” na “Nyangumi” kwa kuwa wameitwa hivyo watu wa kawaida wamewajengea taswira kuwa ni ng’ombe na nyangumi mkubwa na wa uhakika! Ya pili yake: Hakika sehemu katika Hadithi zimepokewa kwa mujibu wa wingi wa Waislamu katika eneo hilo, au kwa mujibu wa kuwepo hapo serikali ya Kiislamu, au kwa mujibu wa kituo cha ukhalifa wa Kiislamu, lakini imedhaniwa ya kuwa ni yenye kuenea kwa Waislamu wote, na pembe zote za ulimwengu, na licha ya kuwa ni maalumu kwa upande mmoja, ila hakika yake imepokewa kwa yote na kwa ujumla. Mfano: Imepokewa katika Hadithi tukufu: (Hakisimami kiama mpaka isisemwe katika ardhi: Allah.. Allah). Yaani itafungwa milango ya maeneo ya kuleta dhikiri, na itanadiwa adhana na iqama kwa lugha ya Kituruki.
Kama yalivyowekewa pazia mambo ya ghaibu kama ajali na umauti kwa hekima na maslahi mbalimbali, basi hakika ya kiama – ambacho ni sakarati ya umauti wa dunia na ajali ya viumbe na umauti wa wanyama – hakika vilevile kimefichwa kwa maslahi mengi. Kwani laiti kama ajali ingekuwa muda wake unajulikana, uwiano ungeharibika baina ya hofu na matumaini, uwiano huo uliojengwa kwa maslahi na hekima; kwani nusu ya umri ungekuwa ukipita kwenye mghafala mkubwa, ukifuatiwa na hofu kubwa kama mtu anayechungwa hatua kwa hatua kuelekea kwenye kitanzi. Mwisho wa dunia na sakarati yake yaani Kiama inafanana na hili kikamilifu, kwani laiti kama muda wake ungekuwa unajulikana, karne za mwanzo na za kati zisingeliathirika na kushtushwa na kufikiria Akhera isipokua kwa asilimia ndogo. Ama karne nyengine zingekuwa zikiishi kwenye hofu ya daima. Na pasingebaki – kwa muda huo – kwenye maisha starehe wala thamani, wala kwa ibada – ambayo ni mtu kutii kwa hiari yake kwa dhumuni la hofu na kutumaini - kuwa na umuhimu na hekima. Kisha, lau kama wakati wa kiama ungelikuwa unajulikana, sehemu ya hakika za kiimani ingeingia ndani ya mambo ya dhahiri kiakili, yaani watayasadikisha watu wote watake wasitake, na muda huo siri ya taklifu na hekima ya Imani zenye kufungamana na matakwa ya mtu na hiari yake zingeharibika. Na kama hivi yamefichwa mambo ya ghaibu kwa ajili ya maslahi mengi mfano wa haya, akawa mwanaadamu anategemea kuja ajali yake kila dakika kama ambavyo anategemea kubaki duniani, na anayafikiria yote mawili kwa pamoja, na anafanya kila juhudi duniani kwa ajili ya kuelekea Akhera, na kama ambavyo anategemea kusimama kwa Kiama katika kila zama basi vilevile anategemea kudumu kwa dunia ndani yake. Na hapo mwanaadamu atakuwa ni mwenye kumakinika kufanya amali kwa ajili ya maisha ya milele huku naye akiangalia kutoweka kwa dunia, na wakati huo huo anafanya amali kuiimarisha dunia, kana kwamba ataishi milele. Kisha hakika yeye lau kama wakati wa masaibu na mabalaa ungelikuwa unajulikana, angelionja mwanaadamu maudhi na maumivu ya kimaana kwa ajili ya kungojea kutokea msiba na kushuka balaa zaidi na zaidi ya maumivu ya msiba huo huo. Hivyo hekima ya Kiungu na rehema yake iliyoenea imesitiri masaibu, yakawa yaliyojificha na kustiriwa kwa mwanadamu, basi hapati mfano wa maumivu hayo ya kimaanawi. Na hali ya kuwa hakika aghlabu ya matukio ya ghaibu ya kiulimwengu yanakusanya mfano wa hekima hizi, basi kwa hakika imezuiwa kuhabarisha kuhusu ghaibu. Na hata wale ambao wanatoa habari kuhusu ghaibu kwa idhini ya Mola Mlezi, hakika wameeleza kwa sura ya kusharia tu, pamoja na kuficha kidogo pasi na uwazi wenye kufahamika, kwa yale yasiyokuwa katika hakika za kiimani na mambo ya taklifu, na imekuwa hivyo ili kusiwe na uchache wa heshima na kutotekeleza kikamilifu sharia ya Kiungu: قُل لَّا يَعْلَمُ مَن فِي السَّمَاوَاتِ وَالْأَرْضِ الْغَيْبَ إِلَّا اللَّهُ Bali hata bishara zilizopokelewa katika haki ya Mtume wetu mtukufu (s.a.w) katika Taurati, Injili na Zaburi, hakika zimekuja na kitu kisichofahamika na kutokuwa wazi, hali ambayo imewakemea watu wa vitabu hivyo kuzifafanua ishara hizo basi hawakuneemeka na Imani ya Mtume Mtukufu (s.a.w). Ama masuala ambayo ni katika itikadi za kiimani basi kwa muktadha wa hekima ya taklifu kuna haja ya kufikisha kuliko aminika na uwazi uliotimia na ukweli kamili wenye kujirejearejea. Kwa ajili hiyo Qur'an na Mfikishaji wake Mwaminifu (s.a.w) imepambanua na tumebainisha mambo ya Akhera kwa ubainifu timilifu, wakati ambapo viwili hivyo vimetaja matukio ya kidunia ya mustakabali kwa jumla.
