Neno ambalo limefumbua fumbo la Ulimwengu na talasimu lake na kufungua siri kubwa katika siri za Qur’an tukufu
Source text is preserved. When a suitable model is available, translation is displayed separately.
Sözler
The Thirtieth Word
Herufi kutoka katika Kitabu Kikubwa cha «Ana» Nukta kutoka katika Bahari Kubwa ya «Atomu» Neno hili linazingatiwa kuwa na makusudio mawili: Kusudio la kwanza: Linajadili kuhusu ainisho la Ana na matokeo yake. Kusudio la Pili: Linajadili mchakato wa Atomu na majukumu yake.
اِنَّا عَرَض۟نَا ال۟اَمَانَةَ عَلَى السَّمٰوَاتِ وَال۟اَر۟ضِ وَال۟جِبَالِ فَاَبَي۟نَ اَن۟ يَح۟مِل۟نَهَا وَاَش۟فَق۟نَ مِن۟هَا وَحَمَلَهَا ال۟اِن۟سَانُ اِنَّهُ كَانَ ظَلُومًا جَهُولًا Kutoka katika hazina kuu ya aya hii tukufu tutaashiria johari moja katika johari zake. Nayo ni kwamba: Amana ambayo mbingu, Ardhi na milima imeikataa kuibeba, ina maana nyingi na ina pande nyingi. Basi moja katika maana hizo na upande katika pande hizo ni: “Ana”. Naam, hakika “Ana” ni mbegu, ambayo mti wa Tuba mkubwa na wa nuru, umeota kutokana na mbegu hiyo na mti wa kutisha wa Mzakumi. Miti hiyo inayarefusha matawi yake na kuyaeneza katika pande za ulimwengu wa mwanadamu tangu Adam (a.s.) hadi wakati wa sasa. Na kabla ya kuingia katika hakika hii pana, mbele yake tunabainisha “utangulizi” unaorahisisha kuifahamu. Utangulizi Hakika “Ana” ni ufunguo unaofungua hazina zilizofichikana za majina mazuri ya kiungu, kama unavyofungua vifungo vya ulimwengu. Basi hiyo kwa hadi ya dhati yake ni zindiko la ajabu, na kificho cha ajabu. Lakini kwa kujua uhalisia wa “Ana”, linafunguka talasimu la ajabu na kufunuka kificho hicho cha ajabu, na kwa nafasi yake linafumbuka fumbo la ulimwengu na hazina za ulimwengu wa kuwajibika. Na kwa hakika tumetaja yanayohusu maswala haya katika Risala ya “Kupunga Upepo Mwanana wa Uongofu wa Qur’an” kama ifuatavyo: Jua kwamba funguo za ulimwengu zimo katika mkono wa mwanadamu, na katika nafsi yake. Basi viumbe pamoja na kuwa milango yake iko wazi kwa dhahiri, isipokuwa imefungwa. Basi Allah (s.w.) ameweka kwa upande wa amana kwa mwanadamu funguo inayofungua milango yote ya ulimwengu, na talasimu linalofungua hazina zilizofichikana za muumba wa ulimwengu. Na ufunguo huo ni kile kilichomo ndani yako cha “Ana”. Isipokuwa kwamba “Ana” vilevile ni kificho kilichofungwa na talasimu lenye kufungwa. Basi ukiifungua “Ana” kwa kujua asili yake ya kusadikika na siri ya umbo lake, talasimu la viumbe litakufungukia kama ifuatavyo: Hakika ya Allah (s.w.) ameweka mkononi mwa mwanadamu Amana nayo ni: “Ana” ambayo inabeba ishara na vielelezo anavyotolea ushahidi juu ya hakika za sifa za uungu-mlezi wake ulio mtukufu na mambo yake matakatifu. Yaani “Ana” inakuwa ni sehemu ya kipimo ambacho zinatambulika sifa za uungu-mlezi na mambo ya kiungu kwa kipimo hicho. Na katika yanayojulikana ni kwamba hailazimu kuwa sehemu ya kipimo iwe na uwepo wa kiuhakika, bali inayumkinika kuundwa sehemu ya kipimo kwa makadirio na kufikirika, kama misitari ya kukadiria katika Elimu ya Uhandisi. Yaani hailazimu kwa “Ana” iwe na uwepo wa kiuhakika kwa elimu na uhakiki. Swali: Kwa nini maarifa ya kuzijua sifa za Allah (s.w.) na majina yake mazuri yamefungamana na “umimi” wa mwanadamu? Jibu: Hakika kitu huru na chenye kuzunguka, hakiwi na mipaka wala ukomo. Hivyo hakipewi umbo wala hakihukumiwi kwa hukumu yoyote. Na hii ni kwa kutokuwepo uso na sura yake bainifu; kwa ajili hiyo haufahamiki uhakika wa uhalisia wake. Basi mathalani: Mwanga wa kudumu ambao hauingiliwi kati na giza hauhisiwi wala hautambuliki kuwepo kwake isipokuwa ukibainishwa mipaka kwa giza la hakika au la kusadikika. Na namna hii, hakika sifa za Allah (s.w) kama elimu na uweza na majina yake mazuri, kama Al-Hakiim na Ar-Rahiim; kwa sababu ni huru (ya hali zote) hayana mipaka na ni yenye kuzungukia kila kitu, hayana mshirika wala mfano, wala haiwezekani kuyazungukia au kuyadhibiti kwa kitu fulani, hayajulikani uhalisia wake, wala hayahisiwi; kwa hiyo hapana budi kuweka mpaka wa kukadiria na wa kufikirika kwa sifa hizo na majina ya hali zote, ili iwe ni nyenzo ya kuyafahamu, kwa kuwa hayana mipaka wala ukomo wa uhakika wake. Basi hili ndilo linalofanywa na “Umimi” yaani analolifanya “Ana” (Mimi); ambapo anatasawari katika nafsi yake uungu wa kusadikika na umiliki wa kukadiriwa na uweza na elimu. Basi inaweka mipaka maalumu, na kuweka kwa sifa hizo mpaka wa kufikirika kwa sifa zenye kukizunguka (kila kitu) na majina ya hali zote. Anasema mathalani: Kutoka hapa hadi kule ni kwangu, na baada ya eneo hilo anarudi katika sifa hizo. Yaani anaweka namna fulani ya kugawanya mambo, na anajiandaa kwa hili kufahamu kidogokidogo chimbuko la sifa hizo zisizo na mipaka. Na hii ni kwa yale aliyonayo katika vipimo vidogo na vigezo finyu. Basi mathalani: Anafahamu kwa uungu wake wa kufikirika ambao anaujengea picha katika duara la ufalme wake, uungu wa hali zote wa Muumba wake (s.w.) katika duara la yanayowezekana. Na anatambua kwa umiliki wake wa juu-juu, umiliki wa kiuhakika wa muumba wake. Basi husema: Kama ambavyo mimi ni mmiliki wa nyumba hii, basi muumba (s.w.) vilevile ni mmiliki wa ulimwengu huu... Na anajua kwa elimu yake ya sehemu fulani, elimu ya Allah (s.w.) ya hali zote... Na anatambua kwa umahiri wake uliochumwa wa sehemu ndogo, maajabu ya fundi Mtukufu. Basi mathalani anasema: Kama ambavyo mimi nilijenga nyumba hii na kuipangilia, basi vilevile hapana budi kuwepo mwanzilishi wa makao ya Duniani na mpangiliaji wake. Na namna hii... Zimeingia katika “Ana” maelfu ya hali, sifa na hisia zilizobeba maelfu ya siri zilizofungwa ambazo zinaweza kujulisha na kubainisha – kwa kiasi fulani - sifa za kiungu na mambo yake yote yenye hekima. Yaani hakika ya “Ana” katika dhati yake yenyewe haibebi maana, bali inajulisha maana kwa mwingine; kama kioo chenye kuakisi, na mizani ya kupimia, zana ya kifaa cha kugundulia, na maana ya neno-kwa-neno, basi ni unywele wenye hisia kali katika kamba ya uwepo wa mwanadamu mkubwa. Nao ni uzi mwembamba wa kufumia nguo ya uhalisia wa wanadamu. Nao ni herufi ya “Alif” katika kitabu cha haiba ya wana wa Adamu, ambapo herufi hiyo ina pande mbili. Upande mmoja unaelekea katika kheri na uwepo; basi hiyo katika upande huu unapokea yaliyo ya ziada na kuyakubali tu. Yaani unakubali nyongeza tu. Kwani yenyewe ni yenye kushindwa kukifanya kitu kiwepo katika upande huu. Yaani sio mtendaji katika hilo, kwa sababu mkono wake ni mfupi, hauna uwezo wa kufanya kitu kiwepo. Na upande mwingine unaelekea kwenye shari, na unaacha wazi kuelekea kutokuwepo; basi yeye katika upande huu ni mtendaji, na ni mmiliki wa kitendo. Kisha uhalisia wa “Ana” neno-kwa-neno, yaani inajulisha maana kwa kingine. Basi uungu wake ni wa kusadikika, na uwepo wake ni dhaifu na mnyonge kwa kiasi ambacho hawezi kubeba kwa dhati yake chochote kiwacho, na wala hakibebeshwi kitu juu yake, bali hiyo ni mizani tu na si vinginevyo; inabainisha sifa za Allah (s.w.) ambazo ni za hali zote na zenye kuzunguka kila kitu. Kama vile kipima joto na kipima hewa na vipimo vingine vinavyobainisha viwango vya vitu na daraja zake. Basi anayeujua uhalisia wa “Ana” kwa upande huu na kuukiri, kisha akatenda kulingana na hivyo na kwa muktadha wake, anaingia ndani ya bishara ya Allah (s.w.) قَدْ أَفلَحَ مَن زَكّاهَا na anakuwa ameshatimiza haki ya amana. Basi anatambua kwa miwani ya “Ana” uhakika wa viumbe na majukumu wanayoyatimiza. Na zinapokuja taarifa kutoka anga za nje kwenda katika nafsi, utaikuta “Ana” yapo inayoyasadikisha. Basi taarifa hizo zinatulia zikiwa ni elimu za nuru na hekima zenye kusibu katika nafsi, wala hazipinduki kuwa ni magiza ya kipuuzi. Na wakati ambapo “Ana” inatekeleza jukumu lake kwa sura hii, inaacha uungu wake wa kusadikika na umiliki wake wa kukadiriwa – ambao ni mizani ya kupimia na sio vinginevyo - na kuegemeza ufalme kwa Allah peke yake kwa kusema: "لَهُ ال۟مُل۟كُ وَ لَهُ ال۟حَم۟دُ وَ لَهُ ال۟حُك۟مُ وَ اِلَي۟هِ تُر۟جَعُونَ". Basi anavaa vazi lake la uja wa haki, na kupanda katika makamo ya “Ahsani Taqwiim”. Lakini “Ana” ikisahau hekima ya muumba wake na ikaitazama nafsi yake kwa maana ya kinomino, ikiacha jukumu lake la kimaumbile, huku ikiitakidi kwa nafsi yake kuwa yeye ndiyo mmiliki, basi ameifanyia hiana amana, na imeingia katika onyo la kiungu: (وَقَدْ خَابَ مَن دَسَّاهَا) Na namna hiyo... Hakika mbingu, ardhi na milima kuhofia kuibeba amana, na hofu yao kutokana na ushirikina unaodhaniwa na wenye kukadiriwa, hakika hayo ni kwa upande huu wa umimi” ambao unazalisha aina zote za ushirikina, shari na upotevu. Naam, hakika “Ana” pamoja na kuwa ni watumwa elfu moja, uzi mwembamba, na mstari wa kubuni, isipokuwa kwamba kama halikujulikana chimbuko lake basi hukua katika uficho, kama kumea kwa mbegu chini ya mchanga, na kukua kidogokidogo hadi inaenea katika pande zote za uwepo wa mwanadamu. Hapo hummeza sawa na linavyomeza joka kubwa. Hivyo mtu huyo kwa ukamilifu wake na upole wa namna zake zote na hisia zake anakuwa ni namna fulani ya “Ana”. Kisha “umimi” unaipa nguvu aina ya mpulizo ndani yake ambayo mna roho ya ubaguzi wa sampuli na utaifa. Basi hushupaa kwa kuuegemea ”umimi” huu mpaka inakuwa kama Shaytan Rajiim anayekaidi amri za Allah na kuzipinga. Kisha anaanza kupima watu wote, bali vitu vyote (anavipima) kwa nafsi yake na kulingana na matamanio yake. Basi anaugawanya ufalme wa Allah (s.w.) kwa vitu hivyo na juu ya sababu. Na kwa hivyo huporomoka katika shirki kubwa, inayobainika ndani yake maana ya aya tukufu: إِنَّ الشِّرْكَ لَظُلْمٌ عَظِيمٌ . Kwani kama ambaye anaiba Dinari arobaini kutoka