بِسْمِ اللّٰهِ الرَّحْمٰنِ الرَّحِيمِ وَمَنْ يُؤْتَ الْحِكْمَةَ فَقَدْ اُو۫تِىَ خَيْرًا كَث۪يرًا Neno hili linaashiria kulinganisha kwa ujumla kati ya hekima tatakifu ya Qur’an yenye kutukuzwa na hekima ya falsafa. Pia linaashiria muhtasari wa yale yanayofundishwa na Qur’an katika malezi ya mwanadamu katika maisha yake binafsi na ya kijamii. Ukiongezea kwamba inajumuisha ishara kwenye upande wenye kutiliwa nguvu na Qur’an tukufu na ubora wake dhidi ya maneno mengine ya kiungu na kuwa na hadhi ya juu kuliko maneno yote. Kwa maana kuwa kuna misingi minne katika Neno hili:
Source text is preserved. When a suitable model is available, translation is displayed separately.
Sözler
The Twelfth Word
Kupitia miwani ya hekaya hii ya kupigiwa mfano, tazama tofauti kati ya hekima ya Qur’an tukufu na hekima ya sayansi: Mtawala mkubwa mwenye uchamungu na wema na mwenye umahiri na ufundi alitaka kuandika Qur’an Al-Hakiim kwa uandishi utakaokubaliana na utakatifu wa maana zake tukufu na unaonasibiana na kuwa ni muujiza wa ajabu katika maneno yake. Akataka kuivisha Qur’an tukufu kile kinachonasibiana na Qur’an hiyo kuwa ni muujiza wa hadhi ya juu katika nguo maridadi ya kufurutu ada mfano wake. Akawa anaandika Qur’an. Naye ni mwenye kuyasanifu na kuyafunda vyema maandishi ya ajabu mno! Akitumia aina zote za johari za tunu na vito vya thamani; ili kwa hayo aashirie kutanzuka kwa hakika zake tukufu. Akaandika baadhi ya herufi zake zilizoundwa kwa almasi na zumaradi, na sehemu yake nyengine ni kwa lulu na marijani, na kundi jengine kati yake kwa johari na akiki (ageti) na aina nyengine kati yake kwa dhahabu na fedha; mpaka akatia uzuri wa kuvutia na umaridadi wenye kuvutia macho, inaishangaaliwa na kila anayeiona, iwe anajua kusoma au hajui. Basi wote wanasimama mbele ya maandishi haya ya ajabu wakihemewa. Ukiwafunika utukuzo na mshangao. Hasa watu wa hakika ambao wameanza kutazama kwa jicho la mshangao (kuvutiwa) na kuthamini sana, kwa wanayoyajua. Kwamba uzuri huu wenye kushangaza unaonesha kilicho chini yake katika uzuri wa maana. Nao uko katika ukomo wa kuangaza na kung’aa na upeo wa ladha tamu na kionjo. Kisha mtawala huyo mkubwa aliionesha Qur’an hii ya maajabu kimaandishi, yenye uzuri wa kuvutia kwa mwanafalsafa wa kigeni na kwa mwanazuoni mwisilamu. Akawaamuru wawili hao: “Kila mmoja wenu nyinyi wawili aandike kitabu kuhusu hekima ya Qur’an hii!” Akiashiria kuwajaribu ili awazawadie. Mwanafalsafa aliandika kitabu, na mwanazuoni Mwislamu aliandika kitabu. Kitabu cha mwanafalsafa kilikuwa kinatafiti nakshi za herufi na uzuri wake, na uhusiano kati yake na kinginecho, na hali za kila moja kati yake, na yanayohusu johari zake na tofauti zake na sifa zake tu. Wala hakugusia kamwe maana za hiyo Qur’an tukufu katika kitabu chake. Kwani yeye ni mjinga wa lugha ya Kiarabu kwa ujinga mbumbumbu. Bali hakujua kwamba Qur’an hiyo ya ajabu ni kitabu kikubwa. Herufi zake zinajulisha maana tukufu. Lakini