Hakika yamepokewa mambo yenye kufurutu – zaidi ya kawaida – ambayo yanahusu zama za “Dajjali wawili” – yaani Dajjali wa Waislamu na Dajjali wa mkubwa – ni yenye kuunganishwa na kutajwa kwao, yakadhaniwa kana kwamba yatachimbuka kutoka kwenye dhati ya haiba zao na imefahamika hivyo. Kwa ajili hiyo riwaya hizo zimekuwa ni katika mutashaabihati, kwa kufichika maana. Mfano: Kuzunguka kwake kwa ndege na gari moshi. Na mfano: Hakika imekua mashuhuri: Kwamba shetani ambaye anamtumikia Dajjali wa Waislamu atapiga ukelele wakati wa kufa kwake katika eneo la “Dikilitaş” katika Istanbul ukelele ambao watu wote watausikia kuwa “hakika yeye amekufa”, yaani itatangazwa kwenye redio, kutangazwa kwa ajabu, mashetani wenyewe watatahayari kwa ukelele huo. Kisha hakika ya hali za kutisha na taratibu za kushangaza ambazo zinahusu hukumu ya Dajjali, utawala wake, shirika lake na serikali yake, zimepokewa ni zenye kukutana na haiba yake, kana kwamba zina uhusiano na dhati yake, kwa ajili hiyo maana imefichwa na kusitiriwa. Mfano: Kuna mapokeo kwa maana hii: Kuwa yeye anamiliki nguvu na kudumu ambapo hataweza yeyote kumuua ila Sayyidina Issa (a.s) na kama si hivyo hakuna njia ya kumuua. Na hii ina maana: Kuwa ambayo itavunja mfumo wake na utawala wake hatari wenye kutisha na kummaliza kikamilifu si kingine isipokuwa ni dini takatifu ya mbinguni itakayodhihiri kwa watu wa Issa, basi watafuata hakika za Qur'an, na wataungana nazo. Dini hii ya Issa ndio ambayo kwa kushuka kwake Issa (a.s) itafuta mfumo huo wa kukanusha Mungu na itammaliza kikamilifu, na kama si hivyo mtu huyo Dajjali yawezekana akauliwa kwa bakteria au maradhi madogo sana kama mafua. Kisha hakika ya sehemu katika tafsiri za baadhi ya wapokezi na hukumu yao, - inayotokana na juhudi zao binafsi, ambazo zinaweza kuwa za makosa – hakika imechanganyika na matini ya Hadithi ya Mtume, basi inashabihishwa kuwa nayo ni katika matini ya Hadithi hiyo. Na hapo maana inajiziba na kujificha, kwani haidhihiri kuwa Hadithi inaendana na uhalisia, na kwa hivyo inaingia ndani ya hukumu ya Mutashaabihi. Kisha mtu wa kimaanawi wa kikundi na jamii hakuwa wazi kabla, kama alivyo wakati wa sasa, kwani fikra ilikuwa ni ya mtu mmoja mmoja na kumtilia maanani mtu ndio aghlabu; hivyo zimeegemezwa taratibu kubwa kwa kundi na sifa zake kubwa kwa wale ambao wanaliongoza kundi hilo, na hapo husawiriwa viongozi hao kwa taswira ya ajabu kwamba wao wanamiliki sifa za jumla zenye kufurutu, na maumbo makubwa yanayozidi mara mia ya yale waliyokuwa nayo, na kwamba wao wana nguvu na uwezo kupita kawaida, ili ziendane na hizo taratibu za kutisha. Na hali ni kuwa taswira hii haiendani na uhalisia. Hivyo yamekuwa mapokeo hayo ni mutashaabiha. Kisha, hakika yake licha ya kubainika kati ya sifa za “Dajjali wawili” na kuhitalifiana hali zao, jambo linakanganyika katika yale mapokeo yaliyopokewa kwa sura yake iliyoachiwa huria, basi hii hudhaniwa ndio ile. Kisha hakika za “Mahdi Mkubwa” hazifanani na hali za Mahdi waliomtangulia, katika mapokeo yanayowaashiria, basi mapokeo hayo yanakuwa katika hukumu ya Mutashaabihi. Hakika imamu Ali (r.a) anamtaja “Dajjali wa Waislamu” tu. Utangulizi umeisha. Tunaanza masuala hayo. Kati ya mamia ya mifano yenye kutoa dalili juu ya matukio ya ghaibu – kwa muda huu – kwa msaada wa Allah na taufiki yake yatabainishwa masuala ishirini na tatu – kwa muhtasari sana – maswala ambayo wamefanya juhudi wakanusha Mungu kuyavumisha kwa lengo la kuharibu itikadi za Waislamu wa kawaida. Hivi hazikutoka patupu dhana zao, kwani hakika kudhihiri mng’ao wa muujiza wa Mtume Mtukufu katika kila suala miongoni mwa masuala hayo na kuthibitisha fafanuzi zake za kweli na kuziweka wazi, kwa idhini ya Allah itakuwa ni madai ya nguvu na sababu muhimu ya kuegemeza itikadi ya watu wa kawaida na kuithibitisha Imani yao. Hili ndilo ninalolitarajia kutoka kwa rehema ya Allah Mlezi na Mwenye kurehemu, na ninamwomba Allah (s.w) asitiri dhambi zangu na makosa yangu kwa msamaha wake usio na kifani. Hakika Yeye ni Msikivu na Mwenye kujibu dua za waja wake.
Masuala ya Mwale wa Tano
Imepokewa: Kuwa “Sufyani” naye ni katika watu wa zama za mwisho kitatoboka kiganja chake. Hakika moja ya njia za ufafanuzi wa hili na Allah ndiye Mjuzi zaidi: Hayatabaki mali kwenye kiganja chake, kwa kukithirisha kwake kufanya israfu na kuyaharibu katika upumbavu, upuuzi na mambo machafu. Basi mali yatamtoka kwenye kiganja chake na kuyafanyia israfu. Mfano: “fulani kiganja chake kimetoboka”. Yaani ni mwenye kuyatumia vibaya na kuyafanyia israfu. Basi “Sufyani” anawahimiza watu kufanya israfu, anawachochea kuwa na pupa kubwa na kuwatia kwenye tamaa kubwa. Basi anawadhalilisha kupitia madhaifu yao hayo kufikia malengo yake. Hiki ndicho kilichobainishwa na Hadithi tukufu na kutueleza kuwa: Kwamba mwenye kufanya israfu atakua ni katika mateka wake, atataka msaada kwake na atamnyenyekea.
Imepokewa: Kuwa mtu atishae – katika watu wa zama za mwisho – ataamka asubuhi na tahamaki kwenye paji lake la uso kumeandikwa: Huyu ni kafiri. Hakika ufafanuzi wa hili, na Allah ndiye Mjuzi zaidi wa kupatia, ni kuwa: Hakika huyo “Sufyani” atavaa kofia ya kizungu, na atawalazimisha watu kuivaa. Lakini itahusishwa kuvaliwa na watu wote kwa nguvu na sheria, na kofia hio itaongoka kwa idhini ya Allah, ambapo itampelekea mtu kusujudu. Kwa hiyo atakayelazimishwa aivae bila ya kupenda hatokuwa kafiri.
Imepokewa: Kuwa watawala wakandamizaji wa zama za mwisho, na hasa hasa Dajjali watakuwa na Pepo na Moto za bandia. Hakika moja ya njia za ufafanu wa hili na Allah ndiye Mjuzi ni: Kuwa ni ishara ya yaliyokuwemo katika idara za kiserikali katika hali kinzani na zenye kupingana. Kama shule za msingi na gereza, mojawapo ni sura iliyopotoshwa ya Mahuril-ain na Wavulana wa peponi, na nyingineyo ni sehemu ya mateso na gereza.