katika mali za taifa, hapana budi awaridhishe marafiki zake walio pamoja naye kwa kila mmoja kati yao kuchukua Dirhamu moja kutoka kwake ili wizi upendeze kwake. Basi vivyohivyo kwa ambaye anasema: Hakika mimi ni mmiliki wa nafsi yangu, hapana budi aseme na kuitakidi kwamba kila kitu ni milki yake! Na namna hiyo. Basi “Ana” katika hali yake hii, yenye kuchanganyika na kuifanyia hiana amana, hakika imo katika ujinga wenye tabaka, bali ni mjinga wa wajinga. Anajibamiza katika kina cha ujinga uliopandana, hata kama amejua maelfu ya sayansi na sanaa. Hii ni kwa kuwa kinachodakwa na hisia zake na fikira zake kutokana na nuru za maarifa yaliyotawanywa katika mawanda ya ulimwengu, hapati katika nafsi yake maada inayomsadikisha, kumnawirisha na kumdumisha. Na kwa ajili hii, maarifa yote hayo huzimika, na kugeuka kuwa ni giza totoro; kwani kila kinachopita kwake kinajipaka rangi ya nafsi yake yenye giza totoro. Na hata ikipita hekima tupu ya wazi kabisa, basi huvaa katika nafsi yake mavazi ya upuuzi wa hali zote; kwa sababu rangi ya “Ana” katika hali hii ni shirki na kumtenga muumba na kutokana na sifa zake tukufu na kukanusha kuwepo kwake (s.w). Bali lau kama ulimwengu wote ungejaa ishara zenye kung’aa na taa za uongofu, basi hakika ya nukta ya giza iliyopo kwa “Ana” huzima nuru zote hizo zinazokuja, na kuzifunika zisitokeze. Hakika tumeshasema kwa ufafanuzi katika “Neno la Kumi na Moja” kuhusu uhalisia wa mwanadamu na “umimi” uliyomo kwa upande wa maana ya neno-kwa-neno, na huko tumethibitisha kwa hoja ya kukinaisha namna ya kipimo hicho nyeti cha ulimwengu, na kigezo chenye kusibu na makini, na faharisi jumuishi yenye kuzunguka, na ramani kamili, na kioo chenye kukusanya, na kalenda jumla. Basi anayetaka na arejee Risala hiyo. Hadi hapa tunahitimisha utangulizi, tukiwa katika hali ya kutosheka na maelezo yaliyomo katika Risala hiyo. Basi ewe ndugu yangu msomaji, ukiufahamu utangulizi huu, basi hebu tuingie pamoja katika uhakika yenyewe. Uhakika katika historia ya wanadamu tangu zama za Bwana wetu Adamu (a.s.) hadi wakati uliopo. Mirengo miwili mikubwa na minyororo miwili ya fikira, inakwenda pamoja na kupita kwa zama na enzi, kana kwamba viwili hivyo ni miti miwili mikubwa iliyotandaza matawi yake katika kila upande na katika kila tabaka miongoni mwa matabaka ya mwanadamu. Mojawapo ni: Mnyororo wa utume na dini. Na mwingine ni: Mnyororo wa falsafa na hekima. Basi wakati wowote ilipo minyororo hii, imeungana na kuchanganyika. Yaani katika wakati wowote au zama, falsafa hutafuta hifadhi kwa dini na kuifuata na kuwa katika utiifu wake (wa dini). Basi ubinadamu huhuika kwa furaha na kuishi maisha ya kijamii ya furaha. Na wakati wowote kunapopasuka mwanya kati yao na kutengana, nuru na heri yote hukusanyika pembezoni mwa mnyororo wa unabii na dini. Na shari na upotevu wote hukusanyika pembezoni mwa mnyororo wa falsafa. Na sasa na tupate chanzo cha kila moja ya minyororo hiyo miwili na msingi wake. Hakika mnyororo wa falsafa ambao umeasi dini, umechukua sura ya mti mbaya wa Zaqquum unaoeneza giza jingi la shirki na kueneza upotevu pembezoni mwake. Hadi kwamba umeyakabidhi kwenye mkono wa akili za wanadamu katika tawi la nguvu ya akili, matunda ya wanadahari wanamaada na wanaasili. Na kutupa juu ya kichwa cha wanadamu katika tawi la nguvu ya hasira, matunda ya kina Namrudha, Mafirauni na Mashaddadi ... na kuyalea katika tawi la nguvu ya matamanio ya kinyama, matunda ya miungu, masanamu na wenye kudai uungu. Na kando ya mti huu mbaya, mti wa Zaqquum, umeota mti wa Tuba wa uja kwa ajili ya Allah. Huo ndiyo mnyororo wa unabii. Basi, ukazaa matunda matamu na mazuri katika bustani ya tufe la Ardhi, na kuyapeleka kwa wanadamu. Yakaning’inia makonyo ya kuchumwa yaliyokaribia chini kutoka katika tawi la nguvu ya kiakili: Manabii, mitume, wakweli na mawalii wema... Kama ilivyozaa matunda katika tawi la nguvu hamasishi: Watawala waadilifu, na wafalme watoharifu kwa tohara sawa na ya malaika... Na imezaa matunda katika tawi la nguvu ya mvuto: Makarimu na wema wenye murua na tabia bora katika mwenendo mwema na uzuri wa sura wenye kujitunza na kutokuwa na hatia... Mpaka mti huo uliobarikiwa umedhihirisha kwamba mwanadamu, yeye hasa ndio tunda bora kabisa la mti wa ulimwengu. Na namna hii. Basi chanzo cha mti huu uliobarikiwa, na chanzo cha mti ule mbaya, ni pande mbili za “Ana” ambaye amekuwa ni mbegu ya kiasili ya miti hiyo miwili. Pande zake mbili zimekuwa ni chanzo cha kila mmoja kati ya miwili hiyo. Hilo tutalibainisha kwa yafuatayo: Hakika ya unabii unapita ukichukua upande wa “Ana”, na falsafa inakuja ikichukua upande mwingine wa “Ana”. Basi upande wa kwanza ambao unaangalia katika hakika za unabii, upande huu ndio chanzo cha uja safi kwa Allah (s.w.). Yaani kwamba “Ana” inajua kuwa yeye ni mja wa Allah, na ni mtiifu kwa mwabudiwa wake... Na inafahamu kwamba uhalisia wake ni wa neno-kwa-neno. Yaani ni wenye kujulisha maana kwa ajili ya mwingine... Na inaitakidi kwamba uwepo wake ni wa hali ya kufuata. Yaani unasimama kwa kuwepo mwingine na kwa kumfanya awepo... Na inajua kwamba umiliki wake wa vitu ni wa kudhaniwa. Yaani kwamba ina umiliki wa muda mfupi na wa kijuu-juu kwa idhini ya mmiliki wake wa kweli... Na hakika yake ni ya kivuli - sio ya asili – yaani yeye yamkini ni kiumbe kinyonge, na kivuli dhaifu kinachoakisi midhihiriko kwa ajili ya hakika ya wajibu na ya haki... Ama jukumu lake ni kumtii Mola wake kwa utiifu kamili wa kihisia, kwa kuwa kwake ni kipimo cha kujua sifa za muumba wake, na kigezo cha kutambua mambo yake (s.w.). Namna hii ndivyo manabii na mitume (a.s.) na waliowafuata katika wateule na mawalii, walivyoitazama “Ana” kwa upande huu, na wakaushuhudia uhakika wake kwa namna hii. Basi wakatambua hakika yenye kusibu. Na wakauegemeza ufalme wote kwa mmiliki wa ufalme mwenye utukufu. Wote wamekiri kwamba mmiliki huyo aliyetukuka hana mshirika wala mwenza, sio katika ufalme wake wala katika ubwana wake mlezi, wala katika uungu wake. Naye ni wa juu ambaye hahitajii kitu. Basi hana msaidizi wala waziri. Mkononi mwake kuna hatamu ya kila kitu, na yeye ni mweza juu ya kila kitu. Na “Sababu” sio kitu kingine isipokuwa ni mapazia na vizuizi vya nje vinavyojulisha juu ya uweza wake na adhama yake... Maumbile sio kingine isipokuwa ni sharia yake ya asili, na mkusanyiko wa kanuni zake zenye kujiri ulimwenguni, ili kudhihirisha uweza wake na adhama yake (s.w.). Basi upande huu wenye kuangaza, wenye nuru na mzuri, umechukua hukumu ya mbegu yenye maana na hekima. Kutokana na mbegu hiyo, Allah (s.w.) ameumba mti wa Tuba wa kiuja, matawi yake yaliyobarikiwa yamerefuka hadi pande za ulimwengu wa wanadamu wote na kuupamba kwa matunda mazuri yenye kung’aa. Yameondoa giza jingi lote la wakati uliopita. Yamethibitisha kwa haki kwamba muda huo mrefu mno uliopita sio kama inavyouona Falsafa kuwa ni eneo pana la makaburi ya kutisha, na medani ya kutisha ya hukumu za kunyongwa. Bali huo ni bustani katika bustani za nuru kwa roho ambazo zimetua mizigo yao mizito ili kuiondoka dunia hali ya kuwa huru, na ni eneo la nuru na ngazi yenye nuru yenye kutofautiana daraja za roho hizo zilizotoweka ili zigure kwenda Akhera na mustakabali wenye kuchanua na furaha ya milele. Ama upande wa pili: Falsafa imeushika, na imeiangalia “Ana” kwa maana ya kinomino. Yaani inasema: Hakika ya “Ana” inajijulisha yenyewe kwa yenyewe... Na kuhukumu kwamba maana yake ipo katika dhati yake, na inafanyakazi kwa ajili ya nafsi yake... Na inakutana kwamba kuwepo kwake ni kwa shina la mbali la kidhati – na sio kivuli – yaani ina dhati makhususi kwake... Na inadai kwamba ina haki katika kuishi, na kwamba yeye ni mmiliki wa hakika katika duara la usarifu wake, na kudhani madai yake ni ya hakika yenye kuthibiti... Na inafahamu kwamba jukumu lake ni kutukuka na kukamilika kidhati kunakotokana na kuipenda dhati yake... Na hivi ndivyo walivyoegemeza maslaki (nadharia) yao katika misingi mibovu mingi na wameijenga juu ya misingi hiyo yenye kuporomoka na kuanguka. Na hakika tumethibitisha kwa hali ya kukinaisha kikamilifu upeo wa uduni wa misingi hiyo na upeo wa ubovu wake katika Risala nyingi na hasa katika “Maneno” na kwa umaalumu zaidi katika “Neno la Kumi na Mbili” na la “Ishirini na Tano” yale yanayohusu miujiza ya Qur’an. Wakuu wa falsafa, viongozi wake na mabingwa wao – mfano wa: Plato, Aristotle, Ibn Sina na Al-Farabi – kwa mujibu wa misingi hiyo mibovu - wameitakidi kwamba shabaha ya mbali ya ukamilifu wa utu ni “kushabihiana na wajibu”! Yaani na Muumba (s.w.). Wakaipa jina kuwa ni hukumu ya kifirauni yenye kuvuka mpaka, na wamewafungulia njia wengi kati ya makundi yenye kujihusisha na sampuli za shiriki. Mfano: Waabudu Sababu, waabudu masanamu, waabudu Asili, na waabudu nyota; na hii ni kwa wao kuuchochea “umimi” ili upite huru katika mabonde ya shiriki na upotevu. Wakaziba njia ya uja kwa Allah, na kufunga milango ya ajizi, udhaifu, ufukara, uhitaji, kasoro na upungufu unaoingia katika maumbile ya mwanadamu. Wakapotea katika matope ya asili, na hawakuokoka kabisa kutokana na tope za ushirikina wala kuuona mlango mpana wa shukurani. Wakati ambapo wale ambao wamo katika njia ya unabii; wamehukumu kwa hukumu ambayo ujazo wake ni uja safi kwa Allah peke yake, na wameamua kwamba shabaha kuu ya utu na jukumu la msingi la wanadamu ni kujipamba kwa tabia za kiungu. Yaani kujipamba kwa tabia njema na matendo mema - ambazo Allah (s.w.) anaziamrisha - na mwanadamu ajue ajizi yake. Hivyo akimbilie kwenye uweza wake (s.w.), na aone udhaifu wake. Hivyo ajihami kwa nguvu