Sözler

The Twenty-First Word

Source: risaleinur multilingual dataset, risale.site source · Risale-Nur multilingual research corpus
Risale reading plan
§1

بِسْمِ اللّٰهِ الرَّحْمٰنِ الرَّحِيمِ اِنَّ الصَّلٰوةَ كَانَت۟ عَلَى ال۟مُؤ۟مِنٖينَ كِتَابًا مَو۟قُوتًا Wakati fulani, mtu mmoja aliyekuwa na umri na umbo kubwa pamoja na hadhi aliniambia, “Swala ni nzuri, lakini kuziswali kwa kila siku mara tano ni nyingi sana. Kwa kuwa haziishi kamwe na zinachosha.” Muda mrefu baada ya mtu huyo kusema maneno hayo, niliisikiliza nafsi yangu na kuisikia ikisema maneno hayo hayo. Niliichunguza na kuona kuwa kwa uvivu wake, imejifundisha somo hilo hilo kutoka kwa Shetani. Nikafahamu kuwa ilitamka maneno hayo kwa amri ya nafsi zenye kuamuru maovu, au vinginevyo imeshawishiwa. Nikasema; “Nafsi yangu inaamuru uovu na mtu asiyebadili nafsi yake mwenyewe hataweza kuwabadili wengine. Kwa hali yoyote, nitaanzia kwangu mwenyewe. Nilisema: Ewe nafsi yangu! Sikiliza maonyo matano kuhusu maneno yale uliyoyasema kwa ujinga ulio changanyikana, katika kochi la uvivu, katika usingizi wa ughafilikaji.

§2

Ewe nafsi yangu usiyejiweza! Kwani maisha yako ni ya milele, ninashangaa? Kwani una waraka usiobadilishika unaoonesha kuwa utaishi mpaka mwakani, au hata mpaka kesho? Kinacho kusababishia uchovu wako ni fikra zako kuwa utaishi milele. Unalalamika kana kwamba utaishi duniani milele ili kujifurahisha. Kama utafahamu kuwa maisha yako ni mafupi na kuwa yanapita kwa hasara, kwa hakika haitaleta uchovu, bali ari halisi na furaha ya kukubalika ya kupitisha saa moja kati ya ishirini na nne katika kitendo kizuri, cha kupendeza, chepesi na cha neema cha ibada ambacho ni njia ya kupata furaha ya kweli ya maisha ya milele.

§3

Ewe nafsi yangu yenye kuabudu tumbo! Kila siku unakula mkate, unakunywa maji, na kupumua hewa, je hayo yanakuchosha? Hayakuchoshi, kwa kuwa haja hufanywa upya, swala tano za kila siku zisikuchoshe. Kwani zinavutia haja za wenzako kwenye nyumba ya mwili wangu, mlo wa moyo wangu, maji ya uhai wa roho yangu, na hewa ya ufahamu wangu ulio mpambanuzi. Ndiyo, ni kwa kubisha hodi kwa njia ya dua mlangoni kwa Mwingi wa Rehema na Mwingi wa Ukarimu kuwa riziki na nguvu zinaweza kupatikana kwa ajili ya moyo uliopatwa na majonzi yasiyo na kikomo na huzuni na kutekwa na furaha na matumaini yasiyo na mwisho. Na pia ni kwa kugeukia katika chemchemi ya rehema za Mwenye Kupendwa Milele kwa njia ya swala tano za kila siku ambapo maji ya uzima yanaweza kunywewa na roho iliyoungana na viumbe wengi wenye kuondoka polepole kutoka dunia hii ya mpito huku wakilia kwa utengano. Na kuwa na haja sana ya hewa katika hali za kuhuzunisha, kupondeka, kukatisha tamaa, za mpito, nyeusi na za kusonga koo ya dunia, ni kwa kupitia dirisha la swala tu ndipo akili tambuzi ya ndani na werevu stadi wenye nuru vinaweza kupumua, ambavyo kwa hali zake za kawaida, vinatamani uzima wa kudumu na vimeumbwa kwa ajili ya milele na tena ni kioo cha Aliye Wa Milele na Milele na vina ulaini na upambanuzi usio na kikomo.