Imepokewa: Kwamba hatobaki mwenye kusema: Allah.. Allah katika zama za mwisho. Hakika ufafanuzi wa hili – na hakuna ajuae ghaibu ila Allah – ni: Kwamba pande zinazotajwa ndani yake “Allah.. Allah.. Allah”, na maeneo ya dhikiri na madrasa za kidini milango yake itafungwa, na litawekwa jina lingine badala ya jina la Allah (s.w) katika nembo za Kiislamu kama vile adhana na kukimu sala. Na kama si hivyo basi riwaya hii haina maana ya kuwa watu wote wataingia katika ukafiri wa moja kwa moja; kwa sababu kumkanusha Allah kuko mbali na akili kuliko kuukanusha ulimwengu, kwani akili haikubali watu wengi kutumbukia katika ukanushaji huu, ukiachilia mbali wote. Kwa kujua kwamba makafiri hawakanushi kuwepo kwa Allah bali akili zao zinapotea kwenye kufanya upekuzi wa sifa zake tukufu (s.w). Na ufafanuzi wake mwingine ni: Kwamba roho za waumini zitatolewa karibu na kusimama kwa Kiama ili wasije wakaona vitisho vya matukio yake, hivyo basi Kiama kitazuka vichwani mwa makafiri peke yao.
Imepokewa: Kwamba Dajjali na mfano wake watadai uungu katika zama za mwisho na kuwalazimisha watu wawasujudie. Moja ya njia za ufafanuzi wa hili, na Allah ndiye Mjuzi zaidi ni: Ikiwa kiongozi mpumbavu anakanusha uwepo wa mfalme, atajenga taswira katika nafsi yake na wengine aina ya ufalme, kila mmoja kwa namna atakavyohukumia, vilevile wale ambao wanaongoza dhehebu la watu wa kimaumbile na kimaada wanajenga picha katika nafsi zao aina fulani ya Rububiyya (Uungu), kila mmoja kwa kiasi cha ngazi yake. Basi - Dajjali - atawaongoza wafuasi wake kuitumikia nguvu yake na atawafanya wawe ni wenye kunyenyekea unyenyekevu wa kumuabudu yeye na masanamu yake, yaani atawafanya wayainamishie vichwa vyao.
Imepokewa: Kuwa fitina ya zama za mwisho ni kubwa kiasi ambacho hakuna yeyote atakayeimiliki nafsi yake hadi umma ukajikinga kutokana nayo tokea karne ya kumi na tatu, kama alivyoamrisha kwayo Mtume (s.a.w), basi umma ukaifanya fitina hiyo kuwa ni uhusiano ili ujikinge na adhabu ya kaburi. Hakika ufafanuzi wa hili na Allah ndiye Mjuzi zaidi wa kupatia ni: Kwamba fitina hizo zinazipeleka upogo nafsi na kuzirubuni na kuzivutia upande wake, na zinazifanya zifitinike kwa ajili yake, basi hapo watu watafanya madhambi kwa hiari yao, bali huenda wakawa ni wenye kujipatia utamu kwazo, kama kuchanganyikana wanawake na wanaume wakiwa uchi katika mabafu ya Kirusi. Kwani wanawake wanajitupa kwenye fitina hizi kwa matakwa yao wenyewe, basi watapotea kwa kile wakibebacho katika kupenda kwao kimaumbile kudhihirisha uzuri wao. Ama wanaume ambao kimaumbile wanatamani uzuri, basi wanapigwa mweleka mbele ya matamanio ya nafsi wakajikuta wanaingia kwenye moto huo mkali, na kuungua, wakiwa ni wenye kusisimkwa kwa furaha. Na hivi ndivyo fitina ya zama hiyo itakavyovutia – kwa sehemu zake za michezo/burudani zake, sinema zake, madisko yake na sehemu za uzushi na kutenda dhambi kubwa-kubwa ndani yake – wenye kuabudu nafsi zenye kuamrisha maovu, wanazunguka pembezoni mwa sehemu hizo kama nondo pembezoni mwa moto, na kuvutika humo wakiwa wamechanganyikiwa na kupumbazika. Na kama si hivyo lau kama ingelikuwa ni kwa kulazimishwa kwa moja kwa moja, isingelikuwa ni kwa hiari ya mtu, na kama hali ni hiyo pasingekuwa na dhambi.
Imepokewa: Kuwa “Sufyani” atakuwa ni msomi mkubwa, na atawapoteza watu kwa elimu, na wanazuoni wengi watamfuata. Hakika ufafanuzi wa hili na Allah ndiye Mjuzi ni: Kwamba yeye kwa ustadi wake, fani zake na elimu yake ya kisiasa atapata nafasi hiyo, kwani hana zitakazomfikisha kwenye utawala kama ilivyo kwa watawala wengine kwa kuwepo kwa kundi fulani, nguvu, au kujinasibisha katika kabila na ukoo au ushujaa au utajiri na mengineyo. Basi kwa akili yake atazidhalilisha akili za wanazuoni wengi, na atawafanya wazunguke katika nyota yake na watatoa fatwa mbalimbali kwa maslahi yake, na atawafanya walimu wengi wawe ni wafuasi wake, na atafanya juhudi kueneza elimu isiyokuwa na masomo ya dini na kuifanya ndio njia yenye kushika hatamu.
Riwaya zinabainisha: Kuwa fitina ya kutisha ya Dajjali itaingia kwenye safu za Waislamu mpaka umma wote utajikinga na fitina hiyo. Hakika ufafanuzi wa hili, na hakuna anayejua ghaibu ila Allah, ni: Kwamba Dajjali wa Waislamu sio Dajjali wa Makafiri, hadi kwamba baadhi ya wanazuoni wahakiki walishasema kama alivyosema Imamu Ali (r.a) Kwamba Dajjali wa Waislamu ni “Sufyani” na atadhihiri baina ya Waislamu na atawafitinisha kwa hadaa na kuzugazuga, wakati ambapo Dajjali mkubwa wa makafiri si “Sufyani”. Na kama si hivyo basi yule asiyeridhia udikteta wa Dajjali mkubwa wa hali zote atauwawa shahidi, na atakayemfuata kwa kulazimishwa na kimabavu hawi kafiri, na pengine asipate dhambi vilevile.
Hakika matukio ya “Sufyani” na matukio ya fitina za zama za mwisho yamesawiriwa katika mapokeo kwamba yatatokea katika maeneo ya Shamu au katika kisiwa cha bara-arabu. Hakika ufafanuzi wa hili na Allah ndiye Mjuzi ni: Kwamba kituo cha ukhalifa hapo awali kilikuwa Iraki, Shamu na Madina, hivyo wapokezi – kwa juhudi zao binafsi – walifasiri na wakasawiri matukio hayo ambayo yanatokea kwenye kitovu cha Dola la Kiislamu – kana kwamba ukhalifa utabaki kuwa hivi – basi wakasema: Katika Shamu... Halab. Wakapambanua kwa juhudi zao binafsi ambayo yamepokewa kwa ujumla katika Hadithi.