yake (s.w.), na ashuhudie ufukara wake. Hivyo ajihifadhi kwa rehema zake (s.w.), na atazame uhitaji wake. Hivyo aombe msaada kutoka katika utajiri wake (s.w.), na atambue kasoro yake. Hivyo aombe maghufira kwa Mlezi wake (s.w.) na ahisi upungufu wake. Basi amsabihi na kuutakasa ukamilifu wake (s.w.). Na namna hii. Basi kwa kuwa falsafa yenye kuasi dini imepotea upotevu wa mbali, “Ana” imekuwa ni yenye kushika hatamu ya nafsi yake hali ya kuharakia katika kila sampuli za upotevu. Na kwa namna hii, mti wa Zaqquum umeota juu ya kilele cha upande huu wa “Ana”. Upotevu wake umefunika nusu ya wanadamu na kuwapotosha kutokana na njia iliyo sawa. Ama matunda ambayo imeyaleta mti huu khabithi, mti wa Zaqquum kwenye macho ya watu ni masanamu na miungu katika tawi la nguvu ya kinyama ya kimatamanio; kwani falsafa inapendelea hasa nguvu, na kuifanya ndio msingi na kanuni yenye kupitishwa kwa mwongozo wake, hadi kwamba msingi wa “hukumu ni ya mshindi” ni kanuni katika kanuni zake. Na kushika msingi wa “haki iko kwenye nguvu” ikapendezwa kiujumla na dhulma na uadui, na kuwachochea matughati, madhalimu na majabari wakaidi mpaka ikawapeleka kudai uungu. Kisha kwamba falsafa imeumilikisha uzuri kwa viumbe na wema kupendeza katika sura yake, kwa kiumbe mwenyewe, na katika sura yenyewe, ikijisahaulisha (falsafa) kuunasibisha uzuri huo kwa kudhihiri kwa uzuri mtakatifu wa Muumba mzuri na kupendeza kutakatifu kwa mwenye kusawiri na mtengenezaji mwema. Ikasema: “uzuri ulioje wa hiki!” badala ya kusema “uzuri ulioje wa uumbaji huu!” Yaani imeufanya uzuri huu kuwa katika hukumu sawa na sanamu lenye kustahiki kuabudiwa! Kisha ikaiona ni mema mionekano ya umashuhuri na kupendeza kwa nje kwa ajili ya ria na kutajika... Kwa ajili hiyo, imewapendelea wenye kujionesha na ikawasukuma katika kumili kwenye upotevu wao kwa kufanya mfano wa masanamu yenye kuabudiwa na waabudiwa wao. Na kulea katika tawi la nguvu ya hasira kwenye vichwa vya wanadamu masikini, Mafirauni, Manamrudha na matughati wadogo na wakubwa. Ama katika tawi la nguvu ya kiakilia; wanadahari, wanamaada, wanaasili na mfano wa hao miongoni mwa matunda khabithi wamewekwa katika akili ya binadamu. Basi ikaiparaganya akili ya mwanadamu kwa mparaganyiko ulioje! Na baada ya hayo... Ili kuuweka wazi uhakika huu, tunafanya mlinganisho kati ya matokeo yaliyokuja kutokana na misingi mibovu ya maslaki (mapito) ya falsafa na matokeo yaliyozaliwa kutokana na misingi yenye kusibu njia ya unabii. Na tutafupisha maneno katika mifano michache tu baina ya maelfu ya milinganisho kati ya mawili hayo. Mfano wa Kwanza: Katika kanuni zilizowekwa kwa ajili ya unabii katika maisha binafsi ya mwanadamu ni kujiweka katika tabia za Allah. Yaani kuweni waja wa Allah wenye ikhlasi, wenye kujipamba kwa tabia za Allah, wenye kujihami kwa himaya yake, wenye kukiri katika kina cha nafsi zenu ajizi (kushindwa) yenu, ufukara wenu na upungufu wenu. Basi iko wapi kanuni hii katika kauli ya falsafa: “jishabihisheni na wajibu!” inayoiweka kuwa ni shabaha kuu ya utu! Uko wapi uhalisia wa mwanadamu ambao umekongweka kwa ajizi, udhaifu, ufukara na uhitaji usio na mipaka katika uhalisia wa aliye wajibu kuwepo. Naye ni Allah Mweza, Mwenye nguvu, Mkwasi na Aliyetakasika!! Mfano wa Pili: Katika kanuni thabiti za unabii katika maisha ya kijamii ni kwamba “kusaidiana” ni kanuni yenye kutamalaki juu ya ulimwengu, kuanzia kwenye jua na mwezi hadi kwenye mimea na wanyama. Basi utaona mimea inawakimu wanyama, na wanyama wanamkimu mwanadamu, bali atomu za chakula zinazikimu chembe za mwili na kuzisaidia. Basi iko wapi kanuni hii nyoofu, kanuni ya kusaidiana na kanuni ya ukarimu na sharia ya kukirimu kutoka ndani ya kanuni ya “mapambano” ambayo falsafa inaieleza kuwa ndiye hakimu wa maisha ya kijamii. Kwa kujua kwamba “mapambano” hutokea tu kwa baadhi ya madhalimu na wanyama pori washambuliao kutokana na matumizi mabaya ya maumbile yao. Bali falsafa imetokomea katika upotevu wake mpaka ikaifanya kanuni hii ya “mapambano” kuwa ni hakimu mwenye kutamalaki juu ya vilivyopo vyote. Ikaweka kanuni kwa upumbavu uliofikia kikomo kwamba: “hakika ya uhai ni mabishano na mapambano”. Mfano wa Tatu: Katika matokeo ya kimfano ya unabii na katika kanuni zake za hadhi ya juu katika Tawhiid ni kwamba “moja haitokei isipokuwa kutoka kwa mmoja”. Yaani kila ambacho kina umoja hakitokei isipokuwa kutoka kwa mmoja; kwa kuwa katika kila kitu – na katika vitu vyote – kuna umoja wa dhahiri, basi hapana budi kuwa huo ni kutokana na ufanyaji wa uwepo wa dhati moja. Wakati ambapo kanuni ya falsafa ya kale na itikadi yake ni kuwa “hakika mmoja, hakitoki kwake isipokuwa kimoja”. Yaani hakitokei kutokana na dhati moja isipokuwa kimoja. Kisha vitu vingine hutokea kupitia viunganishi. Kanuni hii ya falsafa ya kale inazipa sababu zilizopo na viunganishi aina fulani ya ushirika katika uungu mlezi, na inadhihirisha kwamba yule aliye Mweza juu ya kila kitu, aliye mkwasi wa hali zote na mwenye kutosheka kwa kutohitajia chochote ni muhitaji wa viunganishi vyenye kushindwa! Bali wamepotea upotevu wa mbali hadi wakampa Muumba (s.w.) jina la kiumbe nalo ni “akili ya kwanza”. Wakaugawa ufalme wake mwingine kati ya viunganishi. Hivyo wakafungua njia kuelekea kwenye shirki kubwa. Basi iko wapi hiyo kanuni ya Tawhiid ya unabii ikilinganishwa na kanuni hii - ya falsafa gonjwa na ya kale - iliyochafuliwa na shirki na kupakazwa upotevu? Basi kama wanamrengo wa mashariki (ashraqiyuun) ambao ni wanafalsafa wa juu na wenye hekima kwa kufahamu wakiwa wanatamka upuuzi huu wa maneno basi itakuwaje - unadhani – maneno ya waliokuwa chini yao katika falsafa na hekima katika wanamaada na wanaasili? Mfano wa Nne: Hakika ni katika kanuni za hekima ya unabii, kwamba kila kitu kina hekima nyingi na manufaa mbalimbali mpaka tunda lina hekima kiasi kinachohesabiwa kwa idadi ya matunda ya mti. Kama inavyofahamika kutokana na aya tukufu: (وَإِن مِّن شَيْءٍ إِلاَّ يُسَبِّحُ بِحَمْدَهِ) Basi ikiwa kuna matokeo mamoja – ya kuumba chenye uhai – yenye kukielekea kiumbe chenyewe, na hekima moja ya kuwepo kwake inamrejea yeye, basi maelfu ya matokeo hayo yanarudi kwa Muumba wake Mwenye hekima, na maelfu ya hekima yanaelekea kwa Muumba wake mtukufu. Ama kanuni ya falsafa ni kuwa: “Hekima ya kuumbwa kwa kila kiumbe hai na faida yake ni yenye kumwelekea kiumbe mwenyewe au inarudi kwa manufaa ya mwanadamu na masilahi yake”, kanuni hii inavinyang’anya vilivyopo hekima nyingi zilizokabidhiwa, na kutoa tunda la sehemu ndogo ama punje ya haradali kwa mti mkubwa. Hivyo kuvigeuza vilivyopo kuwa ni upuuzi usio na faida nyuma yake. Basi iko wapi hiyo hekima yenye kusibu kutokana na kanuni hizi mbovu za falsafa - iliyo tupu bila ya hekima – ambayo imeubatiza uwepo wote kuwa ni upuuzi! Kwa hakika tumefupisha maneno hapa kwa kadiri hii, ambapo tumeujadili uhakika huu katika Hakika ya Kumi kutoka katika Neno la Kumi kwa kiasi fulani cha ufafanuzi. Na baada ya hayo... inayumkinika kupima kwa uelekeo wa mifano hii maelfu ya vielelezo na mifano, na tumekwishaashiria sehemu fulani kati yake katika Risala ya “Ming’ao”. Na kwa kuangalia kuegemea kwa falsafa kwenye mfano wa misingi hii migonjwa na matokeo yake mabaya, basi hakika wanafalsafa hodari wa Kiislamu ambao mandhari ya falsafa imewang’arisha, wakaelekea katika njia yake kama Ibn Sina na Al-Farabi, hawakupata kingine isipokuwa kiasi cha chini cha daraja za imani, daraja ya muumini wa kawaida, bali Hujjat Al-Islamu Al-Imamu Al-Ghazali hakuwapa hata daraja hiyo; vivyohivyo maimamu wa Mu’utazila, ambao nao ni katika maulamaa wa Elimu ya Alkalamu waliozama. Hii ni kwa kuwa wamefitinika na falsafa na mapambo yake na wakakazia uhusiano wao na hiyo falsafa, na wakatumia akili kuhukumu, basi hawakuambulia chochote isipokuwa daraja ya muumini mzushi na fasiki. Na kadhalika Abuu Al-A’laa Al-Maary ambaye ni katika wanazuoni wakubwa wa wanafasihi wa Waislamu na maarufu kwa kuwa na matumaini mabaya na Umar Al-Khayyaam mwenye kusifiwa kwa masikitiko yake ya kiyatima, na mifano wa hao wawili miongoni mwa wanafasihi wakubwa katika ambao yameshughulishwa matamanio yao na zikastaajabishwa nafsi zao zenye kuamuriwa na hiyo falsafa... Basi hawa wamepokea kofi la kutiwa adabu na pigo la kudhalilishwa na kukufurishwa na watu wa hakika na ukamilifu. Wakawakemea kwa kusema: “Enyi wapumbavu, hakika nyinyi mnafanya upumbavu na adabu mbaya, na mnapita njia ya wazandiki, na mnawalea wazandiki katika mbeleko za fasihi yenu!”