aliufunga mtazamo wake katika kuvutia kwa herufi zake na uzuri wake wenye kufurutu ada. Hata hivyo, yeye ni mhandisi mbobezi, msanifu msanii, mkemia hodari, na fundi mahiri. Kwa ajili hii, amekiandika kitabu chake hiki kulingana na anayoyaweza vyema katika stadi na sanaa anazozimudu vyema. Ama mwanazuoni mwislamu, kutazama tu maandishi yale ya kupendeza, alitambua kwamba hiki: Ni kitabu dhahiri na Qur’an yenye hekima. Basi hakuelekeza umuhimu wake katika pambo lake la nje. Wala hakuishughulisha nafsi yake kwa marembo ya herufi zake za ajabu. Bali alielekea mzima-mzima - naye akiwa na shauku mno ya haki – kwenye kile ambacho kina hadhi ya juu zaidi, chenye thamani zaidi, chema zaidi, kitukufu zaidi, chenye manufaa zaidi na kijumuishi zaidi kuliko kile alichoshughulika nacho mwanafalsafa wa kigeni kwa mamilioni ya maradufu. Akatafiti yaliyo chini ya nakshi hizo nzuri katika hakika za thamani ya juu na tukufu, na siri zenye nuru na za ajabu. Akaandika kitabu chake kikiwa ni tafsiri yenye thamani ya Qur’an hii yenye hekima tele. Basi akafanya vizuri na vyema. Kila mmoja kati yao alipeleka alichokiandika kwa mtawala mkuu. Yule mtawala, kwanza akapokea kitabu cha mwanafalsafa. Akakitazama kwa muda. Akaona kwamba yule mwenye kuistaajabia nafsi yake na mwenye kuitukuza Asili, katu hakuandika hekima ya kiuhakika, ingawa, alijitolea kila kilicho katika uwezo wake. Kwani hakufahamu maana za kitabu kile. Bali huenda alikwenda upogo, na jambo likamkanganya, akadhihirisha kutoheshimu na kutotukuza Qur’an ile. Ambapo hakufahamu maana zake za hadhi ya juu. Akadhani kuwa ni nakshi nzuri tu na herufi za ajabu. Akaipunja haki ya Qur’ani na kuibeza kwa upande wa maana. Kwa ajili hiyo, mtawala mwenye hekima alikirudisha kitabu cha yule mwanafalsafa na kumpiga nacho usoni mwake na akamfukuza katika ofisi yake. Kisha akakichukua kitabu cha mwanazuoni mwislamu, mhakiki, na mwenye kufuatilia kwa makini; akaona kwamba hiyo ni tafsiri yenye thamani mno, yenye upeo wa manufaa. Akaibariki kazi yake, na kuthamini juhudi yake, na kumpongeza kwa hilo. Akasema: Hii ndio hekima hasa. Kwa hakika hupewa jina la mwanazuoni na mwenye hekima hasa yule mwenye kitabu hiki. Yule mwingine sio lolote isipokuwa ni msanii, fundi aliyepitiliza na kuvuka mpaka wake. Baadaye alimpa mwanazuoni yule mwislamu malipo yake makubwa. Akiamuru atunukiwe Lira kumi za dhahabu kwa kila herufi katika herufi za kitabu chake. Ukifahamu – ewe ndugu yangu – makusudio ya hikaya hii ya kupigiwa mfano, basi hebu angalia kwa upande wa uhakika: Hiyo Qur’an tukufu yenye kung’aa, ni huu ulimwengu wa ajabu... Huyo mtawala mwenye taadhima, ni mfalme wa azali na milele (s.w.). Watu wawili: Wa kwanza; yaani yule mgeni - ni elimu ya Falsafa na wanahekima wake. Na mwingine: Ni Qur’an tukufu na wanafunzi wake. Naam, kwa hakika Qura’n tukufu “yenye kusomwa” ni tafsiri kubwa sana na ya hadhi ya juu. Malimani fasaha sana na wa juu zaidi wa ulimwengu