Hakika mapokeo yametaja uwezo mkubwa wenye kufurutu ada wa watu wa zama za mwisho. Hakika ufafanuzi wa hili na elimu ipo kwa Allah, ni: Kwamba hiyo ni kinaya ya ukubwa wa haiba ya kimaanawi ambayo wanaiwakilisha. Kama ambavyo amesawiriwa wakati huo kiongozi wa Japani ambaye aliisambaratisha Urusi, kwamba mguu wake mmoja upo katika bahari kuu na mwingine katika ngome ya Port Arthur. Yaani Kwamba haiba ya mtu wa kimaanawi ni kubwa ya kutisha, inasawiri katika mwakilishi wa haiba hiyo na katika maumbo ya mwakilishi huyo mkubwa. Ama uwezo wao wa hali ya juu na nguvu zao zenye kufurutu ada, ni kwa kuwa taratibu zao nyingi ni za uharibifu, kuchochea matamanio na kusisimua raghba, jambo ambalo linadhihirisha ushindani usio wa kawaida, kwani kubomoa ni jambo jepesi. Kwani njiti moja ya kiberiti inaweza kuunguza kijiji kizima, na kuchochea matamanio na kusisimua raghba kunaenea haraka kutokana na nafsi kupenda hayo.
Imepokewa: Hakika katika zama za mwisho wanawake arobaini watakuwa na msimamizi mmoja tu. Hakika ya hili lina fafanuzi mbili na Allah ndiye mjuzi zaidi wa kupatia: Ya Kwanza: Hakika ndoa za kisheria zitapungua katika zama hizo au kuondoshwa kabisa, kama ilivyotokea Urusi; basi mtu anayetangatanga aliyeacha kufungamana na mwanamke mmoja, atawasimamia wanawake waovu arobaini. Ya Pili: Hakika hiyo ni kinaya ya kuangamia wanaume wengi katika vita ambavyo vitatokea katika fitina hiyo. Na kuwa wengi watakaozaliwa ni wanawake kwa mujibu wa hekima ya kiungu. Na huenda ikachochea wanawake kuwa huru kwa uhuru wa hali zote kwa shahawa zao na kuwashinda kimaumbile waume zao. Jambo ambalo litasababisha mtoto kufanana na sura yake hivyo wanawake watakuwa ni wengi sana kwa amri ya kiungu.
Imepokewa katika mapokeo: Kuwa siku moja ya Dajjali ni sawa na mwaka mmoja, na siku ya pili ni mwezi mmoja, na ya tatu ni wiki moja, na ya nne ni kama masiku mengine. Hili lina fafanuzi mbili, na hakuna anayejua ghaibu ila Allah. Wa Kwanza: Kuwa hiyo ni ishara na kinaya ya kudhihiri Dajjali mkubwa katika eneo la ncha ya kaskazini na upande wa kaskazini mwa ulimwengu; kwani mwaka katika eneo la ncha ya kaskazini ni kama mchana na usiku. Lau mmoja wao atasafiri kutokea huko na kueleka pande zetu kwa gari moshi siku nzima ataliona jua halizami mwezi mzima katika Kiangazi. Na atakapokurubia kwa gari siku nyingine ataliona jua wiki nzima. Na hakika nilikuwa karibu na sehemu hii wakati nilipokuwa mateka huko. Kwa maana kwamba hii ni habari ya kimuujiza kuwa Dajjali mkubwa atapita kutokea kaskazini kuelekea upande huu. Ama ufafanuzi wa pili ni: Kuwa kuna masiku matatu kwa maana duru tatu za utawala wa kimabavu wa Dajjali mkubwa na Dajjali wa Waislamu: Siku yake ya kwanza: Yaani katika duru ya serikali yake, atafanya harakati kubwa ambazo zisizoweza kumalizika ndani ya miaka mia tatu. Siku yake ya pili, yaani duru yake ya pili: Kuwa atafanya harakati ndani ya mwaka mmoja ambazo haiwezekani kuzifanya ndani ya miaka thelathini. Siku yake ya tatu na duru yake: Atafanya mabadiliko katika mwaka mmoja ambayo hayawezi kufanywa ndani ya muda wa miaka kumi. Siku yake ya nne na duru yake: Itakuwa ya kawaida, hatafanya kitu isipokuwa atajitahidi kuilinda hali ya mambo. Na hivi ndivyo Mtume Mtukufu (s.a.w) ameuhabarisha umati wake kwa balagha yake ya upeo wa juu kitakachotokea katika matokeo ya mustakabali.
Katika mapokeo sahihi: Hakika Issa (a.s) atamuua Dajjali mkubwa. Na hili vilevile lina pande mbili na elimu ipo kwa Allah: Upande wa kwanza: Kwamba Dajjali anayejihifadhi kwa mambo yake yenye kufurutu ada ambayo anawalaghai watu kwayo na kuwadhalilisha kwa kutumia uchawi na kiini macho na mizimu na mfano wake, hataweza mtu kumuua na kubadilisha mwenendo wake isipokuwa mwenye kufurutu ada, na mwenye miujiza na mwenye kuridhiwa na wote na ambaye ni mwingi wa uhusiano na mafungamano, na watu wengi kuuamini utume wake, huyo ni Mtume Issa (a.s). Upande wa pili ni: Kuwa ambaye ataiua haiba ya kimaanawi ya mtu Dajjali – mwenye kuuliwa kwa upanga wa mtu Issa (a.s) – na ataiangamiza dhana iliyotapakaa ya kumkana Mungu na umaada wa kushangaza aliyouunda, na atayaondosha yale anayoyalingania katika ukafiri kwa kukanusha Uluhiyya (Uungu), nao ni maruhani wa Kinasara, basi maruhani hawa watamuangamiza – na watamuua kimaana – kwa nguvu yenye kuchimbuka kutoka kwenye kuchanganya kwao hakika ya kinasara na hakika za Kiislamu. Hadi kwamba yaliyopokewa kuwa Issa (a.s) atashuka na kumfuata Al-Mahdiy katika swala, yanaashiria kwenye itifaki hii, na kutawala kwa ukweli wa Qur’an na nguvu yake.
Imepokewa: Kwamba Wayahudi ndio nguvu kuu ya Dajjali na wanamfuata kwa kumtii. (a.s) Basi tunaweza kusema na Allah ndiye Mjuzi zaidi: Hakika sehemu ya ufafanuzi wa mapokeo haya umethibiti Urusi, Kwani Wayahudi ambao walizipima dhulma licha ya kuwa serikali zote zilijikusanya kwa wingi huko Ujerumani, ili walipize kisasi kwa madola na watu. Na Myahudi (Trotoski) ilikuwa ana mkono mrefu katika kuasisi taasisi ya Ukomunisti, mpaka wakamfikisha kwenye uongozi mkuu, na baada ya hapo walimueka kwenye uongozi wa serikali ya Urusi kumrithi “Linin” ambaye amemlea, wakaibomoa Urusi vibaya-vibaya na wakaangamiza mavuno yake ya miaka elfu moja. Na wakadhihirisha – yaani Wayahudi – kwa kufanya hivyo kwamba wao ni katika taasisi ya Dajjali mkubwa na ni watekelezaji wa kazi zake. Na hakika waliuteteresha muundo wa serikali nyengine vilevile na wakaacha ndani yake migogoro na machafuko.