. Kisha miongoni mwa matokeo ya misingi mibovu ni kwamba “Ana” ambayo haina chochote katika dhati yake isipokuwa uhalisia dhaifu kana kwamba ni hewa au mvuke, lakini kwa ubaya wa mtazamo wa falsafa, na kuona kwake vitu kwa maana ya kinomino (jina), inayeyuka. Kisha kwa sababu ya upatano na kuzama katika mambo ya kimaada na matamanio mabaya kana kwamba inaganda, kisha inafunikwa na mghafala na kukanusha, basi “umimi” huo huwa mgumu. Kisha kwa kuziasi amri za Allah huchafuka “Ana” na kupoteza hali yake ya kuonesha (usafi) na kubaki yenye giza. Kisha hushupaa kidogokidogo hadi kummeza mwenyewe. Bali “Ana” haisimami katika mpaka huu tu, bali inafura na kupanuka kwa mawazo ya mwanadamu na inaanza kuwapima watu – mpaka Sababu - juu ya nafsi yake, basi huipa ufirauni wenye kuvuka mipaka – licha ya kuukataa na kujikinga nao – na wakati huo huchukua hatua ya hasimu wa amri za kiungu na kusema: (مَنْ يُحْيِي الْعِظَامَ وَهِيَ رَمِيمٌ) kana kwamba inampa changa moto Allah (s.w.) na kumtuhumu mweza juu ya kila kitu kwa ajizi. Kisha jambo hili linamfikisha kuingilia katika sifa tukufu za Allah, basi inakanusha au inapotosha au inakataa kila kisichokubaliana na matamanio ya nafsi yake au yasiyopendeza ufirauni wa nafsi yake. Basi mathalani: Kundi la wanafalsafa limempa jina Allah (s.w.): “Mwenye kuwajibisha kwa dhati” wakakanusha utashi na hiari kwake (s.w.) wakikadhibisha ushahidi wa ulimwengu wote juu ya utashi wake wa hali zote. Fayaa Subhanalllah! Ajabu iliyoje ya mwanadamu huyu! Hakika vilivyopo vyote kuanzia atomu hadi majua (sayari) vinajulisha kwa namna ya wazi juu ya utashi wa Muumba Mwenye hekima; kwa bainisho zake, na kupangika kwake, na hekima zake, na vipimo vyake; vipi jicho la falsafa haliyaoni hayo? Allah apofue macho yao! Na kundi jengine katika wanafalsafa limedai kwamba: “elimu ya kiungu haina uhusiano na sehemu ndogondogo”, wakikanusha kwa elimu ya Allah (s.w.) kukizunguka kila kitu, wakikataa ushahidi wa vilivyopo vya ukweli juu ya elimu yake Allah yenye kuenea kila kitu. Kisha falsafa inazipa Sababu taathira, na inaipa Asili kuwepo na kuanzisha (vitu). Basi haioni ishara zenye kumeremeta juu ya kila kilichopo kinachojulisha juu ya Muumba mtukufu - kama tulivyothibitisha katika “Neno la Ishirini na Mbili” - ukiongezea kuwa inaegemeza kuumba sehemu ya vilivyopo – ambayo ni maandishi ya kiungu ya Swamdaaniyyah (ya mwenye kukusudiwa kwa kila haja) – kwenye Asili yenye kushindwa yasiyo na uhai na yenye kukosa utambuzi, na ambayo hakuna mikononi mwake isipokuwa sadfa ya holela na nguvu pofu, ikiifanya iwe na – yaani Asili – hali ya kuwa ni chanzo katika uumbaji wa vitu, na ufanyaji katika kuathiri! Basi ikazuia maelfu ya hekima zenye kuingia katika vilivyopo. Kisha falsafa haikuuona mlango mpana wa Akhera, ikakanusha ufufuo, na kudai uazali (utangu) wa roho, hali ya kujua kwamba Allah (s.w.) kwa majina yake yote mazuri, na ulimwengu pamoja na hakika zake zote, na manabii na mitume watukufu (a.s.) pamoja na yote waliyoyaleta katika mambo ya hakika, na vitabu vya mbinguni na aya zake tukufu zote... vinabainisha ufufuo na Akhera kama tulivyolithibitisha hilo katika “Neno la Kumi”. Na kwa hivi inayumkinika kwako kuyapima maswala mengine ya falsafa juu ya uzushi huu wa kipumbavu. Naam, kana kwamba mashetani wamezinyakua akili za wanafalsafa wapagani (wakanaji Mungu) kwa midomo mirefu (kama ya ndege) ya “Ana” na makucha yake na kuzitupa katika mabonde ya upotevu na kuyararua vibaya vibaya. Basi “Ana” katika ulimwengu mdogo (mwanadamu) ni kama ilivyo Asili katika ulimwengu mkubwa. Vyote hivyo viwili ni katika Matwaghuti. فَمَن۟ يَك۟فُر۟ بِالطَّاغُوتِ وَيُؤ۟مِن۟ بِاللّٰهِ فَقَدِ اس۟تَم۟سَكَ بِال۟عُر۟وَةِ ال۟وُث۟قٰى لَا ان۟فِصَامَ لَهَا وَاللّٰهُ سَمٖيعٌ عَلٖيمٌ Hakika nimeona tukio la kumpigiwa mfano kabla ya kuanza kuandika Risala hii kwa miaka minane nilipokuwa mji wa Istanbul ndani ya mwezi wa Ramadhani uliobarikiwa. Wakati huo Saidi wa zamani - ambaye ameshughulika na falsafa - alikuwa karibuni ageuke kuwa Saidi mpya... Katika kipindi hiki hasa, na nilipokuwa nikitafakari katika maslaki (mapito) tatu zilizoashiriwa mwishoni mwa Surat Al-fatiha (صِرَاطَ الَّذِينَ أَنعَمتَ عَلَيهِمْ غَيرِ المَغضُوبِ عَلَيهِمْ وَلاَ الضَّالِّينَ) nimeona tukio hilo la kimawazo. Nalo ni tukio linalofanana mno na inavyokuwa njozi. Nikalisajili wakati uleule katika kitabu changu “Ming’ao” kwa sura ya utalii wa kimawazo na kwa namna inayofanana na nudhumu. Sasa umefika wakati wa kutaja maana yake na kulisherehesha, kwani linaangazia juu ya uhakika ulioelezwa. Nilikuwa ninaiona nafsi yangu ipo katikati ya jangwa pana na kubwa, na mbingu imefunikwa na mawingu yenye giza totoro, hadi pumzi inakaribia kukabwa juu ya Ardhi yote. Basi, hakuna upepo wala mwanga wala maji; vyote hivyo havipo. Nilidhani kwamba Ardhi imejaa wanyamapori wakali na wanyama wenye kudhuru. Yakapita mawazo katika moyo wangu kwamba ng’ambo nyingine ya Ardhi kunapatikana upepo mwanana, maji matamu na mwanga mzuri. Basi hakuna namna ya kuvuka kwenda huko... Kisha nikajikuta ninapelekwa huko bila kutaka... Nikaingia pangoni chini ya Ardhi inayofanana na yanavyokuwa matobo ya chini ya milima. Nikatembea chini ya Ardhi hatua kwa hatua nami nikishuhudia kwamba wengi wamenitangulia kupita katika njia hii chini ya Ardhi bila ya kukamilisha mwendo kwani wamebaki katika mahali pao hali ya kuwa wanakabwa na pumzi. Nilikuwa nikiona athari za nyayo zao, na – wakati mwingine - nikisikia sauti za idadi kati yao... kisha sauti zinakatika. Basi ewe rafiki yangu ambaye kwa mawazo yake anaambatana nami katika matembezi yangu haya ya kimawazo! Hakika Ardhi hiyo ni Asili na “falsafa ya kiasili. Ama lile tobo ni maslaki (mapito) ambayo wanafalsafa wameyapasua kwa fikira zao ili kuufikia uhakika. Ama athari za nyayo ambazo nimeziona, basi hizo ni za wanafalsafa mashuhuri kama Pilato na Aristotle . Na nilizozisikia katika sauti ni sauti za mahodari kama Ibn Sina na Al-Farabi... Naam, nilikuwa nakuta kauli za Ibn Sina na kanuni zake katika sehemu kadhaa, lakini sauti zilikuwa zikikatika kabisa. Kwa maana ya kuwa hazikuweza kuendelea. Yaani amekabwa pumzi... Kwa hali zote, nimekwisha kukubainishia baadhi ya hakika zilizomo chini ya mawazo ili nikurahisishie hamu yako na shuku yako... Na sasa narudi kuelezea matembezi yangu: Niliendelea kutembea, na tahamaki kuna vitu viwili vinafanywa mbele yangu. Cha Kwanza: Taa ya umeme, inaondosha giza jingi nene la Asili chini ya Ardhi. Na Kingine: Kifaa kikubwa, kinavunja mawe makubwa sana mfano wa milima... Tahamaki njia inanifungukia. Wakati huo ilinong’onwa sikioni mwangu kwamba: Taa hii na kifaa hiki, umetunukiwa wewe kutoka katika hazina ya Qur’an tukufu... Kwa hali hii, nimekwenda kwa muda juu ya mwelekeo huu, mpaka nikajikuta nimefika ng’ambo nyingine. Tahamaki jua linachomoza katika mbingu safi na nzuri isiyo na mawingu, na siku hii ni siku ya machipuo yenye kufurahisha, na upepo mwanana unaipunga roho, na maji baridi na matamu (salsabila) yanatiririka. Kwa hakika nimeuona ulimwengu wote umejawa na furaha kila mahali. Nikamhimidi Allah (s.w.). Kisha nikaitazama nafsi yangu nikaikuta kwamba mimi siimiliki na wala siwezi kuitawala, kana kwamba mmoja wao ananiweka mimi mahali pa majaribu. Kwa ghafla nilijikuta mara nyingine katika jangwa hilo pana, na yamefunika mawingu mazito tena. Mbingu zikawa na giza, na pumzi zinakaribia kukabwa kutokana na dhiki... Nikahisi mwongozaji ananipeleka kwenye njia nyingine. Ambapo mara hii nilijiona natembea juu ya Ardhi na sio chini yake, njiani mwangu kuelekea ng’ambo nyingine... Katika kwenda kwangu huku, niliona mambo ya ajabu na mandhari mageni yasiyoelezeka; basi bahari ni yenye kunikasirikia, na kimbunga kinanitisha, na kila kitu kinatupa mbele yangu vikwazo na misukosuko. Isipokuwa, mishkeli hiyo inalainishwa kwa fadhila ya niliyopewa kutoka katika Qur’an tukufu katika nyenzo ya kimatembezi. Basi nikawa ninayashinda kwa nyenzo hizo... Nikaanza kukata mbuga hatua kwa hatua. Nikakuta miili ya wasafiri na majeneza yametupwa juu pembezoni mwa njia huku na huko. Kwani hakumaliza safari hii isipokuwa mmoja tu kati ya elfu... Na kwa hali yoyote ile, kwa hakika nimeokoka kutokana na giza jingi la mawingu yenye kuziba pumzi na nimefika ng’ambo nyingine ya Ardhi. Nikalielekea jua la hakika na zuri, na nimepunga hewa mwanana, na nikaanza kutembea katika ulimwengu huo wenye kufurahisha kama Pepo huku nikikariri: Alhamdulillah. Kisha nikaona kwamba mimi sitoachwa hapa, kuna ambaye kana kwamba anataka kunionesha njia nyingine, mara moja akanirejesha nilipokuwa... kwenye jangwa lile pana. Nikatazama. Tahamaki kuna vitu vinashuka kutoka juu kama zinavyoshuka lifti (za umeme) kwa maumbo tofauti na mitindo mbalimbali, baadhi yake yanafanana na ndege na baadhi yanafanana na magari, na mengine kama vikapu vyenye kuning’inia, na hali kama hiyo. Basi mwanadamu yeyote awezaye kuning’inia mojawapo ya vitu hivyo, kulingana na ukubalifu wake na nguvu yake, basi kwa hakika hupazwa kuelekea juu... Nikapanda moja wapo. Tahamaki ndani ya dakika moja niko juu ya mawingu na juu ya milima mizuri iliyopiga rangi ya kijani kiwiti. Bali mawingu hayafikii nusu ya milima hiyo mikubwa... Kila mahali kunashuhudiwa mwanga mzuri mno, na maji matamu mno na upepo mwanana mno... Nilipotupa macho yangu kuangalia pande zote, niliona nyumba hizo za nuru – zenye kufanana na lifti – zimeenea kila mahali. Na nilikuwa nimekwishashuhudia mfano wake katika ng’ambo nyingine ya Ardhi katika matembezi hayo mawili yaliyotangulia... Lakini sikufahamu kitu chochote kutokana na hayo, licha ya kuwa mimi sasa nafahamu kwamba nyumba hizi kwa hakika ni midhihiriko ya aya za Qur’an tukufu. Na namna hii. Basi njia ya Kwanza: Ni njia ya wapotevu iliyoashiriwa kwa (الضَّالِّينَ). Nayo ni maslaki (mapito) ya wale ambao wameteleza katika mtazamo wa “Asili” na kushika fikra za wana-Asili... Mmeshatambua kiasi cha ugumu wa kufika katika hakika kupitia njia hii iliyojaa mishkeli na vikwazo. Njia ya Pili: Ni ile iliyoashiriwa kwa (المَغضُوبِ عَلَيهِمْ). Hayo ni maslaki ya waabudu sababu na ambao wanaelekeza uumbaji na ufanyaji kitu kiwepo kwa viunganishi, na wanaegemeza taathira kwa vitu hivyo, na wanataka kufikia hakika ya haki, na kumjua Allah (s.w.) kupitia akili na fikira peke yake. Kama vile wanafalsafa wa mrengo wa Mashaiina (Peripatetikos). Ama njia ya Tatu: Ni ile iliyoashiriwa kwa: (الَّذِينَ أَنعَمتَ عَلَيهِمْ). Hiyo ni njia iliyonyooka na njia ya nuru ya watu wa Qur’an ambayo ni fupi kabisa, salama zaidi, nyepesi yake zaidi, na iko wazi mbele ya watu wote waipite. Nayo ni maslaki (mapito) ya kimbingu, ya kirehema na yenye nuru.