§4

Ewe nafsi yangu usiye na subira! Je inaingia akilini leo kufikiria taabu zilizopita zilizotokana na ibada, taabu za swala, na matatizo ya mikosi, na kuanza kuhuzunika, na kufikiria wajibu ujao wa ibada, kutekeleza swala, na huzuni za balaa, na kuanza kukosa uvumilivu? Basi, kukosa subira kunafanana na kamanda mpumbavu ambaye, ingawa ubavu wa upande wa kuume wa adui umeungana na upande wake wa kuume na kuwa na majeshi mapya kwa ajili yake, anatuma jeshi kubwa katika upande wa kuume na kudhoofisha katikati. Kisha katika wakati kunapokosekana wanajeshi wa adui katika ubavu wa upande wa kushoto, anatuma jeshi kubwa huko na kuwapa amri ya kushambulia. Kisha hakuna majeshi yanayobakia katikati halafu adui anaona hilo na anashambulia sehemu hiyo na kumshinda kabisa. Ndio, unafanana na hivyo, kwani taabu za jana, leo zimebadilishwa na kuwa neema, maumivu yameondoka na kubakia furaha. Shida imegeuka kuwa baraka, na taabu kuwa malipo katika hali yoyote usijisikie kuchoshwa nayo, bali fanya bidii ya kuendelea na ari mpya na shauku mpya. Ama kuhusu wakati ujao, bado haujawadia, hivyo, kuufikiria kwa sasa na kujisikia kuchoka ni wazimu kama vile leo kufikiria njaa na kiu ijayo, na kuanza kupiga kelele na kulia kwa sauti. Kwa kuwa huo ndio ukweli, kama una mantiki, kuhusu ibada, utafikiria leo tu na kusema: “Ninaitumia saa yake moja katika kitendo cha ibada cha kukubalika, kizuri na kitukufu chenye malipo makubwa na taabu zake ni chache.” Basi hali yako chungu ya kukata tamaa itabadilika na kuwa jitihada tamu. Ewe nafsi yangu isio na subira! Una wajibu wa kuwa na subira katika sehemu tatu za kuzingatia. Kwanza ni subira katika ibada, nyingine ni subira katika kujiepusha na dhambi, na ya tatu ni subira katika kukabili taabu. Kama una akili, fanya mwongozo wako katika ukweli ulio dhahiri katika mlinganisho katika hili Onyo la Tatu. Tamka kiuanaume: “Ewe Mwingi wa Subira!” na ubebe aina hizo tatu za subira. Kama hufanyi ufujaji katika namna batili, majeshi ya subira aliyokupa Allah (s.w), yatatosha kukabili tatizo na janga lolote. Basi shikilia majeshi hayo!

§5

Ewe nafsi yangu pumbavu! Kwani wajibu huu wa ibada hauna matunda na kwani ina malipo kidogo ndiyo yanayokusababishia uchovu? Kwani kama mtu angekupa pesa chache au kukutisha, angeweza kukufanya ufanye kazi mpaka jioni na ungefanya kazi bila ya kuzembea. Kwani swala za faradhi hazina faida, ambapo katika nyumba hii ya wageni ya dunia ni riziki na mali kwa ajili ya moyo wako dhaifu, na katika kaburi lako, itakayokuwa makazi yako ya hakika, riziki na nuru, na katika ufufuo, siku utakapohukumiwa, waraka na miliki, na katika daraja la Swirat, ambapo lazima upite, itakuwa nuru na kipando? Je fidia zake ni haba? Mtu anakuahidi zawadi ya thamani ya Lira (Pesa za Uturuki) mia moja na anakupa kazi ya siku mia moja. Unamwamini mtu huyo ambaye huenda asitimize ahadi yake na wewe unafanya kazi kwa bidii. Kwa hivyo, kama yule Ambaye kuvunja ahadi hakuwezekani Kwake, Anakuahidi fidia kama pepo na zawadi kama furaha ya kudumu na anakutuma kazi kwa muda mfupi sana katika wajibu wenye kuwafikiana sana, kama hutafanya hayo, au unatenda katika namna ya kushutumu ahadi Zake au kupuuza zawadi zake kwa kuufanya wajibu huo bila kupenda kama mtu aliyelazimishwa kufanya kazi, au kwa kuchoshwa, au kwa kufanya kwa shingo upande, utakuwa unastahili kupewa karipio kali na adhabu ya kutisha. Je hujapata kufikiria hilo? Ingawa unafanya kazi ya kidunia bila ya kulegea kwa kuogopa kufungwa jela, kwani hofu ya kufungwa jela daima huko Jahanamu haikujazi shauku kwa ajili ya nuru ya kweli na kitendo muwafaka cha kazi?