Hakika Qur'an tukufu ambayo inasimulia matukio ya Yaajuju na Maajuju kwa ujumla Hadithi tukufu inayataja kwa upambanuzi kidogo, lakini upambanuzi huo si Muhkam kama ule ujumla wa Qur'an bali huenda yakahesabiwa ni katika Mutashaabih kwa kiasi fulani, basi yakahitaji ufafanuzi bali yatahitaji maelezo kwa kuchanganyika na Ijtihadi za wapokezi ndani yake. Hakika ufafanuzi wa hili na hakuna ajuae ghaibu ila Allah ni: Hakika hiyo ni kinaya na ishara kuwa makabila ya Manjuri na Maghuli – ambao Qur'an inawaita kwa lugha ya Mbinguni Yaajuju na Maajuju – wataubomoa ulimwengu wote katika zama zijazo kama walivyovamia mara kadhaa Asia na Ulaya pamoja na makabila ya China yale yanayowazunguka, na wakaeneza ndani yake fitina na shari. Hata magaidi mashuhuri katika taasisi za wakomunisti hivi sasa wananasibika nao. Naam, hakika nadharia ya ujamaa ilizalika kwenye mapinduzi ya Ufaransa na ikalelewa na sera zake hadi kupata huru, na ilivyokuwa nadharia hii ya ujamaa inalingania kwenye kubomoa moja ya sehemu takatifu basi hatimaye iligeuka na kuwa chama cha Bolshevik. Na hakika vilevile Bolshevik ilieneza mbegu za ufisadi ili kuzivunja sehemu nyingi takatifu na tabia njema na za kiutu. Na mbegu hizo kwa hakika hatimaye zitatoa matango mwitu ya ghasia na ugaidi ambayo hayajui mpaka wa kitu, wala hauwezi kupimika. Kwani moyo wa kibinaadamu utakapong’olewa upole, huruma na heshima basi akili na uhodari vitatawala – muda huo – katika hatamu ya mwanaadamu na vitawafanya watu hao kuwa kama wanyama wakali wenye kudhuru na mbwa vichaa basi udhibiti wa kisiasa hautafaa kitu kwao. Hakika zizi lenye rutuba zaidi kwa nadharia ya vurugu na ugaidi ni zile sehemu zenye msongamano wa wakandamizwaji, na makabila yaliyo mbali na maendeleo, na mbali na serikali na dola, na ambazo zimezoeleka kwa uporaji na uvamizi. Basi masharti haya yanaendana na makabila ya Manjur na Maghur na sehemu katika makabila ya (Qargheez) ambayo walikuwa ndio sababu ya kujengwa ukuta wa china kwa urefu wa siku arobaini na ambao unaingia kwenye maajabu saba ya dunia. Na hivi basi Mtume Mtukufu (s.a.w) ambaye anafasiri yaliyokusanywa na Qur'an kwa hakika ameyatolea habari kwa njia ya kimuujiza, wenye kuthibiti.
Katika muktadha wa Issa (a.s) kumuua Dajjali mapokeo yanabainisha kuwa Dajjali ana umbo kubwa lenye kufurutu ada na urefu mpaka anaipita minara kwa urefu, na kwamba Issa (a.s) ni mdogo sana kulinganisha naye. Hakika moja ya njia ya ufafanuzi wa hili ni, na hapana anayejua ghaibu ila Allah inatakikana iwe hivi: Hakika hiyo ni kinaya na ishara kuwa wale ambao wanamjua Issa (a.s) na kumfuata kwa nuru ya Imani – na ni kundi la maruhaniyyina wenye kupigania jihadi – wao ni wachache sana kulinganisha na jeshi la Dajjali kielimu na kimaada yaani kisomi na kijeshi.
Imesimuliwa: kuwa dunia itasikia kudhihiri kwa Dajjali siku ya kudhihiri kwake, na atatembea ardhini kwa muda wa siku arobaini, na ana punda naye ni mnyama mwenye kufurutu ada. Mapokeo haya ili yasihi yana fafanuzi kadhaa na Allah ni Mjuzi zaidi, ni: Kwamba mapokeo haya yanahabarisha kimuujiza kwamba vyombo vya usafiri na upelelezi vitaendelea katika zama za kudhihiri Dajjali kiasi ambacho tukio moja litasikika katika siku moja pembe zote za dunia, basi atapiga ukelele kwenye redio na wataisikia mashariki na magharibi, na litasomwa tukio hilo katika magazeti na majarida yake. Na kwamba mwanadamu ataweza kutembea katika ulimwengu wote ndani ya siku arobaini. Atayaona mabara yake saba na serikali zake sabini. Basi mapokeo haya yanahabarisha kimuujiza kuhusu telegrafu, simu, redio na ndege kabla ya kudhihiri kwake kwa muda wa karne kumi. Kisha Dajjali hatosikika ulimwenguni kwa kuwa yeye ni Dajjali, bali ni kwa sifa ya Mfalme na Mtawala wa kimabavu kwa hali zote, na kwamba kutembea kwake ardhini si kwa ajili ya kuyapora maeneo yote bali ni kwa ajili ya kuamsha fitina, upotoshaji na ushawishi. Ama mnyama wake na punda wake, ima ni gari moshi ambayo sikio lake moja na kichwa chake ni chimbuko la moto kama moto wa Jahanamu, na sikio lake jingine ni sehemu iliyotandikwa vizuri na yenye kupambwa kama pepo ya uongo. Basi maadui zake atawatupa kwenye kichwa chenye moto na marafiki zake atawaweka kwenye kichwa kilichoandaliwa kwa ajili ya wageni... Au kwamba punda wake na mnyama wake ni gari la ajabu... au ndege... au... (Inalazimu kunyamaza).
Imesimuliwa kuwa: Utakaponyooka umati wangu basi una siku moja, yaani utadumu ufalme wake na utawala wake kwa muda wa miaka elfu moja kudumu kulikotimia na uwezo wa kupitisha mambo, kwa dalili ya aya tukufu: فِي يَوْمٍ كَانَ مِقْدَارُهُ أَلْفَ سَنَةٍ Na kama utaenda upogo basi una nusu siku. Yaani utahifadhi utawala wake na udhibiti wake kwa muda wa takriban miaka mia tano. Hakika mapokeo haya – na Allah ndiye Mjuzi zaidi – si kuhabarisha kuhusu Kiama, bali ni mapokeo yanayohusu nguvu ya Uislamu na utawala wa kiukhalifa. Na hakika yalitimia kivitendo na yakawa ni hakika thabiti na muujiza wa ghaibu. Kwani Dola la Abbasiyya liliishi kwa takribani miaka mia tano mpaka muda ambao watawala wanasiasa walipoteza njia ya kuwa na unyoofu. Ila umma wa Kiislamu kwa ujumla wake uliutunza unyoofu kwa ajili hiyo ukaurefusha ukhalifa wa Othmaniyya, utawala ukadumu kwa takribani miaka elfu moja na mia tatu. Kisha pale wanasiasa wa Othmaniyya waliposhindwa kuutunza unyoofu, kwa mara nyengine ukaishi miaka mia tano kwenye ukhalifa. Basi ukhalifa wa Othmaniyya ukasadikisha habari ya muujiza wa Hadithi hii tukufu kwa kufa kwake. Na ambapo sisi tumeizungumzia hadithi hii katika Risala nyingine, hapa tumeifupisha.