Linahusu Mabadiliko ya Atomu Linaashiria Atomu kutoka katika Hazina ya Aya hii Tukufu وَقَالَ الَّذٖينَ كَفَرُوا لَا تَا۟تٖينَا السَّاعَةُ قُل۟ بَلٰى وَ رَبّٖى لَتَا۟تِيَنَّكُم۟ عَالِمِ ال۟غَي۟بِ لَا يَع۟زُبُ عَن۟هُ مِث۟قَالُ ذَرَّةٍ فِى السَّمٰوَاتِ وَلَا فِى ال۟اَر۟ضِ وَلَٓا اَص۟غَرُ مِن۟ ذٰلِكَ وَلَٓا اَك۟بَرُ اِلَّا فٖى كِتَابٍ مُبٖينٍ Makusudio haya yanabainisha punje ya atomu kutoka katika hazina kubwa ya aya hii tukufu. Yaani yanabainisha kiini ambacho ndani yake kimo kijisanduku cha atomu, na yanaelezea sehemu ndogo sana katika mchakato wa atomu na wadhifa wake; na hayo ni katika nukta tatu pamoja na utangulizi.
Hakika mabadiliko ya atomu na matembezi yake ni kitu kama mitetemeko ya atomu na kugura kwake wakati wa kuandika kwa kalamu ya uweza wa kiungu wa aya za uumbaji katika kitabu cha ulimwengu. Basi hiyo atomu siyo kama wanavyoidhania wanamaada na wana-Asili kwamba ni mchezo wa sadfa katika mchakato holela usio na maana wala makusudio; na hii kwa kuwa kila atomu inasema mwanzoni mwa mchakato wake: “Bismillah” (kwa jina la Allah) - kama vilivyopo vyote vinavyosema hilo -ambapo inabeba mizigo mikubwa inayozidi sana uwezo wake mdogo mno, kama mbegu ya msonobari kuubeba mti wake mkubwa juu ya mabega yake. Kisha wakati wa kumaliza jukumu lake husema: “Alhamdu lillah” (himidi zote ni za Allah). Kwa kuwa imedhihirisha athari ya ajabu, kana kwamba inaimba kasida nzuri katika kumsifia Mtengenezaji mtukufu, kwa yaliyomo katika uzuri wa ufundi wenye hekima, na kupendeza kwa sura yenye kudhihirisha maana ya kina yenye kuitahayarisha akili. Ukitaka, basi tazama kwa makini komamanga na atomu. Naam, hakika mabadiliko ya atomu na kugura kwake, ni kitu kama mitikisiko na mitetemeko yenye maana ya kina inayotokana na kuandika maneno ya uweza wa kiungu na kuyafuta maneno hayo katika ubao “wa kufuta na kuthibitisha” ambao ni hakika ya zama zenye kuyoyoma na ukurasa wake wa kupigiwa mfano, kwa kunukuu kutoka katika kitabu kibainifu ambacho ni anuani ya uweza wa kiungu na utashi wake, na mhimili wa kusarifu katika kuvifanya vitu viwepo na kuvipa maumbo katika ulimwengu wa kushuhudia na zama za sasa, kulingana na kanuni za Al-Imamu Al-Mubiin ambaye ndiye mkusanyaji wa vitendea kazi vya vitu katika mashina yake na matawi yake – yaani asili ya kila kitu kilichopita na kila kizazi kijacho – ambavyo vimekunjwa na ghaibu, pamoja na sifa zake pambanuzi, na anuani ya elimu ya kiungu na amri yake.
Nayo ni Maudhui Mbili Maudhui ya Kwanza: Kwa hakika katika mtikisiko wa kila atomu na katika kutulia kwake zinang’aa nuru mbili za Tawhidi kama ni majua (sayari) mawili yenye kuangaza. Na kwa hakika tumethibitisha kwa yakini kwa uthibitisho jumla katika ishara ya kwanza, kutoka katika “Neno la Kumi” na tulifafanua katika “Neno la Ishirini na Mbili” kwamba kila atomu katika atomu kama isipoamuriwa kwa amri za Allah (s.w.) na kama haikutikisika kwa idhini yake na utendaji wake, na isipogeuka kwa elimu yake na uweza wake, basi hapana budi kuwa kila atomu ina elimu isiyo na ukomo, na uweza usio na mpaka, na jicho linaloona kila kitu, na uso unaoelekea kila kitu, na amri tendaji katika kila kitu. Kwa kuwa kila atomu katika atomu za vitu, hufanya – au yamkini kufanya – utendaji wenye kupangika katika mwili wa kila kiumbe hai, kwa kujua kwamba mifumo ya vitu na kanuni za miundo yake ni yenye kutofautiana baadhi yake na baadhi nyingine. Na haiwezekani kufanya kitu kisichojulikana mifumo yake, na hata kama atomu ingetenda jambo bali haliachi kuwa na kosa, ilhali matendo yanatimizwa bila ya kosa. Kwa hivyo basi, ima hizo atomu zenye kutenda zinatenda kwa mujibu wa amri za mwenye kumiliki elimu yenye kuzungukia kila kitu, na kwa idhini yake, na elimu yake, na kwa utashi wake... au yatakikana (kwa hiyo atomu) kuwa na mfano wa elimu hiyo yenye kuzungukia kila kitu na uweza wa hali zote! Kisha kila atomu katika atomu za hewa, inaweza kuingia katika mwili wa kila kiumbe hai, na katika tunda la kila ua, na katika ujenzi wa kila jani, na kufanya kazi katika kila moja miongoni mwao; kwa kujua kwamba jengo la kila moja kati yake linatofautiana na lingine, na mfumo wake ni tofauti na mwingine. Basi kama kingekuwa kiwanda cha mti wa tini - mathalani – kinafanana na kiwanda cha nguo, basi kiwanda cha tunda la mkomamanga kingekuwa ni shabihi ya kiwanda cha sukari. Hivyo, miundo ya kila kimoja kati ya viwili hivyo, na jengo la kila kimoja kati yake ni tofauti na kingine. Basi atomu hizi za hewa zinaingia katika kila moja kati yao – au zinaweza kuingia - na zinafanyakazi kwa umahiri wa hali ya juu na kwa hekima timilifu, na kuchukua hali maalumu ndani yake. Kisha pale ambapo jukumu lake linakwisha inaziacha zikipita na hali yake. Basi na hali iko namna hii. Hivyo, atomu yenye kufanya mchakato kwenye hewa yenye kuchakatika; ima ni kuwa inajua sura zilizovikwa juu ya wanyama na mimea, na juu ya matunda yake na maua yake, na vilevile inajua vipimo vya kila moja kati yake na mitindo ya usanifu wake! Au atomu hiyo ni yenye kuamuriwa kwa amri ya anayejua yote hayo na inafanyakazi kwa utashi wake (huyo Mjuzi). Na pia kila atomu iliyotulia katika mchanga uliotulia tuli, ni yenye kutayarishwa ili kuwa ni maoteo ya mbegu zote za mimea yenye kuchanua maua na miti yenye kuzaa matunda; kiasi kwamba lau ungetupiwa katika gao la mchanga – ulioundika kutokana na atomu zenye kufanana kana kwamba ni atomu moja - na kukutana na atomu zilizomo; ima ikute kiwanda maalumu kwake, pamoja na yanayohitajiwa na jengo lake miongoni mwa yanayolazimu na zana mbalimbali. Yaani iwe katika hilo gao la mchanga kuna viwanda vya kimaanawi vingi na madhubuti, kwa idadi ya sampuli za mimea, miti na matunda! Au iwepo elimu pana na uweza wenye kukizunguka kila kitu unaoanzisha kila kitu kutokana na kutokuwepo... Au kwamba kazi hizo kwa hakika zinafanyika kwa uweza na nguvu ya Allah juu ya kila kitu na Mjuzi wa kila kitu. Kama mtu atasafiri kwenda Ulaya, na yeye ni mjinga wa mifumo ya ustaarabu kwa ujinga mbumbumbu, hata hivyo yeye ni kipofu haoni, na kama ataingia huko katika viwanda vyote, na akafanikisha kazi nzuri ajabu katika kila aina za ufundi na katika aina za majengo kwa mpangilio kamili na hekima ya juu na umahiri uliyozitahayarisha akili... basi hapana shaka mwenye punje ndogo ya utambuzi atatambua kwa yakini kwamba mtu huyo hafanyi anayoyafanya kutokana na nafsi yake, bali yupo ustadhi mjuzi anayemfundisha na kumtumia. Na vilevile kama kungekuwa na mwenye kushindwa (asiyejiweza), kipofu, kiwete, amekaa katika kibanda chake kidogo, hatikisi chenye kutulia. Imeingizwa kwake kiasi cha punje kidogo na vipande vya mifupa na kiasi kidogo cha pamba. Tahamaki kibanda kidogo kinatoa tani kadhaa za sukari, na majora ya nguo, na maelfu ya vipande vya johari, pamoja na mavazi katika mapambo ya fahari na sampuli ya fahari zaidi, pamoja na vyakula vizuri vyenye utamu wa hali ya juu... Je hatosema yule ambaye ana chembe ya akili kwamba: Kipofu yule aliyepweteka, yeye si lolote isipokuwa ni mlinzi dhaifu wa kiwanda chenye muujiza, na ni mtumishi kwa mwenye kiwanda chenye miujiza? Na hali iko namna hiyo kwenye michakato ya atomu za hewa na majukumu yake katika mimea, miti, maua na matunda; ambazo kila moja kati yake ni maandishi ya kiungu ya mwenye kukusudiwa kwa kila haja, na ni ajabu katika maajabu (ya kuvutia) ya ufundi wa kiungu, na ni muujiza katika miujiza ya uweza wa kiungu, na ni kufurutu ada miongoni mwa vyenye kufurutu ada vya hekima ya kiungu. Hivyo, atomu hizo hazitikisiki wala haziondoki kutoka mahali kwenda pengine isipokuwa kwa amri ya Mtengenezaji, Mwingi wa Hekima na Mwenye utukufu, na kwa utashi wa Muumba Mkarimu Mwenye utukufu. Na upime juu ya