huu wa ajabu ni ile Qur’an nyingine tukufu “yenye kuonekanwa”. Naam, hiyo Al-Furqaanul hakiim ndiyo ambayo inawaongoza majini na watu kwenye aya za kilimwengu ambazo kalamu ya uweza wa kiungu imeziandika juu ya kurasa za ulimwengu mpana na kuzitia nakshi katika karatasi za zama na enzi. Na hiyo ndiyo inayoangalia vilivyopo – ambavyo kila moja kati yao ni herufi yenye maana - kwa maana ya nano-kwa-neno – yaani inaangalia kwa upande wa kumjulisha mtengenezaji mukufu. Basi inasema: Ni uzuri ulioje wa umbo lake! Ni uzuri ulioje wa umbo lake! Ni dalili kubwa iliyoje juu ya uzuri wa mwanzilishi mtukufu. Na hivi ndivyo inavyoufunua uzuri wa uhakika wa viumbe mbele ya macho. Ama wanachokiita kuwa ni Elimu ya Hekima ambayo ni falsafa, imeghariki katika mapambo ya herufi za vilivyopo, na imebaki kuwa ni yenye kuhemewa mbele ya mahusiano ya baadhi yake na baadhi nyingine, mpaka ikapotea na kutouona uhakika. Wakati ambapo ilikuwa ni juu yake itazame kwenye kitabu cha ulimwengu. Falsafa hiyo kutazama katika herufi - zinazojulisha mwandishi wake – itakuwa imeziangalia kwa maana ya kijina (kinomino). Yaani kwamba vilivyopo ni vyenye kusimama kwa dhati yao, ikaanza kuvizungumzia kwa sura hii. Inasema: Ni uzuri ulioje wa hiki! Badala ya kusema: Uzuri ulioje wa umbile hili! Kwa kauli hii, inaupokonya uzuri wa kweli wa kitu hicho. Basi kwa kuuegemeza uzuri kwenye kitu chenyewe, itakuwa imevibeza vilivyopo vyote. Mpaka ikavifanya viumbe vyote kuwa ni vyenye kuvishitakia juu ya hilo Siku ya Kiama. Naam, falsafa ya kipagani (kumkana Mungu), kwa hakika ni ghiliba (maneno ya hila) isiyo na ukweli wowote, na ni kuudharau ulimwengu na kuukejeli.
Ili kufikia kiwango cha tofauti kati ya malezi ya kitabia ambayo Qur’an tukufu inawalea wanafunzi wake kwa malezi hayo na somo ambalo hekima ya falsafa inalifundisha, tunaona tuwaweke wanafunzi wawili wa sehemu hizo mbili katika ulinganishi. Mwanafunzi mwenye ikhalsi kwa falsafa ni (Firauni), lakini ni firauni dhalili. Kwani anaabudu kitu duni kabisa kwa ajili ya manufaa yake na anajifanyia kila kinachomfaa kuwa ni Mola wake. Kisha, yule mwanafunzi mpingaji (asi na mkaidi), lakini ni asi maskini, anauridhia ukomo wa udhalili kwa ajili ya nafsi yake katika njia ya kupata ladha tamu. Yeye ni mkaidi dhalili. Kwani anajidhalilisha na kuwapembejea watu amba ni kama mashetani. Bali anaibusu miguu yao! Kisha, mwanafunzi huyo mkanushaji “mwenye kughururika na ni jabari” lakini, ni jabari mwenye kushindwa (asiyejiweza) kwa hisia zake katika ukomo wa kushindwa katika dhati yake. Ambapo moyoni mwake, hapati wa kumwegemea. Kisha mwanafunzi huyo “wa kimanufaa na kimaslahi”, haoni chochote isipokuwa dhati yake. Basi upeo wa hima yake ni kuitikia raghaba za nafsi, tumbo na utupu. Huyo ni “mwenye hila na vitimbi”; anatafuta masilahi yake binafsi ndani ya masilahi ya umma. Ilhali mwanafunzi wa Qur’an tukufu mwenye ikhlasi, ni “mtumwa”, lakini ni mtumwa mtukufu asiyejidhalilisha