§6

Ewe nafsi yangu yenye kuabudu dunia! Ugoigoi wako katika ibada na uzembe kwenye swala za faradhi unatokana na kukithiri kwa kazi zako za kidunia au kwa ukosefu wa muda kwa sababu ya kupigania maisha. Kwani wewe uliumbwa kwa ajili ya dunia ndio maana unatumia muda wako wote juu yake? Unajua kuwa kulingana na werevu wako, wewe ni mbora kuliko wanyama wote, lakini kwa mujibu wa kupata mahitaji ya lazima ya maisha ya kidunia, hutaweza kushindana hata na shorewanda. Hivyo, kwa nini huwezi kufahamu kuwa wajibu wako wa msingi si kufanya kazi kama mnyama, bali kuhangaikia uzima wa kweli, wa kudumu, kama mwanadamu wa kweli. Kwa kuongezea, mambo unayoyaita shughuli za kidunia, nyingi hazikuhusu; bali ni mambo ya kipuuzi unayoingilia. Unapuuzia mambo muhimu na unapitisha muda wako katika kutafuta habari kana kwamba utaishi miaka elfu moja. Kwa mfano, unafuja muda wako wa thamani kubwa juu ya mambo yasiyo na thamani kama vile kujifundisha juu ya maduara yanayozunguka sayari ya Zohali yalivyo au kuna kuku wangapi huko Marekani, kana kwamba unakuwa mtaalamu wa unajimu au takwimu. Kama utasema: “Kinachonifanya nisiswali na kufanya ibada na kunisababishia uvivu si mambo yasiyo muhimu kama hayo, bali ni mambo ya lazima kwa uzima kama vile kuchuma riziki,” basi jibu langu ni hili: kama unafanya kazi kwa mshahara wa kila siku wa kurushi mia moja halafu mtu anakujia na kukwambia: “Njoo ulime hapa kwa dakika kumi na utapata almasi na zumaridi za thamani ya lira mia moja” na unajibu: “Hapana, sitakuja kwa sababu nitakatwa kurushi kumi katika mshahara wangu na riziki yangu itapungua,” kwa hakika, utafahamu kiasi cha upumbavu wa kisingizio hicho kitakavyokuwa. Katika hali hiyo hiyo, unafanya kazi katika shamba hili kwa ajili ya kuchuma riziki. Kama utaacha swala za faradhi, matunda yote ya juhudi zako yatakuwa yamezuilika katika maisha yako ya kidunia, yasiyo muhimu na yasiyo na tija. Lakini kama nyakati zako za kupumzika utapitisha utazitumia kwenye swala, ambazo zinaupa moyo wako nafasi ya kupumzika na moyo kupumua, utagundua migodi miwili ambayo ni chanzo muhimu, kwa ajili ya chumo lenye tija la kidunia, pia na chumo na riziki ya akhera. Mgodi wa kwanza: Kwa nia njema, utapata gawio la sifa na utukuzaji unaofanywa na mimea na miti yote, iwe ya maua au ya matunda, unayootesha katika bustani. Mgodi wa Pili: Chochote kinacholiwa katika mazao ya bustani, iwe na wanyama au wanadamu, mifugo au wadudu, wanunuzi au wezi, kitakuwa kama umetoa zaka, lakini kwa sharti kuwa ufanye kazi kwa ajili ya Mpaji wa kweli na ndani ya mipaka ya anachoruhusu, na ujione kama afisa ugavi anayetoa mali yake kuwapa viumbe wake. Basi angalia hasara kubwa anayopata mtu anayeacha swala za faradhi. Ni mali muhimu sana anayopoteza, amenyimwa matokeo yale mawili na migodi ambavyo vinginevyo vingemfanya afanye kazi kwa ari na kuhakikisha kuwa hamasa yake ni imara; anakuwa muflisi. Zaidi ya hivyo, kadiri anavyozeeka atachoka kushughulikia bustani na kukosa utashi nayo, huku akisema: “Inanihusu nini mimi? Hata