hili atomu za mchanga ambao ni maoteo ya mashuke ya mbegu na kokwa, ambazo kila moja kati yao ni sawa na mashine ya ajabu inayotofautiana na nyingine, na ni kiwanda cha kuchapa kilicho tofauti na kingine, na ni hazina iliyo mbali na nyingine, na ni bango la matangazo linalotangaza majina mazuri ya Allah yenye kupambanuka na mengine, na ni kasida safi inayosifia makamilifu yake (s.w.). Hapana shaka kwamba mbegu hizi za ajabu hazikuwa ni zenye kuunda miti ile na mimea, isipokuwa kwa amri ya Allah Mwenye kumiliki amri ya (كُنْ فَيَكُوْن) na kila kitu ni chenye kutumikishwa kwa amri yake, na hakitendi ila kwa idhini yake, utashi wake na nguvu yake... Hili ni yakini na lenye kuthibiti kwa kukata shauri... Tumeamini. Maudhui ya Pili: Maudhui hii ni ishara nyepesi katika majukumu na hekima zilizomo kwenye michakato ya atomu. Hakika ya wanamaada ambao akili zao zimetumbukia kwenye macho yao, hawaoni isipokuwa maada. Wanaona kwa hekima yao isiyo na hekima na kwa falsafa yao iliyojengwa juu ya msingi wa upuuzi katika uwepo. Kwamba mabadiliko ya atomu yamefungamana na sadfa. Hadi wameifanya kuwa ni kanuni iliyowekwa kwa taratibu zao zote, wakiifanya kuwa ndio chanzo cha kufanywa viwepo viumbe wa Bwana Mlezi! Basi anayemiliki chembe ya utambuzi anajua kwa yakini kiwango cha wao kuwa mbali na mantiki ya akili katika wao kuviegemeza viumbe hivi vilivyopambwa kwa hekima nyingi, kwenye kitu chenye kuchanganyika na cha kiholela kisicho na hekima wala maana. Ama mtazamo wa Qur’ani na hekima yake, kwa hakika inaona kwamba kugeuka kwa atomu kuna hekima nyingi mno na shabaha zisizodhibitika na majukumu yasio na mpaka. Aya tukufu inaliashiria hilo: (وَإِنْ مِنْ شَيْءٍ إٍلَّا يُسَبِّحُ بِحَمْدِهِ) na mfano wake katika aya nyingi. Na sisi hapa tunaashiria chache tu kati ya hizo kwa njia ya kutoa mfano: Kwanza: Hakika Allah (s.w.) kwa ajili ya kuleta upya midhihiriko ya kukifanya kitu kiwepo katika uwepo, anazipa mchakato atomu na kuzitumikisha kwa uweza wake, akijaalia kutokana na kila roho moja «kielelezo». Akakivisha kiwiliwili kipya katika miujiza ya uweza wake katika kila mwaka. Na kutoka katika kila kitabu kimoja-kimoja kwa hekima yake timamu, ananukuu maelfu ya vitabu anuai, na anadhihirisha hakika moja katika mitindo tofauti na sura mbalimbali, na kutanua uwanja na kuandaa mahali kwa ajili ya kupatikana viumbe vipya na limwengu mpya, na vilivyopo vipya, kundi baada ya kundi. Pili: Hakika ya Maalikulmulki Dhuljalaali, ameiumba Dunia hii na hasa uso wa Ardhi kwa umbo la shamba pana. Yaani ameliandaa ili iwe ni yenye kukubali kukua kwa mavuno ya vilivyomo, na kuzaliwa kwake, na kudhihiri kwa upya wake na upevu wake. Yaani ipate kulimwa humo miujiza ya uweza wake isiyo na ukomo na kuivuna. Basi katika shamba lake hili pana ambalo ni pana kama mgongo wa Ardhi, Subhanahu anadhihirisha kutokana na miujiza ya uweza wake viumbe vipya katika kila enzi, katika kila majira, kila mwezi, kila siku, bali kila saa. Anaupa uwanja wa Ardhi mavuno mapya anuai, kwa kuzipa atomu michakato kwa hekima kamili na kuzikabidhi majukumu kwa mfumo wa ufundi makini, huku (s.w.) akibainisha kwa michakato ya atomu hizi zawadi za rehema zake zinazotoka katika hazina yake isiyokwisha, na vielelezo vya miujiza ya uweza wake ambavyo havitindiki. Tatu: Hakika (s.w.) anaziweka atomu katika mchakato kwa hekima kamili na kuzitumikisha katika majukumu yaliyopangika kwa ajili ya kudhihirisha maajabu ya vilivyopo ili majina mazuri yafundishe maana za kudhihirika kwake kusiko na ukomo. Basi (s.w.) anatoa kutoka katika pahala padogo kiasi kisicho na mpaka katika maajabu ya sura zenye kujulisha midhihiriko hiyo isiyo na ukomo. Anaandika katika ukurasa finyu aya za uumbaji zisizo na mpaka, zinazoelezea maana za hadhi ya juu zisizo na mpaka. Naam, hakika ya mavuno ya mwaka uliopita na matokeo yake katika vilivyopo, na mavuno ya mwaka huu na matokeo yake, kwa upande wa chimbuko ni katika hukumu moja, isipokuwa kwamba maana zake na mafahamisho yake ni yenye kutofautiana sana. Kwani kwa kubadilisha ishara za kimazingatio, basi na maana zake hubadilika, hukithiri na kuongezeka. Na kwa kuwa ishara za kimazingatio na maumbo ya muda maalumu hubadilishwa, nayo ni yenye kutoweka katika hali ya dhahiri, isipokuwa kwamba maana zake nzuri hutunzwa, huendelea, hubakia na kuthibiti. Basi majani ya mti huu, maua yake na matunda yake ambayo yalikuwa katika majira ya machipuo yaliyopita – kwa sababu hayabebi roho kama mwanadamu – ndiyo mifano yake yenyewe hiyohiyo katika majira haya ya machipuo kama ikitazamwa katika pembe ya uhakika. Isipokuwa, tofauti imo katika kushika maumbo ya kimazingatio. Ushikaji huu wa maumbo umekuja katika majira haya ya machipuo ili kushika mahali pa kuchukua nafasi ya ushikaji maumbo kulikotangulia. Na hilo ni kwa ajili ya kufidisha maana ya mambo ya majina ya kiungu ambayo huja upya midhihiriko yake mfululizo. Nne: Hakika ya Mwingi wa hekima Mwenye utukufu anazichakata atomu katika shamba la dunia hii finyu na kuzifuma katika kiwanda cha Ardhi, akivifanya viumbe kuwa ni vyenye kutiririka na vilivyopo kuwa ni vyenye kutembea. Na hii ni kwa ajili ya kuandaa vinavyowiana miongoni mwa yanayolazimu au mapambo au mavuno ya limwengu pana zisizo na mpaka. Kama ulimwengu wa mfano na ulimwengu mpana mno wa Malakuut (ufalme usioonekana) na baki ya limwengu za Akhera zisizo na ukomo. Basi (s.w.) anaandaa katika Ardhi hii ndogo mavuno na matokeo mengi ya kimaanawi kwa ajili ya limwengu hizo kubwa na pana mno. Na hupitisha kutoka duniani mtiririko usio na ukomo unaochimbuka kutoka katika hazina ya uweza wake wa hali zote na kuumimina katika ulimwengu wa ghaibu, na fungu jengine analimimina katika limwengu za Akhera. Tano: Allah (s.w.) anaziweka atomu katika michakato kwa uweza wake katika hekima kamili na kuzitumikisha katika majukumu yaliyopangika kwa ajili ya kudhihirisha makamilifu ya kiungu yasiyo na mwisho, na midhihiriko ya uzuri usiyo na mpaka, na midhihiriko ya kiutukufu isiyo na ukomo, na tasbihati za uungu wa Bwana Mlezi zisizo na idadi, katika Ardhi hii finyu yenye mpaka, na katika muda mchache wenye ukomo wa udogo. Basi (s.w.) anavijaalia vilivyopo vinaleta tasbihi zisizo na mwisho katika muda wenye kuisha na katika eneo lenye mpaka, akibainisha kwa hilo midhihiriko yake ya uzuri, ukamilifu na utukufu wa hali zote, akizifanya ziwepo hakika nyingi za ghaibu na matunda mengi ya Akhera, na mengi katika maajabu ya kupigiwa mfano – za sura za wenye kutoweka na nyasifu zao zenye kubaki - na mingi ya mifumo ya mabango yenye hekima. Basi yule ambaye anazipa atomu mchakato na kudhihirisha makusudio haya makubwa na hekima hizi kubwa, kwa hakika huyo ni mmoja wa pekee. Kama si hivyo, basi inapasa kila punje iwe na akili ya ukubwa wa jua! Na namna hii. Ipo mifano mingi mno juu ya mabadiliko ya atomu, ambazo zinapewa michakato kwa hekima ya hali ya juu, kama vielelezo hivi vitano. Bali huenda vinavuka zaidi ya mifano elfu tano. Isipokuwa, wanafalsafa hao wapumbavu wamezidhania kuwa ziko tupu bila ya hekima! Hakika wamedai – katika ukweli – kwamba atomu na katika michakato yake miwili ambayo kwa michakato hiyo hufanya utendaji wake kuwa katika uchangamfu na mvuto wa uungu wa Bwana Mlezi, mmoja wapo ni wa kiupeo wa kifikra, na mwingine ni wa kinafsi, na wenye kutopea katika dhikiri na tasbihi ya kiungu kama Muridi wa Meulawi. Kwa hakika hutenda hilo kutokana na nafsi yake yenyewe, na kucheza kwa mshituko na kuzunguka. Tunafupisha kutokana na hili kwamba: Ujuzi wa wanafalsafa hao sio ujuzi, bali ni ujinga. Na kwamba hekima yao ni upuuzi na ni tupu haina hekima! (Tutaeleza katika Nukta ya Tatu hekima nyingine ndefu ambayo ni ya Sita).