Hakika kuna habari tofauti kuhusu Mahdi ambaye ni katika Ahlul Bayt, na kudhihiri kwake ni katika dalili za Kiama. Hata baadhi ya wanazuoni na mawalii wamehukumu kutangulia kudhihiri kwake. Hakika maana ya mapokeo haya yenye kutofautiana na Allah ndiye Mjuzi zaidi wa lililo sahihi ni: Kuwa Mahdi mkuu ana majukumu na nyadhifa nyingi, pia ana shughuli kwenye limwengu na nyanja nyingi kama ulimwengu wa siasa, ulimwengu wa dini, ulimwengu wa utawala na ulimwengu wa Jihadi. Pia watu wa kila zama wanahitaji mtu kama Mahdi pale wanapogubikwa na kukata tamaa ili aimarishe nguvu yao kimaanawi, au wanahitaji kungojea kuja kwa Mahdi na kudhihiri kwake ili awasaidie wakati huo. Hivyo amedhihiri katika Ahlul Bayt ambaye ni kama Mahdi katika kila duru na kila zama kwa rehema kutoka kwa Allah (s.w), akaitunza sharia ya babu yake mtukufu, na kuhuisha sunna yake tukufu. Mfano: Amedhihiri Mahdi Al-Abbasy kwenye ulimwengu wa siasa na nchi, na amedhihiri Shkekh Al-Kilany na Shah An-Nakshabandi na magwiji wanne na maimamu kumi na mbili na mfano wao katika watukufu kwenye ulimwengu wa dini na Imani, wakatekeleza sehemu ya majukumu ya Mahdi na nyadhifa zake. Kwa kudhihiri hawa na kutenda kwao sehemu ya kazi za Mahdi - ambazo zinaelekea katika kuhuisha sharia na sunna za Mtume (s.a.w ) - na kuwa kwao sehemu ya mtazamo wa Mtume Muhammad (s.a.w), mapokeo yaliyomsimulia Mahdi yametofautiana, ikapelekea sehemu ya watu wa hakika kusema: Kuwa ameshadhihiri katika muda uliyopita. Na kwa hali yoyote ile “Risale-i Nur” imebainisha suala hili, tunaelekeza kwake ila sisi tunasema: Hakuna duniani kote kundi lenye kushikamana, tukufu na lenye heshima linaloweza kuifikia heshima ya Ahlul Bayt na daraja yao, na hakuna kabila lenye kuwafikiana na utukufu wa Ahlul Bayt, wala hakuna jamii au kundi lenye nuru zaidi ya jamii ya Ahlul Bayt. Naam, hakika Ahlul Bayt ambao wamelelewa kwa roho ya hakika ya Qur’an, na kufyonza nuru ya Imani na heshima ya Uislamu wakapanda kwenye makamilifu, na kuzaa mamia ya mashujaa wa kipekee, wakaleta maelfu ya viongozi wa kimaanawi kwa ajili ya kuuongoza umma... hapana budi kuwa wataidhihirishia dunia uadilifu uliokamilika kwa kiongozi wao mkuu Mahdi mkuu, na ustahiki wake kwa kuhuisha sharia ya Muhammad na hakika ya ki-Furqan na Sunna ya Muhammad na kuitangaza na kuitekeleza. Na jambo hili lipo katika upeo wa akili ukiachilia mbali kuwa katika upeo wa ulazima, bali ndio muktadha wa desturi za maisha ya kijamii-kibinaadamu.
Kuchomoza jua kutoka magharibi na kudhihiri mnyama wa ardhini. Ama kuchomoza jua kutoka magharibi ni alama ya wazi ya kusimama Kiama na kutokana na uwazi wake maana yake imekuwa dhahiri haina haja ya tafsiri wala ufafanuzi. Kwani ni tukio la kimbinguni ambalo kwalo mlango wa tauba uliofungamana na hiari ya akili utafungwa... isipokuwa kuna jambo nalo ni kuwa sababu ya dhahiri ya kuchomoza huko – na Allah ndiye mjuzi zaidi – ni: Kuwa wakati tu Qur’an itakapo ondolewa ardhini - ambayo ndiyo akili yake – ardhi itapoteza usahihi wake na hivyo itagongana - kwa idhini ya kiungu – na sayari nyingine, basi itarudi kinyumenyume kwenye mzunguko wake, na mzunguko wake - kwa utashi wa Allah (s.w) - utakuwa kutoka mashariki kwenda magharibi badala ya magharibi kwenda mashariki, na hapo jua litaanza kuchomoza kutoka magharibi. Naam, nguvu ya mvuto wa Qur’an tukufu itakapokatika ambayo ni kamba imara ya Allah na ambayo inaivuta ardhi kwa jua, na tandiko kwa arshi, vizuizi vya tufe la ardhi vitafunguka, na kuendelea kuzunguka mzunguko wa ovyo, na hapo jua litachomoza kutoka magharibi kutokana na kukosekana nidhamu katika mzunguko wake na kwenda kwake kinyumenyume. Na Hadithi ina maana nyingine ni kuwa Kiama kitasimama kutokana na kugongana na sayari nyingine kwa amri ya kiungu iliyokadiriwa. Ama “mnyama wa ardhini” kuna ishara yake katika upeo wa ujumla ndani ya Qur’an tukufu pamoja na maneno ya muhtasari kwa ulimi wa hali yake. Ama ufafanuzi wake kwa sasa siujui barabara na kwa ukinaifu uliyo kamili, kama masuala mengine, ila naweza kusema, na hapana ajuaye ghaibu ila Allah: Kama Allah (s.w) alivyoidhinisha nzige na chawa kufanya maafa kwa watu wa Firauni, na akawapa uwezo (طَيْرًا أَبَابِيلَ) dhidi ya watu wa Abraha waliyokuja kubomoa Kaaba. Vilevile wale wanaopelekwa kwa hiari yao na kwa elimu ya fitina za “Sufyani na Madajjali” wanazama katika uasi na ufisadi, na katika ukanaji Mungu, ukafiri, ukatili na khiyana kwa kichocheo cha ugaidi na fujo anayoishi nayo Yaajuja wa Maajuja, atawatokea mnyama kutoka ardhini – kwa hekima ya kiungu ili kuurejesha usahihi wao – na kuwapa nguvu dhidi yao na kuwaangamiza kabisa. Hakika ya mnyama huyo – na Allah ndiye Mjuzi zaidi – ni aina na sio mnyama mmoja, kwani kama angelikuwa ni mnyama mmoja mkubwa sana, asingelimfikia kila mtu katika kila pahala. Kwa hiyo ni kundi la wanyama lenye kutisha, na huenda ni mnyama kama mchwa anayekula mbao kama aya tukufu inavyoashiria: إِلَّا دَابَّةُ الْأَرْضِ تَأْكُلُ مِنسَأَتَهُ Mnyama huyu pia anakula mifupa ya mwanadamu na kuitoboa kama mchwa anavyotoboa mbao na anakaa katika sehemu zote za mwili wa mwanadamu kuanzia katika meno yake hadi katika kucha zake. Na aya tukufu imemtamkisha mnyama huyu kuhusu Imani ikiashiria: Kuwa waumini wataokoka kwa Baraka ya Imani, na kujiepusha kwao na ujinga, israfu na tabia mbaya. رَبَّنَا لَا تُؤَاخِذ۟نَٓا اِن۟ نَسٖينَٓا اَو۟ اَخ۟طَا۟نَا سُب۟حَانَكَ لَا عِل۟مَ لَنَٓا اِلَّا مَا عَلَّم۟تَنَٓا اِنَّكَ اَن۟تَ ال۟عَلٖيمُ ال۟حَكٖيمُ