hivyo, ninaondoka duniani, kwa nini nijipe taabu?” Atazama katika uvivu. Lakini mtu yule wa kwanza anasema: “Nitafanya juhudi katika ibada na mambo halali ili kupeleka nuru zaidi kaburini kwangu na kupata riziki zaidi kwa ajili ya maisha yangu ya akhera.” Kwa Ufupi: Ewe nafsi yangu! Jua kuwa jana imeshakuacha na kuhusu kesho, huna cha kuthibitisha kuwa itakuwa ya kwako. Katika hali yoyote, tambua kuwa maisha yako ya kweli ni leo. Basi tumia angalau moja katika saa zake msikitini au kwenye mswala, sanduku kwa ajili ya akhera kama mfuko wa fedha wa akiba, uliowekwa kwa ajili ya hapo baadaye. Pia tambua kuwa kwako wewe na kwa kila mmoja kuwa kila siku mpya ni mlango wa kwendea dunia mpya. Kama huswali, dunia yako siku hiyo itaondoka ikiwa giza na kutokujiweza na kushuhudia dhidi yako katika Dunia ya Milinganisho. Kila siku, kila mmoja ana dunia yake binafsi ndani ya dunia hii na jinsi ilivyo, inategemea moyo na matendo ya mtu, kama lilivyo kasri zuri lenye kuakisi katika kioo, linachukua rangi ya kioo, kama ni cheusi, litaonekana jeusi; kama ni chekundu, litaonekana jekundu. Pia linachukua ubora wa kioo; kama kioo ni laini, kinaonesha kasri kuwa ni zuri, na kama sivyo, kinaonesha kuwa ni baya. Kadiri kinavyovifanya vitu laini vionekane vya kukwaruza, basi unabadili umbo la dunia yako kwa moyo wako, akili, matendo na utashi. Unaweza kuifanya ama itoe ushahidi wa kukutetea au dhidi yako. Kama unaswali swala tano za kila siku na kwa swala hizo unageuziwa upande wa Muumbaji Mtukufu wa dunia yako, basi ghafla, dunia yako inayokutazama, inatiwa nuru. Kwa kawaida kabisa, kana kwamba swala ni taa ya umeme, na nia yako ya kuziswali inabonyeza swichi, inaondoa giza la dunia na kuonesha mabadiliko na nyendo ndani ya umaskini wa vurugu za kidunia kuwa na utulivu na mpangilio wa makusudi na maandiko muhimu ya uwezo wa kiungu. Zinatawanya moyoni mwako kote, nuru moja za aya iliyojaa nuru, اَللّٰهُ نُورُ السَّمٰوَاتِ وَاْلاَرْضِ na dunia yako katika siku hiyo inatiwa nuru kwa kuakisi nuru. Itaisababisha kukutetea kupitia nuru yake. Tahadhari, usiseme: “Ni nini swala zangu ikilinganishwa na uhalisia wa swala?”, kwa sababu kama ilivyo kokwa ya tende inaeleza sifa za mti mkubwa, ndivyo swala yako zinavyoeleza mti wako. Tofauti ipo katika muhtasari na utendaji tu; kama vile swala za walii mkubwa, swala za watu wa kawaida kama wewe au mimi zina mgawo wa nuru hiyo, hata kama hawana habari nayo. Kuna muujiza katika ukweli huu, hata kama akili tambuzi haitambui hilo, lakini inakunjuka na kutoa nuru katika hali tofauti kwa mujibu wa viwango vya wanaozitekeleza. Hata hivyo, hatua nyingi na viwango huko ni kutokana na kokwa ya tende mpaka mti kubwa. Viwango vya swala na hatua zao ni nyingi pia. Lakini umuhimu wa ukweli huo wenye nuru upo katika viwango vyote. اَللّٰهُمَّ صَلِّ وَسَلِّم۟ عَلٰى مَن۟ قَالَ «اَلصَّلَاةُ عِمَادُ الدّٖينِ» وَعَلٰى اٰلِهٖ وَصَح۟بِهٖ اَج۟مَعٖينَ

Private reading note

This note stays on this device and is never uploaded to a server.

Up to 1,200 characters