Kwa hakika katika kila atomu zipo shuhuda mbili za kweli juu ya kuwepo kwa Allah (s.w.) na juu ya upekee wake. Ndiyo, hakika atomu kwa kutimiza majukumu makubwa mno, na kubeba mizigo mizito mno inayozidi uwezo wake, katika ukomo wa utambuzi pamoja na kutojiweza kwake na kuwa ni yabisi, inashuhudia ushahidi wa kukinaisha juu ya kuwepo kwa Allah (s.w.), na kwamba inashuhudia ushahidi wa kweli pia juu ya umoja-pekee wa Allah na upekee wa maalikul mullki walmalakuti (mmiliki wa ufalme wa dhahiri na wa siri); kwa kuratibika mchakato wake na kupatana kwake pamoja na mfumo jumla unaojiri kwenye ulimwengu na kuchunga mpangilio wake kila mahali ilipo, na kukaa huko kana kwamba ni makazi yake. Yaani kwa nani umiliki wa atomu unarejea, na hatamu ya atomu iko mkononi mwa nani? Basi mahali pa mizunguko yake ni ufalme wake na unarudi kwake. Kwa maana kwamba yule ambaye atomu ni yake, basi kwa hakika maeneo yote ambayo inayatembea ni yake pia. Yaani kwa kuwa atomu ni yenye kushindwa (haijiwezi) na mzigo wake ni mzito mno, na majukumu yake ni mengi yasiyo na mpaka, hayo yanajulisha kwamba atomu ni yenye kusimama na kuchakatika kwa jina la Mweza mwenye uweza wa hali zote na kwa amri yake. Kisha, kuuafikisha mchakato wake na kuufanya upatane pamoja na mifumo mikuu yote katika ulimwengu, na kana kwamba ina ujuzi nayo, na kuingia kila mahali na bila ya kizuizi kinachoizuia; inajulisha kwamba hiyo inafanya inachofanya kwa uweza wa mmoja mjuzi mwenye ujuzi wa hali zote na kwa hekima yake kunjufu. Naam, hakika ya askari ana uhusiano na kujinasibisha pamoja na kila kikosi chake, brigedi yake, batalioni yake, jenerali wake, na kikundi chake; kama ambavyo kila kimoja katika ya hayo kina jukumu maalumu kwa kadiri ya uhusiano huo. Na kwamba kuratibu mchakato na kupatana pamoja na mahusiano yote haya na mafungamano ni kwa kuyajua na kujua majukumu yake katika kila kitengo, pamoja na kutimiza mambo ya wajibu wa kiaskari ikiwemo mazoezi na kuchukua mafunzo kulingana na mifumo yake... Yote hayo kwa hakika yanatokea kwa kufuata amri za kiongozi mkuu ambaye anaongoza vitengo hivyo vyote na kufuata kanuni zake. Kama jambo liko namna hii kwa askari mmoja, basi vivyohivyo kila atomu katika atomu zenye kuingia katika miundo yenye kuingiliana baadhi yake na nyingine, ina hali zenye kuwiana katika kila moja kati yao, na mahali penye kunasibiana panajengeka juu yake masilahi anwai, na majukumu mbalimbali yaliyopangika, na matokeo tofauti yenye hekima. Basi hapana budi kwamba kuipa uenyeji atomu hiyo kati ya mifumo hiyo, kwa uupaji uenyeji ambao hautii dosari matokeo na hekima zitokanazo na kunasibiana huko na majukumu, pamoja na kuyatunza mahusiano yote na majukumu, ni mahususi kwa Maalikul Mulk (Mmiliki wa ufalme) ambaye mkononi mwake zimo hatamu za kila kitu. Basi mathalani: Hakika ya atomu iliyotulia katika mboni ya jicho la “Tevfik” ina uhusiano na mishipa ya neva za jicho yenye mchakato na hisia, pamoja na mishipa midogo-midogo na neva zilizomo ndani yake, na pamoja na uso, kichwa, kisha pamoja na kiwiliwili, na pamoja na mwanadamu kiwiliwili kizima. Ukiongezea kwamba katika kila moja kati ya hizo ina jukumu na faida fulani. Basi kuwepo kwa minasaba hiyo, katika kila moja kati yake, na mahusiano na faida pamoja na hekima kamili na ufundi timamu, vinabainisha kwamba yule ambaye ameuumba mwili huo pamoja na viungo vyake vyote, ndiye ambaye anaiwezesha atomu hiyo kuthibiti mahali hapo, na hasa atomu zenye kuleta riziki. Basi atomu hizo zinazoenda pamoja na msafara wa riziki na kusafiri pamoja nao, kwa hakika huenda kwa mpangilio na kutembea kwa hekima inayozifanya akili kutahayari. Kisha inaingia katika hatua mbalimbali na kuzunguka katika matabaka anwai kwa mpangilio makini. Basi inapiga hatua zenye utambuzi, bila ya kukosea hadi inakuja kidogo-kidogo mpaka katika mwili hai. Na huko huchujwa katika machujio manne ndani yake, mpaka kufika katika viungo na vipenyo vidogo-vidogo vinavyohitajia riziki, na kuvipa. Na kuvisaidia kwa kanuni ya ukarimu ikibebwa na seli nyekundu za damu. Inafahamika kwa uwazi kwamba yule ambaye ameziamrisha atomu hizi kupitia maelfu ya vituo mbalimbali na matabaka tofauti, na kuzipeleka namna hii kwa hekima, hapana budi na bila ya chembe ya shaka kuwa yeye ndiye Razzaaq, Kariim, Khallaaq, Rahiim (Mwenye kuruzuku, Mkarimu, Muumbaji, Mwenye huruma); mbele ya uweza wake, nyota na atomu vinakuwa sawasawa. Kisha, kila atomu miongoni mwa atomu inafanyakazi ya kufanya sura ya kupendeza na nakshi ya kuvutia kwa viumbe, kiasi kwamba ima ipo pahali pa hakimu mwenye kutawala juu ya kila atomu moja miongoni mwa atomu na kwa kundi lake, na zenye kutawaliwa wakati huohuo chini ya amri ya kila atomu moja katika atomu na amri ya kundi lake, na kwamba inatambua utambuzi kamili kwa sura yenye kupendeza yenye kuzishangaza akili na nakshi ya kuvutia yenye kujaa hekima, basi huifanya iwepo! Na hili ni muhali kwa mihali elfu... au ni nukta yenye kuamrishwa kwa mchakato unaotokana na kalamu ya uweza wa Allah (s.w.) na kanuni ya kudura yake. Basi mathalani: Kwa hakika mawe yaliyopo katika kuba la “Aya Sofya” yasipokuwa tiifu kwa amri ya wajenzi wake, basi inapasa kila jiwe katika kuba hilo liwe ni mahiri katika tasnia ya ujenzi kama “mhandisi majengo Sinan” mwenyewe kabisa, na liwe (jiwe) ni lenye kuyahukumu mawe mengine na ni lenye kuhukumiwa kwa amri yao katika wakati huohuo. Yaani inayumkinika kwa jiwe hilo kuyahukumu mawe mengine na kuyaambia: “Haya enyi mawe, na tuungane hadi tuweke kizuizi tusianguke”! Na jambo hilo liko hivyohivyo katika atomu zilizomo ndani ya viumbe, ambavyo ni vyenye kutengenezwa vyema zaidi na kwa umakini zaidi, na ni vyenye kupendeza zaidi na kushangaza zaidi, na ni vyenye hekima zaidi kuliko kuba la Aya Sofia kwa maelfu ya mara. Kama atomu hizi hazifuati amri ya Muumba mtukufu, Muumba wa ulimwengu, basi inapasa kila moja kati ya hizo ipewe sifa za ukamilifu ambazo hazistahiki isipokuwa kwa Allah (s.w.). Fa yaa Subhaanallah! Yaa lal-ajab (Ajabu iliyoje!) Hakika ya wanamaada wazandiki makafiri walipomkanusha Allah ambaye ni wa wajibu kuwepo, kulingana na madhehebu yao, wamelazimika kuiitakidi miungu batili kwa idadi ya atomu. Na kutokana na upande huu, unaona kwamba kafiri mwenye kukanusha kuwepo kwa Allah (s.w.) vyovyote atavyokuwa ni mwanafalsafa na mwanazuoni, basi yuko katika ujinga mkubwa, na yeye ni mjinga wa ujinga wa hali zote.
Nukta hii ni ishara ya hekima kubwa ya sita ambayo imeahidiwa kwenye hitimisho la Nukta ya Kwanza. Nayo ni: Kwa hakika imeelezwa katika tanbihi ya swali la pili kutoka katika “Neno la Ishirini na Nane” kwamba: Hekima nyingine katika maelfu ya hekima ambazo zimo ndani ya mabadiliko ya atomu na michakato yake katika viwiliwili vya wenye uhai ni kuzinawirisha atomu kwa uhai na kuvuna kwake maana na faida ili atomu ziwe ni zenye kustahiki kuujenga ulimwengu wa Akhera. Naam, hakika (kiumbe) mnyama na binadamu, na hata mimea ni sawa na mahala pa ugeni kwa atomu hizo na ni kambi ya mazoezi kwake. Ni madrasa ya kimalezi ambayo zinapokea ndani yake maelekezo kiasi kwamba atomu hizo yabisi zinaingia hapo na kupata nuru, kana kwamba zinapata mafunzo na kupokea amri na maelekezo. Basi huwa na upole, na kwa kila moja kati yake hutekeleza jukumu fulani. Hivyo, hupata ukakamavu na ufanisi, ili ziwe ni atomu za ulimwengu wa kubakia na makazi ya Akhera yaliyo hai kwa uhai wenye kukusanya sehemu zake zote. Swali: Hutambulikaje uwepo wa hekima hii katika michakato ya atomu? Jibu: Kwanza: Hutambulika uwepo wake kwa hekima ya Allah mwingi wa hekima (s.w.). Ni hekima thabiti kwa mifumo iliyopo katika vilivyopo vyote na kwa hekima zinazofungamana nazo; kwani hekima ya kiungu ambayo imezikabidhisha hekima nzima-nzima nyingi mno kwa kitu kidogo sana cha kijisehemu fulani, haiyumkiniki kuiacha michakato ya atomu burebure bila ya hekima! Ni hiyo michakato inayojiri katika mfereji wa viumbe, na ambayo inaonesha utendaji mkubwa katika uwepo, na ambayo ndiyo sababu ya kudhihirisha maajabu yenye hekima. Kisha, hekima ya kiungu na utawala wake ambao haukipuuzi kiumbe kidogo mno bila ya malipo, au bila ya ukamilifu, au bila ya makamo, kutokana na jukumu analolitimiza, vipi awapuuze waamrishwa wake na watumiwa wake wengi mno, atomu... bila ya nuru au bila ya ujira. Pili yake: Hakika Al-Hakiim Al-Aliim anazipa mchakato chembe na kuzitumia ili zitekeleze majukumu matukufu. Basi huzipandisha cheo kuwa katika daraja la madini, ikiwa ni malipo yake katika njia ya ukamilifu... Na huzipa mchakato atomu za madini na kuzitumikisha katika majukumu fulani na kuzifundisha tasbihi zake maalumu kwake. Hivyo huzitunuku cheo hai cha mimea... Na huzipa mchakato atomu za mimea na kuzipa majukumu, na kuzifanya ziwe ni riziki kwa wengine. Hivyo basi huzineemesha juu yake kwa kuzinyanyua hadi cheo chema cha wanyama... Na anazitumia atomu za wanayama – kwa njia ya riziki – basi huzinyanyua hadi daraja la uhai wa mwanadamu... Na kwa kupitisha atomu za kiwiliwili cha mwanadamu kupitia vichujio kadhaa kwa mara kadhaa, na kuzisafisha na kuzifanya kuwa ni njema. Basi huzipandisha hadhi hadi katika mahali pema zaidi na eneo tukufu mno katika kiwiliwili nalo ni ubongo na moyo. Kutokana na yaliyoelezwa, inafahamika kwamba michakato ya atomu sio ya burebure, na sio kwamba michakato yake ni mitupu isiyo na hekima. Bali huharakishwa