Kwenye mapokeo jina la Al-Masihi ameitwa kwalo Issa (a.s) na jina hilo hilo wameitwa Madajjali pia, kama ilivyokuja katika Istiadha: “Kutokana na fitina ya Masihi na Dajjali”. Nini hekima ya jina hilo na nini maana yake? Jibu: Hekima yake – Allah ndiye Mjuzi zaidi – ni kuwa Issa (a.s) ameondosha kwa amri ya Allah sehemu ya takalifu ngumu ambazo zilikuwa katika sharia ya bwana wetu Musa (a.s) na kuhalalisha baadhi ya vinavyotamaniwa na nafsi kama pombe. Hivyo pia ndiyo anavyofanya Dajjali mkubwa, kwa ghilba inayotokana na shetani na nguvu yake. Hivyo hufuta sehemu ya hukumu za sharia ya bwana wetu Issa (a.s) na kuharibu mafungamano ambayo kwayo maisha ya kijamii hupatikana kwa Wanasara na huku wakiandaa mazingira ya fujo na ugaidi na kuja kwa Yajuja na Majuja. Vilevile “Sufyani” ambaye ni Dajjali wa Waislamu anafanya juhudi kuondoa sehemu ya hukumu za sharia za milele za Muhammad (s.a.w ) kwa hila za nafsi iamrishayo maovu na kwa usaidizi wa shetani, na hivyo kuharibu mafungamano ya kimaada na kimaanawi ya wanadamu na kuziachia nafsi zenye kutahayari, zenye ubaguzi na fadhaa kutoka kifungoni mwake ili zipotee na kuzurura. Na hivyo kuondoa vifungamanishi vya kinuru vinavyowafungamanisha watu wa jamii ya kibinaadamu kama heshima na upendo, na kuwalazimisha watu juu ya uhuru ambao ndio dhulma yenyewe, ili nafsi zilizopotea kupambana ndani ya dimbwi la matamanio duni, ikifungua njia kuelekea kwenye ugaidi mbaya na fujo la kutisha ambapo haiwezekani - wakati huo – watu hao kuwa katika nidhamu ila kwa dhulma na ukatili mkali.
Mapokeo yametaja matendo ya kufurutu ada watakayoyafanya Madajjali hao wawili, na kuhusu uwezo wao usio wa kawaida, na kuhusu haiba na utukufu wao, mpaka ikapelekea kwa baadhi ya watu wenye simanzi kuwaegemezea kitu kama Uungu! Hivi ndivyo ilivyokuja katika mapokeo... nini sababu ya hili? Jibu: Na elimu ipo kwa Allah. Ama matendo yao kuwa makubwa na yenye kufurutu ada, ni kwa sababu mengi kati yake huelekea kwenye uharibifu, na kusukuma kwenye matamanio ya nafsi. Hivyo, wanaweza kwa wepesi mkubwa kufanya mambo yasiyo ya kawaida, kwa sababu ni uharibifu. Hadi kwamba kilichosimuliwa katika Hadithi kuwa: “Siku kama mwaka” yaani wanayoyafanikisha ndani ya mwaka mmoja hayawezi kutekelezwa ndani ya miaka mia tatu. Ama sababu ya kudhihiri uwezo wao katika namna ambayo si ya kawaida, kuna sababu na pande nne: Upande wa Kwanza: Kuegemeza kwao kwa dhulma, uzushi na kwa kuhadaa kila kilicho ndani ya serikali zao kubwa za ukandamizaji katika mambo mazuri na maendeleo yaliyopatikana kwa nguvu ya jeshi shujaa na umma shupavu, ndiyo yanayosababisha kudhani kuwa watu wao wana uwezo wa watu elfu moja. Kwa kujua kuwa kanuni na uhakika unahukumu kwamba: Kinachotokana na utendaji wa wengi katika mambo mazuri na chanya, na heshima, na ngawira hugawanywa kwa watu hao na kurejea kwao, wakati ambapo mambo mabaya na hasi, hasara na uharibifu huegemezwa kwenye uongozi wa Mkuu wa kundi na mapungufu yake. Mfano: Ikiwa jeshi litaivamia ngome na kuikomboa, basi heshima ya ushindi na ngawira watakazozipata zitarejea kwenye nguvu ya silaha zao. Ama yakipatikana mambo hasi na hasara basi hurejea kwa kiongozi wao. Na kama hivi ni kinyume cha desturi hii ya msingi iliyojengwa juu ya haki na ukweli wanaoupata viongozi hao wa kutisha kwa ushawishi na hadaa ya upendo wa walioghafilika, ingawa wanastahiki kuchukiwa na watu wote, na hiyo ni kwa kuegemeza kwao mambo mazuri, mambo chanya na maendeleo kwenye nafsi zao na kuegemeza mambo mabaya, mambo hasi, na makosa kwa umma wao masikini. Upande wa Pili na Sababu ya Pili: Hakika Madajjali wote wawili wanaendesha uongozi wao kwa ukandamizaji usiyo na mpaka, ugaidi mkubwa, dhulma kubwa na ukatili wa mwisho kabisa, hivyo huonekana ni uwezo mkubwa. Naam, hakika ukandamizaji wao ni wa ajabu mpaka wanaingilia – kwa kisingizio cha sheria - kwenye moyo wa kila mtu, na mambo yake takatifu, bali hata aina ya nguo zake. Na kuingiza kuwa walinganiaji wa uhuru katika Waislamu na Waturuki - katika zama za mwisho – wameuhisi ukandamizaji huu kabla ya kutokea, wakaishambulia kwa mikuki yao kwa sana, isipokuwa wamehadaika kikamilifu, na kukosea kulenga, kwani walishambulia sehemu iliyo tofauti na kundi lengwa! Ama dhulma yao na ukatili wao ni mbaya kiasi cha kuangamiza, kwa kosa la mtu mmoja vitongoji mia moja. Na kuwaadhibu wasiyo na hatia, na kuhamishwa kutoka sehemu zao na kudhalilishwa. Upande wa Tatu na Sababu ya Tatu: Hakika Madajjali wote wawili wanapata msaada wa mashirika ya siri ya Kiyahudi yenye chuki kubwa dhidi ya Uislamu na Wanasara, na msaada wa shirika jingine la kutisha linalotenda chini ya pazia la uhuru wa wanawake; hata Dajjali wa Waislamu