kwa chochote hata kwa kiumbe mkuu kabisa. Wala haridhii hata Pepo – ambayo ni neema kubwa kuliko. Upeo wa utumwa wake ni kwa ajili ya Allah. Kisha, yeye ni mwanafunzi “mnyenyekevu, laini na mwepesi”, lakini hajidhalilishi kwa utashi wake kwa asiyekuwa muumba wake mtukufu na pasipo amri yake na idhini yake. Kisha, yeye ni “fakiri na dhaifu” mwenye yakini na ufakiri wake na udhaifu wake, lakini yeye ni mwenye kukinai kila kitu kwa yale aliyolimbikiziwa na mmiliki wake mkarimu katika hazina zisizomalizika huko Akhera. Yeye ni “mwenye nguvu” kwa kuiegemea nguvu ya Bwana wake ya hali zote. Kisha yeye hatendi lolote isipokuwa kwa ajili ya dhati ya Allah. Bali hahangaikii jambo isipokuwa lile lililo ndani ya radhi zake ili kuzifikia fadhila na kuzieneza. Hivi ndivyo hufahamika malezi ambayo hekima hizo mbili zimeleleka, wakati wa ulinganishi kati ya wanafunzi wa viwili hivyo.
Ama kile kinachotolewa na hekima ya falsafa na hekima ya Qur’an katika malezi ya jamii ya mwanadamu ni kwamba: Hekima ya falsafa inaiona “nguvu” kuwa ni nukta ya kuegemea katika maisha ya kijamii, na inalenga kwenye manufaa katika kila kitu. Inayachukulia “mapambano” kuwa ni kanuni ya maisha. Inashikamana na “ubaguzi na utaifa hasi” kuwa ndio fungamano la jumuiya mbalimbali. Ama matunda yake ni kushibisha raghaba za matamanio na mielekeo ya nafsi ambayo lengo lake ni kuchochea utukutu wa nafsi na kuamsha matamanio ya nafsi. Ni jambo linalojulikana kwamba hali ya “nguvu” ni “kufanya uadui”... na hali ya “manufaa” ni “kusongamana”. Kwani haitoshi kukidhi haja za wote na kuitikia raghba zao... Hali ya “mapambano” ni “ugomvi na mabishano”... Na hali ya “ubaguzi” ni “kufanya uadui”. Kwani hukuwa kwa kummeza mwinginewe na kupanuka kwa gharama ya wengine. Kutokea hapa, utatambua ni kwa nini furaha ya ubinadamu imenyang’anywa kutokana na kupupia nyuma ya hekima hii. Ama hekima ya Qur’an tukufu inayoikubali “haki” kuwa ni nukta ya kuegemea katika maisha ya kijamii, badala ya “nguvu”... Na kujaalia “kumridhisha Allah (s.w.)” na kupata fadhila ndiyo shabaha husika, badala ya “manufaa”... Na kuifanya kanuni ya “kusaidiana” ndio msingi wa maisha, badala ya kanuni ya “mapambano”... Na kufuata fungamano la “dini”, dhehebu na taifa ili kufungamanisha makundi ya jumuiya mbalimbali, badala ya ubaguzi na utaifa vilivyo hasi... Na kujaalia shabaha zake ni zenye mpaka kutokana na kuvuka mpaka kwa nafsi yenye kuamrisha na kuisukuma roho kwenda kwenye mambo ya juu, na kuzishibisha hisia zake za hadhi ya juu ili kumpeleka mwanadamu upande wa ukamilifu na mfano bora wa kiutu. Hakika hali ya “haki” ni “kuafikiana”... Hali ya “fadhila” ni “kuegemeana”... Hali ya kanuni ya “kusaidiana” ni “kila mmoja kumwokoa mwingine”... Hali ya “dini” ni “undugu na kushikamana”... Hali ya “kuitia shemere nafsi” na kuzuia ukorofi wake na kuiachilia roho na kuihimiza kuelekea kwenye ukamilifu ndio “mafanikio ya makazi mawili” (Duniani na Akhera).