atomu na kupelekwa kwenye aina ya ukamilifu unaozistahiki. Tatu: Sehemu fulani katika atomu za kiumbe hai – kama atomu za mbegu na kokwa - hupata nuru za kimaanawi, upole na sifa pambanuzi - kiasi ambacho zinakuwa kama roho na mfalme kwa atomu nyingine, na kwa mti mkubwa wenyewe. Basi atomu hizi – kati ya kundi la atomu za mti mkubwa – kuikwea ngazi hii, kwa hakika ni matokeo ya utekelezaji wake wa majukumu nyeti na kazi tukufu katika hatua za ukuaji wa mti. Jambo linalojulisha kwamba atomu hizo wakati zikitekeleza majukumu yake ya kimaumbile kwa amri ya Muumba Mwenye hekima hupata upole wa kimaanawi na nuru ya kimaanawi na makamo ya juu na mwongozo wa hadhi ya juu, kulingana na michakato yake na kulingana na yanayodhihiri juu yake katika midhihiriko ya majina mazuri, na kutukuka kwa majina hayo. Muhtasari: Hakika Muumba Mwenye hekima zote amebainisha kwa kila kitu nukta ya ukamilifu inayonasibiana na kitu hicho, na ameweka mipaka ya nuru ya uwepo inayoistahikia. Hivyo, hukipeleka kitu hicho katika nukta hiyo ya ukamilifu, kwa matayarisho anayokipa kitu hicho. Kanuni hii ya uungu wa Rububiyya, kama inavyopita katika mimea yote na wanyama, basi pia ni yenye kufanya kazi katika vitu yabisi. Hadi Allah (s.w.) anaupa mchanga wa kawaida cheo hadi kufikia daraja ya almasi na daraja ya mawe ya thamani. Kutokana na hakika hii, inafunguka sehemu ya kanuni kubwa. Nayo ni “Kanuni ya Uungu”. Na kwamba huyo Muumba Mkarimu katika kuwatumikisha wanyama ili kutekeleza kanuni kuu ya kuzaana, huwapa ladha ya kiasi kidogo kutokana na kutekeleza jukumu hilo. Na huwapa wanyama wenye kutumiwa ili kutekeleza amri za kiungu, kama kasuku, ndege shore na nyuki – ujira wa ukamilifu uliotukuka, makamo yanayoleta ashiki na burudani... Kutokana na uhakika huu inafunuka sehemu fulani ya kanuni hii kubwa. Nayo ni: “Kanuni ya Ukarimu”. Kisha, uhakika wa kila kitu unaelekea katika kudhihiri kwa jina fulani miongoni mwa majina mazuri ya kiungu, na yenye kufungamana na uhakika huo. Nayo (majina mazuri) ni kama kioo chenye kuakisi nuru zake. Basi kitu hicho kwa vyovyote kitakavyojifanyia katika hali nzuri, uzuri huo unarejea kwenye utukufu wa jina hilo na hadhi yake ya juu; ambapo jina hilo linaihitajia. Ni sawa kitu hicho kiwe kimejua au hakikujua. Basi hali hiyo nzuri ni yenye kutakiwa katika mtazamo wa uhakika. Kutokana na ukweli huu, inadhihiri sehemu ya kanuni kubwa. Nayo ni: “Kanuni ya Kupendezesha na Urembo”. Kisha, kile alichotoa Muumba Mwenye hekima zote miongoni mwa makamo na ukamilifu kukipa kitu fulani, kwa muktadha wa kanuni ya ukarimu, hakiponi tena, wakati kitu hicho muda wake ukimalizika na kukoma umri wake. Bali hubakisha matunda yake, matokeo yake, wasifu wake wa kimaanawi, maana yake, na roho yake kama kikiwa ni chenye roho. Basi mathalani: (s.w.) anabakisha maana za makamilifu ambayo mwanadamu anayapata na matunda yake, mpaka pale muumini mwenye shukurani akishukuru na kuhimidi juu ya anachokula katika matunda yenye kutoweka. Basi Allah (s.w.) anamrejeshea kwa mara nyingine kwa sura ya tunda zuri lenye umbo katika matunda ya Peponi. Kutokana na ukweli huu, inafunuka sehemu fulani ya kanuni kubwa. Nayo ni: “Kanuni ya Rehema”. Kisha, Muumba Mwenye hekima zote (s.w.), hafanyi israfu katu katika kitu, wala hafanyi mchezo kabisa katika hali zote. Kwani anatumia hadi mabaki ya kimaada ya viumbe waliokufa – ambao majukumu yao yamekwisha – katika majira ya mapukutiko – ili kuviunda viumbe vipya katika majira ya machipuo. Kwa ajili hiyo, katika muktadha wa hekima ya kiungu, kuziingiza atomu hizi yabisi za ardhini, na zisizotambua, na ambazo zimeshatimiza majukumu matukufu katika Ardhi katika sehemu ya majengo ya Akhera, Ardhi ambayo iko hai na yenye utambuzi kwa kila kilichomo, mawe yake na miti yake kwa kumaanisha dalili ya aya tukufu (يَوْمَ تُبَدَّلُ الأَرْضُ غَيْرَ الأَرْضِ) na kwa ishara ya aya tukufu (وَإِنَّ الدَّارَ الْآخِرَةَ لَهِيَ الْحَيَوَانُ لَوْ كَانُوا يَعْلَمُونَ) na kwa sababu kuziacha atomu za Dunia zenye kuvunjika zenyewe Duniani, au kuzitupa zitokomee ni israfu na ni upuuzi. Kutokana na ukweli huu, inafunuka sehemu fulani katika kanuni kubwa. Nayo ni: “Kanuni ya Hekima”. Kisha, athari nyingi mno za Dunia hii na hali zake za kimaanawi, matunda yake na mifumo ya matendo ya wenye kukalifishwa – kama majini na watu - na madaftari ya amali zao, na roho zao na viwiliwili vyao, hupelekwa katika soko la Akhera na maonesho yake. Basi pia ni katika muktadha wa uadilifu na hekima kwa atomu za ardhini ambazo zimefuatana na matunda hayo, maana na wahudumu wake pamoja na mabaki ya Dunia hii ambayo itateketezwa, kupelekwa kwenye ulimwengu wa Akhera na kutumika katika kuujenga. Na hii ni baada ya atomu hizo kukamilika kwa ukamilikaji unaouhusu kwa upande wa jukumu, yaani baada ya kuwa imepata nuru ya uhai kwa wingi na kuutumikia na imekuwa ni nyenzo ya tasbihi za uhai. Kutokana na ukweli huu, inafunuka sehemu fulani ya kanuni kubwa. Nayo ni: “Kanuni ya Uadilifu”. Kisha, roho, kama ambavyo ni yenye kuutawala mwili, basi amri za kuumbwa maada yabisi ambazo zimeandikwa na kudura ya kiungu, ina madaraka pia juu ya maada hizo. Basi maada hizo zinajitengenezea nafasi zake, na zinakwenda kwa mpangilio maalumu kulingana na zinavyoamuriwa na maandishi ya kimaanawi ya kudura ya kiungu. Mathalani: Katika aina za mayai, na vigawanyo vya mafuta ghafi, na aina za kokwa, na spishi za mbegu; maada zinapata nuru mbalimbali na makamo tofauti kulingana na kutofautina kwa amri za uumbaji ambazo kudura ya kiungu imeziandika kwa namna anwai na maumbo yenye kupishana; ambapo maada hizo - kwa kuwa ni maada – huwa katika uhalisia mmoja . Isipokuwa, inakuwa ni nyenzo ya kuzaliwa kiasi kisicho na mpaka cha vilivyopo. Hivyo, inakuwa ni yenye makamo mbalimbali na nuru anwai. Kwa hivyo, hapana budi kama ingepatikana atomu moja katika huduma za uhai na kuingia ndani ya tasbihi za kiungu, ambazo uhai nao husabihi mara kadhaa wa kadhaa, na kutekeleza jukumu lake huko. Hapana shaka basi huandikwa katika uso wake wa kimaanawi hekima za maana hizo, na kalamu ya kudura ya kiungu huzisajili. Kalamu ambayo hakiponyoki kitu chochote isikidiriki. Hili ni kwa muktadha wa elimu ya kiungu yenye kuzunguka. Kutokana na ukweli huu, inafunuka sehemu fulani katika kanuni kubwa. Nayo ni: “Kanuni ya Elimu yenye Kuzunguka”. Basi kwa mujibu wa yaliyotangulia: Atomu, hazikutelekezwa wala kuachwa ziponyoke. Matokeo: Kwa hakika kanuni saba zilizotangulia, yaani kanuni ya uungu wa Rububiyya, kanuni ya ukarimu, kanuni ya uzuri, kanuni ya rehema, kanuni ya hekima, kanuni ya uadilifu, na kanuni ya elimu yenye kukizunguka kila kitu... na mfano wake katika kanuni kubwa-kubwa; kila moja kati ya hizo inakiashiria kile kinachofichuka, ambacho ni jina tukufu zaidi la Allah, na mng’ao tukufu wa hilo jina Ismul A’adhwam (tukufu zaidi). Kutokana na kudhihirika huko inafahamika kwamba: Mabadiliko ya atomu katika Dunia hii pia – ni kama baki ya vilivyopo – vinazunguka kulingana na kudura ya kiungu ilivyoandika kwenye mipaka fulani, na kulingana na amri za uumbaji zinazotolewa na uweza wa kiungu, na kwa msingi wa kipimo nyeti cha kielimu, kwa ajili ya hekima za hadhi ya juu. Kana kwamba vinajiandaa kuondoka kwenda kwenye ulimwengu mwingine wa hadhi ya juu zaidi . Na kutokea hapa, viwiliwili hai vimehisabiwa kana kwamba ni madrasa, ambazo atomu zenye kutembea zinajifunza kwenye madrasa hiyo. Ni kambi yake ya mafunzo, na ni mahali pa mwaliko wa kimalezi. Inafaa sisi kuhukumia kwa makisio ya kweli kuwa viko hivyo. Kwa Ujumla: Kama ilivyoelezwa katika “Neno la Kwanza” na kuthibitishwa huko kwamba: Kila kitu kinasema: “Bismillah”. Basi atomu pia kama vilivyo vilivyopo vyote na kila kundi kati yao na kila jamaa katika jamaa zake wanasema kwa ulimi wa hali: “Bismillah” na kuchakatika kulingana na neno hilo. Naam, kila atomu – kwa dalili ya nukta tatu zilizoelezwa - inasema kwa ulimi wa hali yake mwanzoni mwa mchakato wake: “Bismillahi Rrahmani Rrahiim” yaani nafanya mchakato kwa jina la Allah, kwa nguvu zake, kwa uweza wake, kwa idhini yake na katika njia yake. Kisha inasema - na kila kundi kati yake – baada ya kumaliza harakati zake kwa namna ya anavyosema kiumbe yoyote yule kwa ulimi wa hali yake: Alhamdu Lillah Rabbil A’alamiin. Basi kila atomu inajionesha katika hukumu ya unyoya wa kalamu ndogo ya uweza wa kiungu katika kusawiri kila kiumbe mwenye kupendeza ambaye ni sawa na kasida ya kumsifia na kumhimidi Allah (s.w.). Bali kila atomu inajibainisha katika sura ya ncha ya sindano ya mikono ya kimaanawi isiyo na mpaka, ya mshonaji wa kiungu aliyetukuka. Sindano inazunguka katika magurudumu – nayo ni kazi za ufundi wa kiungu – na kuzitamkisha kasida za kiungu za kumsifia na kumhimidi, na kuziimbisha nashiidi za tasbihi za kiungu… دَع۟وٰيهُم۟ فٖيهَا سُب۟حَانَكَ اللّٰهُمَّ وَتَحِيَّتُهُم۟ فٖيهَا سَلَامٌ وَ اٰخِرُ دَع۟وٰيهُم۟ اَنِ ال۟حَم۟دُ لِلّٰهِ رَبِّ ال۟عَالَمٖينَ سُب۟حَانَكَ لَا عِل۟مَ لَنَٓا اِلَّا مَا عَلَّم۟تَنَٓا اِنَّكَ اَن۟تَ ال۟عَلٖيمُ ال۟حَكٖيمُ رَبَّنَا لَا تُزِغ۟ قُلُوبَنَا بَع۟دَ اِذ۟ هَدَي۟تَنَا وَهَب۟ لَنَا مِن۟ لَدُن۟كَ رَح۟مَةً اِنَّكَ اَن۟تَ ال۟وَهَّابُ اَللّٰهُمَّ صَلِّ عَلٰى سَيِّدِنَا مُحَمَّدٍ صَلَاةً تَكُونُ لَكَ رِضَاءً وَ لِحَقِّهٖ اَدَاءً وَ عَلٰى اٰلِهٖ وَ صَح۟بِهٖ وَ اِخ۟وَانِهٖ وَ سَلِّم۟ وَسَلِّم۟نَا وَ سَلِّم۟ دٖينَنَا اٰمٖينَ يَا رَبَّ ال۟عَالَمٖينَ