anafanikiwa kuwahadaa kamati za kimasoni, na hivyo kupata upendo wao na uungwaji mkono wao. Hivyo hudhaniwa kuwa wana uwezo mkubwa. Na hivi inafahamika kutokana na ufahamu wa baadhi ya mawalii wema: Kuwa “Dajjali Sufyani” ambaye ataongoza dola la Kiislamu... atakuwa na waziri mkuu mwenye uwezo wa hali ya juu, akili na harakati pamoja na kuwa mbali na kupenda kuonekana, na kutojali umashuhuri na kujulikana... na pia atakuwa na mkuu wa majeshi aliye na ushujaa wa hali ya juu, uwezo, na ukakamavu pamoja na uchangamfu wa kudumu na kutojali umashuhuri... “Dajjali Sufyani” atawatumia kwa malengo yake binafsi, na kuegemeza kwake mambo makubwa wanayoyatenda ambayo wanayafanikisha kwa akili yao, akifaidika na kuwa mbali kwao na ria. Na namna hii... kwa njia hii anaegemeza kwake kinachofanywa na nchi na jeshi kubwa katika kujiimarisha, mapinduzi na maendeleo waliyoyapata kwa msukumo wa haja iliyotokana na vita vya dunia. Na anawasukuma wenye kumshabikia ili waeneze kwa watu kuwa katika haiba yake kuna nguvu ya ajabu yenye kufurutu ada na uwezo usio wa kawaida. Upande wa Nne na Sababu ya Nne: Dajjali mkubwa anamiliki uwezo wa hisia wenye taathira unaofanana na kiini macho na kuiathiri roho, na Dajjali wa Waislamu pia katika jicho lake moja ana nguvu ya udhalilishaji yenye mvuto, hadi imesimuliwa kuwa ni “chongo” akielekeza umuhimu kwa jicho lake. Katika hadithi kuna ishara kuwa: Dajjali mkubwa ni chongo. Na mwingine; jicho lake moja limefutwa, yaani ni mfano wa chongo kwa jingine, na kuwa wote wawili ni makafiri ukafiri usio na mpaka, hawana ila jicho moja tu ambalo huona maisha ya dunia tu. Ama jingine ambalo lina uwezo wa kuona Akhera ni chongo limefutwa. Na hakika nimeona kwenye ulimwengu wa kimaana Dajjali wa Waislamu, na nimeshuhudia kwa jicho langu nguvu ya udhalilishaji yenye mvuto, na nimemjua ni mwenye kumkanusha Allah kikamilifu. Ukanushaji huu ndio unamfanya kushambulia bila ya hofu sehemu tukufu, lakini watu wa kawaida hawajui ukweli na kudhani kuwa anafanya mambo yake kwa ushujaa na uwezo mkubwa. Hakika umma shujaa wenye kufanya vizuri – nao unaonja kushindwa – kwa kupendezwa na ushujaa, unausifu ushujaa wa kiongozi huyu mjanja mwenye kuhadaa, ambaye amepata umashuhuri, bahati na ushindi mwingi, na kuondoa uoni wake kwa namna halisi alivyo na kujaribu kuficha maovu yake... basi maangamio yaliyoje kwa umma huo… Lakini kama tunavyofahamu kutokana na mapokeo kuwa nuru na mwanga wa Qur’an uliyopo kwenye roho ya jeshi lenye ushujaa lenye kupigana jihadi na umma uliyoshikamana na dini yake vinawasukuma kushuhudia hali halisi hivyo wanajaribu kujenga aliyoyabomoa vibaya kiongozi huyo.
Nayo ni matukio matatu yenye mazingatio: Tukio la Kwanza: Omar bin Al-Khattab (r.a) aliondoka pamoja na Mtume wa Allah (s.a.w) siku moja, Mtume akamuashiria mmoja wa watoto wa Kiyahudi, akasema: Hii ndiyo sura yake. Omar (r.a) akasema: Niache niikate shingo yake. Akasema (s.a.w): (Akiwa ndio yeye – yaani huyu akiwa Sufyani – na akama siye basi hapana kheri kumuua). Mapokeo haya yanaashiria kuwa sura yake itadhihiri kwenye vitu vingi wakati wa utawala wake na kuwa atazaliwa baina ya Wayahudi. Na cha ajabu ni kuwa Omar (r.a) ambaye amebeba uadui na hasira kali juu ya sura yake inayodhihiri kwa mtoto mpaka akataka kumuua, amekuwa mbele ya Sufyani huyo mtu anayemsifu, kupendezwa naye na kumthamini zaidi… Tukio la Pili Wengi wamenakili: Kuwa Dajjali wa Waislamu alikuwa na shauku ya kujua maana ya sura tukufu: “Naapa kwa tini na zaituni” na kutaka tafsiri yake. Na cha ajabu ni kuwa sura "إقرأ باسم ربك" ni baada ya sura hii: na ndani yake kuna aya tukufu: كَلَّا إِنَّ الْإِنسَانَ لَيَطْغَى ambayo inaashiria sehemu yake na yeye kwa dhati yake – kwa maana yake na kwa hesabu ya elimu ya Jafr – ukiongezea na kuashiria kwake kuvuka mpaka katika uasi kwa wanaosali na misikiti. Yaani kwamba mtu huyo aliyehadaiwa anahisi kuwa sura ndogo ni yenye kumhusu, lakini anakosea na kugonga mlango wa jirani yake. Tukio la Tatu: Katika mapokeo ni kuwa Dajjali wa Waislamu atadhihiri Khurasani. Hakika maana ya hili na hapana ajuaye ghaibu ila Allah ni kuwa Waturuki ambao ndio taifa lenye ushujaa zaidi mashariki, lenye nguvu zaidi, lenye idadi kubwa ya watu na linalokuwa mbele katika jeshi la Kiislamu, walikuwa wakiishi pembezeni mwa Khurasani wakati wa mapokeo hayo, na walikuwa bado hawajaanza kuishi Anatolia. Hivyo mapokeo hayo yanaashiria – kwa kutaja kwake makaazi yao wakati huo – kudhihiri kwa Dajjali “Sufyani” kati yao. Na ni jambo la ajabu sana kuwa Waturuki ambao walikuwa ndio alama ya heshima ya Uislamu na utukufu wake na upanga wa almasi mzuri mkononi mwa Uislamu na Qur’an muda wote wa miaka mia saba, “Dajjali Sufyani” anafanya juhudi kuwatumia - kwa muda fulani - taifa hili la Kituruki dhidi ya sehemu ya nembo za Uislamu. Lakini hilo lipo mbali, hatofaulu katika jambo, bali mwishowe atarudi nyuma bila ya shaka, kama inavyofahamika kutokana na mapokeo: “Kuwa jeshi lenye ushujaa litaiokoa hatamu yake kutoka mkononi mwake”. Na Allah ni Mjuzi wa lililo sahihi Na hapana ajuaye ghaibu ila Allah

